Al-Qadiyr: Mweza wa yote; Mwenye Uwezo mkamilifu na mwingi juu ya kila kitu, hakuna kinachomshinda.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara arobaini na tano (45), hasa katika kauli “Hakika Allaah juu ya kila kitu Ni Muweza”. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَمْ يَعْيَ بِخَلْقِهِنَّ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ ۚ بَلَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٣٣﴾
Je, hawaoni kwamba Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na wala Hakuchoka kwa kuziumba kwake, kwamba Yeye Ni Muweza wa Kuwafufua wafu. Naam bila shaka! Hakika Yeye juu ya kila kitu Ni Muweza. [Al-Ahqaaf (46:33)]
Na Anasema pia:
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ ضَعْفٍ قُوَّةً ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ قُوَّةٍ ضَعْفًا وَشَيْبَةً ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْقَدِيرُ ﴿٥٤﴾
Allaah Ndiye Ambaye Amekuumbeni kutokana na udhaifu, kisha Akajaalia baada ya udhaifu nguvu, kisha Akajaalia baada ya nguvu udhaifu na ukongwe. Anaumba Atakacho. Naye Ndiye Mjuzi wa yote, Mweza wa yote. [Ar-Ruwm (30:54)]
Maana Ya Al-Qadiyr:
1-Al-Qadiyr ni neno la kukithirisha; linaonyesha ukamilifu na wingi wa Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) juu ya kila kitu bila ya kuchoka wala kushindwa.
2-Jambo lolote Analolitaka, Huliambia “Kuwa!” nalo likawa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾
Hakika Amri Yake Anapotaka chochote Hukiambia: Kun! (Kuwa), nacho huwa. [Yaasiyn (36:82)]
3-Anaweza kuwakusanya viumbe wote Siku ya Qiyaamah Atakapotaka. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَثَّ فِيهِمَا مِن دَابَّةٍ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ جَمْعِهِمْ إِذَا يَشَاءُ قَدِيرٌ﴿٢٩﴾
Na katika Aayaat (Ishara, Dalili) Zake, ni uumbaji wa mbingu na ardhi, na Aliowatawanya humo kati ya viumbe vinavyotembea, Naye kuwakusanya Atakapo Ni Muweza. [Ash-Shuwraa (42:29)]
4-Ni Mwenye Uwezo juu ya ufalme, heshima na udhalilifu wa viumbe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلِ اللَّـهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٦﴾
Sema: Ee Allaah Mfalme Uliyemiliki ufalme wote, Unampa ufalme Umtakaye, na Unamuondoshea ufalme Umtakaye, na Unamtukuza Umtakaye, na Unamdhalilisha Umtakaye, kheri imo Mkononi Mwako. Hakika Wewe Ni Muweza wa kila kitu. [Aal-‘Imraan (3:26)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Qadiyr:
1-Amini Kwamba Hakuna Gumu Kwa Al-Qadiyr:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Qadiyr, kwamba jambo lolote unaloliona gumu, kwa Allaah ni neno moja tu: “Kuwa!” (rejea Yaasiyn (36:82) juu).
2-Usikate Tamaa Na Kubadilika Kwa Nyoyo, Kwani Al-Qadiyr Anaweza Kuweka Mapenzi Baina Ya Mahasimu:
Tambua kwamba Al-Qadiyr Anaweza kuwageuza maadui kuwa marafiki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
عَسَى اللَّـهُ أَن يَجْعَلَ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَ الَّذِينَ عَادَيْتُم مِّنْهُم مَّوَدَّةً ۚ وَاللَّـهُ قَدِيرٌ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٧﴾
Asaa Allaah Akajaalia mapenzi baina yenu na baina ya wale mlio na uadui nao. Na Allaah Ni Muweza wa yote, na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Mumtahinah (60:7)]
3-Tafakari Hatua Za Maisha Yako Chini Ya Uwezo Wa Al-Qadiyr:
Tafakari, ee Mja wa Al-Qadiyr, jinsi Alivyokuumba ukiwa dhaifu, kisha Akakupa nguvu, kisha Atakurudisha kwenye udhaifu na ukongwe (rejea Ar-Ruwm (30:54) juu); basi zitumie siku za nguvu zako katika kumtii.
4-Ridhika Na Qadar, Na Usiseme “Lau”:
Kumbuka kwamba baada ya kuchukua sababu, yanayokufika ni kwa Uwezo wa Al-Qadiyr na Mapenzi Yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... احْرِصْ عَلَى مَا يَنْفَعُكَ، وَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ وَلاَ تَعْجِزْ، وَإِنْ أَصَابَكَ شَيْءٌ فَلاَ تَقُلْ: لَوْ أَنِّي فَعَلْتُ كَانَ كَذَا وَكَذَا، وَلَكِنْ قُلْ: قَدَرُ اللَّهِ وَمَا شَاءَ فَعَلَ، فَإِنَّ لَوْ تَفْتَحُ عَمَلَ الشَّيْطَانِ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “… Pupia yale yanayokunufaisha, na omba msaada kwa Allaah wala usishindwe. Na likikusibu jambo, usiseme: Lau ningefanya kadhaa, ingekuwa kadhaa na kadhaa; bali sema: Ni Qadar ya Allaah, na Alichotaka Amekifanya; kwani ‘lau’ inafungua kazi ya shaytwaan.” [Muslim]
5-Mtegemee Al-Qadiyr Katika Kila Jambo:
Tambua, ee Mja wa Al-Qadiyr, kwamba anayemtegemea Mweza wa yote hapotei; basi mwachie mambo yako baada ya kuchukua sababu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾
Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatazamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza Kusudio Lake. Allaah Amejaalia makadirio kwa kila kitu. [Atw-Twalaaq (65:3)]
6-Amini Kufufuliwa Kwa Uwezo Wa Al-Qadiyr:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Qadiyr, kwamba Aliyeumba mbingu na ardhi bila kuchoka Anaweza kuhuisha wafu (rejea Al-Ahqaaf (46:33) juu).
7-Mwombe Al-Qadiyr Ufalme Wa Kheri Na ‘Izzah Ya Kweli:
Tambua, ee Mja wa Al-Qadiyr, kwamba ufalme na ‘izzah viko Mkononi Mwake, Anampa Amtakaye (rejea Aal-‘Imraan (3:26) juu); basi usiyatafute kwa njia za haraam.
8-Mtaje Al-Qadiyr Katika Dhikr Ya Baada Ya Swalaah:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Qadiyr, kukamilisha dhikr ya baada ya Swalaah kwa: “…وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ” (…Naye juu ya kila kitu Ni Muweza). Rejea Hadiyth katika 071-Al-Kabiyr [Muslim].
9-Usimwogope Kiumbe, Kwani Uwezo Wote Ni Wa Al-Qadiyr:
Tambua, ee Mja wa Al-Qadiyr, kwamba uwezo wa kila kiumbe ni wa kupewa na una kikomo; basi usimwogope kiumbe kuliko unavyomwogopa Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧٥﴾
Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha marafiki wake wandani. Basi msiwakhofu, na nikhofuni Mimi mkiwa ni Waumini. [Aal-‘Imraan (3:175)]
10-Mwombe Al-Qadiyr Kwa Du’aa Aliyoifundisha Allaah Katika Qur-aan:
Omba du’aa, ee Mja wa Al-Qadiyr, kwa maneno ya Aal-‘Imraan (3:26) juu, ukimsifu kuwa Ni Mfalme wa ufalme wote, na kwamba kheri imo Mkononi Mwake, na Yeye juu ya kila kitu Ni Muweza.
Na Allaah Mjuzi zaidi