Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 095 kati ya 103
Al-Mannaan — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Mannaan: Mwingi wa kuneemesha; Anayetoa neema kubwa bila ya kuombwa wala kutarajia malipo, na Mwenye kustahiki kuzitaja Neema Zake juu ya Waja Wake.

Jina hili tukufu limethibiti katika du’aa ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema kwamba mwenye kuiomba ameomba kwa Jina Tukufu kabisa la Allaah: “…لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ الْمَنَّانُ، بَدِيعُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، يَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ، يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ” [Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Maajah; Al-Haakim ameisahihisha kwa sharti ya Muslim] (rejea Hadiyth kamili katika 007-Al-Qayyuwm).

Na maana yake imekuja katika Qur-aan:

لَقَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ إِذْ بَعَثَ فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْ أَنفُسِهِمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١٦٤﴾

Kwa yakini Allaah Amewafanyia fadhila Waumini pale Alipomtuma kwao Rasuli miongoni mwao wenyewe, anawasomea Aayaat Zake na anawatakasa na anawafunza Kitabu na Hikmah (Sunnah), japokuwa walikuwa kabla katika upotofu bayana. [Aal-‘Imraan (3:164)]

Maana Ya Al-Mannaan:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye kuneemesha kwa neema kubwa kabisa, ikiwemo neema ya kutumwa kwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) (rejea Aal-‘Imraan (3:164) juu).

2-Neema ya imaan ni Neema Yake juu ya waja, si neema yao juu Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَمُنُّونَ عَلَيْكَ أَنْ أَسْلَمُوا ۖ قُل لَّا تَمُنُّوا عَلَيَّ إِسْلَامَكُم ۖ بَلِ اللَّـهُ يَمُنُّ عَلَيْكُمْ أَنْ هَدَاكُمْ لِلْإِيمَانِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿١٧﴾

Wanadhani wamekufanyia fadhila kwamba wamesilimu? Sema: Msidhani mmenifanyia fadhila kusilimu kwenu. Bali Allaah Amekufanyieni fadhila kwamba Amekuongozeni kwenye imaan mkiwa ni wakweli. [Al-Hujuraat (49:17)]

3-Anawaneemesha wanyonge na kuwafanya viongozi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَنُرِيدُ أَن نَّمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ ﴿٥﴾

Na Tukataka Tuwafanyie fadhila wale waliokandamizwa katika ardhi, na Tuwafanye viongozi na Tuwafanye wenye kurithi. [Al-Qaswasw (28:5)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Mannaan:

1-Tambua Kwamba Imaan Yako Ni Neema Ya Al-Mannaan Juu Yako:

Tambua kwamba Al-Mannaan Ndiye Aliyekuongoza kwenye imaan; basi usimsimbulie Allaah wala Rasuli Wake Uislamu wako (rejea Al-Hujuraat (49:17) juu).

2-Mshukuru Al-Mannaan Kwa Neema Ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم):

Kumbuka, ee Mja wa Al-Mannaan, kwamba kutumwa kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ni neema kubwa kabisa kwa Waumini; basi ifuate Sunnah yake.

3-Usizibatilishe Swadaqah Zako Kwa Masimbulizi:

Tahadhari, ee Mja wa Al-Mannaan, na kuwasimbulia watu uliyowapa; kwani masimbulizi yanabatilisha ujira. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُم بِالْمَنِّ وَالْأَذَىٰ كَالَّذِي يُنفِقُ مَالَهُ رِئَاءَ النَّاسِ وَلَا يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ صَفْوَانٍ عَلَيْهِ تُرَابٌ فَأَصَابَهُ وَابِلٌ فَتَرَكَهُ صَلْدًا ۖ لَّا يَقْدِرُونَ عَلَىٰ شَيْءٍ مِّمَّا كَسَبُوا ۗ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿٢٦٤﴾

Enyi walioamini! Msibatwilishe swadaqa zenu kwa masimbulizi na udhia kama yule ambaye anatoa mali yake riyaa-a (kujionyesha) kwa watu wala hamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama jabali juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa ikaliacha tupu. Hawana uwezo juu ya lolote katika waliyoyachuma. Na Allaah Haongoi watu makafiri. [Al-Baqarah (2:264)]

4-Mwenye Masimbulizi Hatazungumzwa Na Allaah Siku Ya Qiyaamah:

Tambua kwamba kusimbulia ni haki ya Al-Mannaan Peke Yake, si ya waja. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((ثَلاَثَةٌ لاَ يُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَلاَ يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ، وَلاَ يُزَكِّيهِمْ، وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ)) ... ((الْمُسْبِلُ، وَالْمَنَّانُ، وَالْمُنَفِّقُ سِلْعَتَهُ بِالْحَلِفِ الْكَاذِبِ))

Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu watatu Allaah Hatawazungumza Siku ya Qiyaamah, wala Hatawatazama, wala Hatawatakasa, na watapata adhabu iumizayo …: Mwenye kuburuza nguo yake (kwa kiburi), mwenye kusimbulia (anachokitoa), na mwenye kuuza bidhaa yake kwa kiapo cha uongo.” [Muslim]

5-Kiri Neema Za Al-Mannaan Kama Walivyokiri Manabii:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Mannaan, kwamba Nabiy Yuwsuf (عليه السلام) alipokutana na nduguze alikiri kwamba Allaah Amewaneemesha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالُوا أَإِنَّكَ لَأَنتَ يُوسُفُ ۖ قَالَ أَنَا يُوسُفُ وَهَـٰذَا أَخِي ۖ قَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا ۖ إِنَّهُ مَن يَتَّقِ وَيَصْبِرْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٩٠﴾

Wakasema: Je, kwani wewe ndio Yuwsuf? Akasema: Mimi ni Yuwsuf, na huyu ni ndugu yangu. Kwa yakini Allaah Ametufanyia ihsaan. Hakika mwenye kuwa na taqwa na akasubiri, basi hakika Allaah Hapotezi ujira wa watendao ihsaan. [Yuwsuf (12:90)]

6-Tambua Kwamba Al-Mannaan Anawaneemesha Wanyonge:

Tambua kwamba Al-Mannaan Anawanyanyua wanyonge (rejea Al-Qaswasw (28:5) juu); basi usikate tamaa wala usiwadharau wanyonge.

7-Taja Neema Za Al-Mannaan Kwa Kushukuru:

Kumbuka kwamba Al-Mannaan Ameamrisha kuzitaja Neema Zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ ﴿١١﴾

Na ama Neema ya Rabb wako, basi ihadithie. [Adhw-Dhwuhaa (93:11)]

8-Usijione Kuwa Umestahiki Neema Kwa Amali Yako:

Tambua kwamba hata Jannah ni kwa Fadhila na Rehma ya Al-Mannaan, si kwa amali peke yake (rejea Hadiyth “لَنْ يُدْخِلَ أَحَدًا عَمَلُهُ الْجَنَّةَ” katika 005-Ar-Rahiym) [Al-Bukhaariy] [Muslim].

9-Tafakari Neema Za Al-Mannaan Zisizohesabika:

Tafakari, ee Mja wa Al-Mannaan, kwamba ukijaribu kuhesabu Neema Zake hutaweza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٨﴾

Na kama mkihesabu Neema za Allaah basi hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika Allaah bila shaka Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [An-Nahl (16:18)]

10-Mwombe Allaah Kwa Jina Lake Al-Mannaan:

Omba du’aa kwa du’aa ambayo ina Jina Tukufu kabisa la Al-Mannaan, iliyotajwa juu, ukimtaja kwa Majina Yake: Al-Mannaan, Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw, Dhul-Jalaali Wal-Ikraam, Al-Hayyu Al-Qayyuwm.

Na Allaah Mjuzi zaidi