Al-Hasiyb: Mwenye Kuhesabu, Mwenye Kutosheleza, Mwenye Kuhifadhi Na Mwenye Kushuhudia
Jina Hili la Allaah limetajwa katika Qur-aan mara tatu: An-Nisaa (4:6), (4:86) na Al-Ahzaab (33:39). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذَا حُيِّيتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا ﴿٨٦﴾
Na mtapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo au yarudisheni hayo hayo. Hakika Allaah daima Ni Mwenye Kuhesabu kila kitu. [An-Nisaa (4:86)]
Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Hasiyb:
1-Ni Mwenye kuwatosheleza Waja Wake katika kila wanachokihitajia, na Mwenye kuwalinda na kila wanachokichukia. Na utoshelezaji Wake huu kwa Waja Wake uko wa aina mbili:
Ya kwanza: Utoshelezaji wa jumla: Ni kwa Waja Wake wote; Amemtosheleza kila kiumbe kwa rizqi na msaada, na Akawaandalia kila aina ya sababu za kuwatosheleza, kuwakinaisha na kuwalisha.
Ya pili: Utoshelezaji mahsusi: Ni kwa Waja Wake wanaompwekesha, wenye kumtakasia ikhlaasw katika ibaada Yake; Huwatosheleza kwa nusura na uangalizi, Huwalinda na kila wanachokichukia, na Huwatosheleza katika mambo yao ya dunia na ya Dini. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّـهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٦٤﴾
Ee Nabiy! Allaah Anakutosheleza wewe pamoja na Waumini waliokufuata. [Al-Anfaal (8:64)]
Yaani Anakutosheleza wewe na Anawatosheleza wafuasi wako; na utoshelezaji huu unakuwa kwa kadiri ya ufuataji. Na mahsusi zaidi ni kwamba Yeye Ndiye Mwenye kumtosheleza anayemtegemea. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾
Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatazamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza Kusudio Lake. Allaah Amejaalia makadirio kwa kila kitu. [Atw-Twalaaq (65:3)]
Yaani Humtosheleza katika mambo yake yote ya Dini na ya dunia, na Humtosheleza asimhitajie kiumbe mwingine yeyote. Na utoshelezaji wa Allaah kwa Mja Wake ni kwa kadiri ya kumfuata kwake Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa dhahiri na kwa siri, na kwa kadiri ya kusimama kwake katika ibaada ya Allaah (تعالى); hapo ndipo hupata utoshelezaji, nguvu na ushindi.1
2-Naye Ndiye Al-Hasiyb, Mwenye kuwahesabu viumbe Wake pindi watakaporejea Kwake kwa matendo yao, na Atawalipa kwa mizani ya haki na uadilifu. Amekihesabu kila kitu kwa hesabu, hakifichiki Kwake kitu wala hakitoki katika Ujuzi Wake, hata kikiwa ni uzito wa punje ya hardali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ ﴿٤٧﴾
Na Tutaweka mizani za uadilifu Siku ya Qiyaamah. Basi nafsi haitodhulumiwa kitu chochote. Na japo ikiwa (amali ina) uzito wa punje ya haradali, Tutaileta. Nasi Tunatosha Kuwa Wadhibiti hesabu. [Al-Anbiyaa (21:47)]
3-Yeye Ndiye Al-Hasiyb Ambaye Anadhibiti idadi ya viumbe Wake, aina zao na yanayowapambanua, na Anadhibiti vipimo vyao na sifa zao, na Anahesabu idadi ya waliokalifishwa katika madaftari Yake mbalimbali.2 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَّقَدْ أَحْصَاهُمْ وَعَدَّهُمْ عَدًّا ﴿٩٤﴾
Kwa hakika Amewadhibiti barabara, na Akawahesabu hesabu ya sawasawa. [Maryam (19:94)]
Na Allaah Anayapambanua matendo mema na maovu, na Anajua kila kinachostahiki malipo na kipimo cha thawabu na adhabu.3
4-Na Allaah (تعالى) Ni Mwepesi zaidi wa kuhisabu kuliko wote wanaohisabu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
ثُمَّ رُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ ۚ أَلَا لَهُ الْحُكْمُ وَهُوَ أَسْرَعُ الْحَاسِبِينَ ﴿٦٢﴾
Kisha watarudishwa (wote waliofishwa) kwa Allaah Rabb wao wa haki. Tanabahi! Hukumu ni Yake Pekee! Naye Ni Mwepesi zaidi wa Kuhisabu kuliko wote wanaohisabu. [Al-An’aam (6:62)]
Hakuna aliye mwepesi zaidi wa kuhesabu matendo ya Waja na ajali zao kuliko Yeye; kwa sababu Yeye Hahesabu kwa kuhitajia idadi wala kwa vidole kama wanavyohesabu wanaohesabu, wala hesabu ya mtu mmoja haimshughulishi na hesabu ya mwingine. Bali Atawahesabu viumbe Wake wote baada ya kuwafufua na kuwakusanya kwa mara moja, kama ambavyo kuwaumba kwao na kuwafufua kwao ni kama nafsi moja tu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَّا خَلْقُكُمْ وَلَا بَعْثُكُمْ إِلَّا كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ ۗ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ ﴿٢٨﴾
Hakukuwa kuumbwa kwenu wala kufufuliwa kwenu isipokuwa ni kama nafsi moja tu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Luqmaan (31:28)]
Kwa ujumla, Jina Hili tukufu limekusanya maana ya kuhesabu, kutosheleza, kuhifadhi na kushuhudia, pamoja na ukamilifu wa ilimu ambao sifa hizo zinaulazimu.
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Hasiyb:
1-Mtegemee Al-Hasiyb Na Useme: حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ
Tambua kwamba Allaah Ni Hasiyb wa kila mmoja na Mwenye kumtosheleza. Wala usidhani kwamba mtoto mchanga anayemhitajia mama yake amnyonyeshe na amtunze kuwa Allaah Si Hasiyb wake wala Si Mwenye kumtosheleza; bali Allaah Amemtosheleza pale Alipomuumba mama yake, Akaumba huruma moyoni mwake juu yake, Akaumba maziwa katika matiti yake na Akamuongoza mtoto kuyanyonya. Basi mtegemee Al-Hasiyb katika mambo yako yote. Na Allaah Amewasifu Waja Wake wanaompwekesha na kumtegemea, ambao walimfanya Yeye Pekee kuwa Mwenye kuwatosheleza, Naye Akawatosheleza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ ﴿١٧٣﴾
Wale walioambiwa na watu: Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni. Lakini hilo liliwazidishia imaan wakasema: Hasbuna-Allaah! (Allaah Anatutosheleza) Mzuri Alioje Mtegemewa. [Aal-‘Imraan (3:173)]
Na maneno haya matukufu yalisemwa na Manabii wawili watukufu katika nyakati za shida kubwa kabisa:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ، قَالَهَا إِبْرَاهِيمُ عَلَيْهِ السَّلاَمُ حِينَ أُلْقِيَ فِي النَّارِ، وَقَالَهَا مُحَمَّدٌ صلى الله عليه وسلم حِينَ قَالُوا: إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):
حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ
“Allaah Anatutosheleza, Naye Ni Mzuri Alioje Mtegemewa” aliyasema Ibraahiym (عليه السّلام) alipotupwa motoni, na aliyasema Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) pale waliposema: “Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni. Lakini hilo liliwazidishia imaan wakasema: ﴿حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ﴾ (Allaah Anatutosheleza, Naye Ni Mzuri Alioje Mtegemewa).” [Al-Bukhaariy]
2-Ridhika Na Alichokupa Al-Hasiyb:
Tambua, ee Mja wa Al-Hasiyb: Allaah (تعالى) Amewalaumu wanafiki ambao Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alipowapa katika swadaqa waliridhika, na alipowanyima walikasirika; na Akabainisha kwamba lau wangeliridhika na Alichowapa Allaah na Rasuli Wake, na wakasema: “Allaah Anatutosheleza”, ingelikuwa bora kwao. Basi ridhika na Alichokugawia Allaah, na mtegemee Yeye Pekee, kwani mwenye kukinai ni tajiri hata akiwa na kidogo. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((قَدْ أَفْلَحَ مَنْ أَسْلَمَ وَرُزِقَ كَفَافًا وَقَنَّعَهُ اللَّهُ بِمَا آتَاهُ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika amefaulu aliyesilimu, akaruzukiwa rizqi ya kumtosheleza, na Allaah Akamkinaisha kwa kile Alichompa.” [Muslim]
3-Mizani Ya Al-Hasiyb Ni Ya Uadilifu, Hakuna Nafsi Itakayodhulumiwa:
Tambua, ee Mja wa Al-Hasiyb: Hakuna amali, hata iwe sawa na chembe ya hardali, itakayoachwa katika hesabu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ ﴿٤٧﴾
Na Tutaweka mizani za uadilifu Siku ya Qiyaamah. Basi nafsi haitodhulumiwa kitu chochote. Na japo ikiwa (amali ina) uzito wa punje ya haradali, Tutaileta. Nasi Tunatosha Kuwa Wadhibiti hesabu. [Al-Anbiyaa (21:47)]
4-Jihesabu Kabla Hujahesabiwa:
Matendo yote ya mwanaadam yamehesabiwa na yamedhibitiwa, hakipotei chochote katika hayo wala hakiongezwi juu yake. Basi ijengee nafsi yako desturi ya kila siku, kwa mfano kabla ya kulala, ya kukaa na kujihesabu (muhaasabah) kwa ukweli; zijue kasoro zako kuu na uweke mpango wa vitendo wa kuzirekebisha, kabla hujasimamishwa kusoma kitabu chako Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا ﴿١٤﴾
(Ataambiwa): Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosheleza leo kukuhesabu. [Al-Israa (17:14)]
5-Jitahidi Upate Hesabu Nyepesi:
Tambua, ee Mja wa Al-Hasiyb: Anayekaziwa hesabu Siku ya Qiyaamah ameangamia; basi mwombe Allaah hesabu nyepesi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لَيْسَ أَحَدٌ يُحَاسَبُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِلاَّ هَلَكَ)). فَقُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَلَيْسَ قَدْ قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: ﴿فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا﴾؟ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّمَا ذَلِكِ الْعَرْضُ، وَلَيْسَ أَحَدٌ يُنَاقَشُ الْحِسَابَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِلاَّ عُذِّبَ))
Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna yeyote atakayehesabiwa Siku ya Qiyaamah isipokuwa ataangamia.” Nikasema: Yaa Rasula-Allaah! Je, Allaah (تعالى) Hakusema: “Basi yule atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atahesabiwa hesabu nyepesi”? Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hakika hiyo ni kuonyeshwa (amali) tu; na hakuna yeyote atakayekaziwa hesabu Siku ya Qiyaamah isipokuwa ataadhibiwa.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
6-Rejea Kwa Al-Hasiyb Kwa Tawbah Haraka:
Tambua, ee Mja wa Al-Hasiyb: Faida kubwa ya kujihesabu ni kutubia; kwani vipi utatubia ikiwa hutambui kwamba umekosea? Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametujulisha fursa adhimu ya kufutiwa kosa kabla halijaandikwa. Basi unapokaribia kutenda dhambi, kumbuka kwamba itaandikwa na utaonyeshwa Siku ya Hesabu; na ukiteleza, harakisha kutubia na kuomba maghfirah.
عَنْ أَبِي أُمَامَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ صَاحِبَ الشِّمَالِ لَيَرْفَعُ الْقَلَمَ سِتَّ سَاعَاتٍ عَنِ الْعَبْدِ الْمُسْلِمِ الْمُخْطِئِ أَوِ الْمُسِيءِ، فَإِنْ نَدِمَ وَاسْتَغْفَرَ اللَّهَ مِنْهَا أَلْقَاهَا، وَإِلاَّ كُتِبَتْ وَاحِدَةً))
Amesimulia Abu Umaamah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika (Malaika) wa upande wa kushoto huinua kalamu (asiandike) kwa muda wa saa sita kwa mja Muislamu aliyekosea au aliyetenda ovu. Akijuta na akamuomba Allaah maghfirah kwa (ovu) hilo, hulitupa; na asipofanya hivyo, huandikwa (ovu) moja.” [Atw-Twabaraaniy, na ameisahihisha Imaam Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (2097) na As-Silsilah Asw-Swahiyhah (3/210)]
Na mlango wa tawbah uko wazi usiku na mchana; basi usiiahirishe tawbah yako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي مُوسَى (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ، وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ، حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا))
Amesimulia Abu Muwsaa (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah (عزّ وجلّ) Hunyoosha Mkono Wake usiku ili atubie aliyetenda maovu mchana, na Hunyoosha Mkono Wake mchana ili atubie aliyetenda maovu usiku, mpaka jua lichomoze kutoka magharibi yake.” [Muslim]
7-Kuwa Mkweli Katika Miamala Yako:
Hata kama watu hawatagundua kwamba hukuwa mkweli katika miamala yako, Al-Hasiyb Ataliongeza katika hesabu yako. Basi kuwa mkweli daima katika kila muamala unaoufanya; kazini, shuleni, na hata katika kugawanya vitu nyumbani baina ya familia yako na watoto wako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ حَكِيمِ بْنِ حِزَامٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الْبَيِّعَانِ بِالْخِيَارِ مَا لَمْ يَتَفَرَّقَا، فَإِنْ صَدَقَا وَبَيَّنَا بُورِكَ لَهُمَا فِي بَيْعِهِمَا، وَإِنْ كَتَمَا وَكَذَبَا مُحِقَتْ بَرَكَةُ بَيْعِهِمَا))
Amesimulia Hakiym bin Hizaam (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Wauzianaji wawili wana khiyari (ya kuvunja mauzo) madamu hawajaachana. Wakisema kweli na wakabainisha (kasoro), watabarikiwa katika mauzo yao; na wakificha na wakasema uongo, baraka ya mauzo yao itafutika.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
8-Itikia Salaam Kwa Iliyo Bora Zaidi:
Al-Hasiyb Anahesabu hata salaam zetu. Ametuamrisha kuitikia maamkizi kwa yaliyo mazuri zaidi au angalau kuyarudisha hayo hayo, kisha Akamalizia Aayah kwa Jina Lake Al-Hasiyb. Rejea juu: An-Nisaa (4:86). Basi Muislamu anapokusalimia, mwitikie kwa salaam iliyo bora zaidi:
وَعَلَيْكُمُ السَّلاَمُ وَرَحْمَةُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُهُ
au angalau kwa mfano wa aliyokusalimia; kwani kuitikia kwa iliyo bora zaidi kunapendekezwa, na kuitikia kwa mfano wake ni waajib. Na ujira wa salaam unazidi kwa kadiri ya ukamilifu wake:
عَنْ عِمْرَانَ بْنِ حُصَيْنٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: جَاءَ رَجُلٌ إِلَى النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فَقَالَ: السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ. فَرَدَّ عَلَيْهِ السَّلاَمَ ثُمَّ جَلَسَ، فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((عَشْرٌ)). ثُمَّ جَاءَ آخَرُ فَقَالَ: السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَةُ اللَّهِ. فَرَدَّ عَلَيْهِ فَجَلَسَ، فَقَالَ: ((عِشْرُونَ)). ثُمَّ جَاءَ آخَرُ فَقَالَ: السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَةُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُهُ. فَرَدَّ عَلَيْهِ فَجَلَسَ، فَقَالَ: ((ثَلاَثُونَ))
Amesimulia ‘Imraan bin Huswayn (رضي الله عنهما): Alikuja mtu kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema:
السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ
Akamrudishia salaam, kisha (mtu yule) akaketi. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Kumi.” Kisha akaja mwingine akasema:
السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَةُ اللَّهِ
Akamrudishia, naye akaketi. Akasema: “Ishirini.” Kisha akaja mwingine akasema:
السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَةُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُهُ
Akamrudishia, naye akaketi. Akasema: “Thelathini.” [Abuu Daawuwd (5195), At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
9-Usimtakase Mtu Yeyote Mbele Ya Allaah:
Ni juu ya mja kumtegemea Allaah katika kila jambo, hata katika kuwatathmini watu; basi usimsifu mtu kwa kukata kauli kana kwamba unayajua ya ndani yake, bali mwachie Al-Hasiyb Ambaye Pekee Anajua hakika ya hali yake:
عَنْ أَبِي بَكْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: أَثْنَى رَجُلٌ عَلَى رَجُلٍ عِنْدَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فَقَالَ: ((وَيْلَكَ قَطَعْتَ عُنُقَ صَاحِبِكَ، قَطَعْتَ عُنُقَ صَاحِبِكَ)) مِرَارًا، ثُمَّ قَالَ: ((مَنْ كَانَ مِنْكُمْ مَادِحًا أَخَاهُ لاَ مَحَالَةَ فَلْيَقُلْ: أَحْسِبُ فُلاَنًا، وَاللَّهُ حَسِيبُهُ، وَلاَ أُزَكِّي عَلَى اللَّهِ أَحَدًا، أَحْسِبُهُ كَذَا وَكَذَا، إِنْ كَانَ يَعْلَمُ ذَلِكَ مِنْهُ))
Amesimulia Abu Bakrah (رضي الله عنه): Mtu mmoja alimsifu mtu mwingine mbele ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), naye akasema: “Ole wako! Umeikata shingo ya mwenzako! Umeikata shingo ya mwenzako!” Akarudia mara kadhaa, kisha akasema: “Yeyote miongoni mwenu ikimlazimu kumsifu ndugu yake, basi aseme: Namdhania fulani (kuwa hivi), na Allaah Ndiye Hasiyb wake, wala simtakasi yeyote mbele ya Allaah; namdhania kuwa hivi na hivi, ikiwa anajua hivyo kutoka kwake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
10-Tarajia Ujira Kutoka Kwa Al-Hasiyb Pekee:
Ihtisaab ni kutafuta ujira kutoka kwa Allaah (تعالى) kwa ikhlaasw. Basi kila unapotenda jema au unapopatwa na msiba, tarajia ujira wako kutoka kwa Al-Hasiyb Pekee, kwani Hapotezi ujira wa wanaofanya ihsaan. Allaah (تعالى) Amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى: مَا لِعَبْدِي الْمُؤْمِنِ عِنْدِي جَزَاءٌ إِذَا قَبَضْتُ صَفِيَّهُ مِنْ أَهْلِ الدُّنْيَا ثُمَّ احْتَسَبَهُ إِلاَّ الْجَنَّةُ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تعالى) Anasema: Mja Wangu Muumini hana malipo Kwangu Ninapomchukua kipenzi chake miongoni mwa watu wa dunia, kisha akavuta subira akitaraji ujira, isipokuwa Jannah.” [Al-Bukhaariy]
Na Allaah Mjuzi zaidi