As-Sayyid: Bwana; Mwenye ubwana kamili juu ya viumbe vyote, Aliyekamilika katika Utukufu Wake, Anayerejewa na viumbe vyote katika haja zao.
Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنْ مُطَرِّفٍ قَالَ: قَالَ أَبِي: انْطَلَقْتُ فِي وَفْدِ بَنِي عَامِرٍ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) فَقُلْنَا: أَنْتَ سَيِّدُنَا. فَقَالَ: ((السَّيِّدُ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى)). قُلْنَا: وَأَفْضَلُنَا فَضْلاً، وَأَعْظَمُنَا طَوْلاً. فَقَالَ: ((قُولُوا بِقَوْلِكُمْ أَوْ بَعْضِ قَوْلِكُمْ، وَلاَ يَسْتَجْرِيَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ))
Amesimulia Mutwarrif: Baba yangu (‘Abdullaah bin Ash-Shikhkhiyr (رضي الله عنه)) amesema: Nilikwenda pamoja na ujumbe wa Bani ‘Aamir kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), tukasema: Wewe ni bwana wetu. Akasema: “Bwana ni Allaah (تبارك وتعالى).” Tukasema: Na mbora wetu kwa fadhila, na mkubwa wetu kwa ukarimu. Akasema: “Semeni kauli yenu, au sehemu ya kauli yenu, wala shaytwaan asiwafanye kuwa wajumbe wake (kwa kuvuka mipaka).” [Abuu Daawuwd (4806), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
Maana Ya As-Sayyid:
1-Ubwana wa kweli na kamili ni wa Allaah (سبحانه وتعالى) Peke Yake; na ubwana wa viumbe ni wa kiasi na wa kupewa.
2-Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amelifasiri Jina Asw-Swamad kuwa ni: Bwana Aliyekamilika katika ubwana Wake (rejea 008-Asw-Swamad).
3-Neno sayyid limetumika katika Qur-aan kwa maana ya bwana na kiongozi miongoni mwa viumbe, kama Allaah Alivyomsifu Nabiy Yahyaa (عليه السلام). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَنَادَتْهُ الْمَلَائِكَةُ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي فِي الْمِحْرَابِ أَنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكَ بِيَحْيَىٰ مُصَدِّقًا بِكَلِمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَسَيِّدًا وَحَصُورًا وَنَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿٣٩﴾
Malaika wakamwita (Zakariyyaa) naye akiwa amesimama anaswali katika chumba chake cha ibaada wakamwambia: Hakika Allaah Anakubashiria Yahyaa atakayesadikisha Neno (la Kun!) kutoka kwa Allaah. Atakuwa mtu wa kuheshimika, mtawa anayejitenga mbali na matamanio, na Nabiy miongoni mwa Swalihina. [Aal-‘Imraan (3:39)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, As-Sayyid:
1-Tambua Kwamba Ubwana Wa Kweli Ni Wa As-Sayyid Pekee:
Tambua kwamba kila bwana katika viumbe ni Mja wa As-Sayyid; basi usimpe kiumbe utiifu unaopingana na utiifu wa Allaah.
2-Tahadhari Na Kuvuka Mipaka Katika Kuwasifu Watu:
Tahadhari, ee Mja wa As-Sayyid, na kuwasifu watu kwa sifa zinazomhusu Allaah, au kupindukia mipaka katika kuwasifu (rejea Hadiyth juu: “wala shaytwaan asiwafanye kuwa wajumbe wake”).
3-Mpende Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Bila Kupindukia:
Kumbuka, ee Mja wa As-Sayyid, kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ndiye bwana wa wanaadam Siku ya Qiyaamah, lakini hakupenda kupindukiwa katika kusifiwa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَنَا سَيِّدُ وَلَدِ آدَمَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَأَوَّلُ مَنْ يَنْشَقُّ عَنْهُ الْقَبْرُ، وَأَوَّلُ شَافِعٍ، وَأَوَّلُ مُشَفَّعٍ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mimi ni bwana wa wana wa Aadam Siku ya Qiyaamah, na wa kwanza kupasukiwa na kaburi, na wa kwanza kuombea (shafaa’ah), na wa kwanza kukubaliwa uombezi.” [Muslim]
4-Mkimbilie As-Sayyid Katika Haja Zako Zote:
Kumbuka, ee Mja wa As-Sayyid, kwamba viumbe vyote vinamkusudia Bwana wa kweli katika haja zao; basi mkusudie Yeye (rejea 008-Asw-Swamad).
5-Soma Sayyid Al-Istighfaar Asubuhi Na Jioni:
Tambua kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliiita du’aa bora kabisa ya maghfirah “Sayyid Al-Istighfaar” (bwana wa istighfaar), na ndani yake mja anakiri kwamba As-Sayyid Ndiye Rabb wake (rejea du’aa kamili katika 027-Al-Baariu) [Al-Bukhaariy].
6-Unyenyekee As-Sayyid Kama Mja Anavyomnyenyekea Bwana Wake:
Kumbuka, ee Mja wa As-Sayyid, kwamba ‘ibaadah ni unyenyekevu kamili pamoja na mapenzi kamili kwa Bwana wa kweli. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا ﴿٩٣﴾
Hakuna yeyote yule aliyeko katika mbingu na ardhi isipokuwa atamjia Ar-Rahmaan akiwa ni mtumwa Kwake. [Maryam (19:93)]
7-Ukiwa Kiongozi, Tambua Kwamba Ubwana Wako Ni Amana:
Tambua, ee Mja wa As-Sayyid, kwamba kila mwenye ubwana juu ya watu ataulizwa juu ya aliowachunga (rejea Hadiyth “كُلُّكُمْ رَاعٍ” katika 021-Al-Muhaymin) [Al-Bukhaariy] [Muslim].
8-Usijione Bwana Juu Ya Watu Kwa Nasaba Au Mali:
Tahadhari na kujiona bora kuliko wengine; kwani mbora mbele ya As-Sayyid ni mwenye taqwa zaidi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿١٣﴾
Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamme na mwanamke, na Tukakufanyeni mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye na hadhi zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni mwenye taqwa zaidi kati yenu. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Khabari za dhahiri na siri. [Al-Hujuraat (49:13)]
9-Watii Wenye Mamlaka Katika Yasiyo Maasi Ya As-Sayyid:
Kumbuka kwamba utiifu kwa wenye mamlaka ni katika mema tu; na hakuna utiifu katika kumuasi As-Sayyid (rejea Hadiyth katika 027-Al-Baariu) [Al-Bukhaariy] [Muslim]. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾
Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa (4:59)]
10-Mwombe As-Sayyid Kwa Kukiri Uja Wako:
Omba du’aa, ee Mja wa As-Sayyid, kwa kukiri kwamba wewe ni Mja Wake, mwana wa Mja Wake, na kwamba Hukumu Yake inapita kwako (rejea du’aa ya huzuni katika 029-Al-Hakam) [Ahmad; Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha].
Na Allaah Mjuzi zaidi