Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 089 kati ya 103
Al-Jamiyl — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Jamiyl: Mzuri; Mwenye uzuri kamili katika Dhati Yake, Majina Yake, Sifa Zake na matendo Yake, na Anayependa uzuri.

Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لاَ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مَنْ كَانَ فِي قَلْبِهِ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ مِنْ كِبْرٍ)). قَالَ رَجُلٌ: إِنَّ الرَّجُلَ يُحِبُّ أَنْ يَكُونَ ثَوْبُهُ حَسَنًا وَنَعْلُهُ حَسَنَةً. قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ جَمِيلٌ يُحِبُّ الْجَمَالَ، الْكِبْرُ بَطَرُ الْحَقِّ وَغَمْطُ النَّاسِ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hataingia Jannah ambaye moyoni mwake mna kiburi uzito wa chembe.” Mtu mmoja akasema: Hakika mtu hupenda nguo yake iwe nzuri na viatu vyake viwe vizuri. Akasema: “Hakika Allaah Ni Mzuri, Anapenda uzuri. Kiburi ni kuikataa haki na kuwadharau watu.” [Muslim]

Maana Ya Al-Jamiyl:

1-Uzuri wa Allaah (سبحانه وتعالى) ni wa Dhati Yake, na hakuna anayeweza kuudiriki duniani; na neema kubwa kabisa ya watu wa Jannah ni kumwona Yeye. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ صُهَيْبٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِذَا دَخَلَ أَهْلُ الْجَنَّةِ الْجَنَّةَ، قَالَ: يَقُولُ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: تُرِيدُونَ شَيْئًا أَزِيدُكُمْ؟ فَيَقُولُونَ: أَلَمْ تُبَيِّضْ وُجُوهَنَا؟ أَلَمْ تُدْخِلْنَا الْجَنَّةَ وَتُنَجِّنَا مِنَ النَّارِ؟ قَالَ: فَيَكْشِفُ الْحِجَابَ، فَمَا أُعْطُوا شَيْئًا أَحَبَّ إِلَيْهِمْ مِنَ النَّظَرِ إِلَى رَبِّهِمْ عَزَّ وَجَلَّ))

Amesimulia Swuhayb (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu wa Jannah watakapoingia Jannah, Allaah (تبارك وتعالى) Atasema: Je, mnataka kitu chochote Nikuzidishieni? Watasema: Je, Hukuzing’arisha nyuso zetu? Je, Hukutuingiza Jannah na Ukatuokoa na moto? Kisha Ataondoa pazia; basi hawatakuwa wamepewa kitu chochote kinachopendeza zaidi kwao kuliko kumtazama Rabb wao (عزّ وجلّ).” [Muslim]

2-Majina Yake yote ni mazuri, na Sifa Zake zote ni za ukamilifu, na matendo Yake yote ni mazuri na ya hikmah; Ameumba kila kitu kwa uzuri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿٣﴾

Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, na Akakutengenezeni sura, kisha Akafanya nzuri zaidi sura zenu, na Kwake ndio mahali pa kuishia. [At-Taghaabun (64:3)]

3-Na Amepamba mbingu kwa nyota. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّا زَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِزِينَةٍ الْكَوَاكِبِ ﴿٦﴾

Hakika Sisi Tumeipamba mbingu ya dunia kwa mapambo ya nyota. [Asw-Swaaffaat (37:6)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Jamiyl:

1-Tambua Kwamba Kujipamba Si Kiburi:

Tambua kwamba Al-Jamiyl Anapenda uzuri; kujipamba kwa nguo nzuri na viatu vizuri si kiburi, bali kiburi ni kuikataa haki na kuwadharau watu (rejea Hadiyth ya Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) juu).

2-Jipambe Unapokwenda Msikitini:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Jamiyl, kwamba Allaah Ameamrisha kujipamba katika kila Msikiti. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾

Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu (ya mavazi ya sitara na twahara) katika kila mahala pa ibaada. Na kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu. Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu. [Al-A’raaf (7:31)]

3-Usiharamishe Pambo Alilolihalalisha Al-Jamiyl:

Tambua kwamba Al-Jamiyl Amewahalalishia Waja Wake pambo na vizuri katika rizki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللَّـهِ الَّتِي أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ ۚ قُلْ هِيَ لِلَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا خَالِصَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٣٢﴾

Sema: Nani aliyeharamisha Mapambo ya Allaah ambayo Amewatolea Waja Wake na vilivyo vizuri katika rizki? Sema: Hivyo ni kwa ajili ya wale walioamini katika uhai wa dunia, (na) makhsusi (kwa Waumini) Siku ya Qiyaamah. Hivyo ndivyo Tunavyofasili waziwazi Aayaat (na Hukmu, Sharia) kwa watu wanaojua. [Al-A’raaf (7:32)]

4-Subiri Subira Nzuri:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Jamiyl, kwamba uzuri unatakiwa hata katika subira: subira isiyo na malalamiko kwa viumbe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَاصْبِرْ صَبْرًا جَمِيلًا﴿٥﴾

Basi subiri, subira njema. [Al-Ma’aarij (70:5)]

5-Samehe Msamaha Mzuri:

Tambua, ee Mja wa Al-Jamiyl, kwamba msamaha mzuri ni ule usio na lawama wala masimbulizi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ ۗ وَإِنَّ السَّاعَةَ لَآتِيَةٌ ۖ فَاصْفَحِ الصَّفْحَ الْجَمِيلَ﴿٨٥﴾

Na Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake isipokuwa kwa haki. Na hakika Saa bila shaka itafika. Basi samehe msamaha mzuri. [Al-Hijr (15:85)]

6-Ukilazimika Kuwaacha Watu, Waache Kwa Uzuri:

Kumbuka kwamba Al-Jamiyl Amefundisha hata namna nzuri ya kujitenga na wanaokuudhi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاهْجُرْهُمْ هَجْرًا جَمِيلًا﴿١٠﴾

Na subiri juu ya yale wayasemayo, na wahame, mhamo mzuri. [Al-Muzzammil (73:10)]

7-Pamba Tabia Yako, Kwani Ndio Uzuri Wa Kweli:

Tambua, ee Mja wa Al-Jamiyl, kwamba uzuri wa ndani wa tabia ni bora kuliko uzuri wa nje. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ مِنْ خِيَارِكُمْ أَحْسَنَكُمْ أَخْلاَقًا))

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika miongoni mwa walio bora wenu ni wenye tabia nzuri kabisa.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

8-Tafakari Uzuri Wa Uumbaji Wa Al-Jamiyl:

Tafakari, ee Mja wa Al-Jamiyl, uzuri wa mbingu na nyota zake (rejea Asw-Swaaffaat (37:6) juu), na uzuri wa wanyama na mimea; kila uzuri unaouona ni athari ya Uumbaji wa Al-Jamiyl.

9-Tamani Kumwona Al-Jamiyl Katika Jannah:

Kumbuka kwamba neema kubwa kabisa ya Jannah ni kumtazama Al-Jamiyl (rejea Hadiyth ya Swuhayb (رضي الله عنه) juu); basi fanya amali zinazokufikisha huko.

10-Mwombe Al-Jamiyl Akuongoze Kwenye Tabia Nzuri Kabisa:

Omba du’aa, ee Mja wa Al-Jamiyl, kama alivyokuwa akiomba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kufungua Swalaah:

عَنْ عَلِيِّ بْنِ أَبِي طَالِبٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ كَانَ إِذَا قَامَ إِلَى الصَّلاَةِ قَالَ: ((... وَاهْدِنِي لأَحْسَنِ الأَخْلاَقِ لاَ يَهْدِي لأَحْسَنِهَا إِلاَّ أَنْتَ، وَاصْرِفْ عَنِّي سَيِّئَهَا لاَ يَصْرِفُ عَنِّي سَيِّئَهَا إِلاَّ أَنْتَ ...))

Amesimulia ‘Aliy bin Abiy Twaalib (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anaposimama kuswali husema: …

وَاهْدِنِي لأَحْسَنِ الأَخْلاَقِ لاَ يَهْدِي لأَحْسَنِهَا إِلاَّ أَنْتَ، وَاصْرِفْ عَنِّي سَيِّئَهَا لاَ يَصْرِفُ عَنِّي سَيِّئَهَا إِلاَّ أَنْتَ

Na Uniongoze kwenye tabia nzuri kabisa, hakuna anayeongoza kwenye nzuri kabisa isipokuwa Wewe; na Uniepushe na tabia mbaya, hakuna anayeniepusha nazo isipokuwa Wewe … [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi