Al-Muqtadir: Mwenye Uwezo uliokamilika kabisa; Ambaye Uwezo Wake unadhihirika katika kuwakamata madhalimu na kutekeleza Analolitaka bila ya kizuizi.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara tatu kwa umoja, na mara moja kwa wingi (Muqtadiruwn). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَقَدْ جَاءَ آلَ فِرْعَوْنَ النُّذُرُ ﴿٤١﴾ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كُلِّهَا فَأَخَذْنَاهُمْ أَخْذَ عَزِيزٍ مُّقْتَدِرٍ ﴿٤٢﴾
Na kwa yakini watu wa Firawni walifikiwa na maonyo mengi. Walikadhibisha Aayaat (Ishara, Miujiza, Dalili) Zetu zote, Tukawakamata mkamato wa Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Uwezo wa juu kabisa. [Al-Qamar (54:41-42)]
Na Anasema kuhusu Waumini wenye taqwa:
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَهَرٍ ﴿٥٤﴾ فِي مَقْعَدِ صِدْقٍ عِندَ مَلِيكٍ مُّقْتَدِرٍ ﴿٥٥﴾
Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na mito. Katika makao ya haki kwa Mfalme Mwenye Nguvu zote, Mwenye Uwezo wa juu kabisa. [Al-Qamar (54:54-55)]
Maana Ya Al-Muqtadir:
1-Al-Muqtadir ni Mwenye Uwezo uliofika kilele cha ukamilifu; Anakamata kwa ukamataji wa Mwenye Enzi ya Nguvu, bila ya kushindwa na chochote (rejea Al-Qamar (54:41-42) juu).
2-Uwezo Wake unaonekana katika kubadilika kwa hali za dunia: uhai, kisha kunyauka na kupeperushwa na upepo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنَ السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الْأَرْضِ فَأَصْبَحَ هَشِيمًا تَذْرُوهُ الرِّيَاحُ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقْتَدِرًا ﴿٤٥﴾
Na wapigie mfano wa uhai wa dunia. Ni kama maji Tuliyoyateremsha kutoka mbinguni, ikachanganyika nayo mimea ya ardhi (ikasitawi), kisha ikawa mikavu iliyovurugika, inapeperushwa na upepo. Na Allaah daima Ni Mwenye Uwezo wa juu kabisa kwa kila kitu. [Al-Kahf (18:45)]
3-Na Ni Mwenye Uwezo wa kutimiza Alichowaahidi wakanushaji, ikiwa ni katika uhai wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) au baada yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَإِمَّا نَذْهَبَنَّ بِكَ فَإِنَّا مِنْهُم مُّنتَقِمُونَ﴿٤١﴾ أَوْ نُرِيَنَّكَ الَّذِي وَعَدْنَاهُمْ فَإِنَّا عَلَيْهِم مُّقْتَدِرُونَ﴿٤٢﴾
Na hata kama Tukikuondoa (kukufisha), basi hakika Sisi Ni Wenye Kuwalipizia. Au Tukuonyeshe yale Tuliyowatishia, basi hakika Sisi Ni Wenye Uwezo juu yao. [Az-Zukhruf (43:41-42)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muqtadir:
1-Tahadhari Na Kudanganyika Kwa Muda Anaowapa Al-Muqtadir Madhalimu:
Tahadhari, ee Mja wa Al-Muqtadir, na kudhani kwamba dhalimu ameachwa; bali Allaah Anampa muda kisha Anamkamata. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي مُوسَى (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لَيُمْلِي لِلظَّالِمِ حَتَّى إِذَا أَخَذَهُ لَمْ يُفْلِتْهُ)) قَالَ: ثُمَّ قَرَأَ: ﴿وَكَذَلِكَ أَخْذُ رَبِّكَ إِذَا أَخَذَ الْقُرَى وَهِيَ ظَالِمَةٌ إِنَّ أَخْذَهُ أَلِيمٌ شَدِيدٌ﴾
Amesimulia Abuu Muwsaa (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Humpa muda dhalimu, mpaka Anapomkamata Hamwachi.” Kisha akasoma: “Na hivyo ndivyo ukamataji wa Rabb wako Anapokamata miji nayo ni dhalimu. Hakika ukamataji Wake ni wenye kuumiza, mkali.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
2-Tafakari Hatima Ya Kaumu Zilizoangamizwa Na Al-Muqtadir:
Tafakari, ee Mja wa Al-Muqtadir, jinsi kila kaumu ilivyokamatwa kwa dhambi yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَكُلًّا أَخَذْنَا بِذَنبِهِ ۖ فَمِنْهُم مَّنْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِ حَاصِبًا وَمِنْهُم مَّنْ أَخَذَتْهُ الصَّيْحَةُ وَمِنْهُم مَّنْ خَسَفْنَا بِهِ الْأَرْضَ وَمِنْهُم مَّنْ أَغْرَقْنَا ۚ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٤٠﴾
Basi kila mmoja Tulimchukua kumwadhibu kwa mujibu wa dhambi yake. Miongoni mwao wale Tuliowapelekea tufani, na miongoni mwao wale waliochukuliwa na ukelele angamizi, na miongoni mwao wale Tuliowadidimiza ardhini, na miongoni mwao wale Tuliowagharikisha. Na Allaah Hakuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao wenyewe. [Al-‘Ankabuwt (29:40)]
3-Tamani Kuwa Karibu Na Maliyk Muqtadir Katika Makao Ya Ukweli:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Muqtadir, kwamba wenye taqwa watakuwa katika makao ya ukweli kwa Mfalme Mwenye Uwezo (rejea Al-Qamar (54:54-55) juu); basi jitahidi kuwa miongoni mwao.
4-Usiifungamanishe Nafsi Yako Na Dunia Inayonyauka:
Tambua, ee Mja wa Al-Muqtadir, kwamba dunia ni kama mmea unaostawi kisha ukanyauka (rejea Al-Kahf (18:45) juu); basi tanguliza mema yanayobakia.
5-Kuwa Na Yakini Kwamba Ahadi Za Al-Muqtadir Zitatimia:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Muqtadir, kwamba Ahadi ya Allaah kwa Waumini na onyo Lake kwa wakanushaji vitatimia, hata kama mtu hatayashuhudia katika uhai wake (rejea Az-Zukhruf (43:41-42) juu).
6-Mche Al-Muqtadir Ukiwa Na Mamlaka Juu Ya Wengine:
Tambua kwamba uwezo wako juu ya wengine ni mdogo mbele ya Uwezo wa Al-Muqtadir juu yako; basi usiwadhulumu walio chini yako.
7-Mkimbilie Al-Muqtadir Unapodhulumiwa:
Kumbuka kwamba Al-Muqtadir Hakughafiliki na matendo ya madhalimu, bali Anawaakhirisha tu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّـهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ ﴿٤٢﴾
Na wala usidhanie kabisa kwamba Allaah Ameghafilika na yale wanayoyatenda madhalimu. Hakika Anawaakhirisha kwa ajili ya Siku ambayo macho yatakodoka. [Ibraahiym (14:42)]
8-Tubia Kabla Ukamataji Wa Al-Muqtadir Haujakufika:
Tambua, ee Mja wa Al-Muqtadir, kwamba muda unaopewa ni fursa ya kutubia, si ruhusa ya kuendelea na maasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَمْلَيْتُ لَهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ ثُمَّ أَخَذْتُهَا وَإِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿٤٨﴾
Na miji mingapi Nimeipa muhula hali ya kuwa imedhulumu, kisha Nikaikamata (Kuiadhibu)? Na Kwangu Pekee ni mahali pa kuishia. [Al-Hajj (22:48)]
9-Tegemea Uwezo Wa Al-Muqtadir Na Si Uwezo Wako:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Muqtadir, kusema: “لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ” (Hapana uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Allaah), kwani ni hazina miongoni mwa hazina za Jannah (rejea 076-Al-Qaadir) [Al-Bukhaariy] [Muslim].
10-Jikinge Kwa ‘Izzah Ya Al-Muqtadir Na Uwezo Wake:
Omba du’aa ukijikinga kwa ‘Izzah ya Al-Muqtadir na Uwezo Wake kutokana na kila shari unayoihisi au kuiogopa: “أَعُوذُ بِعِزَّةِ اللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ” (rejea 022-Al-‘Aziyz) [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy; Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha].
Na Allaah Mjuzi zaidi