Al-Haliym: Mvumilivu, Mpole Asiyeharakisha Kuadhibu
Al-Haliym Ni Mpole mwenye kuwavumilia Waja Wake, Mwingi wa huruma, Ambaye Haharakishi kuwaadhibu Waja Wake pamoja na kuwa na uwezo wa kuwaadhibu, na Huwasamehe wanapomuomba msamaha. Yeye Ni Mwenye kusamehe na kustahamili; ghadhabu haimchochei, wala ujinga wa mjinga wala maasi ya muasi hayamtikisi. Ni Mvumilivu kwa anayemuasi; Hazuii Neema Zake wala Fadhila Zake kwa Waja Wake kwa sababu ya madhambi yao, akitaraji watubie. Na Upole Wake uko pamoja na Ilimu Yake, ukamilifu wa Uwezo Wake na kuzunguka Kwake kila kitu. Na Imaam Al-Ghazaaliy (رحمه الله) amesema: Al-Haliym Ni Yule Anayeona maasi dhidi Yake, lakini ghadhabu haimchochei, wala hasira haimshiki, wala haraka na pupa havimsukumi kuharakisha kulipiza kisasi, ingawa Yeye Ana uwezo kamili wa kufanya hivyo.
Jina Hili la Allaah, Al-Haliym, limetajwa katika Qur-aan mara kumi na moja; mara likiwa pamoja na maghfirah (Ghafuwr Haliym), mara pamoja na ukwasi (Ghaniyy Haliym), mara pamoja na shukurani (Shakuwr Haliym), na mara pamoja na ilimu (‘Aliym Haliym). Miongoni mwa Aayah hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا ۚ وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤١﴾
Hakika Allaah Anazuia mbingu na ardhi zisitoweke. Na zikitoweka, hakuna yeyote wa kuzishikilia baada Yake. Hakika Yeye daima Ni Mvumilivu, Mwingi wa Kughufuria. [Faatwir (35:41)]
Na mzizi wa neno haliym ni ح ل م, nao una maana tatu: kuwa mvumilivu, mpole na mwenye kusamehe; kuwa mtulivu; na kutokuwa na haraka na kuwa wastani. Na al-hilm ni subira inayotokana na utulivu wa kina na upole, ama as-swabr ni subira inayotokana na kujizuia na kustahamili jambo bila ya kulalamika. Na subira imo ndani ya hilm; na kutokuwa na haraka (al-anaah) hupelekea hilm, na hilm hupelekea hikmah.
Na Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Haliym, Aliyekamilika katika kila upande wa sifa hii:
1-Yeye (تبارك وتعالى) Ndiye Mwenye upole na uvumilivu uliokamilika, Ambaye wema Wake na Upole Wake umeenea kwa makafiri, mafasiki na waasi, na Huzuia Adhabu Yake isiwafikie madhalimu haraka; Huwasubirisha na kuwapa muda zaidi ili wapate kutubia, na Huwakumbusha ili warejee. Lakini Hawaachi daima wakiendelea kushikilia tabia zao hizo na kuendelea katika uovu wao.1
2-Yeye Ni Mvumilivu Ambaye Upole Wake hautikiswi na ghadhabu, wala uasi wa mwenye kuasi,2 pamoja na ukamilifu wa Uwezo Wake na kulipiza Kwake kisasi.
3-Na miongoni mwa Upole Wake ulioenea kwa Waja Wake ni kwamba mja hupetuka mipaka, lakini Allaah Humhurumia kwa Upole Wake; na mja akitubia na akajikurubisha Kwake, huwa kama kwamba hajawahi kufanya kosa lolote.3
4-Na miongoni mwa Upole Wake (تعالى) ni kwamba Huwapa Neema Zake za siri na za dhahiri wenye kuasi, kama Anavyowapa wenye kutii.
5-Na Yeye Ndiye Anayewaakhirishia Waja Wake wenye kumtii ili wazidishe utiifu na thawabu, na Huwaakhirishia wenye kuasi, huenda wakarejea kwenye haki na usawa. Na lau Angewaharakishia Waja Wake malipo, asingebakia yeyote bila adhabu.
6-Na miongoni mwa uvumilivu Wake ni kwamba Hawaharakishii adhabu na kulipiza kisasi wenye kuasi na madhalimu, na pamoja na hayo Hawazuilii kwa sababu ya madhambi yao kheri, fadhila na neema.
7-Na lau si Upole Wake kwa mwenye kufanya jinai na msamaha Wake kwa mwenye kuasi, mbingu na ardhi zisingetulia mahali pake, kama ilivyotajwa katika Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea juu: Faatwir (35:41).
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Haliym:
1-Al-Haliym Anawaakhirisha Waasi Ili Watubie:
Tambua, ee Mja wa Al-Haliym: Upole wa Allaah ndio unaowabakisha waasi juu ya ardhi, Hawaadhibu mara moja. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۖ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِعِبَادِهِ بَصِيرًا ﴿٤٥﴾
Na lau Allaah Angeliwaadhibu watu kwa sababu ya waliyoyachuma, Asingeliacha juu ya ardhi kiumbe chochote kitembeacho, lakini Anawaakhirisha mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Na utakapofika muda wao, basi hakika Allaah daima Ni Mwenye Kuona Waja Wake. [Faatwir (35:45)]
2-Al-Haliym Hakuchukulii Kwa Viapo Visivyokusudiwa:
Tambua, ee Mja wa Al-Haliym: Katika Upole Wake ni kutomchukulia mja kwa yale asiyoyakusudia moyoni mwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَّا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا كَسَبَتْ قُلُوبُكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ حَلِيمٌ ﴿٢٢٥﴾
Allaah Hatokushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi lakini Atakuchukulieni kwa yaliyochuma nyoyo zenu. Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufiria, Mvumilivu. [Al-Baqarah (2:225)]
3-Usighurike Na Upole Wa Al-Haliym:
Upole wa Allaah unaonekana ardhini; unawaona makafiri na watu wa maasi wakiwa na afya, wakistarehe katika Neema za Allaah. Basi Ametakasika Yule Anayepa muhula lakini Hapuuzi! Na watu wanaweza kughurika na muhula huo, nyoyo zao zisihisi Rehma ya Allaah, mpaka Awachukue kwa Uadilifu Wake na Nguvu Zake utakapofika muda wao waliowekewa. Na ghururi ya baadhi yao huzidi mpaka hufanya kiburi juu ya Upole Wake na muhula Wake kwa kuomba waharakishiwe adhabu. Kwa hiyo tambua kwamba Al-Haliym Amekuwekea sharia, na usiutumie kamwe vibaya Upole Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۖ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِعِبَادِهِ بَصِيرًا ﴿٤٥﴾
Na lau Allaah Angeliwaadhibu watu kwa sababu ya waliyoyachuma, Asingeliacha juu ya ardhi kiumbe chochote kitembeacho, lakini Anawaakhirisha mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Na utakapofika muda wao, basi hakika Allaah daima Ni Mwenye Kuona Waja Wake. [Faatwir (35:45)]
4-Mshukuru Al-Haliym Na Urudi Kwake Baada Ya Kutenda Dhambi:
Kama ambavyo ungemshukuru yeyote anayepuuza makosa yako na kasoro zako, tambua upole mkubwa wa Al-Haliym kwako, na urudi Kwake baada ya kutenda dhambi. Fikiria umekamatwa ukifanya jambo baya, lakini mtu yule akakuachia bila ya kukuadhibu wala kukuaibisha; je, usingeona haya, faraja na shukurani, ukamwambia hutorudia tena? Basi itakuwaje kwa Allaah? Kila siku tunafanya yasiyotupasa, na mara nyingi Anatuachia, kwa sababu Yeye Ni Al-Haliym, na Upole Wake uko juu mno ya upole wowote anaoweza kuuonyesha mwana-Aadam. Na nani aliyeweka huruma kubwa na upole katika moyo wa mama anayempenda mwanawe? Ni Allaah Al-Haliym:
عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) قَالَ: قُدِمَ عَلَى النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) سَبْيٌ، فَإِذَا امْرَأَةٌ مِنَ السَّبْيِ قَدْ تَحْلُبُ ثَدْيَهَا تَسْقِي، إِذَا وَجَدَتْ صَبِيًّا فِي السَّبْيِ أَخَذَتْهُ فَأَلْصَقَتْهُ بِبَطْنِهَا وَأَرْضَعَتْهُ، فَقَالَ لَنَا النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَتُرَوْنَ هَذِهِ طَارِحَةً وَلَدَهَا فِي النَّارِ؟)) قُلْنَا: لاَ، وَهِيَ تَقْدِرُ عَلَى أَنْ لاَ تَطْرَحَهُ. فَقَالَ: ((لَلَّهُ أَرْحَمُ بِعِبَادِهِ مِنْ هَذِهِ بِوَلَدِهَا))
Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه): Waliletwa kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) mateka, na mara mwanamke mmoja miongoni mwa mateka matiti yake yalikuwa yakitoa maziwa. Alipomkuta mtoto miongoni mwa mateka, alimchukua akamkumbatia tumboni mwake na akamnyonyesha. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akatuambia: “Je, mnaona mwanamke huyu atamtupa mwanawe motoni?” Tukasema: Hapana, na hali yeye anaweza kutomtupa. Akasema: “Allaah Ni Mwenye kuwarehemu zaidi Waja Wake kuliko mwanamke huyu kwa mwanawe.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
5-Kuwa Mvumilivu Kwa Wengine:
Tambua, ee Mja wa Al-Haliym: Allaah Amewagawia Waja Wake fungu la sifa hii, kama Alivyomsifu Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) kuwa ni mwingi wa kunyenyekea, mvumilivu, Anaposema (سبحانه وتعالى):
وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ ﴿١١٤﴾
Na haikuwa Ibraahiym kumuombea maghfirah baba yake isipokuwa kwa sababu ya ahadi aliyoahidiana naye. Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui wa Allaah, alijiepusha naye. Hakika Ibraahiym ni mwenye huruma mno na mvumilivu. [At-Tawbah (9:114)]
Basi jitahidi kuchukua kiasi unachoweza katika sifa hii, kwani inavunja makali ya ghadhabu yako na huondoa hamu ya kulipiza kisasi kwa aliyekukosea. Kila mmoja, vyovyote ilivyo hasira yake, anaweza kujizoesha uvumilivu. Je, ni hilm unapopuuza jambo mara moja au mbili, kisha ukalipuka mara ya tatu kwa sababu ya chuki uliyoibeba ndani? Mahusiano mengi huvunjika kwa sababu ya dakika za hasira. Hilm ni pale unapokuwa na uwezo wa kuonyesha hasira yako lakini ukaizuia. Na hata ukihisi hasira, jilazimishe kuwa mvumilivu kwa ajili ya Al-Haliym, na jiambie: Ninazuia hasira yangu kwa sababu nampenda Allaah na ninataka Anipende, na nataka kumtii Rasuli Wake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Ashajj wa ‘Abdul-Qays:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) لِلأَشَجِّ أَشَجِّ عَبْدِ الْقَيْسِ: ((إِنَّ فِيكَ خَصْلَتَيْنِ يُحِبُّهُمَا اللَّهُ: الْحِلْمُ وَالأَنَاةُ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Ashajj wa ‘Abdul-Qays: “Hakika ndani yako kuna sifa mbili anazozipenda Allaah: uvumilivu na kutokuwa na haraka.” [Muslim]
6-Upole Na Kutoharakisha Ni Tabia Anazozipenda Allaah:
Tambua kwamba upole na kutoharakisha ni tabia zinazopendwa na Al-Haliym; basi jipambe nazo.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimsifu Ashajj ‘Abdul-Qays kwa sifa mbili:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) لِلأَشَجِّ أَشَجِّ عَبْدِ الْقَيْسِ: ((إِنَّ فِيكَ خَصْلَتَيْنِ يُحِبُّهُمَا اللَّهُ: الْحِلْمُ وَالأَنَاةُ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Al-Ashajj, Ashajj ‘Abdul-Qays: “Hakika una sifa mbili anazozipenda Allaah: upole na kutoharakisha mambo.” [Muslim]
7-Jiepushe Na Hasira:
Tambua, ee Mja wa Al-Haliym: Mtu mmoja alimwomba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) wasiya:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَجُلاً قَالَ لِلنَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم): أَوْصِنِي. قَالَ: ((لاَ تَغْضَبْ)). فَرَدَّدَ مِرَارًا، قَالَ: ((لاَ تَغْضَبْ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba mtu mmoja alimwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Niusie. Akasema: “Usikasirike.” Akarudia mara kadhaa, (na kila mara) akisema: “Usikasirike.” [Al-Bukhaariy]
8-Vuta Subira Na Usamehe:
Allaah Ameijaalia sifa ya hilm kuwa miongoni mwa tabia Anazozipenda kwa mja, na Ameipandisha hadi daraja ya mambo ya kuazimiwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿٤٣﴾
Na atakayevuta subira na akasamehe, hakika hilo bila shaka ni katika mambo ya kuazimiwa. [Ash-Shuwraa (42:43)]
9-Mwonyeshe Mtenda Dhambi Mfano Mwema Bila Ya Kiburi:
Usimfanyie kiburi kamwe mtu anayetenda dhambi, bali jaribu kumnasihi kwa upole na kwa kumwonyesha mfano mwema. Jiambie: Huenda siku moja mtenda dhambi huyu akarejea kwa Al-Haliym kwa tawbah ya kweli, akawa bora na kipenzi zaidi kwa Allaah kuliko mimi. Na umkanye mtu kwa ajili ya Allaah tu, ili atambue matokeo ya matendo yake na arejee kwa Allaah. Tazama upole wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَامَ أَعْرَابِيٌّ فَبَالَ فِي الْمَسْجِدِ، فَتَنَاوَلَهُ النَّاسُ، فَقَالَ لَهُمُ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((دَعُوهُ، وَهَرِيقُوا عَلَى بَوْلِهِ سَجْلاً مِنْ مَاءٍ، أَوْ ذَنُوبًا مِنْ مَاءٍ، فَإِنَّمَا بُعِثْتُمْ مُيَسِّرِينَ، وَلَمْ تُبْعَثُوا مُعَسِّرِينَ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Bedui mmoja alisimama akakojoa msikitini, watu wakamshambulia (kwa maneno). Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akawaambia: “Mwacheni, na mwagieni juu ya mkojo wake ndoo ya maji, kwani hakika mmetumwa kuwa wenye kuwepesisha, na hamkutumwa kuwa wenye kutia uzito.” [Al-Bukhaariy]
10-Muombe Al-Haliym Katika Dhiki:
Muombe Al-Haliym Akuvumilie wewe na wapendwa wako, na umuombe maghfirah, kwani Yeye Pekee Ndiye Anayeweza kukukinga na Ghadhabu Yake. Na miongoni mwa Du’aa za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati wa dhiki ni kumtaja Allaah kwa Jina Lake Al-Haliym; na kuunganishwa kwa Majina Al-‘Adhwiym na Al-Haliym kunaonyesha kwamba Utukufu Wake haukumzuia kuwa Mvumilivu kwa viumbe Wake, wala Upole Wake haukutokana na udhaifu, bali ni kutokana na ukamilifu wa Utukufu na Ujalali:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ عِنْدَ الْكَرْبِ: ((لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ الْعَظِيمُ الْحَلِيمُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ رَبُّ السَّمَوَاتِ وَرَبُّ الأَرْضِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema wakati wa dhiki:
لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ الْعَظِيمُ الْحَلِيمُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ رَبُّ السَّمَوَاتِ وَرَبُّ الأَرْضِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ
Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, Mwenye Taadhima, Mvumilivu. Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, Rabb wa ‘Arsh Adhimu. Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, Rabb wa mbingu, na Rabb wa ardhi, na Rabb wa ‘Arsh Tukufu. [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Na Allaah Mjuzi zaidi