An-Naswiyr: Mwenye kunusuru; Anayewasaidia na kuwanusuru Waumini dhidi ya maadui zao, na hakuna wa kushinda Anayemnusuru.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara nne, na mara nyingi limeambatana na Jina Al-Mawlaa au Al-Waliyy. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِن تَوَلَّوْا فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَوْلَاكُمْ ۚ نِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ﴿٤٠﴾
Na wakikengeuka, basi jueni kwamba Allaah Ni Mawlaa wenu; Mawlaa Mzuri Alioje, na Mnusuruji Mzuri Alioje! [Al-Anfaal (8:40)]
Na Anasema pia:
وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِأَعْدَائِكُمْ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَلِيًّا وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ نَصِيرًا ﴿٤٥﴾
Na Allaah Anawajua zaidi maadui zenu, na Allaah Anatosha kuwa Rafiki Mlinzi na Allaah Anatosha kuwa Mwenye Kunusuru. [An-Nisaa (4:45)]
Maana Ya An-Naswiyr:
1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye kunusuru kwa kweli; Akimnusuru mtu, hakuna wa kumshinda, na Akimwacha, hakuna wa kumnusuru. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِن يَنصُرْكُمُ اللَّـهُ فَلَا غَالِبَ لَكُمْ ۖ وَإِن يَخْذُلْكُمْ فَمَن ذَا الَّذِي يَنصُرُكُم مِّن بَعْدِهِ ۗ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١٦٠﴾
Akikunusuruni Allaah, basi hakuna wa kukushindeni. Na Akikutelekezeni, basi nani atakunusuruni baada Yake? Na kwa Allaah Pekee watawakali Waumini. [Aal-‘Imraan (3:160)]
2-Nusura Yake ni kwa Rusuli Wake na Waumini, duniani na Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ﴿٥١﴾
Hakika Sisi bila shaka Tutawanusuru Rusuli Wetu na wale walioamini katika uhai wa dunia, na Siku watakayosimama mashahidi. [Ghaafir (40:51)]
3-Na Aliwanusuru Waumini katika Badr wakiwa wachache na dhaifu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ بِبَدْرٍ وَأَنتُمْ أَذِلَّةٌ ۖ فَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٢٣﴾
Kwa yakini Allaah Alikunusuruni katika Badr na hali nyinyi ni wanyonge. Basi mcheni Allaah mpate kushukuru. [Aal-‘Imraan (3:123)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, An-Naswiyr:
1-Tafuta Nusura Kwa An-Naswiyr Pekee:
Kumbuka kwamba nusura haitoki kwa wingi wa watu wala silaha, bali inatoka kwa An-Naswiyr (rejea Aal-‘Imraan (3:160) juu); basi mtegemee Yeye.
2-Mnusuru Allaah Kwa Kutii Amri Zake, Naye Atakunusuru:
Tambua, ee Mja wa An-Naswiyr, kwamba Nusura ya Allaah ina sababu zake, na kubwa zaidi ni kuinusuru Dini Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ﴿٧﴾
Enyi walioamini! Mkisaidia kunusuru Dini ya Allaah, (Allaah) Atakunusuruni na Ataithibitisha miguu yenu. [Muhammad (47:7)]
3-Kuwa Na Yakini Kwamba Nusura Ya An-Naswiyr Iko Karibu:
Kumbuka kwamba An-Naswiyr Hawaachi vipenzi Vyake, hata baada ya mitihani mikubwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُم ۖ مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاءُ وَالضَّرَّاءُ وَزُلْزِلُوا حَتَّىٰ يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ مَتَىٰ نَصْرُ اللَّـهِ ۗ أَلَا إِنَّ نَصْرَ اللَّـهِ قَرِيبٌ ﴿٢١٤﴾
Je, mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali bado haijakufikieni (mitihani) kama ya wale waliopita kabla yenu? Ziliwagusa dhiki za umasikini na maafa ya magonjwa na njaa, na wakatetemeshwa mpaka Rasuli na wale walioamini pamoja naye wakasema: Lini itafika Nusura ya Allaah? Tanabahi! Hakika Nusura ya Allaah iko karibu. [Al-Baqarah (2:214)]
4-Mnusuru Nduguyo, Dhalimu Au Mdhulumiwa:
Tambua kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameamrisha kumnusuru ndugu yako kwa namna inayompendeza An-Naswiyr:
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((انْصُرْ أَخَاكَ ظَالِمًا أَوْ مَظْلُومًا)). قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، هَذَا نَنْصُرُهُ مَظْلُومًا، فَكَيْفَ نَنْصُرُهُ ظَالِمًا؟ قَالَ: ((تَأْخُذُ فَوْقَ يَدَيْهِ))
Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mnusuru ndugu yako akiwa dhalimu au akiwa amedhulumiwa.” Wakasema: Yaa Rasula-Allaah! Huyu tunamnusuru akiwa amedhulumiwa; basi vipi tutamnusuru akiwa dhalimu? Akasema: “Umzuie asidhulumu.” [Al-Bukhaariy]
5-Wajali Wanyonge, Kwani Kwa Sababu Yao Mnanusuriwa:
Kumbuka kwamba An-Naswiyr Huwanusuru Waislamu kwa baraka ya du’aa na ikhlaasw ya wanyonge wao. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ مُصْعَبِ بْنِ سَعْدٍ قَالَ: رَأَى سَعْدٌ (رضي الله عنه) أَنَّ لَهُ فَضْلاً عَلَى مَنْ دُونَهُ، فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((هَلْ تُنْصَرُونَ وَتُرْزَقُونَ إِلاَّ بِضُعَفَائِكُمْ))
Amesimulia Mus’ab bin Sa’d: Sa’d (رضي الله عنه) aliona kwamba yeye ana ubora juu ya walio chini yake. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Je, mnanusuriwa na kuruzukiwa isipokuwa kwa sababu ya wanyonge wenu?” [Al-Bukhaariy]
6-Usiwafanye Makafiri Kuwa Wanusuru Wako Badala Ya Waumini:
Tahadhari, ee Mja wa An-Naswiyr, na kutafuta nusura kwa maadui wa Dini; kwani Al-Waliyy wa Waumini Ni Allaah na Rasuli Wake na Waumini (rejea Al-Maaidah (5:55) katika 049-Al-Waliyy). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّمَا وَلِيُّكُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَالَّذِينَ آمَنُوا الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ رَاكِعُونَ ﴿٥٥﴾
Hakika Rafiki wenu Mlinzi ni Allaah na Rasuli Wake na wale walioamini, ambao wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah hali ya kuwa wananyenyekea. [Al-Maaidah (5:55)]
7-Kuwa Na Subira Na Taqwa, Kwani Ni Silaha Za Nusura:
Tambua kwamba An-Naswiyr Anawaahidi nusura wenye subira na taqwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
بَلَىٰ ۚ إِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا وَيَأْتُوكُم مِّن فَوْرِهِمْ هَـٰذَا يُمْدِدْكُمْ رَبُّكُم بِخَمْسَةِ آلَافٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُسَوِّمِينَ ﴿١٢٥﴾
Bali, naam! Mkisubiri na mkashikamana na taqwa na hata wakikujieni kwa ghafla hivi (kukumalizeni), basi (mkitekeleza mawili hayo), Rabb wenu Atakuongezeeni nguvu kwa Malaika elfu tano waliojitia wenyewe na farasi wao alama maalum. [Aal-‘Imraan (3:125)]
8-Tosheka Na An-Naswiyr Kama Mlinzi Na Mnusuru:
Kumbuka kwamba An-Naswiyr Anatosha kuwa Mlinzi na Anatosha kuwa Mnusuru (rejea An-Nisaa (4:45) juu); basi usiogope wingi wa maadui.
9-Mshukuru An-Naswiyr Kwa Kila Ushindi:
Tambua kwamba baada ya nusura na ushindi, An-Naswiyr Aliamrisha tasbiyh, himdi na istighfaar, si kiburi na majivuno. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّـهِ وَالْفَتْحُ ﴿١﴾ وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّـهِ أَفْوَاجًا ﴿٢﴾ فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا ﴿٣﴾
Itakapokuja Nusura ya Allaah na ushindi. Na ukawaona watu wanaingia katika Dini ya Allaah makundi makundi. Basi hapo sabbih na mhimidi Rabb wako (kwa wingi zaidi) na muombe maghfirah. Hakika Yeye daima Ni Mwingi mno wa Kupokea tawbah. [An-Naswr (110:1-3)]
10-Mwombe An-Naswiyr Akunusuru Dhidi Ya Makafiri:
Omba du’aa, ee Mja wa An-Naswiyr, kwa du’aa inayohitimisha Suwrah Al-Baqarah:
لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنتَ مَوْلَانَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴿٢٨٦﴾
Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake. Itapata malipo ya (mema) iliyoyachuma, na itabeba (matokeo ya maovu) iliyojichumia. Rabb wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Rabb wetu! Usitubebeshe mzigo kama Uliowabebesha waliokuwa kabla yetu. Rabb wetu! Usitutwike tusiyoyaweza, na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe Ni Mawlaa wetu, basi Tusaidie tuwashinde watu makafiri. [Al-Baqarah (2:286)]
Na Allaah Mjuzi zaidi