Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 071 kati ya 103
Al-Kabiyr — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Kabiyr: Mkubwa kabisa; Ambaye kila kitu ni kidogo mbele ya Ukubwa Wake, katika Dhati Yake, Sifa Zake na Matendo Yake.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara sita, na mara nyingi limeambatana na Jina Al-‘Aliyy, na mara moja na Jina Al-Muta’aal. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ ﴿٩﴾

Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, Mkubwa kabisa Mwenye Uluwa. [Ar-Ra’d (13:9)]

Na Anasema pia:

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٦٢﴾

Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ndiye wa Haki, na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili, na kwamba Allaah Ndiye Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa. [Al-Hajj (22:62)]

Maana Ya Al-Kabiyr:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mkubwa kuliko kila kitu; mbingu saba na ardhi ni kidogo mbele ya Ukubwa Wake. Rejea Az-Zumar (39:67) katika 058-Al-‘Adhwiym.

وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٦٧﴾

Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Na hali ardhi yote Ataikamata Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah, na mbingu zitakunjwa kwa Mkono Wake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha. [Az-Zumar (39:67)]

2-Ukubwa Wake umekamilika katika Sifa Zake zote: Ujuzi Wake, Uwezo Wake, Rehma Yake na Hikmah Yake, hazina upungufu wala kikomo.

3-Na Ukubwa Wake unadhihirika katika Hukumu Yake; Hukumu ni Yake Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

ذَٰلِكُم بِأَنَّهُ إِذَا دُعِيَ اللَّـهُ وَحْدَهُ كَفَرْتُمْ ۖ وَإِن يُشْرَكْ بِهِ تُؤْمِنُوا ۚ فَالْحُكْمُ لِلَّـهِ الْعَلِيِّ الْكَبِيرِ﴿١٢﴾

(Wataambiwa): Hivyo kwenu ni kwa sababu Alipoombwa Allaah Pekee, mlikufuru, na aliposhirikishwa, mliamini. Basi hukumu ni ya Allaah Pekee Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa. [Ghaafir (40:12)]

4-Na ndiyo maana Allaah Ameamrisha Atukuzwe kwa Takbiyr: “اللَّهُ أَكْبَرُ” (Allaah Ni Mkubwa zaidi). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾

Na sema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Ambaye Hakujifanyia mwana na wala Hakuwa na mshirika katika ufalme, na wala Hakuwa dhalili hata Awe (Anahitaji) mlinzi (na msaidizi), na mtukuze matukuzo makubwa kabisa. [Al-Israa (17:111)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Kabiyr:

1-Mtukuze Al-Kabiyr Kwa Moyo Wako Kabla Ya Ulimi Wako:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Kabiyr, kwamba unaposema “اللَّهُ أَكْبَرُ” katika Swalaah na nje ya Swalaah, unakiri kwamba Allaah Ni Mkubwa kuliko kila kitu kinachokushughulisha; basi moyo wako ukubaliane na ulimi wako. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ﴿٣﴾

Na Rabb wako mtukuze. [Al-Muddath-thir (74:3)]

2-Mtukuze Al-Kabiyr Kwa Neema Ya Uongofu:

Tambua kwamba baada ya kukamilisha Swawm ya Ramadhwaan, Al-Kabiyr Ameamrisha Atukuzwe kwa Uongofu Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٨٥﴾

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na baatwil). Kwa hiyo atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inampasa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu ili mkamilishe idadi na ili mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongozeni, na ili mpate kushukuru. [Al-Baqarah (2:185)]

3-Mtukuze Al-Kabiyr Katika Ibaada Ya Kuchinja:

Kumbuka kwamba katika kuchinja Hady na Udhwhiyah, lengo ni taqwa na kumtukuza Al-Kabiyr, si nyama wala damu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ ۗ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ ﴿٣٧﴾

Hazimfikii Allaah nyama zake wala damu zake, lakini inamfikia taqwa kutoka kwenu. Hivyo ndivyo Tulivyowatiisha kwenu ili mpate kumtukuza Allaah kwa kuwa Amekuongozeni. Na wabashirie wafanyao ihsaan. [Al-Hajj (22:37)]

4-Usimtukuze Kiumbe Kama Unavyomtukuza Al-Kabiyr:

Tahadhari na kukipa kiumbe chochote utukufu Anaoustahiki Al-Kabiyr Pekee; kwani waabudiwa wote badala Yake ni baatwil. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٣٠﴾

Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ndiye wa Haki, na kwamba wale wanaowaomba badala Yake, ni baatwil, na kwamba Allaah Ndiye Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa. [Luqmaan (31:30)]

5-Nyenyekea, Kwani Ukubwa Ni Wa Al-Kabiyr Pekee:

Tambua kwamba kila mkubwa katika viumbe ni mdogo mbele ya Al-Kabiyr; basi usijikweze kwa mali, cheo wala nguvu.

6-Mche Al-Kabiyr Katika Usimamizi Wako Wa Walio Chini Yako:

Kumbuka kwamba Al-Kabiyr Aliwaonya wanaume kwa Majina Yake Al-‘Aliyy na Al-Kabiyr baada ya kuwapa usimamizi juu ya wake zao (rejea An-Nisaa (4:34) katika 042-Al-‘Aliyy).

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا ﴿٣٤﴾

Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine, na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. Basi wanawake wema ni wale watiifu, wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. Na wale ambao mnakhofu uasi wao wa ndoa, basi wanasihini na wahameni katika malazi na wapigeni (kipigo kisichodhuru). Wakikutiini, basi msitafute njia dhidi yao (ya kuwaudhi). Hakika Allaah daima Ni Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa. [An-Nisaa (4:34)]

7-Mtukuze Al-Kabiyr Unapopanda Mahali Pa Juu:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Kabiyr, Sunnah ya Swahaba (رضي الله عنهم) safarini:

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنهما) قَالَ: كُنَّا إِذَا صَعِدْنَا كَبَّرْنَا، وَإِذَا نَزَلْنَا سَبَّحْنَا

Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): Tulikuwa tunapopanda (mahali pa juu) tunasema: اللَّهُ أَكْبَرُ; na tunaposhuka tunasema: سُبْحَانَ اللَّهِ. [Al-Bukhaariy]

8-Mtukuze Al-Kabiyr Baada Ya Kila Swalaah:

Dumisha, ee Mja wa Al-Kabiyr, dhikr hii baada ya kila Swalaah ya faradhi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ سَبَّحَ اللَّهَ فِي دُبُرِ كُلِّ صَلاَةٍ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، وَحَمِدَ اللَّهَ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، وَكَبَّرَ اللَّهَ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، فَتِلْكَ تِسْعَةٌ وَتِسْعُونَ، وَقَالَ تَمَامَ الْمِائَةِ: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، غُفِرَتْ خَطَايَاهُ وَإِنْ كَانَتْ مِثْلَ زَبَدِ الْبَحْرِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayemsabbih Allaah baada ya kila Swalaah mara thelathini na tatu, na akamhimidi Allaah mara thelathini na tatu, na akamtukuza Allaah (kwa Takbiyr) mara thelathini na tatu, hizo ni tisini na tisa; na akasema kukamilisha mia:

لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Peke Yake, Hana mshirika, ni Wake ufalme na ni Zake Himdi, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza; ataghufuriwa makosa yake hata kama yatakuwa mfano wa povu la bahari.” [Muslim]

9-Mtukuze Al-Kabiyr Kabla Ya Kulala:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Kabiyr, wasiya wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ‘Aliy na Faatwimah (رضي الله عنهما) walipomwomba mtumishi:

عَنْ عَلِيٍّ (رضي الله عنه) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ لَهُ وَلِفَاطِمَةَ: ((إِذَا أَخَذْتُمَا مَضَاجِعَكُمَا فَكَبِّرَا أَرْبَعًا وَثَلاَثِينَ، وَسَبِّحَا ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، وَاحْمَدَا ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، فَهُوَ خَيْرٌ لَكُمَا مِنْ خَادِمٍ))

Amesimulia ‘Aliy (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia yeye na Faatwimah: “Mtakapokwenda kulala, semeni اللَّهُ أَكْبَرُ mara thelathini na nne, na سُبْحَانَ اللَّهِ mara thelathini na tatu, na الْحَمْدُ لِلَّهِ mara thelathini na tatu; hilo ni bora kwenu kuliko mtumishi.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

10-Tafakari Ukubwa Wa Al-Kabiyr Siku Ya Qiyaamah:

Tafakari jinsi Malaika watakavyofazaika kwa Ukubwa Wake watakaposikia Wahyi, kisha waseme: “Haki,” Naye Ndiye Al-‘Aliyy, Al-Kabiyr (rejea Sabaa (34:23) katika 042-Al-‘Aliyy).

وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ ۚ حَتَّىٰ إِذَا فُزِّعَ عَن قُلُوبِهِمْ قَالُوا مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ ۖ قَالُوا الْحَقَّ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٢٣﴾

Na wala haitofaa shafaa’ah (uombezi) mbele Yake isipokuwa kwa yule Aliyempa idhini. Mpaka litakapoondolewa fazaiko nyoyoni mwao watasema: Amesema nini Rabb wenu? Watasema: Ya haki, Naye Ni Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa. [Saba-a (34:23)]

Na Allaah Mjuzi zaidi