Kumsomea Mwenye Majini Aayah Za Qur-aan Kwa Kiswahili Ikiwa Hawezi Kusoma Kiarabu

 

SWALI:

Kutoka kwenye mawaidha ya video kwenye alhidaaya.com yenye kicha cha habari ULIMWENGU WA MAJINI ('Abdul-Latwiyf 'Abdul-Kariym )

Je katika kumsomea mgojwa mwenye jini inawezekana kusoma zile aya za Quran zilizotajwa kwa kutumia tafsiri ya kiswahii au ni lazima ujue kusoma Quran.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala ya kutoa majini. Mara nyingi huwa tunaposoma au kusikia mambo huona jambo hilo ni sahali.

 

Mwanzo tufahamu kuwa kutoa jini aliyemvaa mtu ni fani kama fani nyingine na hivyo kutaka uzoefu kwa hilo. Haiwezekani kwa mtu kuingia mara moja katika suala hilo kabla ya mwanzo kufuata na mjuzi wa suala hilo ili kuona kinachofanywa. Maana inasemwa na hao watoaji kuwa ukikosea kidogo tu basi jini huyo huenda akatoka kwa mgonjwa na kukuingia wewe unayetaka kumtibu. Hivyo, ni vyema tuwe na tahadhari kuhusu hilo.

 

Ama kumsomea mgonjwa huyo aliyekumbwa na jini kwa lugha nyingine yoyote kama vile Kiswahili haifai kwani hiyo si Qur-aan bali tunaiita tafsiri au tarjuma. Na katika tafsiri huwa yapo mambo mengi na mara nyingine pia hupati maana sawa ya neno fulani. Hata hilo lingekuwa linatekelezeka pia haingekuwa ni Qur’ani.

 

Kwa muhtasari tunasema kuwa ni lazima umsomee kwa ile ile Qur-aan ya asili ambayo ipo katika lugha ya Kiarabu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share