Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 067 kati ya 103
Ash-Shaafiy — Majina Mazuri ya Allaah

Ash-Shaafiy: Mwenye Kuponyesha

Jina Hili la Allaah limethibiti katika Sunnah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa akimtembelea mgonjwa au akiletewa mgonjwa alikuwa akisema:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ إِذَا أَتَى مَرِيضًا أَوْ أُتِيَ بِهِ قَالَ: ((أَذْهِبِ الْبَاسَ رَبَّ النَّاسِ، اشْفِ وَأَنْتَ الشَّافِي، لاَ شِفَاءَ إِلاَّ شِفَاؤُكَ، شِفَاءً لاَ يُغَادِرُ سَقَمًا))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapomjia mgonjwa au akiletewa mgonjwa husema:

أَذْهِبِ الْبَاسَ رَبَّ النَّاسِ، اشْفِ وَأَنْتَ الشَّافِي، لاَ شِفَاءَ إِلاَّ شِفَاؤُكَ، شِفَاءً لاَ يُغَادِرُ سَقَمًا

Ondosha dhara Yaa Rabb wa watu, ponyesha, Wewe Ndiye Ash-Shaafiy (Mponyeshaji), hakuna ponyo isipokuwa ponyo Lako, ponyo lisiloacha ugonjwa wowote. [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Mponyeshaji wa haki:

1-Ambaye Huondosha dhara na maradhi, na Humponyesha mgonjwa kwa sababu na bila sababu; Anaweza kumponyesha mgonjwa bila ya kuwepo dawa, na Anaweza kumponyesha kwa kupitia dawa. Naye Ndiye Mwenye kupanga sababu za kupona, na yote hayo ni kwa Uwezo wa Allaah.1

2-Na Yeye (تعالى) Ni Mponyeshaji; kama Anavyoponyesha viwiliwili kutokana na maradhi, vivyo hivyo Huponyesha nyoyo kutokana na maradhi yake na vifua kutokana na yaliyomo ndani yake.2 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٧﴾

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rehma kwa Waumini. [Yuwnus (10:57)]

3-Allaah Pekee Ndiye Mponyeshaji, Hana mshirika, na hakuna ponyo isipokuwa ponyo Lake, kama alivyosema Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام):

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾

Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye Ananiponyesha. [Ash-Shu’araa (26:80)]

Na kama ilivyo katika kauli ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika du’aa iliyotangulia: “... hakuna ponyo isipokuwa ponyo Lako.” Rejea juu.

Na miongoni mwa utukufu wa ponyo Lake (تعالى) ni kwamba Yeye Ameumba sababu za ponyo na Akaweka matokeo yake juu ya sababu zake; na mtu huponyeka kwa sababu hizo na kwa zisizokuwa hizo.3

Na miongoni mwa Utukufu Wake ni kwamba Amefanya kupigana na makafiri wanaopigana na Waumini kuwa ni ponyo la nyoyo za Waja Wake wema kutokana na dhiki na huzuni. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَاتِلُوهُمْ يُعَذِّبْهُمُ اللَّـهُ بِأَيْدِيكُمْ وَيُخْزِهِمْ وَيَنصُرْكُمْ عَلَيْهِمْ وَيَشْفِ صُدُورَ قَوْمٍ مُّؤْمِنِينَ ﴿١٤﴾

Piganeni nao, Allaah Atawaadhibu kwa mikono yenu, na Atawahizi na Atakunusuruni dhidi yao, na Atapozesha vifua vya kundi la Waumini. [At-Tawbah (9:14)]

Na hii ni dalili ya Mapenzi ya Allaah kwa Waumini na kujali Kwake hali zao, kiasi kwamba miongoni mwa makusudio ya kisharia ni kuponyesha yaliyomo vifuani mwao na kuondosha ghadhabu zao.

Na katika utukufu wa tiba Yake (تعالى) ni kwamba Hakuteremsha ugonjwa isipokuwa Ameteremsha pia dawa yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أُسَامَةَ بْنِ شَرِيكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَتِ الأَعْرَابُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَلاَ نَتَدَاوَى؟ قَالَ: ((نَعَمْ يَا عِبَادَ اللَّهِ تَدَاوَوْا، فَإِنَّ اللَّهَ لَمْ يَضَعْ دَاءً إِلاَّ وَضَعَ لَهُ شِفَاءً، أَوْ قَالَ: دَوَاءً، إِلاَّ دَاءً وَاحِدًا)). قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، وَمَا هُوَ؟ قَالَ: ((الْهَرَمُ))

Amesimulia Usaamah bin Shariyk (رضي الله عنه): Mabedui walisema: Yaa Rasula-Allaah! Je, tusijitibu? Akasema: “Ndio, enyi Waja wa Allaah, jitibuni; kwani Allaah Hakuweka ugonjwa wowote isipokuwa Ameuwekea ponyo (au alisema: dawa), isipokuwa ugonjwa mmoja.” Wakasema: Yaa Rasula-Allaah! Ni upi huo? Akasema: “Uzee.” [At-Tirmidhiy (2038) na amesema: Hasan Swahiyh, Abuu Daawuwd (3855), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

Na katika Utukufu Wake ni kwamba Ameteremsha ponyo kubwa kabisa na tukufu zaidi, nalo ni Maneno Yake Mwenyewe, yaani Qur-aan tukufu. Hakuteremsha Allaah kutoka mbinguni ponyo lililoenea na lenye manufaa zaidi kuliko Qur-aan. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ۙ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴿٨٢﴾

Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rehma kwa Waumini na wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa khasara. [Al-Israa (17:82)]

Na Anasema (سبحانه وتعالى):

وَلَوْ جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا أَعْجَمِيًّا لَّقَالُوا لَوْلَا فُصِّلَتْ آيَاتُهُ ۖ أَأَعْجَمِيٌّ وَعَرَبِيٌّ ۗ قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ۖ وَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ فِي آذَانِهِمْ وَقْرٌ وَهُوَ عَلَيْهِمْ عَمًى ۚ أُولَـٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ ﴿٤٤﴾

Na lau Tungekifanya kisomeke kwa lugha isiyokuwa ya Kiarabu wangelisema: Mbona hazikufasiliwa waziwazi Aayaat zake? Ah! Cha lugha ya kigeni na hali (Nabiy) ni Mwarabu!? Sema: Hii (Qur-aan) kwa walioamini ni mwongozo na shifaa. Na wale wasioamini, wana uziwi masikioni mwao nayo ni upofu kwao. Hao wanaitwa kutoka mahali mbali. [Fusw-swilat (41:44)]

Qur-aan tukufu ni rutuba ya nyoyo, ponyo la vifua, nuru ya macho na uhai wa roho. Kwa hiyo Qur-aan ni ponyo la yaliyomo vifuani, na hata kama wagonjwa wengi hawajiponyeshi kwayo, yenyewe ni ponyo, akijitibu nayo mtu au asijitibu.

Ni juu ya kila mukallaf kuamini kwamba Mwenye kuponyesha ni Allaah Pekee, na kwamba dawa na nyinginezo ni sababu tu. Hivyo basi ni wajibu kwa mja kuzingatia mambo matatu kuhusiana na sababu:

1-Asizifanye kuwa ni sababu isipokuwa zile zilizothibiti kuwa ni sababu kwa njia ya kisharia au kwa njia ya Qadar (uzoefu wa kawaida uliothibitishwa).

2-Asizitegemee sababu, bali amtegemee Mwenye kuzisababisha na Mwenye kuzikadiria, pamoja na kutekeleza zilizowajibishwa na kujali zenye manufaa.

3-Ajue kwamba hata sababu zikiwa kubwa na zenye nguvu kiasi gani, zote zimefungamana na Hukumu ya Allaah na Makadirio Yake, hazitoki humo; na Akitaka Huzibadilisha Anavyotaka, ili Waja wasizitegemee, na wajue Uwezo Wake na Ukamilifu wa Uwezo Wake.4

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ash-Shaafiy:

1-Usitafute Ponyo Kwa Njia Za Shirki:

Ukiamini kwamba Ash-Shaafiy Pekee Ndiye Mponyeshaji, hutaitafuta ponyo kwa hirizi, kwa waganga wanaodai kujua ghaibu, wala kwa ruqyah zenye maneno ya shirki; kwani hayo yanaharibu Tawhiyd yako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((إِنَّ الرُّقَى وَالتَّمَائِمَ وَالتِّوَلَةَ شِرْكٌ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakika ruqyah (zenye shirki), hirizi na tiwalah (uchawi wa kupendezesha) ni shirki.” [Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Ibn Maajah (2861) na As-Silsilah Asw-Swahiyhah (331)]

2-Ash-Shaafiy Pekee Ndiye Anayeponyesha:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shaafiy: Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) alinasibisha maradhi kwake mwenyewe kwa adabu, na ponyo kwa Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾

Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye Ananiponyesha. [Ash-Shu’araa (26:80)]

3-Tafuta Dawa Na Umtegemee Ash-Shaafiy:

Kutafuta dawa hakupingani na kumtegemea Allaah; bali ni katika kuchukua sababu Alizoziweka. Basi jitibu kwa dawa za halali, lakini moyo wako umtegemee Ash-Shaafiy, kwani dawa haiponyeshi isipokuwa kwa Idhini Yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ جَابِرٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ قَالَ: ((لِكُلِّ دَاءٍ دَوَاءٌ، فَإِذَا أُصِيبَ دَوَاءُ الدَّاءِ بَرَأَ بِإِذْنِ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ))

Amesimulia Jaabir (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kila ugonjwa una dawa yake; dawa ya ugonjwa ikipatikana (sawasawa), (mgonjwa) hupona kwa Idhini ya Allaah (عزّ وجلّ).” [Muslim]

4-Jitibu Kwa Qur-aan:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shaafiy: Kwa kuwa Qur-aan ni ponyo, basi jitibu kwayo wewe na ahli zako; soma Al-Faatihah, Aayat Al-Kursiy na Al-Mu’awwidhaat, na ujipulizie na kujipangusa kama alivyofanya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ إِذَا اشْتَكَى يَقْرَأُ عَلَى نَفْسِهِ بِالْمُعَوِّذَاتِ وَيَنْفُثُ، فَلَمَّا اشْتَدَّ وَجَعُهُ كُنْتُ أَقْرَأُ عَلَيْهِ وَأَمْسَحُ بِيَدِهِ رَجَاءَ بَرَكَتِهَا

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapougua anajisomea Al-Mu’awwidhaat (Suwrah Al-Ikhlaasw, Al-Falaq na An-Naas) na kujipulizia. Na maumivu yake yalipozidi, nilikuwa nikimsomea na nikipangusa kwa mkono wake nikitaraji baraka zake. [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Tumia Asali Ambayo Ash-Shaafiy Ameijaalia Kuwa Ponyo:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shaafiy: Katika Neema za Allaah ni kuweka ponyo ndani ya vitu Alivyoviumba, kama asali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

ثُمَّ كُلِي مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ فَاسْلُكِي سُبُلَ رَبِّكِ ذُلُلًا ۚ يَخْرُجُ مِن بُطُونِهَا شَرَابٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ فِيهِ شِفَاءٌ لِّلنَّاسِ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴿٦٩﴾

Kisha kula katika kila matunda, na fuata njia za Rabb wako zilizofanywa nyepesi (kuzipita). Kinatoka katika matumbo yao kinywaji cha rangi mbali mbali, ndani yake mna shifaa (ya magonjwa) kwa watu. Hakika katika hayo, bila shaka kuna Aayah (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa watu wanaotafakari. [An-Nahl (16:69)]

6-Ponyesha Moyo Wako Kwanza:

Maradhi ya moyo, ya shubha (utata katika Dini) na ya shahawaat (matamanio), ni hatari zaidi kuliko maradhi ya mwili; kwani moyo ukitengemaa, mwili wote hutengemaa. Basi muombe Ash-Shaafiy Aponyeshe moyo wako, na utibu kwa Qur-aan, dhikr na ilimu yenye manufaa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((... أَلاَ وَإِنَّ فِي الْجَسَدِ مُضْغَةً، إِذَا صَلَحَتْ صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّهُ، وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ، أَلاَ وَهِيَ الْقَلْبُ))

Amesimulia An-Nu’maan bin Bashiyr (رضي الله عنهما): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “... Tanabahi! Hakika katika mwili kuna kipande cha nyama; kikitengemaa, mwili wote hutengemaa, na kikiharibika, mwili wote huharibika. Tanabahi! Nacho ni moyo.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

7-Mtembelee Mgonjwa Na Umwombee Ponyo:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shaafiy: Kumtembelea mgonjwa ni katika haki za Muislamu juu ya Muislamu mwenzake, na ni sababu ya kupata fadhila kubwa. Na unapomtembelea, mwombee kwa du’aa aliyofundisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Rejea juu. Na amesema (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ ثَوْبَانَ (رضي الله عنه) مَوْلَى رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ عَادَ مَرِيضًا لَمْ يَزَلْ فِي خُرْفَةِ الْجَنَّةِ)). قِيلَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، وَمَا خُرْفَةُ الْجَنَّةِ؟ قَالَ: ((جَنَاهَا))

Amesimulia Thawbaan (رضي الله عنه), mwachwa huru wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayemtembelea mgonjwa, anaendelea kuwa katika khurfah ya Jannah.” Ikaulizwa: Yaa Rasula-Allaah! Ni nini khurfah ya Jannah? Akasema: “Ni matunda yake yanayochumwa.” [Muslim]

8-Subiri Katika Maradhi:

Maradhi ni mtihani na ni kafara ya madhambi kwa Muumini anayesubiri. Basi usilalamike wala usikate tamaa; bali subiri, mhimidi Allaah na umuombe Ash-Shaafiy Akuponyeshe. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ وَأَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنهما) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَا يُصِيبُ الْمُسْلِمَ مِنْ نَصَبٍ وَلاَ وَصَبٍ وَلاَ هَمٍّ وَلاَ حُزْنٍ وَلاَ أَذًى وَلاَ غَمٍّ، حَتَّى الشَّوْكَةِ يُشَاكُهَا، إِلاَّ كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا مِنْ خَطَايَاهُ))

Wamesimulia Abu Sa’iyd Al-Khudriy na Abu Hurayrah (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakimsibu Muislamu uchovu, wala maradhi, wala hamu, wala huzuni, wala udhia, wala dhiki, hata mwiba unaomchoma, isipokuwa Allaah Humfutia kwacho baadhi ya makosa yake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Mzungue Mgonjwa Kwa Ruqyah Ya Jibriyl (عليه السلام):

Tambua, ee Mja wa Ash-Shaafiy: Jibriyl (عليه السلام) alimzungua Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa mgonjwa kwa maneno haya:

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه) أَنَّ جِبْرِيلَ (عليه السلام) أَتَى النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) فَقَالَ: يَا مُحَمَّدُ اشْتَكَيْتَ؟ فَقَالَ: ((نَعَمْ)). قَالَ: بِاسْمِ اللَّهِ أَرْقِيكَ، مِنْ كُلِّ شَيْءٍ يُؤْذِيكَ، مِنْ شَرِّ كُلِّ نَفْسٍ أَوْ عَيْنِ حَاسِدٍ، اللَّهُ يَشْفِيكَ، بِاسْمِ اللَّهِ أَرْقِيكَ

Amesimulia Abuu Sa’iyd (رضي الله عنه) kwamba Jibriyl (عليه السلام) alimjia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: Yaa Muhammad! Je, unaumwa? Akasema: “Ndiyo.” Akasema:

بِاسْمِ اللَّهِ أَرْقِيكَ، مِنْ كُلِّ شَيْءٍ يُؤْذِيكَ، مِنْ شَرِّ كُلِّ نَفْسٍ أَوْ عَيْنِ حَاسِدٍ، اللَّهُ يَشْفِيكَ، بِاسْمِ اللَّهِ أَرْقِيكَ

Kwa Jina la Allaah nakuzungua, kutokana na kila kitu kinachokudhuru, kutokana na shari ya kila nafsi au jicho la hasidi. Allaah Akuponye. Kwa Jina la Allaah nakuzungua. [Muslim]

10-Muombe Ash-Shaafiy Kwa Du’aa Ya Maumivu:

Unapohisi maumivu mwilini mwako, weka mkono wako mahali panapouma na umuombe Ash-Shaafiy kama alivyofundisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ عُثْمَانَ بْنِ أَبِي الْعَاصِ الثَّقَفِيِّ (رضي الله عنه) أَنَّهُ شَكَا إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) وَجَعًا يَجِدُهُ فِي جَسَدِهِ مُنْذُ أَسْلَمَ، فَقَالَ لَهُ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((ضَعْ يَدَكَ عَلَى الَّذِي تَأَلَّمَ مِنْ جَسَدِكَ، وَقُلْ: بِاسْمِ اللَّهِ، ثَلاَثًا، وَقُلْ سَبْعَ مَرَّاتٍ: أَعُوذُ بِاللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ وَأُحَاذِرُ))

Amesimulia ‘Uthmaan bin Abil-‘Aasw Ath-Thaqafiy (رضي الله عنه): Alimshitakia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) maumivu aliyokuwa akiyahisi mwilini mwake tangu alipoingia Uislamu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: “Weka mkono wako mahali panapouma mwilini mwako na useme mara tatu:

بِاسْمِ اللَّهِ

Kwa Jina la Allaah,

na useme mara saba:

أَعُوذُ بِاللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ وَأُحَاذِرُ

Najikinga kwa Allaah na kwa Uwezo Wake kutokana na shari ya ninachokihisi na ninachokihadhari.” [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Asmaa Allaah Al-Husnaa, Dkt. Ar-Ridhwaaniy (626).
  • 2Asmaa Allaah Al-Husnaa, Abu ‘Abdillaah Ar-Ramliy (98).
  • 3Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa, Dkt. Ar-Ridhwaaniy (626).
  • 4Fiqh Al-Asmaa Al-Husnaa, Dkt. ‘Abdur-Razzaaq Al-Badr (290).