Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah059 - Al-Hamiyd

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 059 kati ya 103
Al-Hamiyd — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Hamiyd: Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa Kwa Yote

Al-Hamiyd Ni Msifiwa, Mwenye Kushukuriwa kwa yote daima; Mwenye kuhimidiwa na kustahiki Himdi kwa Matendo Yake kwa viumbe Wake, kwa Neema na Fadhila Alizowapa. Ni Zake Himdi zote kwa ukamilifu wake; basi Yeye Ni Al-Hamiyd katika Dhati Yake, Sifa Zake na Matendo Yake. Naye Ndiye Anayestahiki Himdi daima, sawa Akihimidiwa au Asihimidiwe. Na al-hamd ni pana zaidi kuliko ash-shukr (shukurani); kwa sababu unamhimidi mtu kwa sifa zake za dhati na kwa kutoa kwake, lakini humshukuru kwa sifa zake. Na Himdi ni za aina mbili: Himdi kwa ihsaan Yake (تعالى), na Himdi kwa Majina Yake Mazuri na Sifa Zake za juu; basi Yeye Ana Himdi kamilifu.

Jina Hili la Allaah, Al-Hamiyd, limetajwa katika Qur-aan mara kumi, na mara nyingi huja pamoja na Jina Lake Al-Ghaniyy. Miongoni mwa Aayah hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿٢٦﴾

Ni vya Allaah Pekee vyote vile vilivyomo katika mbingu na ardhi. Hakika Allaah Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Luqmaan (31:26)]

Na mzizi wake ح م د una maana tatu: kumsifu kwa mapenzi ya kina na kunyenyekea; kumheshimu na kumtaja kwa wema; na kumsifu mtu kwa anayoyafanya kwa hiari yake. Na al-hamd imejengeka juu ya mapenzi na kutukuza; inajumuisha kustaajabia na kumshukuru anayehimidiwa. Na herufi “al” katika “al-hamd” inaifanya sifa kuwa kamili na ya Kwake Pekee; yaani kila aina ya sifa na kila namna ya shukurani wakati wote ni Haki ya Allaah (عزّ وجلّ) Pekee.

Na Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Hamiyd Mwenye Himdi zote duniani na Aakhirah:

1-Mwenye Himdi zote na kusifiwa kote: Anastahiki kusifiwa katika Dhati Yake, Majina Yake, Sifa Zake na Matendo Yake. Ana Majina matukufu na Sifa timilifu, na kila Sifa katika Sifa Zake za juu huhimidiwa kwa ukamilifu wa Himdi. Na Matendo Yake ni timilifu na mazuri kabisa; yanazunguka kati ya fadhila na wema, na kati ya hikmah na uadilifu; hakuna tendo lisilo na hikmah wala manufaa, na hakuna kosa katika Matendo Yake.1

2-Naye Mtukufu Ni Mwenye kuhimidiwa kwa Sharia Zake: Sharia Zake ni kamilifu, zenye manufaa kwa viumbe wote, na ndani yake mna uadilifu, hikmah na huruma zisizo na mfano.

3-Mwenye kuhimidiwa katika Utengenezaji Wake: Huhimidiwa katika kuumba Kwake, kuvipa vitu uwepo, kuviandaa na kuvisaidia.2 Anasema (سبحانه وتعالى):

وَتَرَى الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ ۚ صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ ۚ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ ﴿٨٨﴾

Na unaona milima unaidhania imetulia thabiti nayo inapita mpito wa mawingu. Utengenezaji wa Allaah Ambaye Ametengeneza kwa umahiri kila kitu. Hakika Yeye Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myafanyayo. [An-Naml (27:88)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ ۖ وَبَدَأَ خَلْقَ الْإِنسَانِ مِن طِينٍ ﴿٧﴾

Ambaye Amefanya uzuri kila kitu Alichokiumba, na Akaanzisha uumbaji wa binaadam kutokana na udongo. [As-Sajdah (32:7)]

4-Naye Ni Mwenye kuhimidiwa katika Hukumu Zake na Qadar Yake; katika Hukumu Zake za Qadar na za Sharia, duniani na Aakhirah;3 zote ni haki, uongofu na mema, zimeepushwa na shari, upuuzi, dhulma na kila aina ya upungufu.

5-Naye Ni Mwenye kuhimidiwa kwa Upweke Wake daima, na kutakasika Kwake na kila aina ya ushirika na mfanano. Anasema (سبحانه وتعالى):

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾

Na sema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Ambaye Hakujifanyia mwana na wala Hakuwa na mshirika katika ufalme, na wala Hakuwa dhalili hata Awe (Anahitaji) mlinzi (na msaidizi), na mtukuze matukuzo makubwa kabisa. [Al-Israa (17:111)]

6-Naye Ni Mhimidiwa, Msifiwa, Ambaye Amejisifu Mwenyewe; hata kama Waja Wake hawatomhimidi, Yeye Mwenyewe Hujihimidi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:4

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَلَيْسَ أَحَدٌ أَحَبَّ إِلَيْهِ الْمَدْحُ مِنَ اللَّهِ، مِنْ أَجْلِ ذَلِكَ مَدَحَ نَفْسَهُ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “... Na hakuna yeyote anayependa zaidi kusifiwa kuliko Allaah; kwa ajili hiyo Amejisifu Mwenyewe.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Na Allaah Amejihimidi Mwenyewe kwa: Urabb Wake ulioenea, (Rejea chini: Al-Faatihah (1:2)); kuteremsha Kitabu Chake kisicho na upogo, na ukamilifu wa Sharia Zake, (Rejea chini: Al-Kahf (18:1)); kuumba mbingu na ardhi na kujaalia viza na nuru, (Rejea chini: Al-An‘aam (6:1)); ukamilifu na kumiliki kila kitu (Rejea chini: Saba-a (34:1)); Ukubwa Wake mbinguni na ardhini, (Rejea chini: Al-Jaathiyah (45:36-37)); na Matendo Yake, kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۚ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾

AlhamduliLLahi (Himdi Anastahiki Allaah), Mwanzilishi wa mbingu na ardhi, Mwenye Kuwafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili-mbili, na tatu-tatu na nne-nne. Huzidisha katika uumbaji Atakavyo. Hakika Allaah Ni Muweza juu ya kila kitu. [Faatwir (35:1)]

Na Amejihimidi kwa ukamilifu na kumiliki kila kitu, Anaposema (سبحانه وتعالى):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَلَهُ الْحَمْدُ فِي الْآخِرَةِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿١﴾

AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ni Vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Himdi ni Zake katika Aakhirah, Naye Ni Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Saba-a (34:1)]

Na Amejihimidi kwa Ukubwa Wake mbinguni na ardhini, Anaposema (سبحانه وتعالى):

فَلِلَّـهِ الْحَمْدُ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَرَبِّ الْأَرْضِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٣٦﴾ وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٣٧﴾

Basi AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi, Rabb wa walimwengu. Na Ukubwa, Uadhama, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini. Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jaathiyah (45:36-37)]

Na Amejihimidi kwa Urabb Wake kwa walimwengu wote, Anaposema (سبحانه وتعالى):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾

AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki) Allaah Rabb wa walimwengu. [Al-Faatihah (1:2)]

Na Amejihimidi kwa kuteremsha Kitabu Chake kisicho na upogo, Anaposema (سبحانه وتعالى):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَنزَلَ عَلَىٰ عَبْدِهِ الْكِتَابَ وَلَمْ يَجْعَل لَّهُ عِوَجًا ۜ ﴿١﴾

AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Ambaye Amemteremshia Mja Wake Kitabu na wala Hakukifanya kiwe upogo. [Al-Kahf (18:1)]

Na Amejihimidi kwa kuumba mbingu na ardhi na kujaalia viza na nuru, Anaposema (سبحانه وتعالى):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَجَعَلَ الظُّلُمَاتِ وَالنُّورَ ۖ ثُمَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ يَعْدِلُونَ ﴿١﴾

AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na Akajaalia viza na nuru, kisha wale ambao wamekufuru wanawasawazisha wengine na Rabb wao. [Al-An‘aam (6:1)]

Na neno “الْحَمْدُ لِلَّهِ” limetajwa katika Qur-aan mara thelathini na nane; Allaah Amejihimidi kwalo, na baadhi ya Suwrah zinaanza kwalo, ili kutufunza kuanza kila jambo kwa Himdi, na jinsi ya kumhimidi Allaah.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Hamiyd:

1-Al-Hamiyd Hahitaji Himdi Ya Viumbe:

Tambua, ee Mja wa Al-Hamiyd: Allaah Anastahiki Kuhimidiwa kwa Dhati Yake, hata kama viumbe wote wangekufuru. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقَالَ مُوسَىٰ إِن تَكْفُرُوا أَنتُمْ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿٨﴾

Na Muwsaa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote walioko ardhini, basi hakika Allaah Ni Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Ibraahiym (14:8)]

2-Himdi Ni Zake Duniani Na Aakhirah:

Tambua kwamba Al-Hamiyd Anahimidiwa kwa Uumbaji Wake na Neema Zake duniani, na kwa Uadilifu Wake na Rehma Yake Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَلَهُ الْحَمْدُ فِي الْآخِرَةِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿١﴾

AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ni Vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Himdi ni Zake katika Aakhirah, Naye Ni Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Saba-a (34:1)]

3-Mhimidi Al-Hamiyd Katika Hali Zote:

Tambua kwamba Al-Hamiyd Pekee Ndiye Anayehimidiwa katika raha na shida, na katika dhiki na wasaa; Himdi zote ni Zake na katika kila hali, kwa kuwa Yeye Ni Mwenye Hikmah Asiyekosea katika Matendo Yake. Na kila anachohimidiwa nacho kiumbe, kinatoka kwa Muumbaji, kwani Yeye Ndiye Mtoaji wa sifa njema; basi Yeye Ndiye Anayestahiki zaidi Himdi duniani na Aakhirah. Na kwa Muumini daima kuna kheri: akipata raha hushukuru, na akipatwa na shida husubiri. Basi sema: الْحَمْدُ لِلَّهِ عَلَى كُلِّ حَالٍ! Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) إِذَا رَأَى مَا يُحِبُّ قَالَ: ((الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي بِنِعْمَتِهِ تَتِمُّ الصَّالِحَاتُ))، وَإِذَا رَأَى مَا يَكْرَهُ قَالَ: ((الْحَمْدُ لِلَّهِ عَلَى كُلِّ حَالٍ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapoona anachokipenda husema:

الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي بِنِعْمَتِهِ تَتِمُّ الصَّالِحَاتُ

Himdi ni za Allaah Ambaye kwa Neema Yake mema hukamilika.

Na anapoona asichokipenda husema:

الْحَمْدُ لِلَّهِ عَلَى كُلِّ حَالٍ

Himdi ni za Allaah katika kila hali. [Ibn Maajah (3803), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Ibn Maajah (3081)]

4-Usimnasibishie Al-Hamiyd Shari Wala Upungufu:

Tambua, ee Mja wa Al-Hamiyd: Ukamilifu wa Himdi Yake unawajibisha kwamba asinasibishiwe shari, wala uovu, wala upungufu; si katika Majina Yake, wala Matendo Yake, wala Sifa Zake. Na katika Du’aa ya kufungua Swalaah, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema:

عَنْ عَلِيِّ بْنِ أَبِي طَالِبٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) ... ((... لَبَّيْكَ وَسَعْدَيْكَ، وَالْخَيْرُ كُلُّهُ فِي يَدَيْكَ، وَالشَّرُّ لَيْسَ إِلَيْكَ ...))

Amesimulia ‘Aliy bin Abiy Twaalib (رضي الله عنه) kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ... “... Nakuitikia na nimo katika utiifu Wako, na kheri yote imo Mikononi Mwako, na shari hainasibishwi Kwako ...” [Muslim]

5-Himdi Ni Kauli Ya Mwisho Ya Watu Wa Jannah:

Tambua kwamba watu wa Jannah wataendelea kumhimidi Al-Hamiyd kama wanavyovuta pumzi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ ۚ وَآخِرُ دَعْوَاهُمْ أَنِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾

Wito wao humo ni: Subhaanak (Utakasifu ni Wako) ee Allaah! Na maamkizi yao humo ni Salaam! Na wito wao wa mwisho ni AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Rabb wa walimwengu. [Yuwnus (10:10)]

6-Jua Fadhila Za Kumhimidi Allaah:

Tambua kwamba kujua fadhila za ibaada kunakuhamasisha kuzitekeleza! Himdi ni miongoni mwa maneno yanayopendwa zaidi na Al-Hamiyd, na imekuja katika adhkaar nyingi; na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema kwamba Rabb wenu Anapenda Himdi, na kwamba Du’aa bora kabisa ni “الْحَمْدُ لِلَّهِ”. Basi zidisha kusema neno hili zuri katika maisha yako ya kila siku, kwa mapenzi ya kina, kwa kutukuza, kwa unyenyekevu na kwa shukurani kwa Rabb wako. Na ikumbuke Jannah unaposema الْحَمْدُ لِلَّهِ, kwani ndio maneno ya mwisho ya Du’aa ya watu wa Jannah, kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):

دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ ۚ وَآخِرُ دَعْوَاهُمْ أَنِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾

Wito wao humo ni: Subhaanak (Utakasifu ni Wako) ee Allaah! Na maamkizi yao humo ni Salaam! Na wito wao wa mwisho ni AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Rabb wa walimwengu. [Yuwnus (10:10)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي مَالِكٍ الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الطُّهُورُ شَطْرُ الإِيمَانِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ تَمْلأُ الْمِيزَانَ، وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ تَمْلآنِ -أَوْ تَمْلأُ- مَا بَيْنَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ ...))

Amesimulia Abu Maalik Al-Ash‘ariyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Twahara ni nusu ya imaan, na الْحَمْدُ لِلَّهِ hujaza mizani, na سُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ hujaza -au hujaza- yaliyo baina ya mbingu na ardhi ...” [Muslim]

7-Mhimidi Al-Hamiyd Anapokuneemesha:

Tambua, ee Mja wa Al-Hamiyd: Allaah Kukupa ilhamu ya kumhimidi na kumshukuru ni bora zaidi kuliko neema uliyoipata. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَا أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَى عَبْدٍ نِعْمَةً فَقَالَ: الْحَمْدُ لِلَّهِ، إِلاَّ كَانَ الَّذِي أَعْطَاهُ أَفْضَلَ مِمَّا أَخَذَ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Hamneemeshi mja neema yoyote akasema: الْحَمْدُ لِلَّهِ, isipokuwa kile Alichompa (cha kumhimidi) kinakuwa bora kuliko kile alichokichukua.” [Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Ibn Maajah (3082)]

8-Mhimidi Al-Hamiyd Hata Unapopiga Chafya:

Tambua kwamba sura za Himdi zimekuja katika adhkaar nyingi, hata pale mtu anapopiga chafya; na kumhimidi Al-Hamiyd humfanya mtu astahiki kuombewa rehma:

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: عَطَسَ رَجُلاَنِ عِنْدَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فَشَمَّتَ أَحَدَهُمَا وَلَمْ يُشَمِّتِ الآخَرَ، فَقِيلَ لَهُ، فَقَالَ: ((هَذَا حَمِدَ اللَّهَ، وَهَذَا لَمْ يَحْمَدِ اللَّهَ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Watu wawili walipiga chafya mbele ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), akamuombea mmoja wao (kwa kusema: YarhamukaAllaah) na hakumuombea mwingine. Akaulizwa kuhusu hilo, akasema: “Huyu amemhimidi Allaah, na huyu hakumhimidi Allaah.” [Al-Bukhaariy]

9-Kithirisha Maneno Yanayopendwa Zaidi Na Allaah:

Kithirisha maneno haya manne, kwani ndiyo maneno yanayopendwa zaidi na Al-Hamiyd.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ سَمُرَةَ بْنِ جُنْدَبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَحَبُّ الْكَلاَمِ إِلَى اللَّهِ أَرْبَعٌ: سُبْحَانَ اللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، وَاللَّهُ أَكْبَرُ، لاَ يَضُرُّكَ بِأَيِّهِنَّ بَدَأْتَ))

Amesimulia Samurah bin Jundub (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Maneno yanayopendwa zaidi na Allaah ni manne:

سُبْحَانَ اللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، وَاللَّهُ أَكْبَرُ

Utakasifu ni wa Allaah, na Himdi Anastahiki Allaah, na hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, na Allaah Ni Mkubwa zaidi; haikudhuru kwa lipi kati yake umeanza.” [Muslim]

10-Mswalie Nabiy Na Umtaje Allaah Kwa Jina Lake Al-Hamiyd:

Swalaah juu ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) imehitimishwa kwa Majina mawili ya Allaah: Al-Hamiyd na Al-Majiyd; kwa kuwa ukamilifu wote unarejea katika Himdi na Utukufu. Na hilo linaendana na Kauli Yake (تعالى):

قَالُوا أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۖ رَحْمَتُ اللَّـهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ ۚ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَّجِيدٌ ﴿٧٣﴾

(Malaika) wakasema: Je, unastaajabia Amri ya Allaah? Rehma ya Allaah na Baraka Zake ziko juu yenu enyi ahli wa nyumba (ya Nabiy Ibraahiym). Hakika Yeye Ni Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa, Mwenye Utukufu kamili na Enzi. [Huwd (11:73)]

Basi Du’aa hii inajumuisha kumuombea Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) Himdi na Utukufu, na inahitimishwa kwa kumsifu Allaah kwa Himdi na Utukufu:

عَنْ كَعْبِ بْنِ عُجْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَأَلْنَا رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) فَقُلْنَا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، كَيْفَ الصَّلاَةُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ؟ ... قَالَ: ((قُولُوا: اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ، اللَّهُمَّ بَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا بَارَكْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ))

Amesimulia Ka‘b bin ‘Ujrah (رضي الله عنه): Tulimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Yaa Rasula-Allaah! Vipi tukuswalie nyinyi Ahlul-Bayt? ... Akasema: “Semeni:

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ، اللَّهُمَّ بَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا بَارَكْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ

Yaa Allaah, Mswalie Muhammad na ahli wa Muhammad kama Ulivyomswalia Ibraahiym na ahli wa Ibraahiym, hakika Wewe Ni Mwenye Kuhimidiwa, Mtukufu. Yaa Allaah, Mbariki Muhammad na ahli wa Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na ahli wa Ibraahiym, hakika Wewe Ni Mwenye Kuhimidiwa, Mtukufu.” [Al-Bukhaariy]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Sha-an Ad-Du‘aa (78), Tafsiyr As-Sa‘diy (5/624), na Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam (22).
  • 2Tafsiyr Suwrah Luqmaan, Ibn ‘Uthaymiyn (7/248).
  • 3Al-Haqq Al-Waadhwih Al-Mubiyn (39).
  • 4Tafsiyr Suwrah Saba-a (7/204) na Tafsiyr Suwrah Al-Buruwj (10/462), Ibn ‘Uthaymiyn.