Al-Muqiyt: Mwenye Kudhibiti Na Kushuhudia Kila Kitu
Al-Muqiyt Ni Mwenye Uwezo, Mwenye Kudhibiti, Mwenye Kuhifadhi, Mwangalizi na Mwenye Kutoa chakula. Yeye Ndiye Muumbaji wa vyakula na Mwenye kuvifikisha kwenye miili, na Mwenye kufikisha kwenye nyoyo chakula chake ambacho ni maarifa; Amekifikishia kila kilichopo kile kinachokiendesha, Naye Ni Muweza wa kila kitu. Na tofauti baina ya chakula (al-quwt) na rizqi ni kwamba chakula ni kile kinachosimamisha mwili katika vinavyolisha, ama rizqi ni kila kinachoingia katika milki ya mja; kinacholiwa na kisicholiwa.
Jina Hili la Allaah limetajwa katika Qur-aan mara moja tu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَّن يَشْفَعْ شَفَاعَةً حَسَنَةً يَكُن لَّهُ نَصِيبٌ مِّنْهَا ۖ وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقِيتًا ﴿٨٥﴾
Atakayesaidia kufanikisha jambo la kheri atapata fungu lake katika hayo. Na atakayesaidia kuunganisha jambo la shari atapata sehemu yake katika hayo. Na Allaah daima Ni Mwenye Kudhibiti na Mwangalizi wa kila kitu. [An-Nisaa (4:85)]
Na mzizi wake ق و ت una maana nne: kuwapa viumbe mahitaji yao na kuwadumisha; kulisha na kurutubisha; kuhifadhi na kulinda; na kushuhudia na kuangalia. Na mzizi huu umekuja katika Qur-aan mara mbili kwa namna mbili: aqwaatahaa (chakula chake) na muqiytan (Mwenye Kudhibiti).
Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Muqiyt; Mwenye uwezo Ambaye Ndiye Aliyeumba vyakula, na Akadhamini vimfikie kila kiumbe kwa ukamilifu vikiwa vimehifadhika katika kila nchi, na hivyo Anampa kila kiumbe rizqi yake katika nyakati zote kwa kila Alichokiainisha, kwa ukamilifu wa Matakwa Yake na Hikmah Yake daima.
Na kama ambavyo Allaah Hudhamini chakula cha kiwiliwili, vivyo hivyo Hudhamini chakula cha nyoyo kwa ilimu na imaan; na Yeye Ndiye Mwenye kuhifadhi matendo ya Waja Wake bila ya upungufu wala kusahau. Na vyakula na rizqi Allaah Amewakadiria Waja Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ مِن فَوْقِهَا وَبَارَكَ فِيهَا وَقَدَّرَ فِيهَا أَقْوَاتَهَا فِي أَرْبَعَةِ أَيَّامٍ سَوَاءً لِّلسَّائِلِينَ ﴿١٠﴾
Na Akaweka humo milima iliyosimama thabiti juu yake, na Akabariki humo kwa kheri zisizokatika, na Akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Ni idadi madhubuti kabisa kwa wanaouliza. [Fusw-swilat (41:10)]
Yaani Amewakadiria watu wake wanachohitaji katika rizqi, na sehemu mbalimbali ambazo zinalimwa na kupandwa.1 Kwa ujumla, Allaah (تعالى) Ni Mwenye uwezo wa kuhifadhi na kutoa chakula kwa Waja Wake, Mwenye kushuhudia hali zao na Mwangalizi wa mambo yao; na Jina Hili tukufu limekusanya sifa hizo zote.2
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muqiyt:
1-Al-Muqiyt Amekadiria Vyakula Vya Ardhi Tangu Kuiumba:
Tambua, ee Mja wa Al-Muqiyt: Allaah Alikadiria rizki na vyakula vya viumbe katika ardhi kabla ya kuwaumba. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا ۚ كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴿٦﴾
Na Akaweka humo milima iliyosimama thabiti juu yake, na Akabariki humo kwa kheri zisizokatika, na Akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Ni idadi madhubuti kabisa kwa wanaouliza. [Fusw-swilat (41:10)]
2-Tambua Kwamba Kila Kiumbe Kina Chakula Chake Kutoka Kwa Al-Muqiyt:
Kila kiumbe kina chakula chake: chakula cha miili ni vyakula, chakula cha roho ni ilimu, na chakula cha Malaika ni tasbiyh. Kwa ujumla, Allaah Ndiye Al-Muqiyt wa Waja Wake, Mwenye kuwahifadhi, na hakuna anayesimamia maslahi ya Waja isipokuwa Allaah. Na Yeye (سبحانه وتعالى) Amejiwajibishia Mwenyewe kuwaruzuku viumbe Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا ۚ كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٦﴾
Na hakuna kiumbe chochote kitembeacho katika ardhi isipokuwa rizki yake iko kwa Allaah, na (Allaah) Anajua mahali pake pa kustakiri na pa kuhifadhiwa kwake. Yote yamo katika Kitabu kinachobainisha. [Huwd (11:6)]
3-Mshukuru Al-Muqiyt Kwa Chakula Na Amani:
Chakula na amani ni neema mbili kubwa za Al-Muqiyt zinazostahiki kumwabudu Yeye Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَلْيَعْبُدُوا رَبَّ هَـٰذَا الْبَيْتِ ﴿٣﴾ الَّذِي أَطْعَمَهُم مِّن جُوعٍ وَآمَنَهُم مِّنْ خَوْفٍ ﴿٤﴾
Basi wamuabudu Rabb wa Nyumba hii (Ka’bah). Ambaye Anawalisha kuwaokoa na njaa, na Anawapa amani kutokana na khofu. [Quraysh (106:3-4)]
4-Mtegemee Al-Muqiyt Na Usiwe Na Wasiwasi Juu Ya Rizqi Yako:
Al-Muqiyt Anawaruzuku na Anawasimamia viumbe wote bila ya kuchoka; basi kuwa na yakini kwamba Anakusimamia kwa namna iliyo bora kabisa. Mtegemee Yeye Akuruzuku, Akulishe na Akuhifadhi, hasa pale unapozidiwa na matatizo na kupungua kwa kipato chako; kwani imaan juu ya Jina Hili hupelekea mapenzi kwa Allaah (تعالى), utulivu wa moyo na yakini juu ya Uwezo Wake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((لَوْ أَنَّكُمْ كُنْتُمْ تَوَكَّلُونَ عَلَى اللَّهِ حَقَّ تَوَكُّلِهِ لَرُزِقْتُمْ كَمَا تُرْزَقُ الطَّيْرُ تَغْدُو خِمَاصًا وَتَرُوحُ بِطَانًا))
Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Lau kama mngelimtegemea Allaah kwa kweli, basi mngeliruzukiwa kama wanavyoruzukiwa ndege; huondoka asubuhi wakiwa na njaa na hurudi jioni wakiwa wameshiba.” [At-Tirmidhiy (2344) na amesema: Hasan Swahiyh, Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
5-Kula Cha Halali Na Kizuri Kwa Kiasi:
Ni juu ya mja chakula chake kiwe cha halali na kizuri, na kiwe cha hali ya kati kwa kati; kisiwe cha israfu wala cha ubakhili. Wala usitafute rizqi kwa njia za haraam kwa kutilia shaka Uwezo wa Al-Muqiyt wa kukuruzuku. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ كُلُوا مِمَّا فِي الْأَرْضِ حَلَالًا طَيِّبًا وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿١٦٨﴾
Enyi watu! Kuleni katika vilivyomo ardhini vya halali, vizuri na wala msifuate hatua za shaytwaan. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi. [Al-Baqarah (2:168)]
6-Walishe Unaowategemea Na Uwe Sababu Ya Rizqi Kwa Wengine:
Ukimshukuru Al-Muqiyt kwa rizqi Yake, Hifadhi Yake na Neema Zake, Atakufanya kuwa hazina kwa Waja Wake; Atakuwezesha kuwalisha wengine, kuwafundisha ilimu na kuwaongoza kwa Al-Hayyu Al-Qayyuwm. Basi tumia rizqi yako katika yanayomridhisha Yeye na si katika yanayomghadhibisha: toa Zakaah ya mali yako, na toa swadaqa kwa wingi kwa mali yako, wakati wako na ujuzi wako. Lakini anza na wale unaowalisha; kwani Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amefundisha kuanza kwa wale unaowakimu:
عَنْ حَكِيمِ بْنِ حِزَامٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((الْيَدُ الْعُلْيَا خَيْرٌ مِنَ الْيَدِ السُّفْلَى، وَابْدَأْ بِمَنْ تَعُولُ، وَخَيْرُ الصَّدَقَةِ عَنْ ظَهْرِ غِنًى، وَمَنْ يَسْتَعْفِفْ يُعِفَّهُ اللَّهُ، وَمَنْ يَسْتَغْنِ يُغْنِهِ اللَّهُ))
Amesimulia Hakiym bin Hizaam (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mkono wa juu (unaotoa) ni bora kuliko mkono wa chini (unaopokea). Na anza (kutoa) kwa wale unaowakimu. Na swadaqa bora ni ile inayotolewa baada ya kujitosheleza. Na mwenye kujizuia (na kuomba), Allaah Atamwepusha; na mwenye kujitosheleza, Allaah Atamtosheleza.” [Al-Bukhaariy]
7-Usiwanyime Unaowajibika Kuwalisha:
Tahadhari na kuwanyima chakula na mahitaji wale ambao Al-Muqiyt Amekuwajibisha kuwalisha.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((كَفَى بِالْمَرْءِ إِثْمًا أَنْ يَحْبِسَ عَمَّنْ يَمْلِكُ قُوتَهُ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Inamtosha mtu kuwa na dhambi kumzuilia chakula chake yule ambaye yeye ndiye mwenye kumlisha.” [Muslim]
8-Lisha Moyo Wako Kwa Imaan Na Ilimu:
Kama ambavyo mwili unahitaji chakula, vivyo hivyo moyo na roho vinahitaji chakula chake; basi lisha moyo wako kwa kumpwekesha Allaah, na lisha roho yako kwa nguzo za Uislamu: Shahaadah, Swalaah, Zakaah, Swawm na Hajj. Na rizqi bora kabisa Anayomruzuku Allaah mja ni akili; basi Aliyemruzuku akili Amemkirimu. Na mwombe Al-Muqiyt Akuongoze kwenye imaan na uongofu, na kwenye matendo mema na ihsaan, kwani hayo ni bora zaidi kuliko hata chakula cha kiwiliwili. Allaah (تعالى) Amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:
عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِيمَا رَوَى عَنِ اللَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى أَنَّهُ قَالَ: ((... يَا عِبَادِي كُلُّكُمْ ضَالٌّ إِلاَّ مَنْ هَدَيْتُهُ فَاسْتَهْدُونِي أَهْدِكُمْ، يَا عِبَادِي كُلُّكُمْ جَائِعٌ إِلاَّ مَنْ أَطْعَمْتُهُ فَاسْتَطْعِمُونِي أُطْعِمْكُمْ ...))
Amesimulia Abu Dharr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema katika aliyoyapokea kutoka kwa Allaah (تبارك وتعالى) kwamba Amesema: “... Enyi Waja Wangu! Nyote mmepotea isipokuwa Niliyemuongoza, basi niombeni uongofu Nitakuongozeni. Enyi Waja Wangu! Nyote mna njaa isipokuwa Niliyemlisha, basi niombeni chakula Nitakulisheni ...” [Muslim]
9-Mkumbuke Al-Muqiyt Kila Unapokula:
Kila unapoletewa chakula, mkumbuke Al-Muqiyt na Fadhila Zake za ajabu ambazo kwazo umeruzukiwa chakula hicho; na vivyo hivyo katika mahitaji yote ya kila siku ambayo mara nyingi hatuyafikirii, hata ilimu unayoweza kuipata ili kuimarisha akili yako na moyo wako. Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametufundisha kumhimidi Allaah baada ya kula:
عَنْ مُعَاذِ بْنِ أَنَسٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ أَكَلَ طَعَامًا ثُمَّ قَالَ: الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي أَطْعَمَنِي هَذَا الطَّعَامَ وَرَزَقَنِيهِ مِنْ غَيْرِ حَوْلٍ مِنِّي وَلاَ قُوَّةٍ، غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))
Amesimulia Mu‘aadh bin Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayekula chakula kisha akasema:
الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي أَطْعَمَنِي هَذَا الطَّعَامَ وَرَزَقَنِيهِ مِنْ غَيْرِ حَوْلٍ مِنِّي وَلاَ قُوَّةٍ
Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Amenilisha chakula hiki na Akaniruzuku bila ya uwezo wangu wala nguvu zangu,
atafutiwa madhambi yake yaliyotangulia.” [Abuu Daawuwd (4023), At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
10-Mwombe Al-Muqiyt Rizki Ya Kutosha:
Omba du’aa, ee ndugu Muislamu, Al-Muqiyt Akuruzuku rizki ya kukutosheleza bila ya kukughafilisha.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiomba rizki ya kutosha bila ya ziada ya kughafilisha:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((اللَّهُمَّ اجْعَلْ رِزْقَ آلِ مُحَمَّدٍ قُوتًا))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema:
اللَّهُمَّ اجْعَلْ رِزْقَ آلِ مُحَمَّدٍ قُوتًا
Yaa Allaah! Jaalia rizki ya ahli wa Muhammad iwe ya kuwatosheleza (kiasi cha haja zao). [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Na Allaah Mjuzi zaidi