Al-‘Adhwiym: Adhimu, Mwenye Taadhima, Mtukufu
Al-‘Adhwiym Ni Mwenye kusifika kwa utukufu; Mwenye Taadhima, Mkubwa na Mkuu kabisa Aliyetukuka, Mwenye Ujalali na Ukarama. Ni Mwenye ‘adhwamah (utukufu), na maana yake ni kwamba cheo Chake ni kikubwa na hadhi Yake ni tukufu kiasi cha kupita mipaka ya akili, hata haiwezekani kufikiria kuujua undani Wake na uhakika Wake. Nguvu Zake na Ukuu Wake viko ndani ya Dhati Yake; matendo Yake yote ni kamilifu, na Yeye Pekee Ndiye Anayestahiki kutukuzwa na viumbe. Kila kitu kisichokuwa Yeye ni kidogo na duni!
Jina Hili la Allaah, Al-‘Adhwiym, limetajwa katika Qur-aan mara kumi na moja. Miongoni mwa Aayah hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴿٤﴾
Ni Vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, Naye Ni Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mwenye Taadhima. [Ash-Shuwraa (42:4)]
Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):
فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ ﴿٥٢﴾
Basi sabbih kwa Jina la Rabb wako Adhimu. [Al-Haaqqah (69:52)]
Na kilugha ‘adhwamah (utukufu) ni kinyume cha udogo na udhalili, na kitu adhimu ni kitu kikubwa chenye nguvu. Na mzizi wake ع ظ م una maana ya kuwa mkubwa, mpana na mwenye cheo kikubwa; kuwa mwenye nguvu, mwenye hadhi na mwenye kuheshimika; na kuwa juu ya kila upungufu. Na neno ‘adhm lina maana ya mfupa, kwa kuwa ni kitu kigumu kuliko vyote mwilini, na linaashiria nguvu. Na Al-‘Adhwiym huitwa kwa kukusudiwa maana mbili:
Kwanza: Ukubwa wa miili na wingi wa sehemu zake.
Pili: Ujuu, uwezo na hadhi ya juu; na maana hii hutumika kwa vitu vyenye hisia na vyenye akili, na kutokana nayo huitwa watu watukufu; wenye utukufu na uongozi miongoni mwao, kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):
وَقَالُوا لَوْلَا نُزِّلَ هَـٰذَا الْقُرْآنُ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنَ الْقَرْيَتَيْنِ عَظِيمٍ ﴿٣١﴾
Na wakasema: Kwa nini isiteremshwe hii Qur-aan kwa mtu adhimu kutoka miji miwili? [Az-Zukhruf (43:31)]
Na ‘adhwamah ni Sifa ya Allaah ambayo hakuna kiumbe kinachoweza kuisimamia. Allaah Ameweka utukufu miongoni mwa viumbe ambao kwao hutukuzana; wapo wanaotukuza mali, fadhila, ilimu, mamlaka au cheo; na hao wanatukuzwa kwa maana fulani pasina nyingine, ama Allaah (عزّ وجلّ) Hutukuzwa katika hali zote, na Jina hili kwa asiyekuwa Yeye ni kwa kuazima tu.
Na Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-‘Adhwiym kwa maana zifuatazo:
1-Al-‘Adhwiym katika Dhati Yake: Ambaye Hana mfano Wake. Na katika Utukufu Wake ni kwamba mbingu na ardhi ziko katika Kiganja cha Ar-Rahmaan; ni ndogo zaidi (Kwake) kuliko punje ya hardali, kama alivyosema Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) na wengineo. Anasema (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴿٢٥٥﴾
Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Al-Hayyu (Aliye Hai daima) Al-Qayyuwm (Msimamia kila kitu). Haumchukui usingizi wala kulala. Ni Vyake Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya Idhini Yake? Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kufikia kuelewa chochote kuhusu Ujuzi Wake isipokuwa kwa Alitakalo. Imeenea Kursiyy Yake mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Naye ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Taadhima. [Al-Baqarah (2:255)]
Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):
وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٦٧﴾
Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Na hali ardhi yote Ataikamata Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah, na mbingu zitakunjwa kwa Mkono Wake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha. [Az-Zumar (39:67)]
Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا ۚ وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤١﴾
Hakika Allaah Anazuia mbingu na ardhi zisitoweke. Na zikitoweka, hakuna yeyote wa kuzishikilia baada Yake. Hakika Yeye daima Ni Mvumilivu, Mwingi wa Kughufuria. [Faatwir (35:41)]
Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَا السَّمَوَاتُ السَّبْعُ فِي الْكُرْسِيِّ إِلاَّ كَحَلْقَةٍ مُلْقَاةٍ بِأَرْضِ فَلاَةٍ، وَفَضْلُ الْعَرْشِ عَلَى الْكُرْسِيِّ كَفَضْلِ تِلْكَ الْفَلاَةِ عَلَى تِلْكَ الْحَلْقَةِ))
Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mbingu saba kwa kulinganisha na Al-Kursiy si chochote isipokuwa ni kama pete iliyotupwa katika ardhi ya jangwa; na ukubwa wa ‘Arsh kwa kulinganisha na Al-Kursiy ni kama ukubwa wa jangwa hilo kwa kulinganisha na pete hiyo.” [Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (109)]
Ikiwa huu ndio utukufu wa Kursiy na ‘Arsh, navyo ni katika viumbe Vyake, basi itakuwaje Utukufu wa Rabb Mtukufu, Mwenye Sifa za juu kabisa, Aliyestawi juu ya ‘Arsh Yake, na Aliye juu ya viumbe vyote?1 Na ndio maana Allaah Akahitimisha Aayatul-Kursiy kwa Kauli Yake: “Naye Ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Taadhima.”
2-Al-‘Adhwiym katika Sifa Zake na Uwezo Wake: kwani Yeye Anasifika kwa kila sifa ya ukamilifu; Yeye Ni Adhimu katika kila kitu; katika Rehma Yake, katika Uwezo Wake, katika Wasaa Wake na utoaji Wake, katika Uzuri Wake, Ukaribu Wake na kuwa Kwake juu; hakuna aliye sawa Naye wala anayemkaribia.2 Na Allaah (تعالى) Amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:3
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ: الْكِبْرِيَاءُ رِدَائِي، وَالْعَظَمَةُ إِزَارِي، فَمَنْ نَازَعَنِي وَاحِدًا مِنْهُمَا قَذَفْتُهُ فِي النَّارِ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (عزّ وجلّ) Amesema: Kiburi ni joho Langu, na Utukufu ni shuka Langu; basi atakayeshindana Nami katika kimoja kati ya hivyo, Nitamtupa motoni.” [Abuu Daawuwd (4090), Ibn Maajah (4174), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
3-Al-‘Adhwiym katika Matendo Yake: kwani yanaonyesha upana wa Hikmah Yake, Uadilifu Wake, Fadhila Zake, Matakwa Yake, kutekeleza Kwake Alitakalo, na kwamba Yeye Pekee Ndiye Mwenye kusaidia na kunusuru.
4-Na katika maana ya Ukubwa Wake na Utukufu Wake ni kwamba haistahiki kwa kiumbe chochote kujitukuza na kujipa ukubwa kama Anavyotukuzwa Yeye (تعالى); Yeye Pekee Ndiye Mwenye haki ya kutukuzwa kwa nyoyo za watu, ndimi zao na viwiliwili vyao; na hilo ni kwa kujitahidi kumjua, kumpenda na kujidhalilisha Kwake.
5-Yeye (تعالى) Ndiye Anayekuza rizqi za watu, ujira na thawabu kwa Amtakaye miongoni mwa Waja Wake. Anasema (سبحانه وتعالى):
ذَٰلِكَ أَمْرُ اللَّـهِ أَنزَلَهُ إِلَيْكُمْ ۚ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يُكَفِّرْ عَنْهُ سَيِّئَاتِهِ وَيُعْظِمْ لَهُ أَجْرًا ﴿٥﴾
Hiyo ni Amri ya Allaah Amekuteremshieni. Na yeyote anayemcha Allaah, basi Atamfutia maovu yake na Atamuadhimishia ujira. [Atw-Twalaaq (65:5)]
Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ أَحَبَّ أَنْ يُبْسَطَ لَهُ فِي رِزْقِهِ، وَيُنْسَأَ لَهُ فِي أَثَرِهِ، فَلْيَصِلْ رَحِمَهُ))
Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Anayependa akunjuliwe rizqi yake, na arefushiwe maisha yake, basi aunge kizazi chake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-‘Adhwiym:
1-Al-‘Adhwiym Ni Mwenye Utukufu Katika Dhati Yake, Majina Yake Na Sifa Zake:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Adhwiym: Kila kilichomo mbinguni na ardhini ni milki Yake, Naye Ndiye Aliye juu, Mtukufu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ﴿٤﴾
Ni Vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, Naye Ni Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mwenye Taadhima. [Ash-Shuwraa (42:4)]
2-Tafakari Ukubwa Wa Al-‘Adhwiym Siku Ya Qiyaamah:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Adhwiym: Ardhi yote itakuwa katika Mkono Wake Siku ya Qiyaamah, na mbingu zitakunjwa kwa Mkono Wake wa kulia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٦٧﴾
Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Na hali ardhi yote Ataikamata Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah, na mbingu zitakunjwa kwa Mkono Wake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha. [Az-Zumar (39:67)]
3-Tafakari Ukubwa Wa Kursiy Na ‘Arsh Ili Utambue Utukufu Wa Muumba Wake:
Tafakari, ee Mja wa Al-‘Adhwiym, ukubwa wa Al-Kursiy na ‘Arsh, ili utambue utukufu wa Muumba wake.
Rejea juu Hadiyth ya Abuu Dharr (رضي الله عنه) kuhusu ukubwa wa Al-Kursiy na Al-‘Arsh.
4-Mtukuze Al-‘Adhwiym Ipasavyo Na Usimshirikishe:
Tambua kwamba anayemtukuza Al-‘Adhwiym, anaposhuhudia maana za Ujalali na Utukufu, huingia moyoni mwake kumuadhimisha na kumhofu Allaah. Basi inampasa mja amtukuze Allaah ipasavyo kwa kadiri ya uwezo wake; na Utukufu Wake unawajibisha kunyenyekea mbele ya Utukufu Wake. Na kumtukuza Allaah ni kutukuza Majina Yake na Sifa Zake bila ya kuzifananisha na viumbe Wake; na kutomtaja wakati wa upuuzi na mambo ya baatwil, bali kumtaja kwa kutukuza cheo Chake, kuheshimu hadhi Yake na kumuadhimisha. Na kumtukuza Yeye (تعالى) ni kutukuza Vitabu Vyake, Rusuli Wake, Malaika Wake, ibaada Zake na nembo za Dini Yake, na kutukuza vitu Alivyoviharamisha na heshima za Waumini, kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّـهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ عِندَ رَبِّهِ ۗ وَأُحِلَّتْ لَكُمُ الْأَنْعَامُ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ ۖ فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ وَاجْتَنِبُوا قَوْلَ الزُّورِ ﴿٣٠﴾
Ndio hivyo iwe. Na yeyote anayeadhimisha Vitukufu vya Allaah basi hivyo ni kheri kwake mbele ya Rabb wake. Na mmehalalishiwa wanyama wa mifugo isipokuwa wale mnaosomewa. Basi jiepusheni na uchafu wa (kuabudu) masanamu, na jiepusheni na kauli za uongo. [Al-Hajj (22:30)]
Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾
Hayo ndio hivyo. Na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo. [Al-Hajj (22:32)]
Na miongoni mwa makubwa kabisa Aliyoyaharamisha ni kumshirikisha na asiyemiliki manufaa wala madhara; masanamu, mawe na makaburi ambayo wenyewe wamekuwa mifupa iliyooza, basi vipi watakidhi haja, au kuponya mgonjwa, au kumrudisha aliyepotea? Na wale ambao imaan yao ilipungua kufikia Utukufu wa Allaah, Amewaahidi adhabu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
خُذُوهُ فَغُلُّوهُ ﴿٣٠﴾ ثُمَّ الْجَحِيمَ صَلُّوهُ ﴿٣١﴾ ثُمَّ فِي سِلْسِلَةٍ ذَرْعُهَا سَبْعُونَ ذِرَاعًا فَاسْلُكُوهُ ﴿٣٢﴾ إِنَّهُ كَانَ لَا يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ الْعَظِيمِ ﴿٣٣﴾
(Patasemwa): Mchukueni, na mfungeni pingu. Kisha kwenye moto uwakao vikali mno muingizeni aungue. Kisha mtieni pingu katika minyororo yenye urefu wa dhiraa sabini. Hakika yeye alikuwa hamuamini Allaah Mwenye Taadhima. [Al-Haaqqah (69:30-33)]
5-Usimwogope Yeyote Isipokuwa Al-‘Adhwiym Na Umtake Msaada Katika Kila Hali:
Yeye Ndiye Mmiliki wa nguvu zote; kila shida, mtihani au tatizo unalokabiliana nalo ni dogo mno ukilinganisha na Alichokiumba. Al-‘Adhwiym Ameumba mbingu nzuri na milima mikubwa madhubuti; je, hudhani kwamba Ataweza kutatua matatizo yako yote? Basi muombe Al-‘Adhwiym Akusaidie katika kila hali, na umuite kila unapohisi unahitaji nguvu ya kuendelea katika maisha. Na hata mtu mwenye nguvu kabisa duniani si kitu kabisa mbele ya Utukufu na Nguvu za Al-‘Adhwiym, basi usimwogope yeyote wala chochote isipokuwa Yeye. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: كُنْتُ خَلْفَ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَوْمًا فَقَالَ: ((... إِذَا سَأَلْتَ فَاسْأَلِ اللَّهَ، وَإِذَا اسْتَعَنْتَ فَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ، وَاعْلَمْ أَنَّ الأُمَّةَ لَوِ اجْتَمَعَتْ عَلَى أَنْ يَنْفَعُوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ لَكَ، وَلَوِ اجْتَمَعُوا عَلَى أَنْ يَضُرُّوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَضُرُّوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ عَلَيْكَ ...))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nilikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) siku moja akasema: “... Ukiomba, muombe Allaah; na ukitaka msaada, mtake msaada Allaah. Na jua kwamba lau ummah wote utajumuika ili kukunufaisha kwa kitu, hawatokunufaisha isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah Amekwisha kukuandikia. Na lau watajumuika ili kukudhuru kwa kitu, hawatokudhuru isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah Amekwisha kukuandikia ...” [At-Tirmidhiy (2516), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
6-Adhimisha Alama Za Dini Ya Al-‘Adhwiym:
Tambua kwamba kuziadhimisha Amri za Al-‘Adhwiym, Swalaah, Msikiti, Qur-aan na alama za Dini Yake ni dalili ya taqwa iliyomo moyoni. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾
Hayo ndio hivyo. Na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo. [Al-Hajj (22:32)]
7-Mtukuze Al-‘Adhwiym Katika Rukuu’ Yako:
Kwa Hikmah Yake kamilifu, Allaah Amechagua Jina Hili miongoni mwa Majina Yake yote lirudiwe angalau mara tatu katika kila Swalaah; tunalisema tukiwa tumeinama katika rukuu’, tukinyenyekea Ukuu Wake na Nguvu Zake, kwa kusema: “سُبْحَانَ رَبِّيَ الْعَظِيمِ.” Basi unaporukuu, elekeza mwili wako wote na akili yako yote kwa jinsi ulivyo duni mbele ya Al-‘Adhwiym; kwani kuinama ni kukiri na kushuhudia Ukuu na Nguvu za Allaah (عزّ وجلّ)! Na zidisha adhkaar katika rukuu’, kama dhikr ya Sunnah: “سُبْحَانَ ذِي الْجَبَرُوتِ، وَالْمَلَكُوتِ، وَالْكِبْرِيَاءِ، وَالْعَظَمَةِ” (Ametakasika Mwenye Ujabari, Ufalme, Ukubwa na Utukufu) [Abu Daawuud] [An-Nasaaiy]. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... فَأَمَّا الرُّكُوعُ فَعَظِّمُوا فِيهِ الرَّبَّ عَزَّ وَجَلَّ، وَأَمَّا السُّجُودُ فَاجْتَهِدُوا فِي الدُّعَاءِ، فَقَمِنٌ أَنْ يُسْتَجَابَ لَكُمْ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “... Ama rukuu’, mtukuzeni humo Rabb (عزّ وجلّ); na ama sujuwd, jitahidini humo katika Du’aa, kwani inastahiki kujibiwa kwenu.” [Muslim]
8-Jizoeshe Kusoma Aayatul-Kursiy:
Allaah (عزّ وجلّ) Amehitimisha Aayatul-Kursiy kwa Jina Lake Al-‘Adhwiym, nayo ndio Aayah adhimu kabisa ya Qur-aan. Jizoeshe kuisoma baada ya kila Swalaah ya faradhi na kabla ya kulala:
عَنْ أُبَيِّ بْنِ كَعْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((يَا أَبَا الْمُنْذِرِ، أَتَدْرِي أَيُّ آيَةٍ مِنْ كِتَابِ اللَّهِ مَعَكَ أَعْظَمُ؟)) قَالَ: قُلْتُ: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ. قَالَ: ((يَا أَبَا الْمُنْذِرِ، أَتَدْرِي أَيُّ آيَةٍ مِنْ كِتَابِ اللَّهِ مَعَكَ أَعْظَمُ؟)) قَالَ: قُلْتُ: اللَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ. قَالَ: فَضَرَبَ فِي صَدْرِي وَقَالَ: ((وَاللَّهِ لِيَهْنِكَ الْعِلْمُ أَبَا الْمُنْذِرِ))
Amesimulia Ubayy bin Ka‘b (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniuliza: “Yaa Abal-Mundhir! Je, unajua ni Aayah ipi katika Kitabu cha Allaah uliyonayo ambayo ni adhimu kabisa?” Nikasema: Allaah na Rasuli Wake ndio wajuao zaidi. Akauliza tena: “Yaa Abal-Mundhir! Je, unajua ni Aayah ipi katika Kitabu cha Allaah uliyonayo ambayo ni adhimu kabisa?” Nikasema: ﴿اللَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ﴾. Akanipiga kifuani akasema: “Wa-Allaahi, hongera kwa ilimu yaa Abal-Mundhir!” [Muslim]
9-Jaza Mizani Yako Kwa Kumdhukuru Al-‘Adhwiym:
Jizoeshe kumdhukuru Al-‘Adhwiym kila unapopata nafasi; unapofanya kazi, unapopika, unaposubiri au unaposafiri. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((كَلِمَتَانِ خَفِيفَتَانِ عَلَى اللِّسَانِ، ثَقِيلَتَانِ فِي الْمِيزَانِ، حَبِيبَتَانِ إِلَى الرَّحْمَنِ: سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ، سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Maneno mawili mepesi katika ulimi, mazito katika mizani, yanapendwa na Ar-Rahmaan:
سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ، سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ
Ametakasika Allaah na Himdi ni Zake, Ametakasika Allaah Mwenye Taadhima.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
10-Mwombe Al-‘Adhwiym Wakati Wa Dhiki:
Omba du’aa hii unapofikwa na dhiki, ukimtaja Al-‘Adhwiym kwa Utukufu Wake na Upole Wake.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiomba wakati wa dhiki:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ عِنْدَ الْكَرْبِ: ((لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ الْعَظِيمُ الْحَلِيمُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ رَبُّ السَّمَوَاتِ وَرَبُّ الأَرْضِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema wakati wa dhiki:
لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ الْعَظِيمُ الْحَلِيمُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ رَبُّ السَّمَوَاتِ وَرَبُّ الأَرْضِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ
Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, Mtukufu, Mvumilivu. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, Rabb wa ‘Arsh adhimu. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, Rabb wa mbingu, na Rabb wa ardhi, na Rabb wa ‘Arsh tukufu. [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Na Allaah Mjuzi zaidi