Al-Baasitw: Mwenye kukunjua; Anayekunjua rizki kwa Amtakaye, Anayekunjua Mkono Wake kupokea tawbah, na Anayekunjua nyoyo kwa furaha na imaan.
Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah pamoja na Jina Al-Qaabidhw, katika Hadiyth ya Anas (رضي الله عنه): “Hakika Allaah Ndiye Mpanga bei, Al-Qaabidhw, Al-Baasitw, Ar-Raaziq…” [Abuu Daawuwd (3451), At-Tirmidhiy (1314); Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha] (rejea 090-Al-Qaabidhw). Na maana yake imekuja katika Qur-aan:
مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ أَضْعَافًا كَثِيرَةً ۚ وَاللَّـهُ يَقْبِضُ وَيَبْسُطُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢٤٥﴾
Ni nani atakayemkopesha Allaah karadha nzuri kisha (Allaah) Amzidishie mzidisho mwingi. Na Allaah Anakunja na Anakunjua, na Kwake mtarejeshwa. [Al-Baqarah (2:245)]
Na kama ilivyobainishwa katika 090-Al-Qaabidhw, ‘Ulamaa wamependekeza Majina haya mawili yatajwe pamoja, ili kuonyesha ukamilifu wa Uwezo na Hikmah ya Allaah.
Maana Ya Al-Baasitw:
1-Anakunjua rizki kwa Amtakaye kwa Ujuzi Wake na Hikmah Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ رَبَّكَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿٣٠﴾
Hakika Rabb wako Anamkunjulia rizki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Hakika Yeye daima kwa Waja Wake Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na za siri, Mwenye Kuona yote. [Al-Israa (17:30)]
2-Mikono Yake yote miwili imekunjuliwa, Anatoa Atakavyo; Ahlus-Sunnah wanaithibitisha Sifa hii bila kuifananisha wala kuuliza namna yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَقَالَتِ الْيَهُودُ يَدُ اللَّـهِ مَغْلُولَةٌ ۚ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا بِمَا قَالُوا ۘ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ ۚ وَلَيَزِيدَنَّ كَثِيرًا مِّنْهُم مَّا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ طُغْيَانًا وَكُفْرًا ۚ وَأَلْقَيْنَا بَيْنَهُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ ۚ كُلَّمَا أَوْقَدُوا نَارًا لِّلْحَرْبِ أَطْفَأَهَا اللَّـهُ ۚ وَيَسْعَوْنَ فِي الْأَرْضِ فَسَادًا ۚ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ ﴿٦٤﴾
Na Mayahudi wakasema: Mkono wa Allaah umefumbwa. Mikono yao ndio iliyofumbwa na wamelaaniwa kwa yale waliyoyasema! Bali Mikono Yake (Allaah) imefumbuliwa Hutoa Atakavyo. Kwa yakini yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako, yatawazidisha wengi miongoni mwao upindukaji mipaka ya kuasi na kufuru. Na Tumewatilia baina yao uadui na bughudha mpaka Siku ya Qiyaamah. Kila wanapouwasha moto wa vita (dhidi yako), Allaah Huuzima. Na wanapania kwa bidii kufanya ufisadi katika ardhi. Na Allaah Hapendi mafisadi. [Al-Maaidah (5:64)]
3-Anakunjua Mkono Wake usiku na mchana kupokea tawbah ya Waja Wake (rejea Hadiyth ya Abuu Muwsaa (رضي الله عنه) katika 038-Al-Ghaffaar) [Muslim].
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Baasitw:
1-Tambua Kwamba Kukunjuliwa Rizki Si Dalili Ya Kupendwa Na Allaah:
Tambua kwamba Al-Qaabidhw Al-Baasitw Anakunjua rizki kwa Amtakaye, Muumini na kafiri; kwa hiyo wingi wa mali si kipimo cha kheri mbele ya Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٦﴾ وَمَا أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُم بِالَّتِي تُقَرِّبُكُمْ عِندَنَا زُلْفَىٰ إِلَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ جَزَاءُ الضِّعْفِ بِمَا عَمِلُوا وَهُمْ فِي الْغُرُفَاتِ آمِنُونَ ﴿٣٧﴾
Sema: Hakika Rabb wangu Anamkunjulia rizki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye), lakini watu wengi hawajui. Na si mali zenu wala watoto wenu ambavyo vitakukurubisheni Kwetu muwe karibu isipokuwa yule aliyeamini na akatenda mema, basi hao watapata malipo maradufu kutokana na yale waliyoyatenda, nao watakuwa katika maghorofa (Jannah) wenye amani. [Saba-a (34:36-37)]
2-Mshukuru Al-Qaabidhw Al-Baasitw Unapokunjuliwa Rizki:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Qaabidhw Al-Baasitw, kwamba neema inadumu kwa shukurani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾
Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (Neema Zangu), na mkikufuru, basi hakika Adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym (14:7)]
3-Usifanye Uasi Unapokunjuliwa Rizki:
Tahadhari kwamba Al-Qaabidhw Al-Baasitw Anajua kwamba lau Angewakunjulia waja wote rizki, wangefanya uasi ardhini; basi usiwe miongoni mwao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ بَسَطَ اللَّـهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَـٰكِن يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَّا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ﴿٢٧﴾
Na lau kama Allaah Angelikunjua rizki kwa Waja Wake, basi wangeruka mipaka katika ardhi. Lakini Anateremsha kwa kadiri ya Akitakacho. Hakika Yeye kwa Waja Wake Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:27)]
4-Unga Ukoo Wako Ukunjuliwe Rizki:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Qaabidhw Al-Baasitw, Hadiyth ya Anas (رضي الله عنه): “Anayependa kukunjuliwa rizki yake, au kurefushiwa umri wake, basi aunge ukoo wake.” (rejea 044-Ar-Raaziq) [Al-Bukhaariy] [Muslim].
5-Kunjua Mkono Wako Kwa Swadaqah, Na Al-Qaabidhw Al-Baasitw Atakurudishia:
Tambua kwamba Al-Qaabidhw Al-Baasitw Hulipa badala ya kila kinachotolewa katika Njia Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٣٩﴾
Sema: Hakika Rabb wangu Anamkunjulia rizki Amtakaye kati ya Waja Wake na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa, Naye Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Saba-a (34:39)]
6-Usifanye Ubadhirifu Hata Ukikunjuliwa:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Qaabidhw Al-Baasitw, kwamba kukunjuliwa rizki si ruhusa ya ubadhirifu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَلَا تُبَذِّرْ تَبْذِيرًا ﴿٢٦﴾ إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ۖ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا ﴿٢٧﴾
Na mpe jamaa wa karibu haki yake, na masikini, na msafiri (aliyeharibikiwa), na wala usifanye ubadhirifu wa ufujaji mkubwa. Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashaytwaan, na shaytwaan amekuwa ni mwingi wa kumkufuru Rabb wake. [Al-Israa (17:26-27)]
7-Mwelekee Al-Qaabidhw Al-Baasitw Kwa Tawbah, Kwani Mkono Wake Umekunjuliwa:
Tambua kwamba Al-Qaabidhw Al-Baasitw Anakunjua Mkono Wake usiku na mchana kupokea tawbah, mpaka jua lichomoze kutoka magharibi; basi usiakhirishe kutubia.
8-Mwombe Al-Qaabidhw Al-Baasitw Akukunjulie Kifua Chako:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Qaabidhw Al-Baasitw, kwamba kukunjuliwa kifua kwa imaan ni neema kubwa kuliko kukunjuliwa mali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَمَن يُرِدِ اللَّـهُ أَن يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ ۖ وَمَن يُرِدْ أَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا كَأَنَّمَا يَصَّعَّدُ فِي السَّمَاءِ ۚ كَذَٰلِكَ يَجْعَلُ اللَّـهُ الرِّجْسَ عَلَى الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٢٥﴾
Basi yule ambaye Allaah Anataka kumhidi, Humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na yule ambaye Anataka kumpotoa, Hufanya kifua chake kiwe na dhiki chenye kubana kama kwamba anapanda kwa tabu mbinguni. Hivyo ndivyo Allaah Anavyojaalia adhabu (au Anavyowasalitishia shaytwaan) kwa wale wasioamini. [Al-An’aam (6:125)]
9-Kunjua Uso Wako Kwa Ndugu Zako:
Tambua kwamba Al-Qaabidhw Al-Baasitw Anapenda upole na uchangamfu; na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ لِيَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((لاَ تَحْقِرَنَّ مِنَ الْمَعْرُوفِ شَيْئًا، وَلَوْ أَنْ تَلْقَى أَخَاكَ بِوَجْهٍ طَلْقٍ))
Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniambia: “Usidharau jema lolote, hata kama ni kukutana na ndugu yako kwa uso mkunjufu.” [Muslim]
10-Mwombe Al-Qaabidhw Al-Baasitw Kheri Ya Dunia Na Aakhirah:
Omba du’aa, ee Mja wa Al-Qaabidhw Al-Baasitw, kwa du’aa aliyokuwa akiikithirisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿٢٠١﴾
Na miongoni mwao kuna wasemao: Rabb wetu Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto. [Al-Baqarah (2:201)]
Na Allaah Mjuzi zaidi