Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 070 kati ya 103
Al-Qawiyy — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Qawiyy: Mwenye Nguvu Zote Daima

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara tisa, na mara mbili kati ya hizo limekuja kwa tamko la Al-Qawiyy (kwa alif na laam). Allaah (تعالى) Amesema:

اللَّـهُ لَطِيفٌ بِعِبَادِهِ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ ﴿١٩﴾

Allaah Ni Latifu kwa Waja Wake, Anamruzuku Amtakaye, Naye Ndiye Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika. [Ash-Shuwraa (42:19)]

Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Mwenye nguvu zote daima, Naye:

1-Ni Mwenye nguvu zote daima, ambazo hazikosekani wakati wowote.

2-Ni Mwenye nguvu ambaye haumwingii udhaifu wala upungufu, wala Hachoki.

3-Ni Mwenye nguvu Asiyeshindwa na mshindaji yeyote, wala hakuna kinachomzuia, wala Hukumu Yake hairudishwi nyuma.

4-Na katika ukamilifu wa nguvu Zake (تعالى) ni kwamba Yeye Ni Muweza wa kila kitu, na udhaifu haumtawali kwa hali yoyote.

5-Ni Mwenye nguvu zote, na nguvu zote za viumbe si chochote mbele ya nguvu Zake (تعالى); Naye Ni Mkali wa kuadhibu kwa anayezikanusha Aayaat Zake.

6-Naye Ni Muweza, Mwenye kupitisha mambo Yake, Mwenye uwezo wa kutekeleza Atakacho wakati wowote Atakao, katika ardhi Yake na mbingu Zake.

7-Naye (تعالى) Ni Mwenye nguvu katika kupiga Kwake kwa Adhabu Yake; Akikipiga kitu Hukiangamiza, na Ana matakwa yote katika Mamlaka Yake. Hakuna anayeweza kurudisha Atakacho, wala hakuna anayeweza kumponyoka kwa kukimbia. Amesema (تعالى) akisimulia kauli ya Muumini miongoni mwa majini:

وَأَنَّا ظَنَنَّا أَن لَّن نُّعْجِزَ اللَّـهَ فِي الْأَرْضِ وَلَن نُّعْجِزَهُ هَرَبًا﴿١٢﴾

Na sisi tulikuwa na yakini kwamba hatutoweza kumshinda Allaah ardhini, na wala hatutoweza kumkwepa kutoroka. [Al-Jinn (72:12)]

Na Allaah (تعالى) Amesema:

كَتَبَ اللَّـهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي ۚ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ﴿٢١﴾

Allaah Amekwishaandika kwamba: Bila shaka Nitashinda Mimi na Rusuli Wangu. Hakika Allaah Ni Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika. [Al-Mujaadalah (58:21)]

Na kuunganishwa huku baina ya nguvu na enzi ya kushinda kumebeba sifa nyingi za ukamilifu. Miongoni mwazo ni kwamba Yeye (تعالى) Ni Mwenye nguvu katika kumwangamiza Anayemtaka kumwangamiza; hakuna anayeweza kujilinda dhidi Yake. Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Hashindwi kumnusuru Mja Wake yeyote.1 Na hili linapinga wanaodhani kwamba kuna upungufu wowote katika haki Yake; yaani kudhani kwamba kwa kuwa Ni Mwenye nguvu juu ya Waja Wake, huenda Asiwe Mwenye nguvu kwa wasiokuwa viumbe hao, hata kama ni katika chembe ya wakati. Hilo limekanushwa kwa Kauli Yake: “Al-‘Aziyz”, yaani Mwenye kushinda kwa ushindi usiofanana na wa yeyote, kiasi kwamba aliyeshindwa hakosi tu njia ya kujiokoa bali hana hata njia ya kukimbia; na huo ndio Wasifu Wake (تعالى) daima.2

Na katika jumla ya Utukufu Wake ni kwamba Yeye Ni:

فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ ﴿١٦﴾

Mwingi wa Kufanya Atakalo, hakuna wa kumzuia. [Al-Buruwj (85:16)]

Hazuiliwi wala Hapingwi na yeyote yule; bali Anapotaka jambo, Husema tu: Kuwa! Nalo likawa.

Na katika utukufu wa nguvu Zake ni kuwaangamiza madhalimu na waovu katika zama zote za historia, vyovyote zilivyokuwa nguvu zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً ۖ أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَهُمْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ ﴿١٥﴾

Ama kina Aad, wao walitakabari katika ardhi bila ya haki, na wakasema: Nani mwenye nguvu zaidi kuliko sisi? Je, hawakuona kwamba Allaah Ambaye Amewaumba Ndiye Mwenye nguvu zaidi kuliko wao? Nao walikuwa wanazikanusha Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) Zetu. [Fusw-swilat (41:15)]

Na Allaah Amewateremshia madhalimu aina mbalimbali za adhabu, na Akawachukua kwa sababu ya madhambi yao; kwani Yeye Ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu.

Na katika Utukufu Wake ni kwamba Allaah Humnusuru anayeinusuru Dini Yake, na Humdhalilisha anayempinga; na Amekwishajiandikia ushindi kwa ajili Yake na mawalii Wake. Rejea juu: Al-Mujaadalah (58:21).

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Qawiyy:

1-Mkadirie Al-Qawiyy Kadiri Anavyostahiki:

Tambua, ee Mja wa Al-Qawiyy: Washirikina hawakumkadiria Allaah kama Anavyostahiki pale walipowaabudu wasioweza hata kuumba nzi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ ضُرِبَ مَثَلٌ فَاسْتَمِعُوا لَهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ ۖ وَإِن يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ۚ ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ ﴿٧٣﴾ مَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٧٤﴾

Enyi watu! Umepigwa mfano basi usikilizeni kwa makini! Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah hawawezi kuumba nzi japo wakijumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu chochote kile hawawezi kukiambua tena. Amedhoofika mwenye kutaka matilabu na mwenye kutakiwa. Hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Hakika Allaah bila shaka ni Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika. [Al-Hajj (22:73-74)]

2-Nguvu Zote Ni Za Allaah:

Tambua kwamba Siku ya Qiyaamah washirikina watatambua kwamba nguvu zote ni za Al-Qawiyy Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ ۗ وَلَوْ يَرَى الَّذِينَ ظَلَمُوا إِذْ يَرَوْنَ الْعَذَابَ أَنَّ الْقُوَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا وَأَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعَذَابِ ﴿١٦٥﴾

Na miongoni mwa watu wako wenye kuwafanya viumbe miungu badala ya Allaah, wanawapenda kama kumpenda Allaah. Na wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah. Na lau wale waliodhulumu wangelitambua watakapoona adhabu, kwamba nguvu zote ni za Allaah, na kwamba hakika Allaah ni Mkali wa Kuadhibu, (basi wasingelimfanyia Allaah washirika). [Al-Baqarah (2:165)]

3-Usiogope Nguvu Za Viumbe:

Viumbe vyote, hata wakikusanyika wote, hawana nguvu yoyote juu yako isipokuwa kwa yale Aliyoyaandika Allaah. Basi mche Al-Qawiyy Pekee, wala usiwaogope wanyonge wenzako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَاعْلَمْ أَنَّ الأُمَّةَ لَوِ اجْتَمَعَتْ عَلَى أَنْ يَنْفَعُوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ لَكَ، وَلَوِ اجْتَمَعُوا عَلَى أَنْ يَضُرُّوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَضُرُّوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ عَلَيْكَ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniambia: “... Na jua kwamba ummah (wote) lau wangekusanyika kukunufaisha kwa jambo, hawatokunufaisha isipokuwa kwa jambo ambalo Allaah Amekwishakuandikia. Na lau wangekusanyika kukudhuru kwa jambo, hawatokudhuru isipokuwa kwa jambo ambalo Allaah Amekwishakuandikia.” [At-Tirmidhiy (2516), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

4-Mnusuru Allaah Kwa Kutii Amri Zake, Al-Qawiyy Atakunusuru:

Kumbuka kwamba Nusura ya Al-Qawiyy inawafikia wanaoinusuru Dini Yake kwa kutii Amri Zake.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِم بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّا أَن يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ۗ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّـهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّهُدِّمَتْ صَوَامِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَاتٌ وَمَسَاجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا اسْمُ اللَّـهِ كَثِيرًا ۗ وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٤٠﴾

Ambao wametolewa majumbani mwao bila ya haki isipokuwa kwa kuwa tu wanasema: Rabb wetu Ni Allaah. Na lau ingelikuwa Allaah Hawakingi watu baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangelivunjwa mahekalu na makanisa, na masinagogi na Misikiti inayotajwa humo Jina la Allaah kwa wingi. Na bila shaka Allaah Atamnusuru yeyote yule anayenusuru Dini Yake. Hakika Allaah bila shaka Ni Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika. [Al-Hajj (22:40)]

5-Muumini Mwenye Nguvu Ni Bora, Basi Pupia Yenye Kukunufaisha:

Tambua kwamba Al-Qawiyy Anampenda Muumini mwenye nguvu katika imaan, mwili na azma; basi pupia yenye kukunufaisha.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الْمُؤْمِنُ الْقَوِيُّ خَيْرٌ وَأَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنَ الْمُؤْمِنِ الضَّعِيفِ، وَفِي كُلٍّ خَيْرٌ، احْرِصْ عَلَى مَا يَنْفَعُكَ، وَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ وَلاَ تَعْجِزْ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muumini mwenye nguvu ni bora na anapendeza zaidi kwa Allaah kuliko Muumini dhaifu, na katika kila mmoja kuna kheri. Pupia yale yanayokunufaisha, na omba msaada kwa Allaah, wala usishindwe.” [Muslim]

6-Jivike Nguvu Katika Kusimamisha Haki:

Tambua kwamba Mja anapozijua nguvu za Al-Qawiyy, inampasa ajivike nguvu katika kusimamisha haki, katika kuamrisha mema na kukataza maovu, na asiogope chochote isipokuwa kumuogopa Allaah Pekee. Na inampasa ayachukue Maamrisho ya Allaah na kuyafanyia kazi kwa azma yake yote na nguvu zake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الْمُؤْمِنُ الْقَوِيُّ خَيْرٌ وَأَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنَ الْمُؤْمِنِ الضَّعِيفِ، وَفِي كُلٍّ خَيْرٌ، احْرِصْ عَلَى مَا يَنْفَعُكَ وَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ وَلاَ تَعْجَزْ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muumini mwenye nguvu ni bora na mpendwa zaidi kwa Allaah kuliko Muumini dhaifu, na katika wote wawili kuna kheri. Shikamana na yale yanayokunufaisha, na omba msaada kwa Allaah, wala usilegee.” [Muslim]

7-Nguvu Ya Kweli Ni Kuimiliki Nafsi Wakati Wa Hasira:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Qawiyy, kwamba nguvu ya kweli si nguvu ya mwili, bali ni kuimiliki nafsi wakati wa hasira.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لَيْسَ الشَّدِيدُ بِالصُّرَعَةِ، إِنَّمَا الشَّدِيدُ الَّذِي يَمْلِكُ نَفْسَهُ عِنْدَ الْغَضَبِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye nguvu si yule anayewaangusha watu mweleka; hakika mwenye nguvu ni yule anayeimiliki nafsi yake wakati wa hasira.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

8-Zingatia Hatima Za Waliotangulia:

Wazingatie kwa nguvu za Allaah na Uwezo Wake wale walioangamizwa kwa Uadilifu Wake na Hikmah Yake, nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko sisi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَكَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۚ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعْجِزَهُ مِن شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَلِيمًا قَدِيرًا ﴿٤٤﴾

Je, hawakutembea katika ardhi, wakatazama vipi ilikuwa hatima ya wale walio kabla yao, nao walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao? Na hakuna lolote limshindalo Allaah mbinguni wala ardhini. Hakika Yeye daima Ni Mjuzi wa yote, Mweza wa yote. [Faatwir (35:44)]

9-Kithirisha Kusema: لَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّهِ:

Chukua nguvu katika kumtii Allaah kwa kukithirisha kauli hii, kwani ni hazina miongoni mwa hazina za Jannah, na ni kukiri kwamba hakuna nguvu yoyote ya mja isipokuwa kwa Allaah Al-Qawiyy:

عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَلاَ أَدُلُّكَ عَلَى كَنْزٍ مِنْ كُنُوزِ الْجَنَّةِ؟)). فَقُلْتُ: بَلَى يَا رَسُولَ اللَّهِ. قَالَ: ((لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ))

Amesimulia Abu Muwsaa Al-Ash‘ariy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniambia: “Je, nikuonyeshe hazina miongoni mwa hazina za Jannah?” Nikasema: Ndio, yaa Rasula-Allaah. Akasema:

لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ

Hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa Allaah. [Al-Bukhaariy] [Muslim]

10-Mwombe Al-Qawiyy Akulinde Na Udhaifu Na Uvivu:

Omba du’aa, ee ndugu Muislamu, Al-Qawiyy Akulinde na udhaifu, uvivu na woga.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiomba:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْعَجْزِ وَالْكَسَلِ، وَالْجُبْنِ وَالْهَرَمِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْعَجْزِ وَالْكَسَلِ، وَالْجُبْنِ وَالْهَرَمِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ

Yaa Allaah! Hakika mimi najikinga Kwako kutokana na kushindwa na uvivu, woga na ukongwe, na najikinga Kwako kutokana na adhabu ya kaburi, na najikinga Kwako kutokana na fitna ya uhai na mauti. [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Al-Baydhwaawiy (3/376).
  • 2Nadhwm Ad-Durar (7/506).