Al-Wakiyl: Mtegemewa Kwa Yote, Mdhamini Na Msimamizi
Allaah (تعالى) Amesema:
الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ ﴿١٧٣﴾
Wale walioambiwa na watu: Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni. Lakini hilo liliwazidishia imaan wakasema: Hasbuna-Allaah! (Allaah Anatutosheleza) Mzuri Alioje Mtegemewa. [Aal-‘Imraan (3:173)]
Na katika Aayaat nyinginezo, Jina Hili limekuja kwa maana ya mwenye kutegemewa. Allaah (تعالى) Amesema akimsimulia Nabiy Ya’quwb (عليه السّلام):
قَالَ لَنْ أُرْسِلَهُ مَعَكُمْ حَتَّىٰ تُؤْتُونِ مَوْثِقًا مِّنَ اللَّـهِ لَتَأْتُنَّنِي بِهِ إِلَّا أَن يُحَاطَ بِكُمْ ۖ فَلَمَّا آتَوْهُ مَوْثِقَهُمْ قَالَ اللَّـهُ عَلَىٰ مَا نَقُولُ وَكِيلٌ ﴿٦٦﴾
Akasema: Sitompeleka pamoja nanyi mpaka mnipe Ahadi ya Allaah kwamba lazima nyinyi mtamrudisha kwangu isipokuwa ikiwa mmezungukwa. Basi walipompa ahadi yao, akasema: Allaah kwa tuyasemayo Ni Mdhamini Anayetegemewa kwa yote. [Yuwsuf (12:66)]
Na limekuja pia kwa maana ya mwenye kuhifadhi na mwenye kusimamia. Allaah (تعالى) Amemwambia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم):
وَكَذَّبَ بِهِ قَوْمُكَ وَهُوَ الْحَقُّ ۚ قُل لَّسْتُ عَلَيْكُم بِوَكِيلٍ ﴿٦٦﴾
Na watu wako wameikadhibisha (Qur-aan) nayo ni haki. Sema: Mimi si mdhamini wenu. [Al-An’aam (6:66)]
Na hali kadhaalika linakusanya maana ya mwenye kutosheleza na mwenye kuenea kwa kila kitu.1
Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Mwenye haki na Jina Hili kuliko yeyote mwingine, kwa kila maana:
1-Kila kiumbe kimemtegemea Yeye katika kupangiwa mambo yake, kuongozwa kwake, kupata kwake, kunusuriwa kwake, rizki yake na kuhifadhiwa kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ﴿٦٢﴾
Allaah Ni Muumbaji wa kila kitu, Naye juu ya kila kitu Ni Mdhamini. [Az-Zumar (39:62)]
Na huu ndio uwakili wa jumla ulio timilifu kwa kila kiumbe, ambao unathibitisha kuenea kwa Ujuzi Wake (تعالى) kwa kila kitu, na ukamilifu wa Uwezo Wake katika kupanga, na ukamilifu wa Hikmah Yake. Yeye (تعالى) Ni Mbora wa wanaotegemewa.
2-Uwakili mahsusi: Ni kwamba Yeye (تعالى) Ni Mtegemewa wa Waumini; Huwasahilishia yaliyo mazito, Huwakinga na yaliyo magumu, na Huwatosheleza katika yanayowahusu katika dunia yao na Aakhirah yao, kwa sababu wao walimtegemea Yeye. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٢﴾
Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia imaan, na kwa Rabb wao wanatawakali. [Al-Anfaal (8:2)]
Na hao ndio waliosema: ﴿حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ﴾ (Allaah Anatutosheleza, Naye Ni Mzuri Alioje Mtegemewa). Rejea juu: Aal-‘Imraan (3:173). Na Amesema (سبحانه وتعالى):
وَيَقُولُونَ طَاعَةٌ فَإِذَا بَرَزُوا مِنْ عِندِكَ بَيَّتَ طَائِفَةٌ مِّنْهُمْ غَيْرَ الَّذِي تَقُولُ ۖ وَاللَّـهُ يَكْتُبُ مَا يُبَيِّتُونَ ۖ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا ﴿٨١﴾
Na wanasema (wanafiki): Tunatii. Lakini wanapotoka kutoka kwako, kundi miongoni mwao hukesha kushauriana na kupanga kinyume na unayoyasema. Na Allaah Anayaandika yale wanayoyapanga usiku. Basi waachilie mbali na tawakali kwa Allaah. Na inatosheleza Allaah kuwa Ni Mtegemewa. [An-Nisaa (4:81)]
Naye (تعالى) Ndiye Mwenye kutosheleza na Mwenye kutegemewa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾
Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatazamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza Kusudio Lake. Allaah Amejaalia makadirio kwa kila kitu. [Atw-Twalaaq (65:3)]
Ukifahamu kwamba mdhamini wako ni Mkwasi, Muweza, basi ipe mgongo dunia yako na uelekee katika ibaada ya Mtegemewa wako. Na atakayemjua Allaah kwa Jina Hili tukufu, inampasa kumtegemea Yeye katika mambo yake yote, na kumkabidhi Yeye mambo yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِذْ هَمَّت طَّائِفَتَانِ مِنكُمْ أَن تَفْشَلَا وَاللَّـهُ وَلِيُّهُمَا ۗ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١٢٢﴾
Pale makundi mawili miongoni mwenu walipofanya wasiwasi kwamba watashindwa na ilhali Allaah Ndiye Rafiki Mlinzi wao. Basi kwa Allaah Pekee Waumini watawakali. [Aal-‘Imraan (3:122)]
Ili hayo yamfikishe mja katika Tawhiyd ya kweli ambayo ni haki ya Allaah juu ya Waja Wake wote.
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Wakiyl:
1-Mfanye Allaah Pekee Kuwa Wakiyl Wako:
Tambua, ee Mja wa Al-Wakiyl: Allaah Ameamrisha kumfanya Yeye Pekee kuwa Mdhamini wa mambo yetu, kwa kuwa Yeye Ndiye Rabb wa Mashariki na Magharibi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
رَّبُّ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَاتَّخِذْهُ وَكِيلًا﴿٩﴾
Rabb wa Mashariki na Magharibi, hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi mfanye kuwa ni Mdhamini wako. [Al-Muzzammil (73:9)]
2-Mtegemee Al-Wakiyl Katika Mambo Yako Yote:
Tawakkul ni kuutegemeza moyo kwa Allaah katika kupata manufaa na kuondosha madhara, pamoja na kuchukua sababu. Basi mkabidhi Al-Wakiyl mambo yako yote; ya Dini yako na ya dunia yako, madogo na makubwa, kwani hakuna anayeweza kukudhuru wala kukunufaisha isipokuwa kwa Idhini Yake. Na hivyo ndivyo alivyofanya Nabiy Ya’quwb (عليه السّلام) baada ya kuwausia wanawe wachukue sababu:
وَقَالَ يَا بَنِيَّ لَا تَدْخُلُوا مِن بَابٍ وَاحِدٍ وَادْخُلُوا مِنْ أَبْوَابٍ مُّتَفَرِّقَةٍ ۖ وَمَا أُغْنِي عَنكُم مِّنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ ۖ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ ۖ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ ۖوَعَلَيْهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُتَوَكِّلُونَ ﴿٦٧﴾
Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie kupitia mlango mmoja, bali ingieni kupitia milango tofauti. Na mimi siwezi kukufaeni chochote kwa Alilolipanga Allaah. Hapana hukumu isipokuwa ya Allaah tu. Kwake natawakali. Na Kwake watawakali wanaotawakali. [Yuwsuf (12:67)]
3-Tawakkul Ni Sifa Ya Waumini Wa Kweli:
Tambua, ee Mja wa Al-Wakiyl: Miongoni mwa sifa za Waumini wa kweli ni kutawakali kwa Rabb wao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٢﴾
Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia imaan, na kwa Rabb wao wanatawakali. [Al-Anfaal (8:2)]
4-Usiwaogope Watu; Al-Wakiyl Anakutosheleza:
Watu wanaweza kukutisha kwa nguvu zao, mali zao au vyeo vyao, lakini wewe unaye Mtegemewa Ambaye Anatosheleza. Basi usikate tamaa na wala usiwaogope; mtegemyaa Allaah Pekee, Naye Atakutosheleza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ ۖ وَيُخَوِّفُونَكَ بِالَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ﴿٣٦﴾
Je, kwani Allaah Si Mwenye Kumtosheleza Mja Wake? Na eti wanakutisha na wale wasiokuwa Yeye. Na ambaye Allaah Amempotoa basi hana wa kumhidi. [Az-Zumar (39:36)]
5-Sema: حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ Wakati Wa Khofu Na Hatari:
Tambua, ee Mja wa Al-Wakiyl: Hii ndiyo kalimah waliyoisema Manabii wakati wa hatari kubwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ ﴿١٧٣﴾
Wale walioambiwa na watu: Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni. Lakini hilo liliwazidishia imaan wakasema: Hasbuna-Allaah! (Allaah Anatutosheleza) Mzuri Alioje Mtegemewa. [Aal-‘Imraan (3:173)]
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: ﴿حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ﴾ قَالَهَا إِبْرَاهِيمُ (عليه السلام) حِينَ أُلْقِيَ فِي النَّارِ، وَقَالَهَا مُحَمَّدٌ (صلى الله عليه وسلم) حِينَ قَالُوا: ﴿إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ﴾
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): “حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ” (Allaah Anatutosheleza, Naye Ni Mbora wa kutegemewa) aliisema Ibraahiym (عليه السلام) alipotupwa motoni, na aliisema Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) walipomwambia: “Hakika watu wamekukusanyikieni, basi waogopeni”, ikawazidishia imaan na wakasema: “Allaah Anatutosheleza, Naye Ni Mbora wa kutegemewa.” [Al-Bukhaariy]
6-Chukua Sababu Kisha Utawakali:
Tambua kwamba tawakkul si kuacha sababu; bali ni kuzichukua sababu za kisharia na za kimaumbile huku moyo ukiwa umetegemea kwa Al-Wakiyl Pekee. Mtu mmoja alipotaka kumwachia ngamia wake bila kumfunga akidai kuwa anatawakali, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَجُلٌ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَعْقِلُهَا وَأَتَوَكَّلُ، أَوْ أُطْلِقُهَا وَأَتَوَكَّلُ؟ قَالَ: ((اعْقِلْهَا وَتَوَكَّلْ))
Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Mtu mmoja alisema: Yaa Rasula-Allaah! Je, nimfunge (ngamia wangu) na nitawakali, au nimwachie na nitawakali? Akasema: “Mfunge, na utawakali.” [At-Tirmidhiy (2517), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
7-Mtegemee Aliye Hai Asiyekufa:
Usimtegemee kiumbe atakayekufa na kukuacha; mtegemee Al-Wakiyl Aliye Hai daima. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ وَسَبِّحْ بِحَمْدِهِ ۚ وَكَفَىٰ بِهِ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا ﴿٥٨﴾
Na tawakali kwa Aliye Hai Ambaye Hafi, na sabihi ukimhimidi. Na Inamtosheleza kuwa Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kuhusu dhambi za Waja Wake. [Al-Furqaan (25:58)]
8-Tawakali Unapotoka Nyumbani Kwako:
Kumbuka kumtegemea Al-Wakiyl kila unapotoka nyumbani kwako, kwa dhikr aliyoifundisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametufundisha dhikr ya kumkabidhi Al-Wakiyl mambo yetu kila tunapotoka nyumbani:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِذَا خَرَجَ الرَّجُلُ مِنْ بَيْتِهِ فَقَالَ: بِسْمِ اللَّهِ، تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّهِ، لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ. يُقَالُ حِينَئِذٍ: هُدِيتَ وَكُفِيتَ وَوُقِيتَ، فَتَتَنَحَّى لَهُ الشَّيَاطِينُ))
Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mtu anapotoka nyumbani kwake akasema:
بِسْمِ اللَّهِ، تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّهِ، لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ
Kwa Jina la Allaah, nimetawakali kwa Allaah, hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa Allaah,
husemwa wakati huo: Umehidiwa, umetoshelezwa na umelindwa; na mashaytwaan humwepuka.” [Abuu Daawuwd (5095), At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
9-Mkabidhi Al-Wakiyl Nafsi Yako Kabla Ya Kulala:
Usingizi ni mauti madogo, na hujui kama utaamka au la. Basi malizia siku yako kwa kumkabidhi Al-Wakiyl nafsi yako na mambo yako, kama alivyofundisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنِ الْبَرَاءِ بْنِ عَازِبٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِذَا أَتَيْتَ مَضْجَعَكَ فَتَوَضَّأْ وُضُوءَكَ لِلصَّلاَةِ، ثُمَّ اضْطَجِعْ عَلَى شِقِّكَ الأَيْمَنِ، ثُمَّ قُلْ: اللَّهُمَّ أَسْلَمْتُ وَجْهِي إِلَيْكَ، وَفَوَّضْتُ أَمْرِي إِلَيْكَ، وَأَلْجَأْتُ ظَهْرِي إِلَيْكَ، رَغْبَةً وَرَهْبَةً إِلَيْكَ، لاَ مَلْجَأَ وَلاَ مَنْجَا مِنْكَ إِلاَّ إِلَيْكَ، آمَنْتُ بِكِتَابِكَ الَّذِي أَنْزَلْتَ، وَبِنَبِيِّكَ الَّذِي أَرْسَلْتَ))
Amesimulia Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniambia: “Unapokwenda kitandani kwako, tawadha wudhuu wako wa Swalaah, kisha lala ubavu wako wa kulia, kisha useme:
اللَّهُمَّ أَسْلَمْتُ وَجْهِي إِلَيْكَ، وَفَوَّضْتُ أَمْرِي إِلَيْكَ، وَأَلْجَأْتُ ظَهْرِي إِلَيْكَ، رَغْبَةً وَرَهْبَةً إِلَيْكَ، لاَ مَلْجَأَ وَلاَ مَنْجَا مِنْكَ إِلاَّ إِلَيْكَ، آمَنْتُ بِكِتَابِكَ الَّذِي أَنْزَلْتَ، وَبِنَبِيِّكَ الَّذِي أَرْسَلْتَ
Yaa Allaah! Nimeusalimisha uso wangu Kwako, na nimekabidhi jambo langu Kwako, na nimeutegemeza mgongo wangu Kwako, kwa kutaraji na kukhofu Kwako. Hakuna pa kukimbilia wala pa kuokolewa Kwako isipokuwa Kwako. Nimeamini Kitabu Chako Ulichokiteremsha, na Nabiy Wako Uliyemtuma.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
10-Shindania Kuwa Miongoni Mwa Wanaomtegemea Rabb Wao:
Tambua, ee Mja wa Al-Wakiyl: Wale watakaoingia Jannah bila hesabu wala adhabu wamesifika kwa kutomtegemea yeyote isipokuwa Rabb wao, na kuepukana na njia za shirki na ushirikina. Basi shindania kuwa miongoni mwao. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amewasifu akisema:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((... هُمُ الَّذِينَ لاَ يَسْتَرْقُونَ، وَلاَ يَتَطَيَّرُونَ، وَلاَ يَكْتَوُونَ، وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema (akiwasifu wale watakaoingia Jannah bila hesabu): “... Hao ni wale wasioomba kusomewa ruqyah, wala hawatafutii nuksi katika ndege (na mfano wake), wala hawajichomi kwa moto, na kwa Rabb wao wanatawakali.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Kama alivyoweka mlango Al-Bukhaariy katika Swahiyh yake: Kitaab At-Tafsiyr, Baab Al-Wakiyl: Al-Muhaafidhw (8/296); At-Tawhiyd, Ibn Mandah (2/196) na Al-Asnaa (1/506).