Kahama Nyumba Kwa Sababu Hataki Kuishi Na Mke Mwenza

 

SWALI:

Kuna ndugu yangu aliachwa na mumewe talaka moja na kabla ya kuondosha vitu vyake yaani (vitanda, makabati n.k), mumewe akamleta mke mwenzie alale chumba kile cha yule ndugu yangu kwa muda kiasi, baada ya hapo akaja kumrejea yule ndugu yangu.

Sasa ndugu yangu hataki kurejea kwa mumewe mpaka mumewe amtafutie sehemu nyingine, na hivi sasa ni kama mwaka mmoja umepita tokea waishi mbali mbali na mumewe na yule mume keshajenga nyumba ila mama wa mume amemwambia mwanaye iwapo watahamia huko kwenye hiyo nyumba, yeye haendi (yaani huyo mama wa mume)

 Sasa msaada wenu wa haraka ili kuinusuru ndoa hii, kwa kuwa huu ndugu yangu sasa hivi anaona ni bora apewe talaka.

Ahsanteni

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo kuhusu mas-ala hayo ya kijamii. Ndoa na tangamano la wanandoa ni makubaliano ili maisha yao yawe mazuri na yenye kupigiwa mfano.

Ni muhimu wanandoa kuelewana, na ni makosa kwa mume kumuingizia mkewe mke mwengine kabla hajaondoa vitu vyake baada ya kuachana. Kama vile ni makosa kwa mume kumtoa mkewe kwenye nyumba baada ya talaka kwani huo ni muda uliowekwa na Muumba na Mjuzi wa maumbile yetu ili wanandoa hao waweze kurudiana kama mume na mke. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuagiza kuwa mke katika kipindi hicho hafai kutoka wala kutolewa ila tu ikiwa mke amefanya jambo la ufasiki ulio wazi, kama Asemavyo Allaah:

“Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Mwenyezi Mungu Ataleta jambo jengine baada ya haya.” (65: 1). Hakika ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) katika wakati wa eda ameziita nyumba hata zikiwa ni za mwanamume kuwa ni nyumba za mke.

Kuna maneno hapa ambayo yanachanganya na huenda mpaka yawekwe wazi ndio tupate ufumbuzi wa haraka. Ibara hiyo ni “..baada ya hapo akaja akamrejea yule ndugu yangu” na “hivi sasa ni kama mwaka mmoja umepita tokea waishi mbali mbali na mumewe”. Maswali ambayo yanajitokeza ni:

  1. Mume alimrudia mkewe katika kipindi cha eda (hedhi au twahara tatu)?

  2. Ikiwa ni hivyo, huo mwaka uliosema wa kuishi mbali mbali umetokea wapi?

  3. Ikiwa alimrudia baada ya eda je, mke aliridhika kuolewa? Je, kulifungwa Nikaah mpya na mke kupatiwa mahari?

Ikiwa eda yake lilipita inabidi mume amuoe kwa ndoa mpya na kabla ya ndoa mke ana haki kuweka masharti yake. Masharti hayo kama kuwa na nyumba yake kando na ya yule mke mwenza na mume akikubali hilo inabidi mume atekeleze. Mara nyingi ni vyema wake wenza hasa ikiwa hawasikilizani wawe na nyumba tofauti ili kusije tokea vurugu baina yao. Tunakuta kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na wake wengi na kila mke alikuwa na chumba chake japokuwa vilikuwa karibu karibu. Lakini wake wengine kama vile Swafiyyah bint Huyayy (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa na nyumba yake kando na zile nyingine. Hata hivyo ikiwa wake hao wanaweza kuishi pamoja kwa masikilizano hilo linakuwa halina tatizo.

Ikiwa mama wa mume ameweka sharti hilo kuwa hawezi kwenda katika nyumba hiyo ikiwa mke atachukuliwa kukaa huko ni bora kwake kuomba apatiwe makazi sehemu nyingine. Ikiwa mume hawezi basi mke mwenyewe asikubali kurudiwa kwani kufanya hivyo itakuwa ni kujitia madhara yeye mwenyewe na Uislamu haukubali hilo. Na ikiwa amekaa mwaka mzima katika eda bila kurudiwa rasmi basi kunakuwa hakuna talaka nyingine ambayo atapewa kwani yeye si mke wa mtu na anaweza kuolewa pindi anapokuja mume mwingine.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka amfanyie sahali dada yako na wengine wenye matatizo mbalimbali.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share