Ash-Shaakir: Mwenye Shukurani
Yeye Anamsifu anayemtii na kumsifia, na Anampa thawabu kwa utiifu wake. Anatoa malipo kwa amali iliyofanywa hata ikiwa ndogo, na Anazikabili shukurani za neema kwa kuziongeza neema hizo duniani na kuwawekea malipo Aakhirah. Qur-aan imejaa sifa za Manabii na Swalihina; Allaah Huwashukuru wenye kushukuru, na Huwataja wenye kumdhukuru kwa kuwasifu katika hadhara Yake ya juu na miongoni mwa Malaika Wake, na Huwawekea shukurani miongoni mwa Waja Wake.
Jina hili la Allaah Ash-Shaakir limetajwa katika Qur-aan mara mbili, na kila mahali limekuja likiambatana na Jina jingine. Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema:
مَّا يَفْعَلُ اللَّـهُ بِعَذَابِكُمْ إِن شَكَرْتُمْ وَآمَنتُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ شَاكِرًا عَلِيمًا ﴿١٤٧﴾
Allaah Hatokuadhibuni ikiwa mtashukuru na mtaamini. Na Allaah daima Ni Mwenye Kupokea Shukurani, Mjuzi wa yote. [An-Nisaa (4:147)]
Na mzizi wake ش ك ر una maana tatu: kumsifu mtu kwa manufaa aliyoyatoa au kukiri wema wake; kuwa na shukurani na kuikiri; na kuzalisha na kutoa kwa wingi. Na kilugha ash-shukr ni kuonekana wazi athari ya chakula katika mwili wa mnyama; na Waarabu humwita mnyama “shakuwr” pale anapolishwa kidogo na kuonekana kunenepa sana. Na herufi “waw” katika Ash-Shakuwr inaonyesha kwamba Allaah (عزّ وجلّ) Ni Mwingi mno wa kushukuru. Na maana ya shukurani ni kutambua wema na kuueneza; na tofauti yake na al-hamd ni kwamba al-hamd ni pana zaidi, kwani unamhimidi mtu kwa sifa zake nzuri na wema wake, lakini humshukuru isipokuwa kwa wema wake tu; basi shukurani haiwi isipokuwa kwa kupewa.
Na Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Anayestahiki zaidi kushukuriwa kuliko chochote chenye kushukuriwa, bali Yeye Ndiye Mshukuriwa wa hakika:
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ash-Shaakir:
1-Ash-Shaakir Hana Haja Ya Kuwaadhibu Waja Wanaoshukuru:
Tambua, ee Mja wa Ash-Shaakir: Allaah Ni Mwenye Kushukuru; Hawaadhibu waja wanaoamini na kushukuru. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَّا يَفْعَلُ اللَّـهُ بِعَذَابِكُمْ إِن شَكَرْتُمْ وَآمَنتُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ شَاكِرًا عَلِيمًا ﴿١٤٧﴾
Allaah Hatokuadhibuni ikiwa mtashukuru na mtaamini. Na Allaah daima Ni Mwenye Kupokea Shukurani, Mjuzi wa yote. [An-Nisaa (4:147)]
2-Ash-Shaakir Anashukuru Hata Amali Ndogo Ya Kujitolea:
Hakuna jema dogo linalopotea mbele ya Ash-Shaakir. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللَّـهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ ﴿١٥٨﴾
Hakika Swafaa na Marwah ni katika Alama za Allaah. Kwa hiyo yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah, hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo. Na atakayejitolea kufanya kheri, basi hakika Allaah Ni Mwenye Kupokea Shukurani, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah (2:158)]
3-Mshukuru Allaah Kwa Kumpwekesha Na Kumtii:
Tambua kwamba shukurani kubwa kabisa kwa Ash-Shaakir ni kumpwekesha, kumwabudu na kumtii; na kumshukuru Allaah ni wajibu kwa kila aliyebaleghe. Na uhakika wa shukurani ni kuonekana athari ya Neema ya Allaah katika ulimi wa mja wake kwa kumsifu na kukiri, na katika moyo wake kwa kushuhudia na kupenda, na katika viungo vyake kwa kunyenyekea na kutii. Na kiigizo chetu ni Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ نَبِيَّ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُومُ مِنَ اللَّيْلِ حَتَّى تَتَفَطَّرَ قَدَمَاهُ، فَقَالَتْ عَائِشَةُ: لِمَ تَصْنَعُ هَذَا يَا رَسُولَ اللَّهِ، وَقَدْ غَفَرَ اللَّهُ لَكَ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِكَ وَمَا تَأَخَّرَ؟ قَالَ: ((أَفَلاَ أُحِبُّ أَنْ أَكُونَ عَبْدًا شَكُورًا))
Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nabiy wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisimama usiku (kuswali) mpaka miguu yake ikapasuka. ‘Aaishah akasema: Kwa nini unafanya hivi yaa Rasula-Allaah, na hali Allaah Amekughufuria madhambi yako yaliyotangulia na yaliyokuja nyuma? Akasema: “Je, nisipende kuwa mja mwingi wa kushukuru?” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
4-Tambua Kwamba Shukurani Huzidisha Neema:
Allaah Amewaamrisha viumbe Wake kushukuru, na Amewaamrisha Manabii Wake, na Amekataza kinyume chake; Amewasifu wenye kushukuru na Amewafanya kuwa ni wateule miongoni mwa viumbe Wake; kama Alivyomsifu Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) na Nabiy Nuwh (عليه السلام) kuwa alikuwa mja mwingi wa kushukuru. Na Ameijaalia shukurani kuwa ni sababu ya Radhi Zake kwa Waja Wake, na Amewaahidi wenye kushukuru malipo bora, na Akawazidishia juu ya malipo hayo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ ﴿٧﴾
Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (Neema Zangu), na mkikufuru, basi hakika Adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym (14:7)]
5-Shukurani Ni Kwa Moyo, Ulimi Na Vitendo:
Tambua kwamba Ash-Shaakir Amewaamrisha ahli wa Daawuwd kushukuru kwa amali, na Akabainisha kwamba wenye kushukuru ni wachache. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِن مَّحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَّاسِيَاتٍ ۚ اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ ﴿١٣﴾
Wanamfanyia kazi atakayo; (kujenga) ngome ndefu za fakhari na tasawiri, na madeste makubwa kama mahodhi na masufuria makubwa yaliyothibiti imara. (Tukasema): Tendeni enyi familia ya Daawuwd kwa shukurani! Na wachache miongoni mwa Waja Wangu ni wenye kushukuru. [Saba-a (34:13)]
6-Iga Shukurani Ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Kwa Rabb Wake:
Tafakari, ee Mja wa Ash-Shaakir, shukurani ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Rabb wake, na uige mfano wake.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisimama usiku mpaka miguu yake ikavimba:
عَنِ الْمُغِيرَةِ بْنِ شُعْبَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَامَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم) حَتَّى تَوَرَّمَتْ قَدَمَاهُ، فَقِيلَ لَهُ: غَفَرَ اللَّهُ لَكَ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِكَ وَمَا تَأَخَّرَ. قَالَ: ((أَفَلاَ أَكُونُ عَبْدًا شَكُورًا))
Amesimulia Al-Mughiyrah bin Shu’bah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisimama (kuswali usiku) mpaka miguu yake ikavimba. Akaambiwa: Allaah Amekughufuria madhambi yako yaliyotangulia na yaliyokuja nyuma! Akasema: “Je, nisiwe mja mwingi wa kushukuru?” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
7-Tumia Neema Za Allaah Katika Kumtii:
Tambua kwamba kwa kila kiungo kuna shukurani yake, na shukurani yake ni kukitumia kwa kumcha Ash-Shaakir. Na Imaam Al-Qurtwubiy (رحمه الله) ametaja nguzo tatu za shukurani: kukiri neema kwa Mneemeshaji; kuitumia katika kumtii na kutoitumia katika maasi; na kumshukuru yule ambaye neema imepitia mikononi mwake. Na ridhaa ni daraja ya kwanza ya shukurani, na imaan ni nusu mbili: nusu shukurani na nusu subira. Na tambua kwamba utaulizwa kuhusu neema hizo:
عَنْ أَبِي بَرْزَةَ الأَسْلَمِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((لاَ تَزُولُ قَدَمَا عَبْدٍ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حَتَّى يُسْأَلَ عَنْ عُمُرِهِ فِيمَا أَفْنَاهُ، وَعَنْ عِلْمِهِ فِيمَ فَعَلَ، وَعَنْ مَالِهِ مِنْ أَيْنَ اكْتَسَبَهُ وَفِيمَ أَنْفَقَهُ، وَعَنْ جِسْمِهِ فِيمَ أَبْلاَهُ))
Amesimulia Abu Barzah Al-Aslamiyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Haitaondoka miguu ya mja Siku ya Qiyaamah mpaka aulizwe kuhusu umri wake ameumalizia katika nini, na ilimu yake ameifanyia nini, na mali yake ameichuma wapi na ameitumia katika nini, na mwili wake ameutumia katika nini.” [At-Tirmidhiy (2417), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
8-Muumini Hushukuru Katika Raha Na Husubiri Katika Shida:
Kumbuka, ee Mja wa Ash-Shaakir, kwamba Muumini yuko katika kheri kila hali: hushukuru katika raha, na husubiri katika shida.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ صُهَيْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((عَجَبًا لأَمْرِ الْمُؤْمِنِ، إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ، وَلَيْسَ ذَاكَ لأَحَدٍ إِلاَّ لِلْمُؤْمِنِ، إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ، وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ))
Amesimulia Swuhayb (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ajabu ya jambo la Muumini! Hakika mambo yake yote ni kheri, na hilo si kwa yeyote isipokuwa kwa Muumini. Akipatwa na furaha hushukuru, ikawa kheri kwake; na akipatwa na dhara husubiri, ikawa kheri kwake.” [Muslim]
9-Washukuru Watu Waliokufanyia Wema:
Tambua kwamba ni wajibu kwa mja kumshukuru yule ambaye Ash-Shaakir Ameipitisha neema katika mikono yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لاَ يَشْكُرُ اللَّهَ مَنْ لاَ يَشْكُرُ النَّاسَ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hamshukuru Allaah yule asiyewashukuru watu.” [Abuu Daawuwd (4811), At-Tirmidhiy (1954), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
10-Sujudu Sijda Ya Shukurani Unapopata Neema Au Habari Njema:
Tambua, ee Mja wa Ash-Shaakir: Ilikuwa ni Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنْ أَبِي بَكْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ كَانَ إِذَا جَاءَهُ أَمْرُ سُرُورٍ أَوْ بُشِّرَ بِهِ خَرَّ سَاجِدًا شَاكِرًا لِلَّهِ
Amesimulia Abuu Bakrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapojiwa na jambo la kufurahisha, au anapobashiriwa nalo, huanguka kusujudu akimshukuru Allaah. [Abuu Daawuwd (2774), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
11-Mshukuru Allaah Baada Ya Kula:
Kumbuka kumshukuru Ash-Shaakir kila unapomaliza kula, kwa maneno aliyoyafundisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ مُعَاذِ بْنِ أَنَسٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ أَكَلَ طَعَامًا ثُمَّ قَالَ: الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي أَطْعَمَنِي هَذَا الطَّعَامَ وَرَزَقَنِيهِ مِنْ غَيْرِ حَوْلٍ مِنِّي وَلاَ قُوَّةٍ، غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))
Amesimulia Mu’aadh bin Anas (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayekula chakula kisha akasema:
الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي أَطْعَمَنِي هَذَا الطَّعَامَ وَرَزَقَنِيهِ مِنْ غَيْرِ حَوْلٍ مِنِّي وَلاَ قُوَّةٍ
Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Amenilisha chakula hiki na Akaniruzuku bila ya ujanja wala nguvu yoyote kutoka kwangu; ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia.” [Abuu Daawuwd (4023), At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
Na Allaah Mjuzi zaidi