Asubiri Kumaliza Shule Kuolewa Au Aendelee Kuwa Na Mahusiano

SWALI:

 

Asalaam alykum warahmatulahie wabarakatuh naomba Allaah swt awalipe malipo wazuri kuhusu kazi mnayoifanya awaweke katika pepo ya juu firdaus ameen Allaahuma ameen mimi. Nilikiwa ninaswahi. Mimi niko na mchumba na tunataka kuowana lakini bado myaka michache nimalize shule na haiwezekani tukafanya harusi kwa sasa lakini nafanya subra mpaka nimalize shule ndo tuowane je kwa hivi sio haram??


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuolewa ukiwa katika masomo. Ndoa katika Uislamu ni maafikiano na ahadi ambazo wanachukua mume na mke katika njia ya halali. Ikiwa tayari umechumbiwa na mume na tayari mumeagana kuoana baada ya masomo inabidi wewe na yeye muepukane kabisa ili msije mkaingia katika madhambi.

 

Haifai Kiislamu watu walioposana kukutana faragha wala kuzungumza hata kwa simu ili lisije likatokea jambo ambalo halifai. Inabidi kila mmoja asubiri na aepukane na vishawishi vyote ambavyo vinaweza kuwakaribisha na zinaa. Ikiwa mnaona ya kwamba hamuwezi kuvumilia basi inabidi muoane ili muepukane na madhambi.

 

Tufahamu kuwa hakuna jambo lisilowezekana, wapo wasichana wengi walioolewa na wakaendelea na masomo bila matatizo. Ikiwa hamuwezi kusubiri na kujizuilia itabidi muoane na lau mtaweza kusubiri bila kuingia katika maasiya basi itabdi mfanye subira hadi mmalize malengo yenu ya masomo ndio muoane.

 

Tunamuomba Allaah Awape subira katika hilo, Aamiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share