Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 093 kati ya 103
Al-Muqaddim — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Muqaddim: Mwenye kutanguliza; Anayetanguliza Amtakaye na Akitakacho kwa Hikmah Yake, katika uumbaji, katika daraja na katika fadhila.

Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah, likiwa pamoja na Jina Al-Muakhkhir:

عَنْ عَلِيِّ بْنِ أَبِي طَالِبٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ كَانَ يَقُولُ فِي آخِرِ صَلاَتِهِ: ((اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي مَا قَدَّمْتُ وَمَا أَخَّرْتُ، وَمَا أَسْرَرْتُ وَمَا أَعْلَنْتُ، وَمَا أَسْرَفْتُ، وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي، أَنْتَ الْمُقَدِّمُ وَأَنْتَ الْمُؤَخِّرُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ))

Amesimulia ‘Aliy bin Abiy Twaalib (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema mwishoni mwa Swalaah yake:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي مَا قَدَّمْتُ وَمَا أَخَّرْتُ، وَمَا أَسْرَرْتُ وَمَا أَعْلَنْتُ، وَمَا أَسْرَفْتُ، وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي، أَنْتَ الْمُقَدِّمُ وَأَنْتَ الْمُؤَخِّرُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ

Yaa Allaah! Nighufurie niliyoyatanguliza na niliyoyaakhirisha, niliyoyaficha na niliyoyadhihirisha, niliyopindukia mipaka, na Unayoyajua zaidi kuliko mimi. Wewe Ndiye Al-Muqaddim (Mwenye kutanguliza), na Wewe Ndiye Al-Muakhkhir (Mwenye kuakhirisha); hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe. [Muslim]

Na kama Al-Qaabidhw na Al-Baasitw, Majina haya mawili hutajwa pamoja; na makala hii inasomwa pamoja na 094-Al-Muakhkhir.

Maana Ya Al-Muqaddim:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Amewatanguliza Manabii juu ya watu wengine, na Akawatanguliza baadhi ya Manabii juu ya wengine. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ ۚ وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ ۗ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِن بَعْدِهِم مِّن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَـٰكِنِ اخْتَلَفُوا فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ وَمِنْهُم مَّن كَفَرَ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ ﴿٢٥٣﴾

Rusuli hao, Tumewafadhilisha baadhi yao juu ya wengine. Miongoni mwao kuna aliyesemeshwa na Allaah, na Akawapandisha baadhi yao vyeo. Na Tukampa ‘Iysaa mwana wa Maryam hoja bayana na Tukamtia nguvu kwa Ruwh Al-Qudus (Jibriyl عليه السلام). Na lau Angelitaka Allaah wasingelipigana waliokuwa baada yao, baada ya kuwajia hoja bayana. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo miongoni mwao ambao waliamini na wengine ambao walikufuru. Na lau kuwa Allaah Angelitaka, wasingelipigana lakini Allaah Anafanya Atakavyo. [Al-Baqarah (2:253)]

2-Anawatanguliza wanaokimbilia kheri katika daraja za juu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ ﴿١٠﴾ أُولَـٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ ﴿١١﴾

Na waliotangulia mbele, watatangulia mbele. Hao ndio watakaokurubishwa. [Al-Waaqi’ah (56:10-11)]

3-Ametanguliza maonyo Yake kabla ya adhabu, ili pasiwe na hoja. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُم بِالْوَعِيدِ﴿٢٨﴾

(Allaah) Atasema: Msibishane Kwangu, na hali Nilishakukadimishieni Onyo Langu! [Qaaf (50:28)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muqaddim:

1-Kimbilia Kheri Ili Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Akutanguliza:

Kumbuka kwamba Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Anawatanguliza waliotangulia kwa amali njema. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ﴿١٣٣﴾

Na kimbilieni maghfirah kutoka kwa Rabb wenu, na Jannah upana wake ni wa mbingu na ardhi imeandaliwa kwa wenye taqwa. [Aal-‘Imraan (3:133)]

2-Usimtangulie Allaah Na Rasuli Wake:

Tahadhari, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, na kutanguliza rai yako juu ya Amri ya Allaah na Sunnah ya Rasuli Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿١﴾

Enyi walioamini! Msikadimishe (lolote) mbele ya Allaah na Rasuli Wake. Na mcheni Allaah, hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Al-Hujuraat (49:1)]

3-Ridhika Na Daraja Aliyokupa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir:

Tambua kwamba Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Hutanguliza Amtakaye kwa Hikmah Yake; basi usiwe na husuda kwa aliyetangulizwa.

4-Tanguliza Mema Kwa Ajili Ya Kesho Yako:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba utakutana na yale uliyoyatanguliza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١٨﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myatendayo. [Al-Hashr (59:18)]

5-Tanguliza Swalaah Kwa Wakati Wake:

Tambua kwamba amali inayopendwa zaidi na Al-Muqaddim Al-Muakhkhir ni Swalaah kwa wakati wake (rejea Hadiyth ya Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) katika 041-Al-Barr) [Al-Bukhaariy] [Muslim].

6-Tanguliza Safu Za Mbele Katika Swalaah:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba kuwahi Msikitini na safu za mbele ni miongoni mwa njia za kutangulizwa kwa Allaah; na wanaoendelea kuchelewa, Allaah Huwachelewesha (rejea 094-Al-Muakhkhir).

7-Tanguliza Mapenzi Ya Allaah Na Rasuli Wake Kuliko Vyote:

Tambua kwamba anayemtanguliza Al-Muqaddim Al-Muakhkhir katika mapenzi yake, Allaah Humtanguliza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ إِن كَانَ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ وَإِخْوَانُكُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ وَعَشِيرَتُكُمْ وَأَمْوَالٌ اقْتَرَفْتُمُوهَا وَتِجَارَةٌ تَخْشَوْنَ كَسَادَهَا وَمَسَاكِنُ تَرْضَوْنَهَا أَحَبَّ إِلَيْكُم مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَجِهَادٍ فِي سَبِيلِهِ فَتَرَبَّصُوا حَتَّىٰ يَأْتِيَ اللَّـهُ بِأَمْرِهِ ۗ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ﴿٢٤﴾

Sema: Ikiwa baba zenu, na watoto wenu, na ndugu zenu, na wake (au waume) zenu, na jamaa zenu, na mali mliyoichuma, na biashara mnayoikhofia kuharibika kwake, na majumba mnayoridhika nayo, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Allaah na Rasuli Wake na kufanya Jihaad katika Njia Yake, basi ngojeeni mpaka Allaah Alete Amri Yake (ya adhabu). Na Allaah Hawahidi watu mafasiki. [At-Tawbah (9:24)]

8-Kumbuka Kwamba Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Hutanguliza Ajali Ya Amtakaye:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba ajali ikifika haitangulizwi wala haiakhirishwi kwa saa moja; basi jiandae. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِظُلْمِهِم مَّا تَرَكَ عَلَيْهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۖ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ لَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً ۖ وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ﴿٦١﴾

Na kama Allaah Angeliwachukulia watu kwa dhulma zao, Asingeliacha juu ya ardhi kiumbe chochote, lakini Anawaakhirisha mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Basi utakapofika muda wao hawatoakhirisha saa na wala hawatotanguliza. [An-Nahl (16:61)]

9-Tanguliza Tawbah Kabla Ya Kuchelewa:

Tambua, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba anayetanguliza tawbah yake hupata Maghfirah, na anayeiakhirisha huenda mauti yakamfikia kabla yake (rejea An-Nisaa (4:17-18) katika 039-At-Tawwaab).

إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُولَـٰئِكَ يَتُوبُ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١٧﴾ وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٨﴾

Hakika tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujahili kisha wakatubia haraka, basi hao Allaah Anapokea tawbah yao. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote. Lakini tawbah si kwa wale wanaofanya maovu mpaka mauti yanapomjia mmoja wao ndipo aseme: Hakika mimi sasa nimetubu. Na wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo. [An-Nisaa (4:17-18)]

10-Mwombe Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Maghfirah Mwishoni Mwa Swalaah:

Omba du’aa, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwa du’aa ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) iliyotajwa juu, mwishoni mwa Swalaah yako kabla ya salaam.

Na Allaah Mjuzi zaidi