Al-Muhiytw: Mwenye Kuzunguka Vyote Kwa Ujuzi Wake
Maana ya Al-Muhiytw katika lugha: حَاطَهُ يَحُوطُهُ yaani amekihifadhi na kukitunza. Na kila aliyekimiliki kitu chote, au ujuzi wake ukafikia upeo wake, basi amekizunguka. Na mwenye kukizunguka kitu ni yule aliyekimiliki na kukusanya pande zake zote na nyanja zake zote, kiasi kwamba hakiwezi kujinasua kutoka kwake wala kumponyoka.1
Jina Hili la Allaah limetajwa katika Qur-aan mara nane: Al-Baqarah (2:19), Aal-‘Imraan (3:120), An-Nisaa (4:108) na (4:126), Al-Anfaal (8:47), Huwd (11:92), Fusw-swilat (41:54) na Al-Buruwj (85:20). Miongoni mwa hizo ni Kauli Yake (سبحانه وتعالى):
أَلَا إِنَّهُمْ فِي مِرْيَةٍ مِّن لِّقَاءِ رَبِّهِمْ ۗ أَلَا إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ مُّحِيطٌ ﴿٥٤﴾
Tanabahi! Hakika wao wamo katika shaka ya kukutana na Rabb wao. Tanabahi! Hakika Yeye Amekizunguka kila kitu. [Fusw-swilat (41:54)]
Al-Muhiytw katika haki ya Allaah (تعالى) ni Yule Ambaye Uwezo Wake umewazunguka viumbe Wake wote, na Ambaye Amekizunguka kila kitu kwa Ujuzi Wake, na Amekidhibiti kila kitu kwa idadi. Na Al-Bayhaqiy amesema: Al-Muhiytw ni Yule Ambaye Uwezo Wake umezunguka kila kinachowezekana, na Ujuzi Wake umezunguka kila kinachojulikana.2
Na makusudio ya Allaah kuwazunguka viumbe Wake si kwamba Yeye ni kama duara na viumbe wamo ndani ya Dhati Yake takatifu; Ametakasika Allaah na hilo utakasifu mkubwa. Bali makusudio ni kuzunguka kwa Utukufu Wake, Wasaa Wake, Ujuzi Wake na Uwezo Wake, na kwamba viumbe vyote mbele ya Utukufu Wake ni kama punje ya haradali. Kama ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba amesema:
مَا السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرَضُونَ السَّبْعُ وَمَا فِيهِنَّ وَمَا بَيْنَهُنَّ فِي يَدِ الرَّحْمَنِ إِلَّا كَخَرْدَلَةٍ فِي يَدِ أَحَدِكُمْ
“Mbingu saba na ardhi saba na vilivyomo ndani yake na vilivyo baina yake, katika Mkono wa Ar-Rahmaan si chochote isipokuwa ni kama punje ya haradali katika mkono wa mmoja wenu.” Basi Allaah Yuko juu ya viumbe Wake, Ametengana nao, na wakati huo huo Amewazunguka wote.3
Kwa hiyo, Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Muhiytw kwa namna zifuatazo:
1-Amekizunguka kila kitu kwa Ujuzi Wake: Ujuzi Wake umezunguka vyote vinavyojulikana; vya dhahiri na vya siri, vilivyofichika na vilivyo wazi, vilivyopita, vilivyopo na vitakavyokuja. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ وَمِنَ الْأَرْضِ مِثْلَهُنَّ يَتَنَزَّلُ الْأَمْرُ بَيْنَهُنَّ لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا﴿١٢﴾
Allaah Ni Yule Aliyeumba mbingu saba na katika ardhi mfano wa hizo, inateremka amri baina yao ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu Ni Muweza, na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa Ujuzi (Wake). [Atw-Twalaaq (65:12)]
2-Uwezo Wake umewazunguka viumbe Wake kikamilifu: hawawezi kumshinda, wala kumponyoka, wala kumkimbia; wote wamo katika Mkono Wake, na hawawezi kutoka nje ya Matakwa Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي تَكْذِيبٍ ﴿١٩﴾ وَاللَّـهُ مِن وَرَائِهِم مُّحِيطٌ ﴿٢٠﴾
Bali wale waliokufuru wamo katika kukadhibisha. Na Allaah Amewazunguka (kwa Ujuzi Wake) nyuma yao. [Al-Buruwj (85:19-20)]
3-Rehma Yake imekizunguka kila kitu: ulimwengu wa juu na wa chini na viumbe vyote vimezungukwa na Rehma ya Ar-Rahmaan Ar-Rahiym; Amewamiminia Neema Zake za dhahiri na za siri, na Amewaepushia madhara na yanayochukiza.
4-Malipo Yake yamezunguka matendo yote ya Waja: Ameyadhibiti, Ameyahesabu, Anajua kiwango chake na kiwango cha malipo yake katika kheri na shari, na Atawalipa kwa ukamilifu kwa mujibu wa Uadilifu Wake na Rehma Yake.4
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muhiytw:
1-Al-Muhiytw Amekizunguka Kila Kitu Kwa Ujuzi Wake, Na Dhati Yake Iko Juu Ya ‘Arsh:
Tambua, ee Mja wa Al-Muhiytw: Allaah (سبحانه وتعالى) Amekizunguka kila kitu kwa Ujuzi Wake, Uwezo Wake na Utukufu Wake, si kwa Dhati Yake kuwa ndani ya viumbe. Dhati Yake (سبحانه وتعالى) Iko juu ya mbingu, juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾
Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma) Yuko juu ya ‘Arsh. [Twaahaa (20:5)]
Na Anasema pia kuhusu kuwa Kwake juu ya ‘Arsh pamoja na Ujuzi Wake:
هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٤﴾
Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arsh. Anajua yale yanayoingia ardhini, na yale yatokayo humo, na yale yanayoteremka kutoka mbinguni, na yale yanayopanda humo. Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah Ni Mwenye Kuona yote myatendayo. [Al-Hadiyd (57:4)]
2-Viumbe Hawawezi Kuuzunguka Ujuzi Wa Al-Muhiytw:
Al-Muhiytw Amekizunguka kila kitu, lakini viumbe hawaizunguki ilimu Yake isipokuwa kwa kiasi Anachokitaka. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴿٢٥٥﴾
Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Al-Hayyu (Aliye Hai daima) Al-Qayyuwm (Msimamia kila kitu). Haumchukui usingizi wala kulala. Ni Vyake Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya Idhini Yake? Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kufikia kuelewa chochote kuhusu Ujuzi Wake isipokuwa kwa Alitakalo. Imeenea Kursiyy Yake mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Naye ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Taadhima. [Al-Baqarah (2:255)]
3-Mtukuze Al-Muhiytw Ambaye Hakuna Kinachofichika Kwake:
Kuamini Jina Hili kunazalisha moyoni kumtukuza Allaah (تعالى) na kutambua ukamilifu wa Sifa Zake, na kwamba hakuna kinachofichika Kwake katika ulimwengu wote. Ujuzi Wake umeizunguka punje katika viza vya ardhi na jani linaloanguka, na zaidi ya hayo, vipimo vya bahari, idadi ya matone ya mvua na idadi ya chembe za mchanga. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٥٩﴾
Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghaibu, hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Anajua yale yote yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani lolote ila Hulijua, wala punje katika viza vya ardhi, wala kinyevu na kikavu isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha wazi. [Al-An’aam (6:59)]
4-Usiogope Hila Za Maadui; Al-Muhiytw Amewazunguka:
Hata wakifanya njama makafiri na maadui wa Dini, wakapanga na kudabiri, basi Allaah (تعالى) Amewazunguka, Ni Muweza wa kuzivunja hila zao na kuzuia shari zao. Basi baada ya kuchukua sababu za kujikinga na shari zao, usiziogope nguvu zao; bali shikamana na subira na taqwa, hila zao hazitakudhuru kitu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِن تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا ۖ وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ ﴿١٢٠﴾
Ikikupateni kheri (nusura, ushindi) inawachukiza, na likikusibuni baya hulifurahia. Na kama mtasubiri na mkashikamana na taqwa, basi hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kuyazunguka wayatendayo. [Aal-‘Imraan (3:120)]
5-Al-Muhiytw Amewazunguka Watu Wote, Basi Usiwaogope:
Tambua kwamba Al-Muhiytw Alimhakikishia Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Amewazunguka watu wote, hivyo hakuna atakayemdhuru bila Idhini Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذْ قُلْنَا لَكَ إِنَّ رَبَّكَ أَحَاطَ بِالنَّاسِ ۚ وَمَا جَعَلْنَا الرُّؤْيَا الَّتِي أَرَيْنَاكَ إِلَّا فِتْنَةً لِّلنَّاسِ وَالشَّجَرَةَ الْمَلْعُونَةَ فِي الْقُرْآنِ ۚ وَنُخَوِّفُهُمْ فَمَا يَزِيدُهُمْ إِلَّا طُغْيَانًا كَبِيرًا ﴿٦٠﴾
Na (kumbuka) Tulipokuambia: Hakika Rabb wako Amekwishawazunguka watu. Na Hatukuijaalia ndoto ambayo Tulikuonyesha isipokuwa ni mtihani kwa watu, na mti uliolaaniwa katika Qur-aan. Na Tunawatisha, basi haiwazidishii isipokuwa upindukaji mipaka mkubwa wa kuasi. [Al-Israa (17:60)]
6-Mche Al-Muhiytw Kwa Siri Na Kwa Dhahiri:
Kuamini kwamba Allaah Amekizunguka kila kitu kwa Ujuzi Wake kunapanda moyoni muraaqabah (kujihisi kuchungwa na Allaah) kwa siri na kwa dhahiri. Basi usijifiche kwa watu ukamsahau Ambaye Yu pamoja nawe kwa Ujuzi Wake popote ulipo; bali likuzuie hilo kuasi Amri Zake, na likuhimize kuzifanya vizuri na kuzikamilisha amali zako. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَسْتَخْفُونَ مِنَ النَّاسِ وَلَا يَسْتَخْفُونَ مِنَ اللَّـهِ وَهُوَ مَعَهُمْ إِذْ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرْضَىٰ مِنَ الْقَوْلِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطًا ﴿١٠٨﴾
Wanajificha watu wasiwaone (wakitenda machafu) na wala hawajifichi kwa Allaah (wakamwonea haya), Naye Yu pamoja nao (kwa Ujuzi Wake) pale wanapokesha kupanga makri kwa maneno Asiyoyaridhia. Na Allaah daima Ni Mwenye Kuyazunguka yale wayatendayo. [An-Nisaa (4:108)]
7-Kimbilia Kwa Al-Muhiytw:
Allaah (تعالى) Amewazunguka Waja Wake, hawawezi kumponyoka wala kumkimbia; bali hakuna pa kukimbilia kutoka Kwake isipokuwa Kwake. Kila kitu unachokiogopa hukikimbia, isipokuwa Allaah (تعالى); kwani wewe unamkimbilia Yeye. Basi mkimbilie kwa tawbah, kwa ibaada na kwa kumtegemea katika kila jambo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَفِرُّوا إِلَى اللَّـهِ ۖ إِنِّي لَكُم مِّنْهُ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٥٠﴾
Basi kimbilieni kwa Allaah. Hakika mimi kwenu ni mwonyaji bayana kutoka Kwake. [Adh-Dhaariyaat (51:50)]
8-Usimdhulumu Yeyote:
Mja anapotafakari Jina la Allaah Al-Muhiytw, na yaliyomo ndani yake ya Ujuzi wa Allaah kuzunguka matendo yake yote na Uwezo Wake kumzunguka, huogopa kumdhulumu mtu yeyote au kumfanyia uadui kwa kauli, kwa kitendo au kwa kumdhania vibaya. Na ukumbusho wa Uwezo huu unaozunguka kila kitu humzuia mja kudanganyika na uwezo wake juu ya watu na kuwadhulumu; kwani Uwezo wa Allaah uko juu ya uwezo wake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((اتَّقُوا الظُّلْمَ فَإِنَّ الظُّلْمَ ظُلُمَاتٌ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ...))
Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Iogopeni dhulma, kwani dhulma ni viza Siku ya Qiyaamah ...” [Muslim]
9-Tarajia Rehma Ya Al-Muhiytw Iliyokizunguka Kila Kitu:
Tambua kwamba Rehma ya Al-Muhiytw imewazunguka viumbe duniani, na itawazunguka Aakhirah kwa ukubwa zaidi. Basi usikate tamaa na Rehma Yake, na zidisha kumtii ili uwe miongoni mwa watakaorehemewa kwa Rehma Zake Siku ya Qiyaamah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ لِلَّهِ مِائَةَ رَحْمَةٍ، أَنْزَلَ مِنْهَا رَحْمَةً وَاحِدَةً بَيْنَ الْجِنِّ وَالإِنْسِ وَالْبَهَائِمِ وَالْهَوَامِّ، فَبِهَا يَتَعَاطَفُونَ، وَبِهَا يَتَرَاحَمُونَ، وَبِهَا تَعْطِفُ الْوَحْشُ عَلَى وَلَدِهَا، وَأَخَّرَ اللَّهُ تِسْعًا وَتِسْعِينَ رَحْمَةً يَرْحَمُ بِهَا عِبَادَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ana Rehma mia; Ameteremsha moja kati ya hizo baina ya majini, wanaadam, wanyama na wadudu. Kwa hiyo (Rehma moja) wanahurumiana, kwa hiyo wanarehemeana, na kwa hiyo mnyama mwitu humhurumia mtoto wake. Na Allaah Ameakhirisha Rehma tisini na tisa ambazo kwazo Atawarehemu Waja Wake Siku ya Qiyaamah.” [Muslim]
10-Omba Hifadhi Ya Al-Muhiytw Kutoka Pande Zote:
Ukitambua kwamba Allaah Ndiye Al-Muhiytw Aliyekuzunguka kutoka kila upande, basi muombe Yeye Akuhifadhi kutoka pande zote; kama alivyokuwa akifanya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kila asubuhi na jioni:
عَنِ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ: لَمْ يَكُنْ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَدَعُ هَؤُلاَءِ الدَّعَوَاتِ حِينَ يُمْسِي وَحِينَ يُصْبِحُ: ((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ فِي دِينِي وَدُنْيَايَ وَأَهْلِي وَمَالِي، اللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي وَآمِنْ رَوْعَاتِي، اللَّهُمَّ احْفَظْنِي مِنْ بَيْنِ يَدَيَّ وَمِنْ خَلْفِي وَعَنْ يَمِينِي وَعَنْ شِمَالِي وَمِنْ فَوْقِي، وَأَعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أَنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحْتِي))
Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa akiziacha du’aa hizi anapoingia jioni na anapoingia asubuhi:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ فِي دِينِي وَدُنْيَايَ وَأَهْلِي وَمَالِي، اللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي وَآمِنْ رَوْعَاتِي، اللَّهُمَّ احْفَظْنِي مِنْ بَيْنِ يَدَيَّ وَمِنْ خَلْفِي وَعَنْ يَمِينِي وَعَنْ شِمَالِي وَمِنْ فَوْقِي، وَأَعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أَنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحْتِي
Yaa Allaah, hakika mimi nakuomba afya njema duniani na Aakhirah. Yaa Allaah, hakika mimi nakuomba msamaha na afya njema katika Dini yangu, dunia yangu, ahli zangu na mali yangu. Yaa Allaah, sitiri aibu zangu na nitulize khofu zangu. Yaa Allaah, nihifadhi kutoka mbele yangu, nyuma yangu, kuliani mwangu, kushotoni mwangu na juu yangu, na najikinga kwa Utukufu Wako nisiangamizwe kwa ghafla kutoka chini yangu. [Abuu Daawuwd (5074), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
Na Allaah Mjuzi zaidi