Al-Mu’twiy: Mwenye kutoa; Anayetoa kila neema kwa viumbe Vyake, Anayempa Amtakaye kwa Hikmah Yake, wala hakuna wa kuzuia Alichokitoa.
Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنْ مُعَاوِيَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((مَنْ يُرِدِ اللَّهُ بِهِ خَيْرًا يُفَقِّهْهُ فِي الدِّينِ، وَاللَّهُ الْمُعْطِي وَأَنَا الْقَاسِمُ))
Amesimulia Mu’aawiyah (رضي الله عنه): Nimemsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Ambaye Allaah Anamtakia kheri, Humfahamisha Dini; na Allaah Ndiye Mwenye kutoa, nami ni mgawaji.” [Al-Bukhaariy]
Maana Ya Al-Mu’twiy:
1-Kila kitu Ametoa Allaah (سبحانه وتعالى); Amekipa kila kiumbe umbo lake kisha Akakiongoza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾
(Muwsaa) akasema: Rabb wetu ni Yule Aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha Akakiongoza. [Twaahaa (20:50)]
2-Utoaji Wake unawaenea Waumini na makafiri duniani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
كُلًّا نُّمِدُّ هَـٰؤُلَاءِ وَهَـٰؤُلَاءِ مِنْ عَطَاءِ رَبِّكَ ۚ وَمَا كَانَ عَطَاءُ رَبِّكَ مَحْظُورًا ﴿٢٠﴾
Wote hao Tunawakunjulia - hawa na hao - katika Hiba za Rabb wako. Na hazikuwa Hiba za Rabb wako zenye kuzuiliwa. [Al-Israa (17:20)]
3-Na utoaji Wake kwa Waumini Aakhirah hautakatika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَمَّا الَّذِينَ سُعِدُوا فَفِي الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ ۖ عَطَاءً غَيْرَ مَجْذُوذٍ﴿١٠٨﴾
Na ama wale walio furahani, basi watakuwa katika Jannah, watadumu humo zitakavyodumu mbingu na ardhi isipokuwa Atakavyo Rabb wako. Ni hiba isiyokatizwa. [Huwd (11:108)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Mu’twiy:
1-Tambua Kwamba Al-Mu’twiy Ndiye Mtoaji Halisi:
Tambua kwamba kila kinachokufikia kupitia watu kinatoka kwa Al-Mu’twiy, na watu ni njia tu; basi mshukuru Yeye kwanza, kisha uwashukuru watu.
2-Zawadi Kubwa Kabisa Ya Al-Mu’twiy Ni Kufahamu Dini:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Mu’twiy, kwamba katika Hadiyth ya Jina hili, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametaja kufahamishwa Dini kuwa ndiyo alama ya kutakiwa kheri; basi jitahidi kujifunza.
3-Kuwa Na Yakini Kwamba Hakuna Wa Kuzuia Anachokitoa Al-Mu’twiy:
Tambua kwamba Al-Mu’twiy Akitaka kukupa, hakuna wa kuzuia; basi mwombe Yeye, na useme baada ya Swalaah: “اللَّهُمَّ لاَ مَانِعَ لِمَا أَعْطَيْتَ…” (rejea 017-Al-Maliyk) [Al-Bukhaariy] [Muslim].
4-Ridhika Na Alichokupa Al-Mu’twiy:
Kumbuka kwamba Al-Mu’twiy Aliahidi Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kumpa mpaka aridhike. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَسَوْفَ يُعْطِيكَ رَبُّكَ فَتَرْضَىٰ ﴿٥﴾
Na bila shaka Rabb wako Atakupa na utaridhika. [Adhw-Dhwuhaa (93:5)]
5-Mkono Wa Juu Ni Bora Kuliko Mkono Wa Chini:
Tambua, ee Mja wa Al-Mu’twiy, kwamba kutoa ni bora kuliko kuomba. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ حَكِيمِ بْنِ حِزَامٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((الْيَدُ الْعُلْيَا خَيْرٌ مِنَ الْيَدِ السُّفْلَى، وَابْدَأْ بِمَنْ تَعُولُ))
Amesimulia Hakiym bin Hizaam (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mkono wa juu (unaotoa) ni bora kuliko mkono wa chini (unaopokea); na anza na wale unaowakimu.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
6-Shukuru Kwa Kheri Nyingi Alizokupa Al-Mu’twiy:
Kumbuka kwamba Al-Mu’twiy Alimpa Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kheri nyingi, na Akamwamrisha kuswali na kuchinja kwa ajili Yake kama shukurani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ﴿١﴾ فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾ إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ ﴿٣﴾
Hakika Sisi Tumekupa Al-Kawthar. Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja. Hakika mbaya wako, yeye ndiye atakayekatiliwa mbali (kizazi na kila kheri). [Al-Kawthar (108:1-3)]
7-Usiwaonee Wivu Wengine Kwa Walichopewa:
Tahadhari, ee Mja wa Al-Mu’twiy, na kutamani kilichopewa wengine kwa husuda; bali mwombe Allaah katika Fadhila Zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَتَمَنَّوْا مَا فَضَّلَ اللَّـهُ بِهِ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبُوا ۖ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبْنَ ۚ وَاسْأَلُوا اللَّـهَ مِن فَضْلِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٣٢﴾
Wala msitamani ambayo Allaah Amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu katika waliyoyachuma, na wanawake wana sehemu katika waliyoyachuma. Na muombeni Allaah katika Fadhila Zake. Hakika Allaah daima Ni Mjuzi wa kila kitu. [An-Nisaa (4:32)]
8-Toa Kama Ulivyopewa:
Tambua kwamba ulichonacho ni utoaji wa Al-Mu’twiy; basi toa katika hicho kabla ya mauti kukufikia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ﴿١٠﴾
Na toeni katika yale Tuliyokuruzukuni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti akasema: Rabb wangu! Lau Ungeliniakhirisha mpaka muda wa karibu hivi, nikatoa swadaqah na nikawa miongoni mwa Swalihina. [Al-Munaafiquwn (63:10)]
9-Omba Kutoka Kwa Al-Mu’twiy Kila Kitu:
Kumbuka kwamba Al-Mu’twiy Hachoki kutoa, wala hazina Zake hazipungui (rejea Hadiyth ya Mkono wa Allaah uliojaa katika 084-Al-Wahhaab) [Al-Bukhaariy] [Muslim].
10-Mwombe Al-Mu’twiy Kheri Ya Dunia Na Aakhirah:
Omba du’aa, ee Mja wa Al-Mu’twiy, kama walivyoomba Waumini:
رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَىٰ رُسُلِكَ وَلَا تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿١٩٤﴾
Rabb wetu! Tupe pia Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah. Hakika Wewe Huendi kinyume na miadi (Yako). [Aal-‘Imraan (3:194)]
Na Allaah Mjuzi zaidi