Ar-Raqiyb: Mwenye Kuchunga, Mwenye Kuhifadhi Na Mwenye Kuangalia Kwa Makini
Ar-Raqiyb ni Mwenye kuchunga, Mwenye kusifika kwa kuchunga na kuhifadhi, na kuangalia kwa makini na hadhari. Jina Hili la Allaah limetajwa katika Qur-aan mara tatu: An-Nisaa (4:1), Al-Maaidah (5:117) na Al-Ahzaab (33:52). Miongoni mwa hizo ni Kauli Yake (سبحانه وتعالى) kuhusu Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام):
مَا قُلْتُ لَهُمْ إِلَّا مَا أَمَرْتَنِي بِهِ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ ۚ وَكُنتُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا مَّا دُمْتُ فِيهِمْ ۖ فَلَمَّا تَوَفَّيْتَنِي كُنتَ أَنتَ الرَّقِيبَ عَلَيْهِمْ ۚ وَأَنتَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿١١٧﴾
Sijawaambia (lolote) ila yale tu Uliyoniamrisha kwamba: Mwabuduni Allaah Rabb wangu na Rabb wenu. Na nilikuwa juu yao shahidi wakati nilipokuwa nao. Uliponikamilishia muda Ukanichukua juu, Ulikuwa Wewe Ndiye Mwangalizi juu yao. Na Wewe Ni Mwenye Kushuhudia kila kitu. [Al-Maaidah (5:117)]
Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Ar-Raqiyb: Mwenye kuangalia yaliyomo ndani ya dhamira za watu na yaliyofichika, Mwenye kuhesabu kila dogo na kubwa; hakifichiki Kwake chochote kilichomo ardhini wala mbinguni, Naye Ndiye Msimamizi wa kila nafsi na ilichokichuma.
Na Yeye (تعالى) Ni Ar-Raqiyb, na hii ni katika Sifa za Dhati Yake (Swifaat Adh-Dhaatiyyah); kwani kuchunga kunarejea katika maana ya ujuzi, kuhifadhi, kudiriki, kuangalia na kutoghafilika. Na hizi ni maana tukufu ambazo haiwezekani Allaah (تعالى) Asifike nazo wakati fulani na Asisifike nazo wakati mwingine; bali Amesifika nazo daima.
Na hakika mtu mwenye yakini kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anamchunga, umri wake haupotei bure, wala haghafiliki katika matumizi ya wakati wake; bali huunganisha usiku wake na mchana wake katika kumtii Rabb wake. Na mwenye kumchunga Allaah kwa siri na kwa dhahiri, na akamcha katika Maamrisho Yake na Makatazo Yake, Allaah Atamuwafikisha katika njia za muamala mwema na daraja za juu za ilimu ya nyoyo, hadi asione chochote isipokuwa Yeye. Na mwenye kumchunga Allaah huacha makatazo kwa kumwonea haya Allaah zaidi kuliko wale wanaoogopa kumuasi kwa sababu ya Adhabu Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَمْ يَعْلَم بِأَنَّ اللَّـهَ يَرَىٰ ﴿١٤﴾
Je, hajui kwamba hakika Allaah Anaona? [Al-‘Alaq (96:14)]
Na mwenye kujua kwamba Allaah Anamuona wakati yeye hamuoni, basi ni vizuri itikadi hii iwe naye daima, kwa kadiri ya kuogopa kwake kuonwa na Allaah. Na hili ndilo daraja la ihsaan ambalo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliliueleza alipoulizwa na Jibriyl (عليه السّلام):
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) ... قَالَ: مَا الإِحْسَانُ؟ قَالَ: ((أَنْ تَعْبُدَ اللَّهَ كَأَنَّكَ تَرَاهُ، فَإِنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فَإِنَّهُ يَرَاكَ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): ... (Jibriyl) akasema: Ihsaan ni nini? (Rasuli wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ni kumwabudu Allaah kana kwamba unamwona, na ikiwa wewe humwoni, basi hakika Yeye Anakuona.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ar-Raqiyb:
1-Ar-Raqiyb Amewaweka Malaika Wanaoandika Kila Neno:
Tambua, ee Mja wa Ar-Raqiyb: Pamoja na Uchunguzi wa Allaah, kuna Malaika waandishi wanaochunga kila tamko. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ﴿١٧﴾ مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾
Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika) wanaokaa kuliani na kushotoni. Hatamki kauli yoyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf (50:17-18)]
2-Ar-Raqiyb Ndiye Mchunguzi Wa Kweli Hata Kwa Manabii Na Ummah Zao:
Tambua kwamba Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) atasema Siku ya Qiyaamah kwamba baada ya kufishwa kwake, Ar-Raqiyb Ndiye Aliyekuwa Mchunguzi wa watu wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَا قُلْتُ لَهُمْ إِلَّا مَا أَمَرْتَنِي بِهِ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ ۚ وَكُنتُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا مَّا دُمْتُ فِيهِمْ ۖ فَلَمَّا تَوَفَّيْتَنِي كُنتَ أَنتَ الرَّقِيبَ عَلَيْهِمْ ۚ وَأَنتَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿١١٧﴾
Sijawaambia (lolote) ila yale tu Uliyoniamrisha kwamba: Mwabuduni Allaah Rabb wangu na Rabb wenu. Na nilikuwa juu yao shahidi wakati nilipokuwa nao. Uliponikamilishia muda Ukanichukua juu, Ulikuwa Wewe Ndiye Mwangalizi juu yao. Na Wewe Ni Mwenye Kushuhudia kila kitu. [Al-Maaidah (5:117)]
3-Tambua Kwamba Ar-Raqiyb Anachunga Moyo Wako Na Matendo Yako:
Ar-Raqiyb Anachunga si dhahiri yako tu, bali pia yaliyomo moyoni mwako ya nia, ikhlaasw na hisia. Basi usijishughulishe na kupamba sura yako mbele ya watu huku ukiusahau moyo wako unaochungwa na Allaah; bali utakase moyo wako na ufanye matendo yako kuwa mema. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلَى صُوَرِكُمْ وَأَمْوَالِكُمْ، وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ وَأَعْمَالِكُمْ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Haangalii sura zenu wala mali zenu, lakini Anaangalia nyoyo zenu na matendo yenu.” [Muslim]
4-Je, Hajui Kwamba Allaah Anaona?
Tambua, ee Mja wa Ar-Raqiyb: Swali hili lilitosha kumkemea aliyemzuia mja kuswali; na linatosha kumzuia kila anayekusudia maasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَمْ يَعْلَم بِأَنَّ اللَّـهَ يَرَىٰ ﴿١٤﴾
Je, hajui kwamba hakika Allaah Anaona? [Al-‘Alaq (96:14)]
5-Mche Ar-Raqiyb Popote Ulipo:
Kwa kuwa Ar-Raqiyb Anakuchunga kila mahali na kila wakati, basi mche Yeye popote ulipo; peke yako au mbele ya watu, nyumbani au safarini. Na ukiteleza, lifuatishe ovu kwa jema lilifute. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((اتَّقِ اللَّهِ حَيْثُمَا كُنْتَ، وَأَتْبِعِ السَّيِّئَةَ الْحَسَنَةَ تَمْحُهَا، وَخَالِقِ النَّاسَ بِخُلُقٍ حَسَنٍ))
Amesimulia Abu Dharr (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniambia: “Mche Allaah popote ulipo, na lifuatishe ovu kwa jema litalifuta, na ishi na watu kwa tabia njema.” [At-Tirmidhiy (1987), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
6-Jihadhari Na Madhambi Ya Faragha:
Muumini anayejua kwamba Ar-Raqiyb Anamchunga hamfanyi Allaah kuwa ni mwepesi zaidi wa kuangaliwa kuliko watu; akiwa peke yake hufanya kama anavyofanya mbele ya watu. Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametutahadharisha na wale wanaovunja Makatazo ya Allaah wanapokuwa faragha:
عَنْ ثَوْبَانَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ قَالَ: ((لأَعْلَمَنَّ أَقْوَامًا مِنْ أُمَّتِي يَأْتُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِحَسَنَاتٍ أَمْثَالِ جِبَالِ تِهَامَةَ بِيضًا، فَيَجْعَلُهَا اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ هَبَاءً مَنْثُورًا)). قَالَ ثَوْبَانُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، صِفْهُمْ لَنَا، جَلِّهِمْ لَنَا، أَنْ لاَ نَكُونَ مِنْهُمْ وَنَحْنُ لاَ نَعْلَمُ. قَالَ: ((أَمَا إِنَّهُمْ إِخْوَانُكُمْ وَمِنْ جِلْدَتِكُمْ، وَيَأْخُذُونَ مِنَ اللَّيْلِ كَمَا تَأْخُذُونَ، وَلَكِنَّهُمْ أَقْوَامٌ إِذَا خَلَوْا بِمَحَارِمِ اللَّهِ انْتَهَكُوهَا))
Amesimulia Thawbaan (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Nawajua watu miongoni mwa ummah wangu watakaokuja Siku ya Qiyaamah na mema mfano wa milima ya Tihaamah, meupe, lakini Allaah (عزّ وجلّ) Atayafanya kuwa ni vumbi lililotawanyika.” Thawbaan akasema: Yaa Rasula-Allaah! Tueleze sifa zao, na utubainishie ili tusiwe miongoni mwao nasi hatujui. Akasema: “Ama hakika wao ni ndugu zenu, na ni wa jinsi yenu, na wanachukua (sehemu ya ibaada) ya usiku kama mnavyochukua nyinyi, lakini wao ni watu ambao wanapokuwa faragha na makatazo ya Allaah huyavunja.” [Ibn Maajah, na ameisahihisha Imaam Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (505)]
7-Mdhukuru Ar-Raqiyb Ukiwa Peke Yako Mpaka Macho Yako Yatokwe Na Machozi:
Tambua kwamba miongoni mwa watu saba watakaofunikwa na kivuli cha Ar-Raqiyb Siku isiyo na kivuli isipokuwa Chake:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمُ اللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لاَ ظِلَّ إِلاَّ ظِلُّهُ ... وَرَجُلٌ ذَكَرَ اللَّهَ خَالِيًا فَفَاضَتْ عَيْنَاهُ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu saba Allaah Atawafunika kwa kivuli Chake Siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa kivuli Chake: … na mtu aliyemdhukuru Allaah akiwa peke yake, macho yake yakatokwa na machozi.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
8-Chunga Ulimi Wako:
Kila neno unalolitamka linaandikwa na Malaika aliyewekwa kukuchunga. Basi kumbuka kwamba Ar-Raqiyb Amekuwekea wachungaji, na pima maneno yako kabla ya kuyatamka; sema la kheri au nyamaza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ ﴿١٨﴾
Hatamki kauli yoyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf (50:18)]
9-Chunga Haki Za Jamaa Zako:
Allaah (تعالى) Ametuamrisha kumcha Yeye na kuunga undugu, kisha Akamalizia Aayah kwa Jina Lake Ar-Raqiyb; ili tujue kwamba Anatuchunga katika namna tunavyowatendea jamaa zetu. Basi waunge jamaa zako, watendee wema na usiwakate. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا ﴿١﴾
Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana (haki zenu kwa kuunga) undugu. Hakika Allaah daima Ni Mwenye Kuwachungeni. [An-Nisaa (4:1)]
10-Chunga Wakati Wako:
Mwenye yakini kwamba Ar-Raqiyb Anamchunga hapotezi umri wake bure; bali hujaza wakati wake kwa yanayomridhisha Allaah. Basi tumia afya yako na faragha yako kabla havijaondoka. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((نِعْمَتَانِ مَغْبُونٌ فِيهِمَا كَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ: الصِّحَّةُ وَالْفَرَاغُ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Neema mbili ambazo watu wengi wamehadaika nazo: afya na faragha (wakati wa kuwa huru).” [Al-Bukhaariy]
Na Allaah Mjuzi zaidi