Ingia Katika Milango Mingi Ya Kheri Ramadhwaan

 

Ingia Katika Milango Mingi Ya Kheri Ramadhwaan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Mwezi mtukufu wa Ramadhwaan unakaribia kutufikia. Chukua fursa ya kujichumia thawabu nyingi kwa sababu malipo ya amali inayotekelezwa humo yanaanzia mara kumi mpaka mara mia saba. Juu ya hivyo, kuna malipo maalum yatokayo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ إِلَّا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ يَدَعُ شَهْوَتَهُ وَطَعَامَهُ مِنْ أَجْلِي لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ فَرْحَةٌ عِنْدَ فِطْرِهِ وَفَرْحَةٌ عِنْدَ لِقَاءِ رَبِّهِ وَلَخُلُوفُ فِيهِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ))

Imepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu): ((Kila amali njema ya mwana   Aadam inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba, na Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema: Isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa. Ameacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Kwa aliyefunga Swawm atapata furaha mbili; furaha anapofuturu na furaha atakapoonana na Rabb wake, harufu inayotoka kinywani mwa aliyefunga ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya misk)) [Muslim na Ahmad]

 

 

Kwanza kabisa inatupasa kutia niyyah ya ikhlaasw moyoni (si kuitamka) kwa sababu ni sharti mojawapo la kutakabaliwa 'amali yoyote, na ili kupata Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema:

 

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاء وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَة

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara.  [Al-Bayyinah: 5]

 

Weka azimio la nguvu kutekeleza ‘amali zifuatazo katika mwezi wa Ramadhwaan.    

 

 

1-Kufunga Swawm kwa iymaan na matarajio ili kufutiwa madhambi:

 

قال صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ صَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))   أخرجه البخاري ومسلم

Amesema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Atakayefunga Ramadhwaan kwa iymaan na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al Bukhaariy na Muslim]

 

 

2-Qiyaamul-Layl - Kusimama usiku katika Swalaah

 

 قال صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ قَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))  أخرجه البخاري ومسلم

Amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallaam) amesema:  ((Atakayesimama [kwa Swalaah ya usiku] kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

3-Kutoa swadaqah

 

 قال صلى الله عليه وسلم: ((أفضل الصدقة صدقة في رمضان)) أخرجه الترمذي عن أنس

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema:   ((Swadaqah bora kabisa ni ile inayotolewa katika mwezi wa Ramadhwaan)) [At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas]

 

 

 

4-Kumfuturisha aliyefunga:

 

 قال صلى الله عليه وسلم : ((مَنْ فَطَّرَ صَائِمًا كَانَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِهِ غَيْرَ أَنَّهُ لَا يَنْقُصُ مِنْ أَجْرِ الصَّائِمِ شَيْئًا )) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألبان

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema: ((Atakayemfuturisha aliyefunga atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy – Ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا﴿٨﴾

Na wanalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini na mayatima na mateka.

 

إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا﴿٩﴾

“Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya Wajihi wa Allaah, hatukusudii kwenu jazaa na wala shukurani.

 

إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا﴿١٠﴾

“Hakika sisi tunakhofu kutoka kwa Rabb wetu siku ya masononeko, ngumu na ndefu mno.

 

فَوَقَاهُمُ اللَّـهُ شَرَّ ذَٰلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا﴿١١﴾

Basi Allaah Atawakinga na shari ya siku hiyo, na Atawapa nuru ya ujamali na furaha.

 

وَجَزَاهُم بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا﴿١٢﴾

Na Atawalipa kwa sababu ya kusubiri kwao, Jannah na nguo za hariri.     [Al-Insaan: 8-12]

 

 

5-Kusoma Qur-aan kwa wingi na kujifunza maana yake.

 

Mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ  

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na upambanuo (wa haki na batili).   [Al-Baqarah: 185]

 

Jitahidi ndugu Muislam uzidishe kusoma Qur-aan na ujitahidi kukhitimisha japo mara moja katika mwezi huu. Jibriyl (‘alayhis-salaam) alikuwa akimfikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kumsikiliza na kumfundisha Qur-aan katika mwezi wa Ramadhwaan. Vile vile  Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia) walikuwa wakijihimiza sana kusoma Qur-aan katika mwezi wa Ramadhwaan;   

 

 

6-Kumdhukuru Allaah baada Swalaah ya Alfajiri hadi jua litoke

 

 عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم، أنه قال: ((مَنْ صَلَّى الفَجْرِ في جَماعَةٍ ثُمَّ قَعَدَ يَذْكُرُ الله تَعالى حتَّى تَطْلُعَ الشَمْسُ، ثُمَّ صَلَّى رَكْعَتَيْنِ كانَتْ كأجْرِ حَجَّةٍ وَعُمْرَةٍ تامَّةٍ تامةٍ تامةٍ)) أخرج الترمذي وصححه الألباني

Imetoka kwa Anas kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa'ah kisha akakaa anamdhukuru Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy].

 

 

Kuswali Jama'ah kumesisitizwa kwa wanaume, ama mwanamke anaweza naye kupata ujira wa thawabu zilizotajwa akiswali nyumbani kwake kama alivyosema Imaam Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah) baada ya kuulizwa: “Naam, intarajiwa kwake hivyo, inatarajiwa kwake khayr hii kubwa.”

 

Thawabu hizo za kama Hajj na ‘Umrah ni katika siku za kawaida ndugu Muislamu, seuze mwezi wa Ramadhwaan?  Usiache fursa hii ikupite.  Ukishindwa kuitekeleza kila siku, basi jitahidi japo wiki mara moja, hapo utakuwa una thawabu za Hajj na 'Umrah mara nne kwa mwezi, na ukiendelea hivyo miezi yote kumi na mbili basi utakuwa na thawabu za Hajj na 'Umrah mara 48 kwa mwaka.  

 

 

7- Kubakia Masjid kwa ajili ya I'tikaaf:

 

عن عائشة  رضي الله عنها   قالت:    "كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَعْتَكِفُ فِي كُلِّ رَمَضَانٍ عَشْرَةَ أَيَّامٍ, فَلَمَّا كَانَ الْعَامُ الَّذِي قُبِضَ فِيهِ اعْتَكَفَ عِشْرِينَ يَوْمًا "  أخرجه البخاري

Kutoka kwa 'Aashah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa I'tikaaf kila Ramadhwaan katika siku kumi za mwisho, na mwaka ambao aliondoka duniani alikaa I'tikaaf siku ishirini. [Al- Bukhaariy]

 

Unapokuwa umo katika I'tikaaf utaweza kutekeleza amali nyingi zitakazokufanya ubakie katika taqwa na iymaan kuzidi moyoni. Utaweza kusoma Qur-aan kwa wingi, kuswali Swalaah za Sunnah, kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kuomba du’aa na maghfirah. Fadhila za I’tikaaf zinazidi inapokuwa katika kumi la mwisho kwa sababu ya usiku mtukufu wa ’Laylatul-Qadr’.    

 

 

8-'Umrah katika mwezi wa Ramadhwaan

 

Ukiwa na uwezo, tekeleza ‘Umrah. Imethibiti katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba thawabu za kutekeleza 'Umrah katika Ramadhwaan ni sawa na thawabu za kutekeleza Hijjah.

   ((عمرة في رمضان تعدل حجة))  أخرجه البخاري و مسلم

(('Umrah katika Ramadhwaan ni sawa [kwa thawabu] na Hijjah))  [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

 

9-Kupata Baraka za Suhuwr (Daku)

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((تَسَحَّرُوا فَإِنَّ فِي السَّحُورِ بَرَكَةً ))     رواه البخاري ومسلم  

((Kuleni daku kwani katika huko kula daku, kuna  baraka)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

10-Kuomba Du'aa

 

Ramadhwaan ni mwezi wa Du'aa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anataja kuhusu kumuomba du’aa baada ya kutufaridhisha Swawm:

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

186. Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka.   [Al-Baqarah:186]

  

Zinaendelea Aayah za kuhusu Swawm baada yake.   

 

 

11-Kuomba maghfirah na tawbah:

 

Omba maghfira na tawbah kabla ya alfajiri. Kufanya hivi utakuwa miongoni mwa waja wema Anaowasifu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):   

 وَبِالأَ سْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ   

Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah [Adh-Dhaariyaat: 18]

 

Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Huteremka nyakati hizo kuweko katika mbingu ya kwanza:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam  amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka kila siku katika mbingu ya dunia  inapobakia thuluthi ya mwisho ya  usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

 

12-Kuunga undugu na jamaa:

 

Jambo muhimu kulitekeleza siku zote. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha kwa anayekata mawasiliano na ndugu au jamaa:  

 

((الرَّحِمُ مُعَلَّقَةٌ بِالْعَرْشِ تَقُولُ: مَنْ وَصَلَنِي وَصَلَهُ اللَّهُ، وَمَنْ قَطَعَنِي قَطَعَهُ اللَّهُ))   رواه البخاري ومسلم

((Fuko la uzazi linaning'inia katika 'Arshi linasema: “Atakayeniunga, Allaah Atamuunga, na atakayenitenga Naye Allaah Atamtenga [Atamkatia]”)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

 

13- Kukesha siku kumiza mwisho:   

 

Utaweza kudiriki Laylatul-Qadr, usiku ambao ‘ibaadah yake ni bora kuliko ‘ibaadah utakazoifanya miezi elfu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾

1. Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatil-Qadr (usiku wa Qadar).

 

وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ ﴿٢﴾

2. Na nini kitakachokujulisha ni nini huo Laylatul-Qadr?

 

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾

3.  Laylatul-Qadr ni mbora kuliko miezi elfu.

 

تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ ﴿٤﴾

4. Wanateremka humo Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Rabb wao kwa kila jambo.

سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ ﴿٥﴾

5.  Amani mpaka kuchomoza Alfajiri [Al-Qadr: 97]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atujaalie tawfiyq kutekeleza yote hayo na Atutakabalie. Aamiyn.

 

 

 

 

 

Share