Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 074 kati ya 103
Nuwr-As-Samaawaati-Wal-Ardhw — Majina Mazuri ya Allaah

Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw: Nuru ya mbingu na ardhi; Ambaye kwa Nuru Yake mbingu na ardhi zimeangazwa, na kwa Uongofu Wake nyoyo za Waumini zimeangaziwa.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

اللَّـهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ مَثَلُ نُورِهِ كَمِشْكَاةٍ فِيهَا مِصْبَاحٌ ۖ الْمِصْبَاحُ فِي زُجَاجَةٍ ۖ الزُّجَاجَةُ كَأَنَّهَا كَوْكَبٌ دُرِّيٌّ يُوقَدُ مِن شَجَرَةٍ مُّبَارَكَةٍ زَيْتُونَةٍ لَّا شَرْقِيَّةٍ وَلَا غَرْبِيَّةٍ يَكَادُ زَيْتُهَا يُضِيءُ وَلَوْ لَمْ تَمْسَسْهُ نَارٌ ۚ نُّورٌ عَلَىٰ نُورٍ ۗ يَهْدِي اللَّـهُ لِنُورِهِ مَن يَشَاءُ ۚ وَيَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣٥﴾

Allaah Ni Nuru ya mbingu na ardhi. Mfano wa Nuru Yake ni kama shubaka, ndani yake mna taa yenye mwanga mkali. Taa hiyo yenye mwanga mkali iko katika (tungi la) gilasi. Gilasi hiyo ni kama kwamba nyota inayong’aa na kumeremeta, inawashwa kutokana na mti wa baraka wa zaytuni, hauko Mashariki wala Magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung’aa japokuwa moto haujayagusa, Nuru juu ya Nuru. Allaah Anamwongoza kwa Nuru Yake Amtakaye. Na Allaah Anapiga mifano kwa watu. Na Allaah kwa kila kitu Ni Mjuzi. [An-Nuwr (24:35)]

Na Siku ya Qiyaamah ardhi itang’aa kwa Nuru ya Rabb wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَشْرَقَتِ الْأَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا وَوُضِعَ الْكِتَابُ وَجِيءَ بِالنَّبِيِّينَ وَالشُّهَدَاءِ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴿٦٩﴾

Na ardhi itang’ara kwa Nuru ya Rabb wake, na Kitabu (cha amali) kitawekwa, na wataletwa Manabii na Mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, nao hawatodhulumiwa. [Az-Zumar (39:69)]

Maana Ya Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw:

1-Nuru ni Sifa miongoni mwa Sifa za Allaah (سبحانه وتعالى) kama ilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah; Ahlus-Sunnah wanaithibitisha bila kuifananisha na nuru ya viumbe, wala kuuliza namna yake, kwani hakuna kitu kinachofanana Naye.

2-Pazia Lake ni Nuru; lau Angeliliondoa, basi Utukufu wa Wajihi Wake ungeliunguza viumbe Vyake (rejea Hadiyth ya Abuu Muwsaa (رضي الله عنه) katika 007-Al-Qayyuwm). Na Abuu Dharr (رضي الله عنه) alimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) قَالَ: سَأَلْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): هَلْ رَأَيْتَ رَبَّكَ؟ قَالَ: ((نُورٌ أَنَّى أَرَاهُ))

Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه): Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Je, ulimwona Rabb wako? Akasema: “(Kulikuwa na) Nuru; vipi nitamwona?” [Muslim]

3-Na kwa Nuru Yake mbingu na ardhi zimeangazwa, na kila nuru katika ulimwengu ni kutoka Kwake.

4-Na Yeye Ndiye Mwenye kuwaongoza Waumini kutoka kwenye giza la ukafiri na maasi kuelekea kwenye nuru ya imaan na utiifu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

اللَّـهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُوا يُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَوْلِيَاؤُهُمُ الطَّاغُوتُ يُخْرِجُونَهُم مِّنَ النُّورِ إِلَى الظُّلُمَاتِ ۗ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٥٧﴾

Allaah Ni Rafiki Mlinzi wa wale walioamini, Anawatoa kutoka katika viza na kuwaingiza katika nuru. Na wale waliokufuru marafiki wao wandani na walinzi ni twaghuti, huwatoa kutoka katika nuru na kuwaingiza katika viza. Hao ni watu wa motoni wao humo watadumu. [Al-Baqarah (2:257)]

5-Na Ameteremsha Qur-aan kuwa ni nuru kwa Waja Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ قَدْ جَاءَكُمْ رَسُولُنَا يُبَيِّنُ لَكُمْ كَثِيرًا مِّمَّا كُنتُمْ تُخْفُونَ مِنَ الْكِتَابِ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ ۚ قَدْ جَاءَكُم مِّنَ اللَّـهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾ يَهْدِي بِهِ اللَّـهُ مَنِ اتَّبَعَ رِضْوَانَهُ سُبُلَ السَّلَامِ وَيُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِهِ وَيَهْدِيهِمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿١٦﴾

Enyi Watu wa Kitabu! Hakika amekwishakujieni Rasuli Wetu anayekubainishieni mengi katika yale mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na ananyamazia mengi (yasiyo na lazima kuyafichua). Kwa yakini imekufikieni kutoka kwa Allaah Nuru na Kitabu kinachobainisha. Allaah Anamwongoza kwacho yeyote atakayefuata Radhi Zake kumfikisha njia za salama, na Anawatoa (walio mfano wa huyo) katika viza kuingia katika nuru kwa Tawfiyq Yake, na Anawaongoza kuelekea njia iliyonyooka. [Al-Maaidah (5:15-16)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw:

1-Tafuta Nuru Kwa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw Pekee:

Tambua, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba asiyejaaliwa nuru na Allaah hana nuru yoyote, hata akiwa na elimu na mali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَوْ كَظُلُمَاتٍ فِي بَحْرٍ لُّجِّيٍّ يَغْشَاهُ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ سَحَابٌ ۚ ظُلُمَاتٌ بَعْضُهَا فَوْقَ بَعْضٍ إِذَا أَخْرَجَ يَدَهُ لَمْ يَكَدْ يَرَاهَا ۗ وَمَن لَّمْ يَجْعَلِ اللَّـهُ لَهُ نُورًا فَمَا لَهُ مِن نُّورٍ ﴿٤٠﴾

Au ni kama viza katika bahari ya kina kirefu, imefunikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake kuna mawingu. (Tabaka za) Viza juu yake viza. Anapoutoa mkono wake, anakaribia asiuone. Na ambaye Allaah Hakumjaalia Nuru, basi hawi na Nuru. [An-Nuwr (24:40)]

2-Ifanye Qur-aan Kuwa Nuru Ya Moyo Wako:

Kumbuka, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba Qur-aan ndiyo nuru Aliyoiteremsha ili ikutoe gizani (rejea Al-Maaidah (5:15-16) juu); basi isome, uizingatie na uifanyie kazi.

3-Mche Allaah Na Mwamini Rasuli Wake Upate Nuru Ya Kutembea Nayo:

Tambua, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba taqwa na kumwamini Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) ni sababu ya kupewa nuru na maghfirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَآمِنُوا بِرَسُولِهِ يُؤْتِكُمْ كِفْلَيْنِ مِن رَّحْمَتِهِ وَيَجْعَل لَّكُمْ نُورًا تَمْشُونَ بِهِ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٨﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na muaminini Rasuli Wake. (Allaah) Atakupeni sehemu mbili ya Rehma Zake, na Atakuwekeeni Nuru mtembee nayo, na Atakughufurieni. Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Hadiyd (57:28)]

4-Dumisha Swalaah, Kwani Ni Nuru:

Kumbuka, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba Swalaah ni nuru katika moyo wako, uso wako na kaburi lako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي مَالِكٍ الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَالصَّلاَةُ نُورٌ، وَالصَّدَقَةُ بُرْهَانٌ، وَالصَّبْرُ ضِيَاءٌ، وَالْقُرْآنُ حُجَّةٌ لَكَ أَوْ عَلَيْكَ ...))

Amesimulia Abuu Maalik Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “… Na Swalaah ni nuru, na swadaqah ni dalili (ya imaan), na subira ni mwangaza, na Qur-aan ni hoja kwa ajili yako au dhidi yako …” [Muslim]

5-Tamani Nuru Ya Siku Ya Qiyaamah:

Tafakari, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, Siku ambayo nuru ya Waumini itakuwa ikienda mbele yao na kuliani mwao, nao wakimwomba Allaah Awakamilishie nuru yao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ ۖ نُورُهُمْ يَسْعَىٰ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٨﴾

Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli), asaa Rabb wenu Akakufutieni maovu yenu, na Akakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito. Siku ambayo Allaah Hatomfedhehesha Nabiy na wale walioamini pamoja naye. Nuru yao itatembea mbele yao na kuliani mwao, watasema: Rabb wetu! Tutimizie Nuru yetu, na Tughufurie, hakika Wewe juu ya kila kitu Ni Muweza. [At-Tahriym (66:8)]

6-Tahadhari Na Maasi, Kwani Yanazima Nuru Ya Moyo:

Tahadhari, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, na maasi, kwani humwondolea mja nuru ya moyo wake, na huziba nyoyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

كَلَّاۖ بَلْۜ رَانَ عَلَىٰ قُلُوبِهِم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿١٤﴾

Laa hasha! Bali yamefanya kutu juu ya nyoyo zao yale waliyokuwa wakiyachuma. [Al-Mutwaffifiyn (83:14)]

7-Kuwa Na Yakini Kwamba Nuru Ya Allaah Haitazimwa:

Kumbuka, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, kwamba maadui wa Dini wanajaribu kuizima Nuru ya Allaah kwa vinywa vyao, lakini Allaah Ataikamilisha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يُرِيدُونَ أَن يُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّـهُ إِلَّا أَن يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ﴿٣٢﴾

Wanataka kuzima Nuru ya Allaah kwa vinywa vyao lakini Allaah Anakataa isipokuwa Atimize Nuru Yake, japo watakirihika makafiri. [At-Tawbah (9:32)]

8-Tafakari Mfano Wa Nuru Ya Imaan Katika Moyo Wa Muumini:

Tafakari mfano Alioupiga Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw wa nuru katika moyo wa Muumini: kama taa ndani ya tundu, nuru juu ya nuru (rejea An-Nuwr (24:35) juu). Basi uhifadhi moyo wako ili nuru hiyo isizimike.

9-Mhimidi Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw Katika Kisimamo Cha Usiku:

Mhimidi, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, katika Swalaah yako ya usiku kwa maneno ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): “…Na Himdi ni Zako; Wewe Ndiye Nuru ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake…” Rejea du’aa kamili katika 007-Al-Qayyuwm [Al-Bukhaariy] [Muslim].

10-Mwombe Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw Akujaalie Nuru Pande Zote:

Omba du’aa, ee Mja wa Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw, kama alivyokuwa akiomba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) فِي صِفَةِ صَلاَةِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) بِاللَّيْلِ، قَالَ: وَكَانَ يَقُولُ فِي دُعَائِهِ: ((اللَّهُمَّ اجْعَلْ فِي قَلْبِي نُورًا، وَفِي بَصَرِي نُورًا، وَفِي سَمْعِي نُورًا، وَعَنْ يَمِينِي نُورًا، وَعَنْ يَسَارِي نُورًا، وَفَوْقِي نُورًا، وَتَحْتِي نُورًا، وَأَمَامِي نُورًا، وَخَلْفِي نُورًا، وَعَظِّمْ لِي نُورًا))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) katika maelezo ya Swalaah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) usiku: Na alikuwa akisema katika du’aa yake:

اللَّهُمَّ اجْعَلْ فِي قَلْبِي نُورًا، وَفِي بَصَرِي نُورًا، وَفِي سَمْعِي نُورًا، وَعَنْ يَمِينِي نُورًا، وَعَنْ يَسَارِي نُورًا، وَفَوْقِي نُورًا، وَتَحْتِي نُورًا، وَأَمَامِي نُورًا، وَخَلْفِي نُورًا، وَعَظِّمْ لِي نُورًا

Yaa Allaah! Jaalia moyoni mwangu nuru, na machoni mwangu nuru, na masikioni mwangu nuru, na kuliani kwangu nuru, na kushotoni kwangu nuru, na juu yangu nuru, na chini yangu nuru, na mbele yangu nuru, na nyuma yangu nuru, na Unikuzie nuru. [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi