Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 073 kati ya 103
Badiy'-As-Samaawaati-Wal-Ardhw — Majina Mazuri ya Allaah

Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw: Mbunifu wa mbingu na ardhi; Aliyeziumba bila ya mfano uliotangulia, kwa ukamilifu na umahiri usio na kasoro.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara mbili (2). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَإِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿١١٧﴾

Mbunifu wa mbingu na ardhi (bila ya mfano uliotangulia). Anapohukumu jambo huliambia Kun! (Kuwa!) Basi nalo huwa. [Al-Baqarah (2:117)]

Na Anasema pia:

بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ وَلَدٌ وَلَمْ تَكُن لَّهُ صَاحِبَةٌ ۖ وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٠١﴾

Mbunifu wa mbingu na ardhi (bila ya mfano uliotangulia). Inamkinikaje kuwa Yeye Ana mwana ilhali Hana mke? Naye Ameumba kila kitu, Naye Ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-An’aam (6:101)]

Maana Ya Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ameanzisha mbingu na ardhi bila ya mfano wowote uliotangulia, wala hakuwa na msaidizi; Alisema: “Kuwa!” navyo vikawa (rejea Al-Baqarah (2:117) juu).

2-Uumbaji Wake umekamilika kwa umahiri usio na kasoro. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَتَرَى الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ ۚ صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ ۚ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ ﴿٨٨﴾

Na unaona milima unaidhania imetulia thabiti nayo inapita mpito wa mawingu. Utengenezaji wa Allaah Ambaye Ametengeneza kwa umahiri kila kitu. Hakika Yeye Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myafanyayo. [An-Naml (27:88)]

3-Uumbaji wa mbingu na ardhi ni mkubwa kuliko uumbaji wa watu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴿٥٧﴾

Bila shaka uumbaji wa mbingu na ardhi ni mkubwa zaidi kuliko uumbaji wa watu, lakini watu wengi hawajui. [Ghaafir (40:57)]

4-Mbingu na ardhi zilikuwa zimeshikana, Akazitenganisha, na Akajaalia kila kitu hai kutokana na maji. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَوَلَمْ يَرَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ كَانَتَا رَتْقًا فَفَتَقْنَاهُمَا ۖ وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ ۖ أَفَلَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٠﴾

Je, hawakuona wale waliokufuru kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeshikamana Tukazibabandua? Na Tukajaalia kutokana na maji kila kitu kilicho hai? Je, basi hawaamini? [Al-Anbiyaa (21:30)]

5-Na Ameijenga mbingu kwa nguvu, na Anaendelea kuipanua. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالسَّمَاءَ بَنَيْنَاهَا بِأَيْدٍ وَإِنَّا لَمُوسِعُونَ ﴿٤٧﴾

Na mbingu Tumezijenga kwa nguvu na qudra, na hakika Sisi Ndio Wenye Kupanua. [Adh-Dhaariyaat (51:47)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw:

1-Tafakari Uanzilishi Wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw:

Tafakari, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, ukubwa wa mbingu na mpangilio wa nyota na sayari; hakuna kasoro wala mpasuko ndani yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا ۖ مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ ۖ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ﴿٣﴾ ثُمَّ ارْجِعِ الْبَصَرَ كَرَّتَيْنِ يَنقَلِبْ إِلَيْكَ الْبَصَرُ خَاسِئًا وَهُوَ حَسِيرٌ﴿٤﴾

Ambaye Ameumba mbingu saba matabaka. Hutaona katika Uumbaji wa Ar-Rahmaan tofauti yoyote. Basi rejesha jicho. Je, unaona mpasuko wowote ule? Kisha rejesha jicho tena na tena, litakupindukia jicho likiwa limehizika, nalo limenyong’onyea. [Al-Mulk (67:3-4)]

2-Tambua Kwamba Aliyeanzisha Ndiye Anayestahiki Kuabudiwa Pekee:

Kumbuka, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba Aliyeanzisha mbingu na ardhi bila mfano Hahitaji mke wala mwana, wala Hana mshirika (rejea Al-An’aam (6:101) juu).

3-Kuwa Na Yakini Kwamba Kila Jambo Ni Jepesi Kwake:

Tambua, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba Aliyeanzisha mbingu na ardhi kwa neno “Kuwa!” hashindwi na jambo lako lolote, hata likiwa zito machoni pako (rejea Al-Baqarah (2:117) juu).

4-Amini Kufufuliwa, Kwani Aliyeanzisha Anaweza Kurudisha:

Kumbuka, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba kuanzisha ni kukubwa kuliko kurudisha; basi kufufuliwa ni jepesi Kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ ۚ وَلَهُ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٧﴾

Naye Ndiye Anayeanzisha uumbaji, kisha Anaurudisha, nayo ni sahali mno Kwake. Naye Ana Sifa za juu kabisa katika mbingu na ardhi. Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Ar-Ruwm (30:27)]

5-Tahadhari Na Uzushi Katika Dini, Kwani Kuanzisha Sharia Ni Haki Ya Allaah Pekee:

Tahadhari, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, na kuanzisha katika Dini jambo lisilotoka kwa Allaah na Rasuli Wake; kwani Uanzilishi wa kweli ni wa Allaah Pekee, na Dini imekamilika. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدٌّ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayezusha katika jambo letu hili (Dini) lisilokuwa ndani yake, basi hilo ni lenye kurudishwa (halikubaliwi).” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

6-Shikamana Na Sunnah Na Ujiepushe Na Kila Bid’ah:

Kumbuka, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akitahadharisha na bid’ah katika khutbah zake:

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنهما) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) إِذَا خَطَبَ ... يَقُولُ: ((أَمَّا بَعْدُ، فَإِنَّ خَيْرَ الْحَدِيثِ كِتَابُ اللَّهِ، وَخَيْرُ الْهُدَى هُدَى مُحَمَّدٍ، وَشَرُّ الأُمُورِ مُحْدَثَاتُهَا، وَكُلُّ بِدْعَةٍ ضَلاَلَةٌ))

Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapotoa khutbah … husema: “Amma ba’d: Hakika mazungumzo bora kabisa ni Kitabu cha Allaah, na uongofu bora kabisa ni uongofu wa Muhammad, na mambo maovu kabisa ni yaliyozushwa, na kila bid’ah ni upotofu.” [Muslim]

7-Tumia Akili Uliyopewa Kutafakari, Si Kupinga:

Tambua, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba kutafakari uumbaji wa mbingu na ardhi ni sifa ya wenye akili, na kunazaa imaan na khofu ya Allaah (rejea Aal-‘Imraan (3:190-191) katika 030-Al-Hakiym).

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana, bila shaka ni Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa wenye akili. Ambao wanamdhukuru Allaah wakiwa wima, au wamekaa au wamejinyoosha, na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako! Basi Tukinge na adhabu ya moto. [Aal-‘Imraan (3:190-191)]

8-Nyenyekea Mbele Ya Uumbaji Mkubwa Wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw:

Kumbuka, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba uumbaji wa mbingu na ardhi ni mkubwa kuliko uumbaji wako (rejea Ghaafir (40:57) juu); basi usijikweze.

9-Shukuru Kwa Uhai Ulioanzishwa Kutokana Na Maji:

Tafakari, ee Mja wa Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba kila kitu hai kimejaaliwa kutokana na maji (rejea Al-Anbiyaa (21:30) juu); basi mshukuru kwa kila tone la maji unalokunywa.

10-Mwombe Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw Kwa Majina Yake:

Omba du’aa kwa du’aa ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema kwamba mwenye kuiomba ameomba kwa Jina Tukufu kabisa la Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, na ndani yake mna Jina hili: “…Al-Mannaan, Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, yaa Mwenye Ujalali na Ukarimu, yaa Uliye Hai daima, yaa Msimamizi wa kila kitu…” Rejea Hadiyth ya Anas (رضي الله عنه) katika 007-Al-Qayyuwm.

Na Allaah Mjuzi zaidi