Al-Majiyd: Mwenye Utukufu Kamili
Al-Majiyd ni Yule Ambaye Anastahiki fahari, ukarimu, utukufu na hadhi ya juu mbinguni na ardhini. Jina Hili la Allaah limetajwa katika Qur-aan mara mbili: Huwd (11:73) na Al-Buruwj (85:15). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالُوا أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۖ رَحْمَتُ اللَّـهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ ۚ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَّجِيدٌ ﴿٧٣﴾
(Malaika) wakasema: Je, unastaajabia Amri ya Allaah? Rehma ya Allaah na Baraka Zake ziko juu yenu enyi ahli wa nyumba (ya Nabiy Ibraahiym). Hakika Yeye Ni Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa, Mwenye Utukufu kamili na Enzi. [Huwd (11:73)]
Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):
ذُو الْعَرْشِ الْمَجِيدُ ﴿١٥﴾
Mwenye Arsh, Al-Majiyd. [Al-Buruwj (85:15)]
Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Majiyd: Ambaye Ukarimu Wake hauna kikomo, Ambaye hakuna ukarimu ulio juu ya Ukarimu Wake, Mtoaji kwa wingi Ambaye utoaji Wake hauna mwisho wala haukatiki.
Yeye Ni Mwenye enzi Asiyeshindika wala Asiyefikiwa, Ameitukuza Nafsi Yake kwa Ukamilifu Wake na Ukubwa Wake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesimulia kwamba Allaah Hujitukuza Mwenyewe:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَرَأَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) هَذِهِ الْآيَةَ وَهُوَ عَلَى الْمِنْبَرِ: ﴿وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴾ قَالَ: ((يَقُولُ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ: أَنَا الْجَبَّارُ، أَنَا الْمُتَكَبِّرُ، أَنَا الْمَلِكُ، أَنَا الْمُتَعَالِي، يُمَجِّدُ نَفْسَهُ)). قَالَ: فَجَعَلَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يُرَدِّدُهَا حَتَّى رَجَفَ بِهِ الْمِنْبَرُ، حَتَّى ظَنَنَّا أَنَّهُ سَيَخِرُّ بِهِ
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliisoma Aayah hii akiwa juu ya minbar: “Na mbingu zitakunjwa kwa Mkono Wake wa kulia. Utakasifu ni Wake, na Ametukuka kutokana na yale yote wanayomshirikisha nayo.” Akasema: “Allaah (عزّ وجلّ) Anasema: Mimi Ni Al-Jabbaar, Mimi Ni Al-Mutakabbir, Mimi Ni Al-Malik, Mimi Ni Al-Muta’aaliy; Anaitukuza Nafsi Yake.” (Ibn ‘Umar) akasema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa anayarudia (maneno hayo) mpaka minbar ikatetemeka, hadi tukadhani kwamba itaanguka naye. [Ahmad (5608), na Ahmad Shaakir ameisahihisha isnaad yake (5/138)]
Na Yeye (تعالى) Yuko katika upeo wa juu kabisa wa utukufu na hadhi kamilifu katika kila ukamilifu, na katika hilo ni upana wa Ufalme Wake na Mamlaka Yake. Kwani Kursiy Yake, kama ilivyothibiti kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما), amesema:
الْكُرْسِيُّ مَوْضِعُ الْقَدَمَيْنِ، وَالْعَرْشُ لَا يَقْدِرُ قَدْرَهُ إِلَّا اللَّهُ
“Kursiy ni mahali pa Nyayo Mbili, na ‘Arsh hakuna anayeweza kukadiria ukubwa wake isipokuwa Allaah.”1 Na ukubwa wa Kursiy hiyo ni kwamba imeenea mbingu na ardhi, kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴿٢٥٥﴾
Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Al-Hayyu (Aliye Hai daima) Al-Qayyuwm (Msimamia kila kitu). Haumchukui usingizi wala kulala. Ni Vyake Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya Idhini Yake? Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kufikia kuelewa chochote kuhusu Ujuzi Wake isipokuwa kwa Alitakalo. Imeenea Kursiyy Yake mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Naye ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Taadhima. [Al-Baqarah (2:255)]
Ikiwa hii ndiyo hali ya Kursiy, kwamba imeenea mbingu na ardhi kwa ukubwa wake, na Kursiy si kiumbe kikubwa kabisa cha Allaah; bali kuna kilicho kikubwa zaidi kuliko hiyo, nacho ni ‘Arsh. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَا السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ فِي الْكُرْسِيِّ إِلاَّ كَحَلْقَةٍ مُلْقَاةٍ بِأَرْضٍ فَلاَةٍ، وَفَضْلُ الْعَرْشِ عَلَى الْكُرْسِيِّ كَفَضْلِ تِلْكَ الْفَلاَةِ عَلَى تِلْكَ الْحَلْقَةِ))
Amesimulia Abu Dharr (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hazikuwa mbingu saba ndani ya Kursiy isipokuwa ni kama pete iliyotupwa katika ardhi ya jangwa, na ubora wa ‘Arsh juu ya Kursiy ni kama ubora wa jangwa hilo juu ya pete hiyo.” [Ameisahihisha Imaam Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (109)]
Kwa ukubwa wa viumbe hivi akili zinatahayari na macho yanashindwa kuona; basi itakuwaje kuhusu Ukubwa wa Muumba Mwenyewe na Uzuri Wake, Ametukuka!2
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Majiyd:
1-Al-Majiyd Ni Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa, Mwenye Utukufu Kamili:
Jina Al-Majiyd limekuja pamoja na Al-Hamiyd katika maamkizi ya Malaika kwa ahli wa nyumba ya Nabiy Ibraahiym (عليه السلام). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالُوا أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۖ رَحْمَتُ اللَّـهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ ۚ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَّجِيدٌ﴿٧٣﴾
(Malaika) wakasema: Je, unastaajabia Amri ya Allaah? Rehma ya Allaah na Baraka Zake ziko juu yenu enyi ahli wa nyumba (ya Nabiy Ibraahiym). Hakika Yeye Ni Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa, Mwenye Utukufu kamili na Enzi. [Huwd (11:73)]
2-Al-Majiyd Ni Mwenye ‘Arsh Tukufu, Mtendaji Wa Ayatakayo:
Tambua, ee Mja wa Al-Majiyd: Utukufu wa Allaah umeambatana na Maghfirah Yake, Mapenzi Yake kwa waja, na Uwezo Wake kamili. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَهُوَ الْغَفُورُ الْوَدُودُ ﴿١٤﴾ ذُو الْعَرْشِ الْمَجِيدُ ﴿١٥﴾ فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ ﴿١٦﴾
Naye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Upendo halisi. Mwenye ‘Arsh, Al-Majiyd. Mwingi wa Kufanya Atakalo, hakuna wa kumzuia. [Al-Buruwj (85:14-16)]
3-Tafakari Uumbaji Wa Al-Majiyd:
Alama za Utukufu wa Allaah zinaonekana kila mahali kutuzunguka; ulimwengu wote na vyote vilivyomo kwa ajili ya manufaa yetu ni dhihirisho la Ukubwa na Ukarimu wa Al-Majiyd. Unapopitia shida na mitihani, tazama kukuzunguka na utambue kwamba ni Al-Majiyd Ambaye Husema: Kuwa! Nacho kinakuwa. Na kama Alivyoumba kila kitu kilicho nje yako na ndani yako kwa ukamilifu, basi kwa hakika Anaweza kukupa njia ya kutoka katika matatizo yako. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا ۖ مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ ۖ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ﴿٣﴾
Ambaye Ameumba mbingu saba matabaka. Hutaona katika Uumbaji wa Ar-Rahmaan tofauti yoyote. Basi rejesha jicho. Je, unaona mpasuko wowote ule? [Al-Mulk (67:3)]
4-Fuata Kitabu Cha Al-Majiyd:
Tambua, ee Mja wa Al-Majiyd, kwamba wewe ni mja wa Aliye Mkamilifu; basi fuata Kitabu Chake, jisalimishe kwa Amri Zake na jiepushe na Makatazo Yake. Jifunze kuisoma Qur-aan, kuielewa na kuishi kwa mujibu wake, ili ujiongezee utukufu na heshima. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ يَرْفَعُ بِهَذَا الْكِتَابِ أَقْوَامًا وَيَضَعُ بِهِ آخَرِينَ))
Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Huwanyanyua kwa Kitabu hiki watu fulani, na Huwashusha kwacho wengine.” [Muslim]
5-Mtukuze Al-Majiyd Katika Kila Rakaa Unaposoma Al-Faatihah:
Tambua, ee Mja wa Al-Majiyd: Katika Hadiyth Al-Qudsiy kuhusu kugawanywa kwa Swalaah (Al-Faatihah) baina ya Allaah na Mja Wake:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: قَسَمْتُ الصَّلاَةَ بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي نِصْفَيْنِ ... وَإِذَا قَالَ: ﴿مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ﴾ قَالَ: مَجَّدَنِي عَبْدِي))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تعالى) Amesema: Nimeigawa Swalaah baina Yangu na Mja Wangu nusu mbili … Na anaposema: ‘Maaliki wa Siku ya Malipo’, (Allaah) Husema: Mja Wangu Amenitukuza.” [Muslim]
6-Mhimidi Na Umtukuze Al-Majiyd Daima:
Mwonyeshe Allaah kwamba unashukuru kwa Neema Zake juu yako, na mhimidi kwa Ukamilifu Wake. Abu Hamzah Al-Baghdaadiy amesema: Haiwezekani udai kwamba unampenda Allaah na usimdhukuru daima; na haiwezekani umdhukuru Allaah daima na usione utamu wa hilo katika maisha haya; na haiwezekani uone utamu wa kumdhukuru Allaah kisha ushughulishwe na kisichokuwa Yeye. Na kutomdhukuru Allaah isipokuwa kidogo ni katika alama za wanafiki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٤٢﴾
Hakika wanafiki (wanadhani) wanamhadaa Allaah, na hali Yeye (Allaah) Ndiye Mwenye kuwahadaa. Na wanaposimama kuswali husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamdhukuru Allaah isipokuwa kidogo tu. [An-Nisaa (4:142)]
Na hakuna udhuru wa kuacha kumdhukuru Al-Majiyd katika hali yoyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾
Mtakapomaliza Swalaah, mdhukuruni Allaah mkiwa wima, mmeketi, au mmejinyoosha. Na mtakapopata utulivu, basi simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekewa nyakati maalumu. [An-Nisaa (4:103)]
7-Watendee Wengine Kwa Heshima Na Ukarimu:
Iache sifa ya utukufu na Ukarimu ya Al-Majiyd ikufungue moyo wako, na uwatendee wengine kwa msamaha na subira. Zungumza na watu kwa upole, watabasamie, na wasaidie kupatana wanapogombana. Toa katika neema ya mali yako kuwasaidia wasiojaaliwa, na pamoja na kutoa kwako kuwa mnyenyekevu na mpole kwao. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((تَبَسُّمُكَ فِي وَجْهِ أَخِيكَ لَكَ صَدَقَةٌ ...))
Amesimulia Abu Dharr (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kutabasamu kwako mbele ya uso wa ndugu yako ni swadaqa kwako ...” [At-Tirmidhiy (1956), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
8-Mtukuze Al-Majiyd Unapoinuka Kutoka Rukuu:
Mtukuze Al-Majiyd unapoinuka kutoka Rukuu kwa maneno haya ya kumhimidi.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema anapoinua kichwa chake kutoka Rukuu:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) إِذَا رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ الرُّكُوعِ قَالَ: ((رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ، مِلْءَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، وَمِلْءَ مَا شِئْتَ مِنْ شَيْءٍ بَعْدُ، أَهْلَ الثَّنَاءِ وَالْمَجْدِ، أَحَقُّ مَا قَالَ الْعَبْدُ، وَكُلُّنَا لَكَ عَبْدٌ: اللَّهُمَّ لاَ مَانِعَ لِمَا أَعْطَيْتَ، وَلاَ مُعْطِيَ لِمَا مَنَعْتَ، وَلاَ يَنْفَعُ ذَا الْجَدِّ مِنْكَ الْجَدُّ))
Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapoinua kichwa chake kutoka Rukuu husema:
رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ، مِلْءَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، وَمِلْءَ مَا شِئْتَ مِنْ شَيْءٍ بَعْدُ، أَهْلَ الثَّنَاءِ وَالْمَجْدِ، أَحَقُّ مَا قَالَ الْعَبْدُ، وَكُلُّنَا لَكَ عَبْدٌ: اللَّهُمَّ لاَ مَانِعَ لِمَا أَعْطَيْتَ، وَلاَ مُعْطِيَ لِمَا مَنَعْتَ، وَلاَ يَنْفَعُ ذَا الْجَدِّ مِنْكَ الْجَدُّ
Rabb wetu! Himdi ni Zako, kiasi cha kujaza mbingu na ardhi, na kujaza chochote Utakacho baada ya hapo. Yaa Mwenye kustahiki kusifiwa na kutukuzwa! Hayo ndiyo ya haki zaidi aliyoyasema mja, na sote ni Waja Wako. Yaa Allaah! Hakuna wa kuzuia Ulichokitoa, wala hakuna wa kutoa Ulichokizuia, wala haumnufaishi mwenye utajiri (au cheo) utajiri wake mbele Yako. [Muslim]
9-Hifadhi Du’aa Ya Kufungulia Swalaah Na Uishi Kwayo:
Maneno haya ya kufungulia Swalaah yanakusanya kumtukuza Al-Majiyd, kumhimidi na kumtakasa kwa namna nzuri kabisa:
عَنِ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ: بَيْنَمَا نَحْنُ نُصَلِّي مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) إِذْ قَالَ رَجُلٌ مِنَ الْقَوْمِ: اللَّهُ أَكْبَرُ كَبِيرًا، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ كَثِيرًا، وَسُبْحَانَ اللَّهِ بُكْرَةً وَأَصِيلاً. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنِ الْقَائِلُ كَلِمَةَ كَذَا وَكَذَا؟)) قَالَ رَجُلٌ مِنَ الْقَوْمِ: أَنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ. قَالَ: ((عَجِبْتُ لَهَا، فُتِحَتْ لَهَا أَبْوَابُ السَّمَاءِ)). قَالَ ابْنُ عُمَرَ: فَمَا تَرَكْتُهُنَّ مُنْذُ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ ذَلِكَ
Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Tulipokuwa tukiswali pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), mtu mmoja miongoni mwa watu alisema:
اللَّهُ أَكْبَرُ كَبِيرًا، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ كَثِيرًا، وَسُبْحَانَ اللَّهِ بُكْرَةً وَأَصِيلاً
Allaah Ni Mkubwa zaidi kwa ukubwa kamili, na Himdi Anastahiki Allaah kwa wingi, na Utakasifu ni wa Allaah asubuhi na jioni.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Nani aliyesema maneno kadhaa na kadhaa?” Mtu mmoja miongoni mwa watu akasema: Ni mimi, yaa Rasula-Allaah. Akasema: “Nimeyastaajabia! Imefunguliwa milango ya mbingu kwa ajili yake.” Ibn ‘Umar akasema: Sijayaacha tangu nilipomsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema hivyo. [Muslim]
Na maana ya سُبْحَانَ اللَّهِ ni: Allaah Ametakasika na kila aibu, kila upungufu na kila kasoro.
10-Mswalie Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Kwa Swalaah Inayomalizika Kwa Jina Hili:
Kumbuka kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Swalaah ya Ibraahiymiyyah inayomalizika kwa Jina Al-Majiyd.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametufundisha kumswalia kwa Swalaah inayomalizika kwa kumtaja Allaah kwa Majina Yake mawili: Al-Hamiyd na Al-Majiyd; kama yalivyokuja pamoja katika Huwd (11:73). Rejea juu.
عَنْ كَعْبِ بْنِ عُجْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَأَلْنَا رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) فَقُلْنَا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، كَيْفَ الصَّلاَةُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ، فَإِنَّ اللَّهَ قَدْ عَلَّمَنَا كَيْفَ نُسَلِّمُ؟ قَالَ: ((قُولُوا: اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ، اللَّهُمَّ بَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا بَارَكْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ))
Amesimulia Ka’b bin ‘Ujrah (رضي الله عنه): Tulimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) tukasema: Yaa Rasula-Allaah! Vipi (tuwaswalie) Swalaah nyinyi Ahlul-Bayt, kwani Allaah Ametufundisha namna ya kusalimia? Akasema: “Semeni:
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ، اللَّهُمَّ بَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا بَارَكْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ
Yaa Allaah! Msalie Muhammad na ahli za Muhammad kama Ulivyomswalia Ibraahiym na ahli za Ibraahiym, hakika Wewe Ni Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa, Mwenye Utukufu. Yaa Allaah! Mbariki Muhammad na ahli za Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na ahli za Ibraahiym, hakika Wewe Ni Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa, Mwenye Utukufu.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Na Allaah Mjuzi zaidi