Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah056 - Al-Khabiyr

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 056 kati ya 103
Al-Khabiyr — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Khabiyr: Mjuzi Wa Khabari Za Dhahiri Na Siri

Yeye Ni Ambaye Ujuzi Wake umevizunguka vitu vya ndani na vilivyofichika kama ulivyovizunguka vya dhahiri. Ni Mjuzi wa Waja Wake wote, Mwenye khabari za mambo yao; Anajua undani wa kitu na uhakika wake, na hakimpotei hata chenye uzito wa chembe ndogo kabisa, wala hakitikisiki wala kutulia kitu isipokuwa Anayo khabari yake. Na maana ya Al-Khabiyr ni sawa na Al-‘Aliym (Mjuzi), lakini ujuzi unapohusishwa na mambo yaliyofichika ya ndani huitwa khibrah, na mwenye nao huitwa Khabiyr.

Allaah (سبحانه وتعالى) Amejiita Al-Khabiyr mara sita katika Qur-aan, na mara nyingi Sifa Yake ya kuwa Khabiyr huja pamoja na Sifa Zake za Al-Hakiym (Mwenye Hikmah), Al-Baswiyr (Mwenye Kuona) na Al-Latwiyf. Miongoni mwa Aayah hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٤﴾

Kwani Hajui Yule Aliyeumba! Na hali Yeye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri! [Al-Mulk (67:14)]

Na Allaah (تبارك وتعالى) Ana maana nyingi katika Jina Hili:

1-Al-Khabiyr Ni Mjuzi wa kila kitu, Mwenye kudhihirisha kila kitu kwa uhakika wake.1 Anasema (سبحانه وتعالى):

الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ الرَّحْمَـٰنُ فَاسْأَلْ بِهِ خَبِيرًا ﴿٥٩﴾

Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arsh. (Yeye ni) Ar-Rahmaan, basi ulizia kuhusu Yeye, kwani Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-Furqaan (25:59)]

2-Naye Ndiye Mjuzi Ambaye ilimu ndio kikomo chake; Mwenye kujua ya ndani na ya dhahiri, Mwenye kujua maslahi ya vitu na madhara yake; mambo hayafichiki Kwake, yawe ni mwanzo wake au matokeo yake.2

3-Naye (سبحانه وتعالى) Ndiye Mjuzi wa yaliyomo ndani ya nyoyo, na yaliyojificha ndani ya mbegu, na yaliyomo ndani ya viza, hata yakiwa madogo kiasi gani.3 Anasema (سبحانه وتعالى):

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾

Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote, Naye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-An‘aam (6:103)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Khabiyr:

1-Aliyeumba Ndiye Anayejua Undani Wa Viumbe Vyake:

Al-Khabiyr Anajua siri za nyoyo na undani wa mambo kwa sababu Yeye Ndiye Muumba wa kila kitu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ﴿١٤﴾

Kwani Hajui Yule Aliyeumba! Na hali Yeye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri! [Al-Mulk (67:14)]

2-Mche Al-Khabiyr Na Ufuate Sharia Zake:

Allaah Kujitaja kwa Jina la Al-Khabiyr kumekuja kuhimiza taqwa, kutahadharisha maasi na kuhimiza utiifu. Na mara nyingi katika Qur-aan, Allaah (عزّ وجلّ) Hutaja Sifa Yake ya kujua yote mnayoyatenda baada ya kutaja moja ya Sharia Zake. Basi fuata kanuni na sharia Alizokuwekea Al-Khabiyr katika Qur-aan na Sunnah kwa kadiri ya uwezo wako. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١٨﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myatendayo. [Al-Hashr (59:18)]

3-Tambua Kwamba Al-Khabiyr Atakujulisha Uliyoyatenda, Na Upate Faraja Kwake:

Allaah Al-Khabiyr Ndiye Pekee Anayejua yote unayoyafanya, unayoyasema, unayoyaficha na unayoyataka; basi jambo hili la ajabu likupe faraja wakati wa shida, na wakati wa raha likukumbushe usishikamane mno na dunia hii na manufaa yake. Na si kwamba Allaah Anajua amali zako zote tu, bali Siku ya Qiyaamah Atakujulisha yote uliyokuwa ukiyatenda. Kumbuka hili kila siku na likuhamasishe kutenda mema, na unapoteleza, muombe maghfirah katika maisha haya ili uokoke na Adhabu Yake katika maisha yajayo. Na Allaah Amekhabarisha kuhusu funguo za ghaibu na mambo ya mustaqbali, na hakuna anayekhabarisha mambo kama hayo isipokuwa Yeye Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ ﴿١٤﴾

Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni. Na Siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu, na wala hakuna atakayekujulisha vilivyo, kama Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Faatwir (35:14)]

4-Jihesabu Kwa Yale Uliyoyatanguliza Kwa Ajili Ya Kesho:

Al-Khabiyr Anajua amali zako zote, basi jitazame kabla hujatazamwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١٨﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myatendayo. [Al-Hashr (59:18)]

5-Al-Khabiyr Anatazama Nyoyo Na Amali, Si Sura Wala Mali:

Kumbuka kwamba Al-Khabiyr Hapimi thamani yako kwa sura yako wala mali yako, bali kwa moyo wako na amali zako.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلَى صُوَرِكُمْ وَأَمْوَالِكُمْ، وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ وَأَعْمَالِكُمْ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Haangalii sura zenu wala mali zenu, lakini Anaangalia nyoyo zenu na amali zenu.” [Muslim]

6-Ijue Kwa Undani Nafsi Yako Na Moyo Wako:

Tambua, ee Mja wa Al-Khabiyr: Inampasa mja awe mjuzi wa yanayopita ndani ya ulimwengu wake wa ndani kabla ya ulimwengu wa nje; na ulimwengu wake wa ndani ni moyo wake na mwili wake, na siri zinazoweza kuwa moyoni kama udanganyifu, khiyana, kuficha shari na kudhihirisha kheri. Kwani nafsi inaweza kumdanganya mwenyewe kwa kujipamba na kuonyesha ikhlaasw nayo haina kitu. Na hila kama hizo za nafsi, mja huzigundua ikiwa ameijua nafsi yake kwa undani na akajua vitimbi vyake, udanganyifu wake na hila zake; basi hujizuia kuangukia katika hila na matamanio ya nafsi. Na mwenye kuijua nafsi yake kwa undani, hupata uwezo wa kuujua ulimwengu wa nje unaomzunguka, na hujua Hikmah ya Allaah katika uumbaji, neema na misiba, hivyo haangukii katika fitnah za viumbe wala vitimbi vya shaytwaan. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... أَلاَ وَإِنَّ فِي الْجَسَدِ مُضْغَةً، إِذَا صَلَحَتْ صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّهُ، وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ، أَلاَ وَهِيَ الْقَلْبُ))

Amesimulia An-Nu‘maan bin Bashiyr (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “... Tanabahi! Hakika katika mwili kuna pande la nyama; likitengenea, mwili wote hutengenea, na likiharibika, mwili wote huharibika. Tanabahi! Nalo ni moyo.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

7-Usiharakishe Kuwahukumu Watu:

Mara nyingi tunaharakisha kuwahukumu wengine. Usisahau kwamba huna ujuzi wa uhakika wa ndani wa watu wengine; Anayeujua ni Al-Khabiyr Pekee. Kwa hiyo kuwa mwangalifu katika kuwahukumu wengine, si kwa kuwakosoa tu bali hata kwa kuwasifu kupita kiasi, na daima sema: Hukumu yako naiachia Allaah! Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلَى صُوَرِكُمْ وَأَمْوَالِكُمْ، وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ وَأَعْمَالِكُمْ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Hatazami sura zenu wala mali zenu, lakini Anatazama nyoyo zenu na amali zenu.” [Muslim]

8-Elewa Uhalisia Wa Dunia Hii:

Al-Khabiyr Anajua uhakika wa dunia hii na thamani yake ndogo. Basi elewa udogo wa dunia hii, lakini wakati huo huo tambua kwamba maisha haya ndiyo fursa yako pekee ya kujitahidi kupata makazi yako ya milele Jannah. Basi yafanye maisha yako yawe na thamani kwa kuzingatia mawaidha ya Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), na uyajaze kwa amali zitakazokunufaisha katika maisha yajayo!

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) مَرَّ بِالسُّوقِ ... فَمَرَّ بِجَدْيٍ أَسَكَّ مَيِّتٍ، فَتَنَاوَلَهُ فَأَخَذَ بِأُذُنِهِ ثُمَّ قَالَ: ((أَيُّكُمْ يُحِبُّ أَنَّ هَذَا لَهُ بِدِرْهَمٍ؟)) فَقَالُوا: مَا نُحِبُّ أَنَّهُ لَنَا بِشَيْءٍ، وَمَا نَصْنَعُ بِهِ؟ قَالَ: ((أَتُحِبُّونَ أَنَّهُ لَكُمْ؟)) قَالُوا: وَاللَّهِ لَوْ كَانَ حَيًّا كَانَ عَيْبًا فِيهِ لأَنَّهُ أَسَكُّ، فَكَيْفَ وَهُوَ مَيِّتٌ! فَقَالَ: ((فَوَاللَّهِ لَلدُّنْيَا أَهْوَنُ عَلَى اللَّهِ مِنْ هَذَا عَلَيْكُمْ))

Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipita sokoni ... akapita karibu na mbuzi mdogo aliyekufa mwenye masikio madogo mno. Akamchukua, akamshika sikio lake, kisha akasema: “Nani kati yenu angependa huyu awe wake kwa dirham moja?” Wakasema: Hatupendi awe wetu kwa kitu chochote, na tutamfanyia nini? Akasema: “Je, mngependa awe wenu (bure)?” Wakasema: Wa-Allaahi, hata kama angekuwa hai angekuwa na kasoro kwa kuwa masikio yake ni madogo mno, basi itakuwaje na yeye amekufa! Akasema: “Basi Wa-Allaahi, dunia ni duni zaidi mbele ya Allaah kuliko huyu alivyo duni mbele yenu.” [Muslim]

9-Jitahidi Kufanya Amali Njema Za Siri:

Jitahidi, ee ndugu Muislamu, kuwa na amali njema za siri zisizojulikana isipokuwa na Al-Khabiyr.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِن تُبْدُوا الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ ۖ وَإِن تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاءَ فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۚ وَيُكَفِّرُ عَنكُم مِّن سَيِّئَاتِكُمْ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿٢٧١﴾

Mkidhihirisha swadaqa basi ni vizuri hivyo, na mkizificha na kuwapa mafakiri, basi hilo ni kheri kwenu. Na Atakufutieni katika maovu yenu. Na Allaah kwa yale myatendayo Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-Baqarah (2:271)]

Hamasika kutenda mema si kwa ajili ya macho ya watu bali kwa ajili ya Allaah Al-Khabiyr! Hii ina maana kwamba utafurahia kikamilifu amali njema unazoweza kuzificha, kwa kuwa unajua unazifanya kwa ajili ya Al-Khabiyr, na ukweli kwamba Yeye Pekee Ndiye Anayezijua utakufanya ujihisi karibu Naye. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amewataja miongoni mwa watu saba ambao Allaah Atawafunika katika kivuli Chake Siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli Chake:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمُ اللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لاَ ظِلَّ إِلاَّ ظِلُّهُ ... وَرَجُلٌ تَصَدَّقَ بِصَدَقَةٍ فَأَخْفَاهَا حَتَّى لاَ تَعْلَمَ شِمَالُهُ مَا تُنْفِقُ يَمِينُهُ، وَرَجُلٌ ذَكَرَ اللَّهَ خَالِيًا فَفَاضَتْ عَيْنَاهُ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu saba Allaah Atawafunika katika kivuli Chake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila kivuli Chake: ... Na mtu aliyetoa swadaqa yake akaificha hadi kwamba mkono wake wa kushoto usijue nini ulichotoa mkono wake wa kulia. Na mtu aliyemdhukuru Allaah kwa siri macho yake yakatokwa machozi.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

10-Mtake Ushauri Al-Khabiyr Kwa Swalaah Ya Istikhaarah:

Kwa kuwa Al-Khabiyr Anajua undani na hatima ya mambo tusiyoyajua, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwafundisha Swahaba du’aa ya Istikhaarah katika mambo yao yote:

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنهما) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يُعَلِّمُنَا الاِسْتِخَارَةَ فِي الأُمُورِ كُلِّهَا كَمَا يُعَلِّمُنَا السُّورَةَ مِنَ الْقُرْآنِ، يَقُولُ: ((إِذَا هَمَّ أَحَدُكُمْ بِالأَمْرِ فَلْيَرْكَعْ رَكْعَتَيْنِ مِنْ غَيْرِ الْفَرِيضَةِ، ثُمَّ لْيَقُلِ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْتَخِيرُكَ بِعِلْمِكَ، وَأَسْتَقْدِرُكَ بِقُدْرَتِكَ، وَأَسْأَلُكَ مِنْ فَضْلِكَ الْعَظِيمِ، فَإِنَّكَ تَقْدِرُ وَلاَ أَقْدِرُ، وَتَعْلَمُ وَلاَ أَعْلَمُ، وَأَنْتَ عَلاَّمُ الْغُيُوبِ...))

Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akitufundisha Istikhaarah katika mambo yote kama anavyotufundisha Suwrah ya Qur-aan, akisema: “Mmoja wenu anapokusudia jambo, aswali Rakaa mbili zisizo za faradhi, kisha aseme:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْتَخِيرُكَ بِعِلْمِكَ، وَأَسْتَقْدِرُكَ بِقُدْرَتِكَ، وَأَسْأَلُكَ مِنْ فَضْلِكَ الْعَظِيمِ، فَإِنَّكَ تَقْدِرُ وَلاَ أَقْدِرُ، وَتَعْلَمُ وَلاَ أَعْلَمُ، وَأَنْتَ عَلاَّمُ الْغُيُوبِ

Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba uniongoze kwenye kheri kwa Ujuzi Wako, na nakuomba uwezo kwa Uwezo Wako, na nakuomba katika Fadhila Zako adhimu; kwani Wewe Unaweza nami siwezi, na Wewe Unajua nami sijui, na Wewe Ndiye Mjuzi wa ghaibu…” [Al-Bukhaariy]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Sha-an Ad-Du‘aa (63).
  • 2Tafsiyr Ibn Jariyr (11/288), na As-Swawaa‘iq Al-Mursalah (2/492).
  • 3Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam (25).