Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 061 kati ya 103
Ash-Shakuwr — Majina Mazuri ya Allaah

Ash-Shakuwr: Mwingi Wa Kupokea Shukurani

Kwake amali ndogo za waja hukua, na Huwarudufishia malipo. Allaah kumshukuru mja ni kumlipa kwa shukurani hizo na kukubali ibaada zake. Yeye Ni Mwenye kushukuru amali ndogo, na kusamehe makosa mengi, wala Hapotezi ujira wa aliyefanya amali nzuri, bali Huuzidisha bila ya hesabu. Na Jina Ash-Shakuwr limekuja pamoja na Al-Ghafuwr; kwani Allaah Ni Mwingi wa kughufuria maovu, Mwingi wa kushukuru mema.

Jina hili la Allaah Ash-Shakuwr limetajwa katika Qur-aan mara nne, na kila mahali limekuja likiambatana na Jina jingine. Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema:

لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٠﴾

Ili (Allaah) Awalipe ujira wao timilifu, na Awazidishie kutokana na Fadhila Zake. Hakika Yeye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwingi wa Kupokea Shukurani. [Faatwir (35:30)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

إِن تُقْرِضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا يُضَاعِفْهُ لَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ شَكُورٌ حَلِيمٌ ﴿١٧﴾

Mkimkopesha Allaah karadha nzuri, Atakuzidishieni maradufu, na Atakughufurieni. Na Allaah Ni Mwenye Kupokea shukurani, Mpole na Mvumilivu. [At-Taghaabun (64:17)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

1-Allaah Humpa thawabu mwenye kumshukuru, bali Humpa bila ya hesabu.

2-Husamehe makosa mengi na Hukubali matendo mema hata yakiwa machache, na Hulipa thawabu nyingi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَذْهَبَ عَنَّا الْحَزَنَ ۖ إِنَّ رَبَّنَا لَغَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٤﴾

Na watasema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Ambaye Ametuondoshea huzuni. Hakika Rabb wetu bila shaka Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwingi wa Kupokea Shukurani. [Faatwir (35:34)]

3-Yeye Mtukufu Huwashukuru Waja Wake kwa kumshukuru Kwao; Huwazidishia kheri na fadhila tele juu ya Neema Alizowapa, na hiyo ndiyo shukurani Yake.

4-Na miongoni mwa ukamilifu wa shukurani Yake (جلّ جلاله) ni kwamba Humpa Mja Wake na Humuwafikisha kwa kile Anachomshukuru nacho; basi Yeye Ndiye Aliyetoa na Ndiye Aliyesifu, Yeye Ndiye Aliyeleta sababu na Ndiye Anayeshukuru matokeo yake. Anasema (سبحانه وتعالى) kuhusu watu wa Jannah:

إِنَّ هَـٰذَا كَانَ لَكُمْ جَزَاءً وَكَانَ سَعْيُكُم مَّشْكُورًا ﴿٢٢﴾

(Wataambiwa): Hakika haya ni jazaa yenu, kwani juhudi zenu zimethaminiwa. [Al-Insaan (76:22)]

Anatupa neema ya kutafuta, Anatuwafikisha na Anatusaidia, kisha Anatushukuru kwayo! Wa-Allaahi, huu ndio upeo wa fadhila na wema; basi shukurani ni za Allaah na Himdi ni Zake.1 Na Imaam Al-Ghazaaliy (رحمه الله) amesema: Rabb (تعالى) Anaposifu amali za Waja Wake, basi Amesifu tendo Lake Mwenyewe, kwa kuwa amali zao ni katika Uumbaji Wake.

5-Na katika ukamilifu Wake ni kwamba Yeye Hushukuru amali chache pamoja na wingi wa Neema Zake. Na kila Aayah iliyotajwa humo Jina la Ash-Shakuwr imekuja pamoja na maneno ya kuzidisha na kurudufisha; kama “Awazidishie kutokana na Fadhila Zake”, “Tutamzidishia humo zuri”, na “Atakurudufishieni na Atakughufurieni, na Allaah Ni Mwingi wa kushukuru, Mvumilivu.”

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ash-Shakuwr:

1-Ash-Shakuwr Anawalipa Waja Ujira Wao Kamili Na Kuwazidishia Katika Fadhila Zake:

Ash-Shakuwr Hulipa amali ndogo kwa malipo makubwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٠﴾

Ili (Allaah) Awalipe ujira wao timilifu, na Awazidishie kutokana na Fadhila Zake. Hakika Yeye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwingi wa Kupokea Shukurani. [Faatwir (35:30)]

2-Mkopeshe Ash-Shakuwr Mkopo Mzuri Akuzidishie:

Anayetoa katika Njia ya Allaah humkopesha Ash-Shakuwr, Naye Humzidishia mara nyingi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِن تُقْرِضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا يُضَاعِفْهُ لَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ شَكُورٌ حَلِيمٌ ﴿١٧﴾

Mkimkopesha Allaah karadha nzuri, Atakuzidishieni maradufu, na Atakughufurieni. Na Allaah Ni Mwenye Kupokea shukurani, Mpole na Mvumilivu. [At-Taghaabun (64:17)]

3-Jitahidi Kuwa Miongoni Mwa Wachache Wenye Kushukuru:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shakuwr: Miongoni mwa faida za shukurani ni kuwa katika kundi la wateule mbele ya Allaah, kwani wao ni wachache katika walimwengu. Na miongoni mwa faida zake ni kupata amani na Adhabu ya Allaah (Rejea juu: An-Nisaa (4:147)).

اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ ﴿١٣﴾

Tendeni enyi familia ya Daawuwd kwa shukurani! Na wachache miongoni mwa Waja Wangu ni wenye kushukuru. [Saba-a (34:13)]

4-Juhudi Ya Anayetaka Aakhirah Hushukuriwa:

Tambua kwamba kila juhudi ya Muumini inayomlenga Ash-Shakuwr haipotei. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾

Na anayetaka Aakhirah na akaifanyia juhudi inayostahiki kufanyiwa, naye ni Muumin, basi hao juhudi zao ni za kushukuriwa. [Al-Israa (17:19)]

5-Tamani Kuambiwa Siku Ya Qiyaamah: Juhudi Yenu Imeshukuriwa:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shakuwr: Haya ni maneno yatakayowapokea watu wa Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ هَـٰذَا كَانَ لَكُمْ جَزَاءً وَكَانَ سَعْيُكُم مَّشْكُورًا﴿٢٢﴾

(Wataambiwa): Hakika haya ni jazaa yenu, kwani juhudi zenu zimethaminiwa. [Al-Insaan (76:22)]

6-Zidisha Mema, Ash-Shakuwr Atakuzidishia:

Ash-Shakuwr Hazidishi tu thawabu za mema, bali Humzidishia mwenye kuyafanya uzuri juu ya uzuri wake. Na katika shukurani Yake kwa Mja Wake ni kwamba atakayeacha kitu kwa ajili ya Allaah, Allaah Atamlipa kilicho bora zaidi kuliko hicho. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَن يَقْتَرِفْ حَسَنَةً نَّزِدْ لَهُ فِيهَا حُسْنًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ شَكُورٌ

Na yeyote anayechuma mazuri, Tutamzidishia humo zuri. Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwingi wa Kupokea Shukurani. [Ash-Shuwraa (42:23)]

7-Usidharau Jema Lolote Hata Likiwa Dogo:

Tumekatazwa kudharau chochote katika amali za wema hata kikiwa kidogo; Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Usidharau chochote katika wema, hata kukutana na nduguyo kwa uso mkunjufu” [Muslim], na amesema: “Jikingeni na moto hata kwa kipande cha tende” [Al-Bukhaariy] [Muslim]. Na kilicho kidogo machoni mwetu kina ujira mkubwa mbele ya Ash-Shakuwr (تعالى); na Allaah Hadhulumu hata uzito wa chembe ndogo kabisa, na likiwa ni jema Hulirudufisha. Anasema (سبحانه وتعالى):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾

Hakika Allaah Hadhulumu hata uzito au chembe (kama atomu). Na ikiwa ni amali njema Huizidisha na Hutoa kutoka Kwake ujira mkuu kabisa. [An-Nisaa (4:40)]

Na tazama shukurani ya Ash-Shakuwr:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((بَيْنَمَا رَجُلٌ يَمْشِي بِطَرِيقٍ اشْتَدَّ عَلَيْهِ الْعَطَشُ، فَوَجَدَ بِئْرًا فَنَزَلَ فِيهَا فَشَرِبَ ثُمَّ خَرَجَ، فَإِذَا كَلْبٌ يَلْهَثُ يَأْكُلُ الثَّرَى مِنَ الْعَطَشِ، فَقَالَ الرَّجُلُ: لَقَدْ بَلَغَ هَذَا الْكَلْبَ مِنَ الْعَطَشِ مِثْلُ الَّذِي كَانَ بَلَغَ مِنِّي، فَنَزَلَ الْبِئْرَ فَمَلأَ خُفَّهُ مَاءً ثُمَّ أَمْسَكَهُ بِفِيهِ حَتَّى رَقِيَ فَسَقَى الْكَلْبَ، فَشَكَرَ اللَّهُ لَهُ فَغَفَرَ لَهُ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mtu mmoja alipokuwa akitembea njiani alipatwa na kiu kali, akakuta kisima akateremka akanywa kisha akatoka. Mara akaona mbwa anahema huku akila udongo kwa kiu. Mtu yule akasema: Kiu imemfikia mbwa huyu kama ilivyonifikia mimi. Akateremka kisimani, akajaza khufu yake maji, kisha akaishika kwa mdomo wake mpaka akapanda, akamnywesha mbwa. Allaah Akamshukuru, Akamghufuria.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

8-Ash-Shakuwr Hughufiria Hata Kwa Amali Ndogo Ya Kuondoa Udhia Njiani:

Tambua kwamba Ash-Shakuwr Hushukuru hata amali ndogo; basi usidharau jema lolote.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((بَيْنَمَا رَجُلٌ يَمْشِي بِطَرِيقٍ وَجَدَ غُصْنَ شَوْكٍ عَلَى الطَّرِيقِ فَأَخَّرَهُ، فَشَكَرَ اللَّهُ لَهُ فَغَفَرَ لَهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mtu mmoja alipokuwa akitembea njiani alikuta tawi la miiba njiani akaliondoa; Allaah Akamshukuru, Akamghufuria.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Mhimidi Allaah Kwa Kila Tonge Na Kila Kinywaji:

Kumbuka kumhimidi Ash-Shakuwr kwa kila tonge unalokula na kila kinywaji unachokunywa.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لَيَرْضَى عَنِ الْعَبْدِ أَنْ يَأْكُلَ الأَكْلَةَ فَيَحْمَدَهُ عَلَيْهَا، أَوْ يَشْرَبَ الشَّرْبَةَ فَيَحْمَدَهُ عَلَيْهَا))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Humridhia mja anayekula chakula kisha akamhimidi kwacho, au anayekunywa kinywaji kisha akamhimidi kwacho.” [Muslim]

10-Muombe Allaah Akusaidie Kumshukuru:

Omba du’aa, ee Mja wa Ash-Shakuwr, Allaah Akusaidie kumdhukuru, kumshukuru na kumwabudu vizuri.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Mu‘aadh bin Jabal (رضي الله عنه) kwamba anampenda, kisha akamuusia:

عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَخَذَ بِيَدِهِ وَقَالَ: ((يَا مُعَاذُ، وَاللَّهِ إِنِّي لأُحِبُّكَ ... أُوصِيكَ يَا مُعَاذُ لاَ تَدَعَنَّ فِي دُبُرِ كُلِّ صَلاَةٍ تَقُولُ: اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ))

Amesimulia Mu‘aadh bin Jabal (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliushika mkono wake akasema: “Ee Mu‘aadh, Wa-Allaahi hakika mimi nakupenda ... Nakuusia ee Mu‘aadh, usiache kusema mwishoni mwa kila Swalaah:

اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ

Yaa Allaah, Nisaidie kukudhukuru, kukushukuru na kukuabudu vizuri.” [Abuu Daawuwd (1522), An-Nasaaiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Tafsiyr Suwrah Aal-‘Imraan, Ibn ‘Uthaymiyn (2/195).