Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 081 kati ya 103
Al-Haqq — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Haqq: Haki; Ambaye kuwepo Kwake ni kwa kweli kusikoweza kukanushwa, Maneno Yake ni kweli, Ahadi Yake ni kweli, na ‘ibaadah ya kweli ni Yake Pekee.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara kumi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّهُ يُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَأَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٦﴾

Hayo (Tuliyoyataja ni dalili) kuwa Allaah Ndiye wa Haki, na kwamba Yeye Anahuisha wafu, na kwamba Yeye juu ya kila kitu Ni Muweza. [Al-Hajj (22:6)]

Na Anasema pia:

فَذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ ۖ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ﴿٣٢﴾

Basi Huyo Ndiye Allaah, Rabb wenu wa haki. Na kuna nini baada ya haki ila upotofu? Basi vipi mnageuzwa? [Yuwnus (10:32)]

Maana Ya Al-Haqq:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Haki katika Dhati Yake na Sifa Zake; kuwepo Kwake ni kwa lazima, na kila kinachoabudiwa badala Yake ni baatwil (rejea Luqmaan (31:30) katika 042-Al-‘Aliyy).

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٣٠﴾

Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ndiye wa Haki, na kwamba wale wanaowaomba badala Yake, ni baatwil, na kwamba Allaah Ndiye Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa. [Luqmaan (31:30)]

2-Maneno Yake ni haki, Ahadi Yake ni haki, na kukutana Naye ni haki; na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akikiri hayo katika Swalaah yake ya usiku: “Wewe Ndiye Haki, na Ahadi Yako ni haki, na kukutana Nawe ni haki…” (rejea du’aa kamili katika 007-Al-Qayyuwm) [Al-Bukhaariy] [Muslim].

3-Siku ya Qiyaamah, Atawalipa watu malipo yao ya haki, na watajua kwamba Allaah Ndiye Haki iliyo wazi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَوْمَئِذٍ يُوَفِّيهِمُ اللَّـهُ دِينَهُمُ الْحَقَّ وَيَعْلَمُونَ أَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ الْمُبِينُ ﴿٢٥﴾

Siku hiyo Allaah Atawalipa kikamilifu malipo yao ya haki, na watajua kwamba Allaah Ndiye wa Haki, Mwenye Kubainisha. [An-Nuwr (24:25)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Haqq:

1-Mwabudu Al-Haqq Pekee, Kwani Baada Ya Haki Hakuna Isipokuwa Upotofu:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Haqq, kwamba ukimwacha Allaah, hakuna chochote kilichobaki isipokuwa upotofu (rejea Yuwnus (10:32) juu).

2-Amini Kufufuliwa, Kwani Al-Haqq Anahuisha Wafu:

Tambua kwamba Al-Haqq Ameunganisha kuwa Kwake Haki na kuwahuisha wafu (rejea Al-Hajj (22:6) juu); basi jiandae kwa kukutana Naye.

3-Kuwa Na Yakini Kwamba Haki Itashinda Batili:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Haqq, kwamba batili ni yenye kutoweka, hata ikionekana kuwa na nguvu kwa muda. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ ۚ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا ﴿٨١﴾

Na sema: Haki imekuja, na ubatili umetoweka. Hakika ubatili ni wenye kutoweka daima. [Al-Israa (17:81)]

4-Usichanganye Haki Na Batili, Wala Usiifiche Haki:

Tahadhari, ee Mja wa Al-Haqq, na kuchanganya haki na batili, au kuificha haki ukiijua. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَا تَلْبِسُوا الْحَقَّ بِالْبَاطِلِ وَتَكْتُمُوا الْحَقَّ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٤٢﴾

Na wala msichanganye haki kwa baatwil na mkaficha haki na hali mnajua. [Al-Baqarah (2:42)]

5-Usianeni Kwa Haki Na Subira:

Tambua, ee Mja wa Al-Haqq, kwamba waliosalimika na hasara ni wale wanaousiana haki na subira. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالْعَصْرِ ﴿١﴾ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ ﴿٢﴾ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ ﴿٣﴾

Naapa kwa Al-‘Aswr (zama). Hakika binaadam bila shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana haki, na wakausiana subira. [Al-‘Aswr (103:1-3)]

6-Sema Kweli Hata Ikiwa Dhidi Ya Nafsi Yako:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Haqq, kwamba ukweli unaongoza kwenye wema, na wema unaongoza kwenye Jannah (rejea Hadiyth katika 041-Al-Barr) [Al-Bukhaariy] [Muslim]; basi simama kwa haki hata ikiwa dhidi ya nafsi yako au jamaa zako (rejea An-Nisaa (4:135) katika 007-Al-Qayyuwm).

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ ۚ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّـهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا ۖ فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا ۚ وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١٣٥﴾

Enyi walioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu kwa nguvu zote (na) wenye kutoa ushahidi kwa ajili ya Allaah tu japokuwa ni dhidi ya nafsi zenu, au wazazi wawili, au jamaa wa karibu. Akiwa tajiri au maskini, Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate hawaa mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkikanusha basi hakika Allaah kwa yale myatendayo Ni Mjuzi daima wa Khabari za dhahiri na siri. [An-Nisaa (4:135)]

7-Ikubali Haki Popote Inapotoka:

Tahadhari, ee Mja wa Al-Haqq, na kiburi kinachokuzuia kuikubali haki; kwani Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameeleza kiburi kuwa ni “kuikataa haki na kuwadharau watu” (rejea Hadiyth katika 024-Al-Mutakabbir) [Muslim].

8-Ishike Qur-aan, Kwani Ni Haki Kutoka Kwa Al-Haqq:

Tambua, ee Mja wa Al-Haqq, kwamba Qur-aan imeteremshwa kwa haki na pamoja na haki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَبِالْحَقِّ أَنزَلْنَاهُ وَبِالْحَقِّ نَزَلَ ۗ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا مُبَشِّرًا وَنَذِيرًا ﴿١٠٥﴾

Na kwa haki Tumeiteremsha (Qur-aan), na kwa haki imeteremka. Na Hatukukutuma isipokuwa ni mbashiriaji na mwonyaji tu. [Al-Israa (17:105)]

9-Kumbuka Kwamba Utarejeshwa Kwa Mawlaa Wako Wa Haki:

Kumbuka kwamba baada ya mauti utarudishwa kwa Al-Haqq, Mawlaa wako wa haki, na Yeye Ni Mwepesi mno wa kuhesabu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

ثُمَّ رُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ ۚ أَلَا لَهُ الْحُكْمُ وَهُوَ أَسْرَعُ الْحَاسِبِينَ ﴿٦٢﴾

Kisha watarudishwa (wote waliofishwa) kwa Allaah Rabb wao wa haki. Tanabahi! Hukumu ni Yake Pekee! Naye Ni Mwepesi zaidi wa Kuhisabu kuliko wote wanaohisabu. [Al-An’aam (6:62)]

10-Mwombe Al-Haqq Akuongoze Kwenye Haki:

Omba du’aa Al-Haqq Akuongoze kwenye haki katika yale ambayo watu wamekhitilafiana, kwa du’aa aliyokuwa akifungulia nayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Swalaah yake ya usiku: “…اهْدِنِي لِمَا اخْتُلِفَ فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِكَ…” (Niongoze kwenye haki katika yale yaliyokhitilafiwa kwa Idhini Yako). Rejea du’aa kamili katika 029-Al-Hakam [Muslim].

Na Allaah Mjuzi zaidi