Al-Muakhkhir: Mwenye kuakhirisha; Anayeakhirisha Amtakaye na Akitakacho kwa Hikmah Yake, Anayewapa madhalimu muda, na Anayeakhirisha adhabu ili waja watubie.
Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah, likiwa pamoja na Jina Al-Muqaddim:
عَنْ عَلِيِّ بْنِ أَبِي طَالِبٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ كَانَ يَقُولُ فِي آخِرِ صَلاَتِهِ: ((اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي مَا قَدَّمْتُ وَمَا أَخَّرْتُ، وَمَا أَسْرَرْتُ وَمَا أَعْلَنْتُ، وَمَا أَسْرَفْتُ، وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي، أَنْتَ الْمُقَدِّمُ وَأَنْتَ الْمُؤَخِّرُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ))
Amesimulia ‘Aliy bin Abiy Twaalib (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema mwishoni mwa Swalaah yake:
اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي مَا قَدَّمْتُ وَمَا أَخَّرْتُ، وَمَا أَسْرَرْتُ وَمَا أَعْلَنْتُ، وَمَا أَسْرَفْتُ، وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي، أَنْتَ الْمُقَدِّمُ وَأَنْتَ الْمُؤَخِّرُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ
Yaa Allaah! Nighufurie niliyoyatanguliza na niliyoyaakhirisha, niliyoyaficha na niliyoyadhihirisha, niliyopindukia mipaka, na Unayoyajua zaidi kuliko mimi. Wewe Ndiye Al-Muqaddim (Mwenye kutanguliza), na Wewe Ndiye Al-Muakhkhir (Mwenye kuakhirisha); hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe. [Muslim]
Makala hii inasomwa pamoja na 093-Al-Muqaddim.
Maana Ya Al-Muakhkhir:
1-Anaakhirisha adhabu ya waja kwa Upole Wake mpaka muda maalumu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِظُلْمِهِم مَّا تَرَكَ عَلَيْهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۖ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ لَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً ۖ وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ﴿٦١﴾
Na kama Allaah Angeliwachukulia watu kwa dhulma zao, Asingeliacha juu ya ardhi kiumbe chochote, lakini Anawaakhirisha mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Basi utakapofika muda wao hawatoakhirisha saa na wala hawatotanguliza. [An-Nahl (16:61)]
2-Anaakhirisha Qiyaamah mpaka muda uliohesabiwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا نُؤَخِّرُهُ إِلَّا لِأَجَلٍ مَّعْدُودٍ﴿١٠٤﴾
Na hatuiakhirishi isipokuwa kwa muda maalumu unaohesabiwa. [Huwd (11:104)]
3-Ajali ya kila nafsi ikifika Haiakhirishi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّـهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا ۚ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١١﴾
Lakini Allaah Haiakhirishi kamwe nafsi yoyote inapokuja ajali yake, na Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myatendayo. [Al-Munaafiquwn (63:11)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muakhkhir:
1-Usidanganyike Na Kuakhirishwa Kwa Adhabu:
Tahadhari, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, na kudhani kwamba kuakhirishwa kwa adhabu ni kusahauliwa; bali ni muda wa kutubia (rejea An-Nahl (16:61) juu).
2-Usiwe Miongoni Mwa Wanaojichelewesha Mpaka Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Akawachelewesha:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaona Swahaba wakichelewa kwenye safu za mbele, akasema:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) رَأَى فِي أَصْحَابِهِ تَأَخُّرًا فَقَالَ لَهُمْ: ((تَقَدَّمُوا فَأْتَمُّوا بِي، وَلْيَأْتَمَّ بِكُمْ مَنْ بَعْدَكُمْ، لاَ يَزَالُ قَوْمٌ يَتَأَخَّرُونَ حَتَّى يُؤَخِّرَهُمُ اللَّهُ))
Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliona Swahaba zake wakichelewa (nyuma), akawaambia: “Songeni mbele mnifuate, na walio nyuma yenu wawafuate nyinyi. Watu hawaachi kujichelewesha mpaka Allaah Awachelewesha.” [Muslim]
3-Tumia Muda Anaokupa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Kabla Haujaisha:
Tambua, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba mauti yakifika hutaweza kuomba muda zaidi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ﴿١٠﴾
Na toeni katika yale Tuliyokuruzukuni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti akasema: Rabb wangu! Lau Ungeliniakhirisha mpaka muda wa karibu hivi, nikatoa swadaqah na nikawa miongoni mwa Swalihina. [Al-Munaafiquwn (63:10)]
4-Subiri, Kwani Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Anaakhirisha Madhalimu Kwa Hikmah:
Kumbuka kwamba Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Hakughafiliki na madhalimu, bali Anawaakhirisha mpaka Siku ya kukodoa macho (rejea Ibraahiym (14:42) katika 021-Al-Muhaymin).
وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّـهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ ﴿٤٢﴾
Na wala usidhanie kabisa kwamba Allaah Ameghafilika na yale wanayoyatenda madhalimu. Hakika Anawaakhirisha kwa ajili ya Siku ambayo macho yatakodoka. [Ibraahiym (14:42)]
5-Usiakhirishe Tawbah Kwa Kutegemea Muda:
Tambua, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba anayeakhirisha tawbah mpaka mauti yamfikie, tawbah yake haikubaliwi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٨﴾
Lakini tawbah si kwa wale wanaofanya maovu mpaka mauti yanapomjia mmoja wao ndipo aseme: Hakika mimi sasa nimetubu. Na wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo. [An-Nisaa (4:18)]
6-Ridhika Na Kucheleweshwa Kwa Matakwa Yako:
Kumbuka kwamba huenda Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Akaakhirisha jambo unalolitaka kwa kheri usiyoijua; basi ridhika na mwombe Yeye. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾
Mmeandikiwa sharia kupigana vita nako kunachukiza mno kwenu. Lakini asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni la kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah (2:216)]
7-Usiakhirishe Kheri Mpaka Ukose Fursa:
Tambua, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba kuakhirisha amali njema ni njia ya shaytwaan; basi kimbilia kheri kabla ya vizuizi.
8-Kumbuka Kwamba Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Ameakhirisha Qiyaamah Kwa Muda Uliohesabiwa:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba Qiyaamah haijaakhirishwa isipokuwa kwa muda uliohesabiwa (rejea Huwd (11:104) juu); basi jiandae nayo.
9-Muombe Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Akuakhirishie Adhabu Na Akupe Muda Wa Kutubia:
Tambua, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwamba katika kuakhirishwa kwa adhabu kuna Rehma ya Allaah; basi tumia kila siku mpya kama fursa ya kurudi Kwake.
10-Mwombe Al-Muqaddim Al-Muakhkhir Maghfirah:
Omba du’aa, ee Mja wa Al-Muqaddim Al-Muakhkhir, kwa du’aa ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) iliyotajwa juu, ukiomba Maghfirah ya uliyoyatanguliza na uliyoyaakhirisha.
Na Allaah Mjuzi zaidi