Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 068 kati ya 103
Ash-Shahiyd — Majina Mazuri ya Allaah

Ash-Shahiyd: Mwenye Kushuhudia Yote Daima

Ash-Shahiyd ni Shahidi, Mwenye kujua vyema yenye kuonekana na yaliyofichika. Jina Hili la Allaah limetajwa katika Qur-aan mara kumi na tisa (19). Miongoni mwa hizo ni Kauli Yake (سبحانه وتعالى):

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالصَّابِئِينَ وَالنَّصَارَىٰ وَالْمَجُوسَ وَالَّذِينَ أَشْرَكُوا إِنَّ اللَّـهَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿١٧﴾

Hakika wale walioamini, na ambao ni Mayahudi, na Wasabai na Manaswara, na Majusi, na wale wanaoshirikisha, hakika Allaah Atahukumu baina yao Siku ya Qiyaamah. Hakika Allaah Ni Shahidi juu ya kila kitu. [Al-Hajj (22:17)]

Allaah (تبارك وتعالى) Ni Ash-Shahiyd: Mwenye kuyaangalia mambo yote, Ambaye hakifichiki Kwake kitu hata kikiwa ni uzito wa punje ya haradali ardhini wala mbinguni; bali vitu vyote Anavijua, na hakipotei Kwake chochote, kiwe cha dhahiri au cha ndani.1 Yeye (تعالى) Husikia sauti zote, zilizofichika na zilizo wazi, na Huona vyote vilivyopo, vidogo na vikubwa, na Ujuzi Wake umeenea kila kitu. Amewashuhudia Waja Wake na matendo yao, Anaziangalia dhamira zao na yaliyofichika ndani yao, na hila za macho na yaliyomo vifuani; basi itakuwaje kwa maneno na matendo ya dhahiri?2 Allaah (تعالى) Amesema:

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ ۚ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٦١﴾

Na hushughuliki katika jambo lolote, wala husomi humo katika Qur-aan, wala hamtendi amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo. Na hakifichiki kwa Rabb wako hata cha uzito wa chembe (kama atomu) katika ardhi, wala mbinguni, wala kidogo kuliko hicho, wala kikubwa zaidi ya hicho, isipokuwa kimo katika Kitabu bainifu. [Yuwnus (10:61)]

Ni ushahidi ulio wazi, mtukufu na wenye uadilifu, uliokusanya pande zote, na Yeye Allaah (تعالى) Yuko juu ya ‘Arsh Yake tukufu. Ushahidi Wake umesimama juu ya yakini na uadilifu, na unakusanya ujuzi, kuona, kupanga na uwezo.1 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ أَيُّ شَيْءٍ أَكْبَرُ شَهَادَةً ۖ قُلِ اللَّـهُ ۖ شَهِيدٌ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۚ وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ ۚ أَئِنَّكُمْ لَتَشْهَدُونَ أَنَّ مَعَ اللَّـهِ آلِهَةً أُخْرَىٰ ۚ قُل لَّا أَشْهَدُ ۚ قُلْ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ وَإِنَّنِي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿١٩﴾

Sema: Kitu gani ushahidi wake ndio mkubwa zaidi? Sema: Allaah. Yeye Ni Shahidi baina yangu na baina yenu. Na nimefunuliwa Wahy hii Qur-aan ili nikuonyeni kwayo na kila itakayemfikia. Je, hivi kweli nyinyi mnashuhudia kwamba wako waabudiwa wengine pamoja na Allaah? Sema: Mimi sishuhudii (hayo). Sema: Hakika Yeye Ni Mwabudiwa wa haki Mmoja (Pekee), na hakika mimi sihusiki na mnavyomshirikisha navyo. [Al-An’aam (6:19)]

Kwa hiyo haijuzu kuingia katika ushahidi Wake yale yanayoingia katika ushahidi wa viumbe Wake, kama kusahau, kukosea na uongo.3 Naye (سبحانه وتعالى) Ni Shahidi, Mwenye kuhifadhi, Yupo Hadhiri Hagibu, Anachunga wala Haghafiliki. Na miongoni mwa utukufu wa ushahidi Wake ni:

1-Amejishuhudia Mwenyewe kwa Upweke na kusimamisha uadilifu juu ya kila kiumbe.4 Allaah (تعالى) Amesema:

شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١٨﴾

Allaah Ameshuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, na (pia) Malaika na wenye ilimu wameshuhudia hilo. Na Yeye mbali ya hilo, Anasifika kwa uadilifu. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Aal-‘Imraan (3:18)]

Aayah hii imekusanya ushahidi ulio wazi zaidi, mkubwa zaidi, mtukufu zaidi na wenye uadilifu zaidi, kutoka kwa Mshuhudiaji mkubwa zaidi juu ya jambo kubwa zaidi linaloshuhudiwa.5

2-Ushahidi Wake (تعالى) juu ya ukweli wa Waumini pale wanapompwekesha, na ushahidi Wake kwa Rusuli Wake na Malaika Wake.6

3-Ushahidi Wake (تعالى) kwa mdhulumiwa ambaye hana shahidi wala mwenye kumnusuru, dhidi ya mwenye kudhulumu na mwenye kufanya uadui, ambaye hakuna duniani wa kumfanyia uadilifu isipokuwa Yeye (تعالى); na ushahidi huu unalazimu msaada na nusura.7

4-Waja humshuhudia kwa Tawhiyd, kwamba Yeye Hana mfano wala mshirika, na wanakiri kwamba wao ni Waja Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ ﴿١٧٢﴾

Na pindi Rabb wako Alipowaleta wana wa Aadam kutoka migongoni mwao kizazi chao, Akawashuhudisha juu ya nafsi zao: Je, Mimi siye Rabb wenu? Wakasema: Sivyo hivyo bali naam tumeshuhudia! (Allaah Akawaambia): Msije kusema Siku ya Qiyaamah: Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya. [Al-A’raaf (7:172)]

5-Ushahidi Wake utadhihiri wazi Siku ya Qiyaamah kwa Waja Wake wote, kwa matendo waliyoyafanya ya dhahiri na ya ndani. Rejea juu: Al-Hajj (22:17).

6-Na katika utukufu wa ushahidi Wake ni kwamba yale Aliyoyashuhudia Huyabainisha na Kuyaweka wazi, kiasi cha kuyafikisha katika daraja la juu kabisa la kudhihiri na kuwa wazi.5

7-Na utukufu wa ushahidi Wake ni kwa kauli na kwa vitendo. Ama kwa kauli, ni kama Anavyomwambia Rasuli Wake:

لَّـٰكِنِ اللَّـهُ يَشْهَدُ بِمَا أَنزَلَ إِلَيْكَ ۖ أَنزَلَهُ بِعِلْمِهِ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ يَشْهَدُونَ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا ﴿١٦٦﴾

Lakini Allaah Anayashuhudia Aliyoyateremsha kwako. Ameyateremsha kwa Ilimu Yake, na Malaika pia wanashuhudia. Na Anatosheleza Allaah kuwa Mwenye Kushuhudia yote. [An-Nisaa (4:166)]

Na ama kwa vitendo: ni Allaah kumwezesha Rasuli Wake katika ardhi, kumnusuru na kuwadhalilisha maadui zake; na huo ni ushahidi mkubwa kwamba yeye yuko katika haki na kwamba maadui zake wako katika batili.8 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۚ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿٩٦﴾

Sema: Anatosheleza Allaah kuwa Shahidi baina yangu na baina yenu. Hakika Yeye daima Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na za siri za Waja Wake, Mwenye Kuona yote. [Al-Israa (17:96)]

Yaani ushahidi Wake (تعالى) unatokana na Ujuzi Wake wa ndani ya mambo, kuchunga Kwake na kuona Kwake kwa Waja Wake wote. Na huu ndio ushahidi mkubwa kabisa, kwa kuwa umesimama juu ya ujuzi, utambuzi wa ndani na kuona, na kuhukumu kwa haki na uadilifu Siku ya Qiyaamah; haidhulumiwi humo chembe ya haradali kwa yeyote katika Waja, wawe ni Waumini au waovu.9

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ash-Shahiyd:

1-Shuhudia Upweke Wa Allaah Kwa Ukweli:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shahiyd: Kwa kuwa Allaah Amejishuhudia Mwenyewe kwa Upweke, na Malaika na wenye ilimu wakashuhudia hilo, basi kuwa miongoni mwa wanaoshuhudia kwa ukweli na yakini kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, na uifanyie kazi shahada hiyo katika maisha yako yote. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عُبَادَةَ بْنِ الصَّامِتِ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ شَهِدَ أَنْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، وَأَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ، وَأَنَّ عِيسَى عَبْدُ اللَّهِ وَرَسُولُهُ، وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَى مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِنْهُ، وَالْجَنَّةُ حَقٌّ، وَالنَّارُ حَقٌّ، أَدْخَلَهُ اللَّهُ الْجَنَّةَ عَلَى مَا كَانَ مِنَ الْعَمَلِ))

Amesimulia ‘Ubaadah bin Asw-Swaamit (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye kushuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Pekee, Hana mshirika, na kwamba Muhammad ni mja Wake na Rasuli Wake, na kwamba ‘Iysaa ni Mja wa Allaah na Rasuli Wake, na Neno Lake (la Kun!) Alilomtupia Maryam na roho kutoka Kwake (Ameiumba), na kwamba Jannah ni haki, na moto ni haki, Allaah Atamuingiza Jannah kwa amali zozote alizonazo.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

2-Ash-Shahiyd Anashuhudia Kila Kitu:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shahiyd: Hakuna jambo lolote, dogo wala kubwa, linalofichikana na Ushahidi Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٩﴾

Ambaye Pekee Ana ufalme wa mbingu na ardhi. Na Allaah juu ya kila kitu Ni Shahidi. [Al-Buruwj (85:9)]

3-Mwonee Haya Ash-Shahiyd:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shahiyd: Katika matunda ya Jina hili tukufu katika maisha ya kila siku ya mja ni kwamba linampelekea mtu kumkhofu Allaah (تعالى) na kumwonea haya kwa sababu ya kushuhudia Kwake juu yako pale unapomuasi, na linakupa matumaini pale unapomtii. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((اسْتَحْيُوا مِنَ اللَّهِ حَقَّ الْحَيَاءِ)). قَالَ: قُلْنَا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّا لَنَسْتَحْيِي وَالْحَمْدُ لِلَّهِ. قَالَ: ((لَيْسَ ذَاكَ، وَلَكِنَّ الاِسْتِحْيَاءَ مِنَ اللَّهِ حَقَّ الْحَيَاءِ أَنْ تَحْفَظَ الرَّأْسَ وَمَا وَعَى، وَالْبَطْنَ وَمَا حَوَى، وَلْتَذْكُرِ الْمَوْتَ وَالْبِلَى، وَمَنْ أَرَادَ الآخِرَةَ تَرَكَ زِينَةَ الدُّنْيَا، فَمَنْ فَعَلَ ذَلِكَ فَقَدِ اسْتَحْيَا مِنَ اللَّهِ حَقَّ الْحَيَاءِ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwoneeni haya Allaah kwa haya ya kweli.” Tukasema: Yaa Rasula-Allaah! Hakika sisi tunaona haya, الْحَمْدُ لِلَّهِ. Akasema: “Si hivyo, lakini kumwonea haya Allaah kwa haya ya kweli ni kuhifadhi kichwa na kilichomo, na tumbo na kilichomo, na kukumbuka mauti na kuoza. Na anayeitaka Aakhirah huacha pambo la dunia. Atakayefanya hivyo, basi amemwonea haya Allaah kwa haya ya kweli.” [At-Tirmidhiy (2458), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

4-Mwabudu Allaah Kwa Ihsaan Kana Kwamba Unamwona:

Kumbuka kwamba Ash-Shahiyd Anakushuhudia katika kila ‘ibaadah yako; basi ifanye kwa ihsaan.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipoulizwa na Jibriyl (عليه السلام) kuhusu ihsaan alisema:

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) فِي حَدِيثِ جِبْرِيلَ، قَالَ: فَأَخْبِرْنِي عَنِ الإِحْسَانِ. قَالَ: ((أَنْ تَعْبُدَ اللَّهَ كَأَنَّكَ تَرَاهُ، فَإِنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فَإِنَّهُ يَرَاكَ))

Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) katika Hadiyth ya Jibriyl (عليه السلام): Akasema: Nijulishe kuhusu ihsaan. Akasema: “Ni umwabudu Allaah kana kwamba unamwona; na ikiwa wewe humwoni, basi hakika Yeye Anakuona.” [Muslim]

5-Viungo Vyako Vitashuhudia Juu Yako Siku Ya Qiyaamah:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shahiyd: Siku hiyo midomo itafungwa, na mikono na miguu itazungumza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٦٥﴾

Leo Tunatia vizibo juu ya vinywa vyao, na mikono yao itusemeshe na miguu yao itoe ushahidi kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. [Yaasiyn (36:65)]

6-Hata Ardhi Itashuhudia Yaliyotendwa Juu Yake:

Tambua, ee Mja wa Ash-Shahiyd: Ardhi uliyoswali juu yake au uliyoasi juu yake itatoa khabari zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَوْمَئِذٍ تُحَدِّثُ أَخْبَارَهَا ﴿٤﴾ بِأَنَّ رَبَّكَ أَوْحَىٰ لَهَا ﴿٥﴾

Siku hiyo itahadithia khabari zake. Kwa kuwa Rabb wako Ameiamuru. [Az-Zalzalah (99:4-5)]

7-Yaa Mdhulumiwa, Ash-Shahiyd Anashuhudia Dhulma Yako:

Ukidhulumiwa na usimpate shahidi wala mwenye kukunusuru, basi jua kwamba Ash-Shahiyd Anaona na Anashuhudia, na Atakulipia. Na wewe ukiwa na mamlaka juu ya wengine, jihadhari kumdhulumu yeyote, kwani du’aa ya mdhulumiwa haina kizuizi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Mu’aadh (رضي الله عنه) alipomtuma Yemen:

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) بَعَثَ مُعَاذًا إِلَى الْيَمَنِ فَقَالَ: ((... وَاتَّقِ دَعْوَةَ الْمَظْلُومِ، فَإِنَّهَا لَيْسَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ اللَّهِ حِجَابٌ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimtuma Mu’aadh Yemen akamwambia: “... Na iogope du’aa ya mdhulumiwa, kwani haina kizuizi baina yake na Allaah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

8-Toa Ushahidi Wa Kweli Na Jiepushe Na Ushahidi Wa Uongo:

Ukijua kwamba Ash-Shahiyd Anashuhudia kila neno lako, basi usitoe ushahidi isipokuwa kwa haki, hata kama ni dhidi ya nafsi yako au jamaa zako; na jiepushe kabisa na ushahidi wa uongo, kwani ni miongoni mwa madhambi makubwa kabisa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي بَكْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَلاَ أُنَبِّئُكُمْ بِأَكْبَرِ الْكَبَائِرِ؟)) ثَلاَثًا. قَالُوا: بَلَى يَا رَسُولَ اللَّهِ. قَالَ: ((الإِشْرَاكُ بِاللَّهِ، وَعُقُوقُ الْوَالِدَيْنِ)). وَجَلَسَ وَكَانَ مُتَّكِئًا فَقَالَ: ((أَلاَ وَقَوْلُ الزُّورِ)). قَالَ: فَمَا زَالَ يُكَرِّرُهَا حَتَّى قُلْنَا: لَيْتَهُ سَكَتَ

Amesimulia Abu Bakrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Je, nikujulisheni madhambi makubwa kabisa kuliko yote?” (Aliuliza) mara tatu. Wakasema: Ndio, yaa Rasula-Allaah. Akasema: “Kumshirikisha Allaah, na kuwaasi wazazi wawili.” Na alikuwa ameegemea, akaketi akasema: “Tanabahi! Na kauli ya uongo (na ushahidi wa uongo).” (Abu Bakrah) akasema: Akaendelea kuyarudia mpaka tukasema: Laiti angenyamaza. [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Kuwa Shahidi Mwadilifu Kama Ummah Wa Kati:

Tambua kwamba Ash-Shahiyd Ameujaalia Ummah huu kuwa ummah wa kati ili uwe shahidi juu ya watu; basi kila Muislamu ashuhudie haki kwa kauli na matendo yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِّتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا ۗ وَمَا جَعَلْنَا الْقِبْلَةَ الَّتِي كُنتَ عَلَيْهَا إِلَّا لِنَعْلَمَ مَن يَتَّبِعُ الرَّسُولَ مِمَّن يَنقَلِبُ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ ۚ وَإِن كَانَتْ لَكَبِيرَةً إِلَّا عَلَى الَّذِينَ هَدَى اللَّـهُ ۗ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٤٣﴾

Na ndivyo hivyo Tumekufanyeni ummah bora na adilifu ili muwe mashahidi juu ya watu na awe Rasuli shahidi juu yenu. Na Hatukukifanya Qiblah ambacho ulikuwa ukikielekea (Baytul-Maqdis) isipokuwa Tupate kupambanua nani anayemfuata Rasuli kikweli, na nani atakayegeuka arudi nyuma. Na hakika ilikuwa ni jambo gumu isipokuwa kwa wale ambao Allaah Amewaongoza. Na Allaah Hakuwa Mwenye Kupoteza imaan yenu. Hakika Allaah Ni Mwenye Huruma mno kwa watu na Mwenye Kurehemu. [Al-Baqarah (2:143)]

10-Tekeleza Amana Yako Na Umfanye Allaah Kuwa Shahidi:

Tambua kwamba amana ni jukumu zito, na Ash-Shahiyd Ni Shahidi juu ya kila amana uliyopewa.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alitekeleza amana ya kufikisha ujumbe kikamilifu, kisha akamfanya Allaah kuwa Shahidi juu ya hilo katika Hajj ya kuaga. Basi tekeleza majukumu yako kwa ikhlaasw, huku ukijua kwamba Ash-Shahiyd Anashuhudia. Amesema katika hotuba yake:

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنهما) ... أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((... وَأَنْتُمْ تُسْأَلُونَ عَنِّي، فَمَا أَنْتُمْ قَائِلُونَ؟)) قَالُوا: نَشْهَدُ أَنَّكَ قَدْ بَلَّغْتَ وَأَدَّيْتَ وَنَصَحْتَ. فَقَالَ بِإِصْبَعِهِ السَّبَّابَةِ يَرْفَعُهَا إِلَى السَّمَاءِ وَيَنْكُتُهَا إِلَى النَّاسِ: ((اللَّهُمَّ اشْهَدْ، اللَّهُمَّ اشْهَدْ)) ثَلاَثَ مَرَّاتٍ

Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): ... Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “... Nanyi mtaulizwa kuhusu mimi, basi mtasema nini?” Wakasema: Tunashuhudia kwamba umefikisha, umetekeleza na umenasihi. Akasema kwa kidole chake cha shahada, akikinyanyua mbinguni na kukielekeza kwa watu: “Yaa Allaah, shuhudia! Yaa Allaah, shuhudia!” mara tatu. [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1a1bMadaarij As-Saalikiyn (3/466).
  • 2Tafsiyr As-Sa’diy (5/303), Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam (21) na Tawdhwiyh Al-Kaafiyah Ash-Shaafiyah (21).
  • 3Tafsiyr Atw-Twabariy (7/103).
  • 4Tafsiyr As-Sam’aaniy (1/301).
  • 5a5bMadaarij As-Saalikiyn (3/450).
  • 6Ahkaam Al-Qur-aan, Ibn Al-‘Arabiy (2/800).
  • 7Sha-n Ad-Du’aa (76).
  • 8Tafsiyr Suwrah Al-‘Ankabuwt (6/645).
  • 9Angalia: Mawsuw’at Al-Asmaa Al-Husnaa (4/90).