Mke Wa Mwanzo Anamuekea Masharti Mumewe

SWALI:

Ahsante sana kwa kunijibu suali langu kwani nitaweza kumfahamisha shoga yangu kama hakufanya kosa ni sawa alivyofanya. lakini pia napenda kuuliza suala jengine:-

kuna mtu ana wake wawili wote anawependa na anafanya kama sheria inavyotaka lakini mke mkubwa baada ya mke mdogo kujifungua alibadilika na kumwambia mumewe yafuatayo:

a) Uniache au umuache mwenzangu

b) usilale zamu

c) Ukimfata ndio talaka yangu

Jee sheikh mwanamke huyu aelezwe vipi ili ajue kama sheria ya uke wenza kaipanga Mungu kwani wanawake tupo wengi? Mke mdogo kamwambia mumewe mimi sipendi umuache mkeo hivyo wewe ishi kama alivyotaka lakini kuruhusiwa hivyo imekua sababu ya kuengeza mizozo kwenye ndoa ya
nyumba ndogo . Suali Sheikh, Mwanamke huyu asiejua sheria itakua vipi? Na ndoa hizi zitakuwa vipi? Na huyu mwanamke afanye vipi? Naomba majibu   



                                                          

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 Shukran dada yetu kwa swali lake ambalo ni nyeti. Hili jambo la ndoa ni muhimu sana na lina matatizo makubwa kwani hatufuati zile kanuni za Kiislamu katika uchaguzi wa mke au mume, hivyo kuwa ni vigumu wanandoa hao wawili kuishi pamoja. Na suala la uke wenza ndio limeleta matatizo zaidi kinyume na lengo la msingi la kuleta utulivu, amani, maelewano, mapenzi na kuondoa tatizo la wanawake ziada ambao wapo ulimwengu. Lakini kwa sababu ya kutoeleweka hasa kwa akina dada ndio linaleta talaka na uhasama baina jamii hizo zilizoungana.

        Masharti katika Uislamu yanatakiwa yaende sambamba na anavyotaka Allah na Mtume Wake na kwenda kinyume na kauli zao ni kuingia katika ufasiki na udhalimu na hata katika ukafiri. Mtume (s.a.w.) amesema: “Hakuna kumtii kiumbe yeyote ikiwa katika hilo kutamuasi Muumba”. Hivyo, mume anatakiwa aendelee kutenda haki kwa wakeze wawili katika kulala kwa zamu na kuwapitia katika tunu, mavazi, chakula na mengineyo. Na haya maneno ya kusema kuwa ima uniache mimi au yeye ni katika vitisho vya kike wala haziathiri, hivyo mume aendelee kuwa na wote wawili. Na jambo la kuelewa hapa ni kuwa talaka haitoki kwa mke na hata akisema “Ukimfata ndio talaka yangu”, talaka inakuwa haijatoka. Mke anaweza kutaka mume amuache lakini ikiwa mume hana makosa itabidi mke amrudishie mahari mumewe.

        Mke au mume anakosa kujua sheria kwa kuwa ima malezi ya wazazi wao hayakuwa mazuri au hawakupata mafunzo ya msingi kabisa. Ndio Mtume Muhammad (s.a.w.) akahimiza sana kwa kusema: “Mke anaolewa kwa sababu ya sifa nne: Kwa mali yake, nasaba yake, uzuri wake na Dini yake. Hivyo, oa aliye na Dini au utahasirika” (al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Abi Hurayrah [r.a]).

        Ikiwa mke ni mchaMungu inakuwa ni rahisi kuweza kuelewa sheria ya Allah, lakini ikiwa ni kinyume na hivyo inakuwa ni matatizo makubwa sana. Lakini Muislamu si mtu wa kukata tama na rehema ya Allah ambaye anasema: “Usikate tamaa na rehema ya Allah kwani hawakati tama ila watu makafiri” (12: 87). 

        Kitu cha kufanya ni kujaribu kutumia mashoga zake au masheikh ili waende wakamnasihi na kumueleza kama mke anatakiwa awe vipi katika maadili na tabia. Mtume Muhammad (s.a.w.) amesema: “Dini ni nasiha” (Muslim kutoka kwa Tamiim ad-Daariy [r.a.]).

        Katika kumpatia nasaha huenda akabadilika na akawa mke mzuri. Na katika kutoa hii nasiha inatakiwa zitumie njia na mbinu mbali mbali ili kumuelimisha na kumfahamisha na kutumike hekima na maneno matamu. Na nina yakini kuwa mke huyo wa mwanzo atakuwa ni mwenye kubadilika na ikawa ni faraja kwa wanandoa hao na familia zao.

        Ikiwa mbinu zote zimetumika na hakuna natija yoyote basi itabidi talaka itoke na hapo mume ndiye atakayekuwa ni mwamuzi wa mwisho. Lakini tunaomba isifike hali hiyo.

        Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share