As-Subbuwh: Mwingi wa kutakaswa; Aliyetakasika na kila aibu, kila upungufu, mshirika, mke na mwana, na kila kisicholingana na Uungu Wake.
Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ فِي رُكُوعِهِ وَسُجُودِهِ: ((سُبُّوحٌ قُدُّوسٌ رَبُّ الْمَلاَئِكَةِ وَالرُّوحِ))
Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema katika Rukuu yake na Sujuud yake: “Mwingi wa kutakaswa, Mtakatifu, Rabb wa Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl).” [Muslim]
Jina hili halikutajwa katika Qur-aan kwa tamko lake, lakini maana yake, yaani Tasbiyh (kumtakasa Allaah), imekuja katika Qur-aan mara nyingi mno; na Allaah (سبحانه وتعالى) Amejitakasa Mwenyewe na Amewaamrisha Waja Wake wamtakase. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾
Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku Mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumebariki pembezoni mwake, ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (Ishara) Zetu (kubwa mno). Hakika Yeye (Allaah) Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Al-Israa (17:1)]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ﴿١﴾
Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jumu’ah (62:1)]
Na Jina hili limekuja katika Hadiyth pamoja na Jina Lake Al-Qudduws; kwani maana zake mbili zinakaribiana: As-Subbuwh Ni Aliyetakasika na kila aibu na upungufu, na Al-Qudduws Ni Aliyetakasika na kila kisicholingana na Muumbaji (rejea 018-Al-Qudduws).
Maana Ya As-Subbuwh:
1-As-Subbuwh limetokana na tasbiyh, nayo ni kumtukuza Allaah na kumtakasa; na limekuja kwa wazani wa (فُعُّول) unaoonyesha wingi na mkazo, yaani Yeye Ndiye Anayetakaswa sana na kwa wingi mno, na hakuna kiumbe kinachoweza kumtakasa kama Anavyostahiki. Amesema Imaam Al-Khattwaabiy:
السُّبُّوحُ: الْمُنَزَّهُ عَنْ كُلِّ عَيْبٍ، جَاءَ بِلَفْظِ فُعُّولٍ، مِنْ قَوْلِكَ: سَبَّحْتُ اللَّهَ، أَيْ: نَزَّهْتُهُ
“As-Subbuwh: Ni Aliyetakasika na kila aibu; limekuja kwa tamko la (fu’’uwl), kutokana na kauli yako: Nimemsabihi Allaah, yaani nimemtakasa.”1
2-Ametakasika na kila upungufu, na kila mshirika, na kila kisicholingana na Uungu Wake. Amesema Imaam An-Nawawiy:
سُبُّوحٌ: الْمُبَرَّأُ مِنَ النَّقَائِصِ وَالشَّرِيكِ وَكُلِّ مَا لَا يَلِيقُ بِالْإِلَهِيَّةِ، وَقُدُّوسٌ: الْمُطَهَّرُ مِنْ كُلِّ مَا لَا يَلِيقُ بِالْخَالِقِ
“Subbuwh: Ni Aliyeepushwa na mapungufu, na mshirika, na kila kisicholingana na Uungu. Na Qudduws: Ni Aliyetakasika na kila kisicholingana na Muumbaji.”2 Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amejitakasa Mwenyewe na kuwa na mwana au mshirika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ ۚ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٩١﴾
Allaah Hakujifanyia mwana yeyote, na wala hakuna pamoja Naye mwabudiwa yeyote. Ingekuwa hivyo, basi kila mwabudiwa angelichukua vile alivyoviumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengineo. Subhaana Allaah (Utakasifu ni wa Allaah) kutokana na ambayo wanayavumisha. [Al-Muuminuwn (23:91)]
3-Ametakasika na mke na mwana, na kila uongo wanaomvumishia washirikina. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ الْجِنَّ وَخَلَقَهُمْ ۖ وَخَرَقُوا لَهُ بَنِينَ وَبَنَاتٍ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿١٠٠﴾ بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ وَلَدٌ وَلَمْ تَكُن لَّهُ صَاحِبَةٌ ۖ وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٠١﴾
Na wakamfanyia Allaah majini kuwa ni washirika Wake ilhali Amewaumba. Na wakampachikia uongo bila ya ujuzi wowote kuwa Ana wana wa kiume na wa kike. Utakasifu ni Wake na Ametukuka kwa ‘Uluwa kutokana na ambayo wanavumisha. Mbunifu wa mbingu na ardhi (bila ya mfano uliotangulia). Inamkinikaje kuwa Yeye Ana mwana ilhali Hana mke? Naye Ameumba kila kitu, Naye Ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-An’aam (6:100-101)]
4-Ametakasika na yote wanayomsifu kwayo wasiomjua, isipokuwa yale Aliyojisifu Nayo Mwenyewe na waliyomsifu kwayo Rusuli Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
سُبْحَانَ رَبِّكَ رَبِّ الْعِزَّةِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿١٨٠﴾ وَسَلَامٌ عَلَى الْمُرْسَلِينَ ﴿١٨١﴾ وَالْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٨٢﴾
Utakasifu ni wa Rabb wako; Rabb wa Enzi ya Nguvu Asiyeshindika kutokana na yale wanayoyavumisha. Na Salaamun! (Amani) iwe juu ya Rusuli. Na AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa walimwengu. [Asw-Swaaffaat (37:180-182)]
5-Viumbe vyote vilivyomo mbinguni na ardhini vinamsabihi As-Subbuwh, kila kimoja kwa namna yake, ingawa sisi hatuzifahamu tasbiyh zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ ۗ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤٤﴾
Zinamsabihi mbingu saba na ardhi na waliomo humo. Na hakuna kitu chochote isipokuwa kinasabihi na kumhimidi Yeye, lakini hamzifahamu tasbihi zao. Hakika Yeye Ni Mvumilivu, Mwingi wa Kughufuria. [Al-Israa (17:44)]
Kwa hiyo As-Subbuwh Ni Ambaye Anatakaswa na kutukuzwa kwa wingi na viumbe Vyake vyote; Ametakasika katika Dhati Yake, Majina Yake, Sifa Zake na Matendo Yake, na kila Alilolihukumu na kulikadiria ni kheri na Hikmah tupu.
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, As-Subbuwh:
1-Mtakase As-Subbuwh Bila Kukanusha Sifa Zake Wala Kuzifananisha:
Tambua kwamba As-Subbuwh Ametakasika na kila aibu na upungufu; na kumtakasa kwa haki ni kumthibitishia Majina na Sifa Alizojithibitishia Mwenyewe na Alizomthibitishia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), bila kuzipotoa, bila kuzikanusha, bila kuzifanyia namna, na bila kuzifananisha na sifa za viumbe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾
Mwanzilishi wa mbingu na ardhi. Amekujaalieni kutokana na nafsi zenu mume na mke, na katika wanyama wa mifugo dume na jike. Anakusambazeni humo. Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:11)]
2-Tafakari Jinsi Viumbe Vyote Vinavyomsabihi As-Subbuwh:
Tafakari, ee Mja wa As-Subbuwh, kwamba walioko mbinguni na ardhini, hata ndege angani, wote wanamsabihi As-Subbuwh, na kila mmoja Ameshajua Swalaah yake na tasbiyh yake; basi usiwe wewe peke yako mwenye kughafilika katika ulimwengu unaomsabihi Rabb wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ ۖ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلَاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ ﴿٤١﴾
Je, huoni kwamba wanamsabihi Allaah walioko mbinguni na ardhini, na (pia) ndege wakiwa wamekunjua mbawa zao. Kila mmoja (Allaah) Amekwishajua Swalaah yake na tasbihi yake. Na Allaah Ni Mjuzi kwa yale wayafanyao. [An-Nuwr (24:41)]
3-Iga Malaika Ambao Hawachoki Kumsabihi As-Subbuwh:
Kumbuka, ee Mja wa As-Subbuwh, kwamba Malaika walio Kwake hawatakabari kumwabudu, wala hawachoki; wanamsabihi As-Subbuwh usiku na mchana bila kuishiwa nguvu. Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akimtaja kwa Jina hili kuwa Ni Rabb wa Malaika na Ar-Ruwh (rejea Hadiyth ya ‘Aaishah (رضي الله عنها) juu). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَمَنْ عِندَهُ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ ﴿١٩﴾ يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ ﴿٢٠﴾
Na ni Wake wote waliomo katika mbingu na ardhi. Na (Malaika) ambao wako Kwake hawatakabari wakaacha kumwabudu, na wala hawachoki. Wanasabihi usiku na mchana, hawaishiwi nguvu. [Al-Anbiyaa (21:19-20)]
4-Mtakase As-Subbuwh Kwa Kuamini Kwamba Hakuumba Chochote Bure:
Tambua kwamba As-Subbuwh Ametakasika na upuuzi na kuumba bila ya Hikmah; basi unapotafakari mbingu na ardhi, na unapofikwa na jambo usilolipenda katika Qadar Yake, mtakase na useme kama walivyosema wenye akili. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾
Ambao wanamdhukuru Allaah wakiwa wima, au wamekaa au wamejinyoosha, na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako! Basi Tukinge na adhabu ya moto. [Aal-‘Imraan (3:191)]
5-Tahadhari Na Kumkadiria As-Subbuwh Isivyostahiki:
Tahadhari, ee Mja wa As-Subbuwh, na kumdhania Rabb wako dhana mbaya, au kumshirikisha, au kumsifu kwa yasiyolingana Naye; kwani hayo ni kutomkadiria Allaah kama Anavyostahiki kukadiriwa, na As-Subbuwh Ametakasika na Ametukuka na yote wanayomshirikisha nayo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٦٧﴾
Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Na hali ardhi yote Ataikamata Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah, na mbingu zitakunjwa kwa Mkono Wake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha. [Az-Zumar (39:67)]
6-Jaza Mizani Yako Kwa Maneno Mawili Yanayopendwa Na As-Subbuwh:
Tambua kwamba As-Subbuwh Anapenda kutakaswa, na miongoni mwa maneno mepesi zaidi kwa ulimi na mazito zaidi katika mizani ni maneno ya tasbiyh. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((كَلِمَتَانِ خَفِيفَتَانِ عَلَى اللِّسَانِ، ثَقِيلَتَانِ فِي الْمِيزَانِ، حَبِيبَتَانِ إِلَى الرَّحْمَنِ: سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ، سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Maneno mawili mepesi kwa ulimi, mazito katika mizani, yanapendwa na Ar-Rahmaan: Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake; Utakasifu ni wa Allaah Mwenye U’adhwama.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Basi yakithirishe maneno haya:
سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ، سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ
Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake; Utakasifu ni wa Allaah Mwenye U’adhwama.
7-Futiwa Madhambi Yako Kwa Kumsabihi As-Subbuwh Mara Mia Kila Siku:
Kumbuka, ee Mja wa As-Subbuwh, kwamba kumtakasa Rabb wako ni sababu ya kufutiwa madhambi hata yakiwa mengi kama povu la bahari. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ قَالَ: سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ، فِي يَوْمٍ مِائَةَ مَرَّةٍ، حُطَّتْ خَطَايَاهُ وَإِنْ كَانَتْ مِثْلَ زَبَدِ الْبَحْرِ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesema: Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake, mara mia kwa siku, atafutiwa makosa yake hata yakiwa mfano wa povu la bahari.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ
Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake.
8-Msabihi As-Subbuwh Asubuhi Na Jioni:
Tambua, ee Mja wa As-Subbuwh, kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amekuamrisha umdhukuru kwa wingi na umsabihi mwanzo wa mchana na mwisho wake; basi zihifadhi adhkaar za asubuhi na jioni, na uufanye ulimi wako uwe mbichi kwa kumtakasa As-Subbuwh. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا ﴿٤١﴾ وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٤٢﴾
Enyi walioamini! Mdhukuruni Allaah kwa wingi mno wa kumdhukuru. Na Msabbihini asubuhi na jioni. [Al-Ahzaab (33:41-42)]
9-Msabihi As-Subbuwh Baada Ya Kila Swalaah:
Kumbuka, ee Mja wa As-Subbuwh, kwamba miongoni mwa nyakati bora za kumtakasa Rabb wako ni baada ya kila Swalaah ya fardhi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ سَبَّحَ اللَّهَ فِي دُبُرِ كُلِّ صَلاَةٍ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، وَحَمِدَ اللَّهَ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، وَكَبَّرَ اللَّهَ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، فَتِلْكَ تِسْعَةٌ وَتِسْعُونَ، وَقَالَ تَمَامَ الْمِائَةِ: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، غُفِرَتْ خَطَايَاهُ وَإِنْ كَانَتْ مِثْلَ زَبَدِ الْبَحْرِ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayemsabihi Allaah baada ya kila Swalaah mara thelathini na tatu, na akamhimidi Allaah mara thelathini na tatu, na akamkabbir Allaah mara thelathini na tatu, hizo ni tisini na tisa, kisha akasema kutimiza mia: Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Pekee, Hana mshirika, Ufalme ni Wake na Himdi ni Zake, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza; atafutiwa makosa yake hata yakiwa mfano wa povu la bahari.” [Muslim]
10-Mtakase As-Subbuwh Katika Rukuu Na Sujuud Yako:
Tambua kwamba As-Subbuwh Anastahiki kutakaswa katika hali ya unyenyekevu mkubwa kabisa, nayo ni Rukuu na Sujuud; na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema humo maneno ya Jina hili (rejea Hadiyth ya ‘Aaishah (رضي الله عنها) juu):
سُبُّوحٌ قُدُّوسٌ رَبُّ الْمَلاَئِكَةِ وَالرُّوحِ
Mwingi wa kutakaswa, Mtakatifu, Rabb wa Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl).
Na alikuwa akisema katika Rukuu na Sujuud:
عَنْ حُذَيْفَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: صَلَّيْتُ مَعَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) ذَاتَ لَيْلَةٍ ... ثُمَّ رَكَعَ فَجَعَلَ يَقُولُ: ((سُبْحَانَ رَبِّيَ الْعَظِيمِ)) ... ثُمَّ سَجَدَ فَقَالَ: ((سُبْحَانَ رَبِّيَ الأَعْلَى))
Amesimulia Hudhayfah (رضي الله عنه): Niliswali pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) usiku mmoja … kisha akarukuu akawa anasema: “Utakasifu ni wa Rabb wangu Mwenye U’adhwama.” … Kisha akasujudu akasema: “Utakasifu ni wa Rabb wangu Mwenye ‘Uluwa.” [Muslim]
سُبْحَانَ رَبِّيَ الْعَظِيمِ
Utakasifu ni wa Rabb wangu Mwenye U’adhwama (katika Rukuu).
سُبْحَانَ رَبِّيَ الأَعْلَى
Utakasifu ni wa Rabb wangu Mwenye ‘Uluwa (katika Sujuud).
11-Msabihi As-Subbuwh Unaposhuka Mahali Pa Chini:
Kumbuka, ee Mja wa As-Subbuwh, kwamba Maswahaba walikuwa wakimtukuza Allaah wanapopanda mahali pa juu, na wakimtakasa As-Subbuwh wanaposhuka mahali pa chini; kwani Yeye Ametakasika na kila hali ya chini na upungufu:
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنهما) قَالَ: كُنَّا إِذَا صَعِدْنَا كَبَّرْنَا، وَإِذَا نَزَلْنَا سَبَّحْنَا
Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): “Tulikuwa tunapopanda (mahali pa juu) tunasema: Allaahu Akbar, na tunaposhuka tunasema: Subhaana Allaah.” [Al-Bukhaariy]
12-Hitimisha Kikao Chako Kwa Kumtakasa As-Subbuwh:
Tambua, ee Mja wa As-Subbuwh, kwamba kumtakasa Rabb wako mwishoni mwa kikao ni kafara ya yaliyotokea humo katika maneno ya upuuzi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنْ جَلَسَ فِي مَجْلِسٍ فَكَثُرَ فِيهِ لَغَطُهُ، فَقَالَ قَبْلَ أَنْ يَقُومَ مِنْ مَجْلِسِهِ ذَلِكَ: سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ، أَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتُوبُ إِلَيْكَ، إِلاَّ غُفِرَ لَهُ مَا كَانَ فِي مَجْلِسِهِ ذَلِكَ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayeketi katika kikao akazidisha humo maneno ya upuuzi, kisha akasema kabla ya kuinuka katika kikao chake hicho: Utakasifu ni Wako Yaa Allaah na Himdi ni Zako, nashuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, nakuomba maghfirah na natubu Kwako; isipokuwa atafutiwa yaliyokuwa katika kikao chake hicho.” [At-Tirmidhiy (3433), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3433)]
سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ، أَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتُوبُ إِلَيْكَ
Utakasifu ni Wako Yaa Allaah na Himdi ni Zako; nashuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe; nakuomba maghfirah na natubu Kwako.
13-Panda Mitende Yako Ya Jannah Kwa Kumtakasa As-Subbuwh:
Kumbuka, ee Mja wa As-Subbuwh, kwamba kila tasbiyh unayoitamka inakupandia mtende katika Jannah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ جَابِرٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ قَالَ: سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ وَبِحَمْدِهِ، غُرِسَتْ لَهُ نَخْلَةٌ فِي الْجَنَّةِ))
Amesimulia Jaabir (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesema: Utakasifu ni wa Allaah Mwenye U’adhwama na Himdi ni Zake, atapandiwa mtende katika Jannah.” [At-Tirmidhiy (3464), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3464)]
سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ وَبِحَمْدِهِ
Utakasifu ni wa Allaah Mwenye U’adhwama na Himdi ni Zake.
14-Omba Maghfirah Kwa As-Subbuwh Pamoja Na Kumtakasa:
Omba du’aa kwa As-Subbuwh, ee Mja wa Allaah, kwa kuchanganya tasbiyh na kuomba maghfirah, kama Alivyomwamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Suwrah An-Naswr (110:3); naye (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiifanyia kazi Aayah hiyo katika Rukuu na Sujuud yake:
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: كَانَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم) يُكْثِرُ أَنْ يَقُولَ فِي رُكُوعِهِ وَسُجُودِهِ: ((سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ رَبَّنَا وَبِحَمْدِكَ، اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي)) يَتَأَوَّلُ الْقُرْآنَ
Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akikithirisha kusema katika Rukuu yake na Sujuud yake: “Utakasifu ni Wako Yaa Allaah, Rabb wetu, na Himdi ni Zako; Yaa Allaah, nighufurie.” Akiifanyia kazi (amri ya) Qur-aan. [Al-Bukhaariy] [Muslim]
سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ رَبَّنَا وَبِحَمْدِكَ، اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي
Utakasifu ni Wako Yaa Allaah, Rabb wetu, na Himdi ni Zako; Yaa Allaah, nighufurie.
15-Omba Du’aa Ya Dhan-Nuwn Kwa As-Subbuwh Unapofikwa Na Dhiki:
Omba du’aa kwa As-Subbuwh unapofikwa na dhiki na ghamu, kwa du’aa aliyoiomba Nabiy Yuwnus (عليه السلام) akiwa ndani ya tumbo la samaki; alimpwekesha Allaah, akamtakasa, kisha akakiri dhulma yake, na Allaah Akamuokoa, na Akaahidi kuwaokoa Waumini vivyo hivyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾ فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾
Na Dhan-Nuwn (Yuwnus), alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha. Akaita vizani kwamba: Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. Basi Tukamuitikia, na Tukamuokoa kutokana na ghamu. Na hivyo ndivyo Tuwaokoavyo Waumini. [Al-Anbiyaa (21:87-88)]
لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ
Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.
16-Mtakase As-Subbuwh Kwa Tasbiyh Iliyo Kubwa Zaidi Kwa Ujira:
Omba du’aa na umtakase As-Subbuwh kwa maneno mafupi yenye ujira mkubwa ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliyafundisha, yanayozidi uzito tasbiyh ya muda mrefu:
عَنْ جُوَيْرِيَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) خَرَجَ مِنْ عِنْدِهَا بُكْرَةً حِينَ صَلَّى الصُّبْحَ وَهِيَ فِي مَسْجِدِهَا، ثُمَّ رَجَعَ بَعْدَ أَنْ أَضْحَى وَهِيَ جَالِسَةٌ، فَقَالَ: ((مَا زِلْتِ عَلَى الْحَالِ الَّتِي فَارَقْتُكِ عَلَيْهَا؟)) قَالَتْ: نَعَمْ. قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((لَقَدْ قُلْتُ بَعْدَكِ أَرْبَعَ كَلِمَاتٍ ثَلاَثَ مَرَّاتٍ، لَوْ وُزِنَتْ بِمَا قُلْتِ مُنْذُ الْيَوْمِ لَوَزَنَتْهُنَّ: سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ عَدَدَ خَلْقِهِ، وَرِضَا نَفْسِهِ، وَزِنَةَ عَرْشِهِ، وَمِدَادَ كَلِمَاتِهِ))
Amesimulia Juwayriyah (رضي الله عنها) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alitoka kwake asubuhi mapema alipokwisha kuswali Swalaah ya Asubuhi, naye (Juwayriyah) akiwa mahali pake pa kuswalia; kisha akarudi baada ya kupanda jua naye akiwa bado ameketi, akasema: “Bado uko katika hali ile niliyokuacha nayo?” Akasema: Ndio. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hakika nimesema baada yako maneno manne mara tatu; lau yangelipimwa kwa yale uliyoyasema tangu leo (asubuhi), basi yangeliyazidi uzito: Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake, kwa idadi ya viumbe Vyake, na kwa kiasi cha Ridhaa Yake, na kwa uzito wa ‘Arsh Yake, na kwa wino wa Maneno Yake.” [Muslim]
سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ عَدَدَ خَلْقِهِ، وَرِضَا نَفْسِهِ، وَزِنَةَ عَرْشِهِ، وَمِدَادَ كَلِمَاتِهِ
Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake, kwa idadi ya viumbe Vyake, na kwa kiasi cha Ridhaa Yake, na kwa uzito wa ‘Arsh Yake, na kwa wino wa Maneno Yake.
Na Allaah Mjuzi zaidi