'Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jama’aah Kuhusu Kutokudumu Milele Waislamu Motoni

 

 

‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah

Kuhusu Kutokudumu Milele Waislamu Motoni

 

Alhidaaya.com

 

‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Kuhusu Kutokudumu Milele Waislamu Motoni

 

 

Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah wanaamini kwamba baadhi ya Waislamu wataingia Jannah bila ya kufanyiwa hesabu au kupewa adhabu. Wengine wataingia Jannah baada ya kufanyiwa hesabu, Wengine wataingia Jannah baada ya kuadhibiwa motoni kama Anavyotaka Allaah ('Azza wa Jalla) kisha Atawatoa humo.

 

 

Kutolewa motoni kisha kuingizwa Jannah hakutawasababishia huzuni au dhiki huko Peponi kwa sababu Jannah (Pepo) ni makazi ya raha tupu. Kama ilivyotajwa katika Qur-aan na Sunnah, watapata kila walichokipata wakaazi wengine wa Peponi.

 

 

Hakuna dalili inayoashiria kwamba watu hao watakuwa na hisia za majuto baada ya kuingia kwao Jannah kutokana na adhabu watakazozipata motoni.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutajia hali zao zitakavyokuwa baada ya kutolewa motoni kama ifutavyo:

 

 

1.  Watatumbukizwa Kwenye Mto Wa Uhai Wabadilike Kuwa Wapya:

 

Imesimuliwa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

 ((إِذَا دَخَلَ أَهْلُ الْجَنَّةِ الْجَنَّةَ وَأَهْلُ النَّارِ النَّارَ يَقُولُ اللَّهُ : مَنْ كَانَ فِي قَلْبِهِ مِثْقَالُ حَبَّةٍ مِنْ خَرْدَلٍ مِنْ إِيمَانٍ فَأَخْرِجُوهُ، فَيَخْرُجُونَ، قَدْ امْتُحِشُوا، وَعَادُوا حُمَمًا، فَيُلْقَوْنَ فِي نَهَرِ الْحَيَاةِ ، فَيَنْبُتُونَ كَمَا تَنْبُتُ الْحِبَّةُ فِي حَمِيلِ السَّيْلِ)) وَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((أَلَمْ تَرَوْا أَنَّهَا تَنْبُتُ صَفْرَاءَ مُلْتَوِيَةً)) رواه البخاري ومسلم
 

((Watu wa Peponi watakapoingia Peponi,   na wa motoni watakapoingia motoni, Allaah Atasema [kuwaambia Malaika]: “Yeyote aliyekuwa na Iymaan moyoni mwake, uzito wa chembe cha atomu, mtoeni!” Watamtoa humo, watatoka kama kwamba ni mifupa iliyounguzwa na watabadilika kuwa makaa. Watatumbukizwa katika mto wa uhai, kisha watakuwa [kimaumbile] humo kama mfano wa mbegu zinapomea katika ufa [mwatuko] wa mafuriko)). Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Je huwaoni wanavyomea [wanavyokuwa kimaumbile] manjano na kupinda?)). [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

2. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba watabadilika watakapotolewa motoni.

 

Imesimuliwa toka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusu Jahannamiyuwn (watu wa motoni):

 

((يَخْرُجُونَ مِنْ النَّارِ بَعْدَ أَنْ يَكُونُوا فِيهَا، فَيَخْرُجُونَ كَأَنَّهُمْ عِيدَانُ السَّمَاسِمِ، فَيَدْخُلُونَ نَهَرًا مِنْ أَنْهَارِ الْجَنَّةِ فَيَغْتَسِلُونَ فِيهِ فَيَخْرُجُونَ كَأَنَّهُمْ الْقَرَاطِيسُ)) رواه مسلم  
 

((Watatolewa motoni baada ya kuweko humo. Kisha watatoka kama kwamba ni matawi ya chembe za ufuta. Kisha wataingia katika Mto miongoni mwa mito ya Jannah ambako wataoga kisha watatoka [weupe] humo kama karatasi)). [Muslim].

 

Imaam An-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema: “Ufuta imekusudiwa chembe za ufuta maarufu zinazotoa mafuta ya ufuta”. 

 

 

Imaam Abuu As-Sa’adaat Al-Mubaarak bin Muhammad bin ‘Abdil-Kariym Al-Jazariyy anayejulikana kama: Ibn Al-Athiyr (Rahimahu Allaah) amesema: “Inamaanisha: Na Allaah Anajua zaidi - kwamba matawi ya ufuta yanapokusanywa na kuachwa juani ili mbegu zake zikusanywe, hubadilika kuwa membamba na meusi kama kwamba zimeunguzwa. Ndio wakafananishwa watu hawa. Kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). ((Kisha watatoka humo kama karatasi)) wamefananishwa kama karatasi kwa sababu watakuwa weupe mno baada ya kuoga mtoni na weusi wote waliokuwa nao utaondoshwa.” [Sharh Muslim].

 

 

Kadhaalika, imesimuliwa na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((يَخْرُجُ مِنْ النَّارِ بِالشَّفَاعَةِ كَأَنَّهُمْ الثَّعَارِيرُ، قُلْتُ: مَا الثَّعَارِيرُ؟ قَالَ: الضَّغَابِيسُ)) البخاري

((Watatoka motoni kwa sababu ya shafaa’ah (uombezi) wakiwa kama matango)). [Al-Bukhaariy].

 

 

Al-Haafidhw Ibn Hajr Al-‘Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema: “Kuhusu matango madogo, makusudio ni, kama kitu cheupe na kidogo.”

 

Tanbihi:

 

Sifa ya weupe huu unakusudiwa vile watakavyokuwa baada ya kukua (kumea) [Fat-h Al-Baaariy (11/429)]. Lakini mwanzo watakapotoka motoni watakuwa kama makaa kama inavyoelezea Hadiyth ifuatayo:

 

 

 

3.  Watakua kama Lulu kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atawaruzuku Radhi Zake na Hatawaghadhibikia tena.

 

Imesimuliwa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((فَيَقُولُ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ : شَفَعَتْ الْمَلَائِكَةُ، وَشَفَعَ النَّبِيُّونَ، وَشَفَعَ الْمُؤْمِنُونَ، وَلَمْ يَبْقَ إِلَّا أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ، فَيَقْبِضُ قَبْضَةً مِنْ النَّارِ فَيُخْرِجُ مِنْهَا قَوْمًا لَمْ يَعْمَلُوا خَيْرًا قَطُّ قَدْ عَادُوا حُمَمًا، فَيُلْقِيهِمْ فِي نَهَرٍ فِي أَفْوَاهِ الْجَنَّةِ يُقَالُ لَهُ " نَهَرُ الْحَيَاةِ " فَيَخْرُجُونَ كَمَا تَخْرُجُ الْحِبَّةُ فِي حَمِيلِ السَّيْلِ ... قَالَ : فَيَخْرُجُونَ كَاللُّؤْلُؤِ فِي رِقَابِهِمْ الْخَوَاتِمُ ، يَعْرِفُهُمْ أَهْلُ الْجَنَّةِ، هَؤُلَاءِ عُتَقَاءُ اللَّهِ الَّذِينَ أَدْخَلَهُمْ اللَّهُ الْجَنَّةَ بِغَيْرِ عَمَلٍ عَمِلُوهُ وَلَا خَيْرٍ قَدَّمُوهُ ، ثُمَّ يَقُولُ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ فَمَا رَأَيْتُمُوهُ فَهُوَ لَكُمْ، فَيَقُولُونَ : رَبَّنَا أَعْطَيْتَنَا مَا لَمْ تُعْطِ أَحَدًا مِنْ الْعَالَمِينَ، فَيَقُولُ لَكُمْ عِنْدِي أَفْضَلُ مِنْ هَذَا ، فَيَقُولُونَ: يَا رَبَّنَا أَيُّ شَيْءٍ أَفْضَلُ مِنْ هَذَا، فَيَقُولُ  رِضَايَ فَلَا أَسْخَطُ عَلَيْكُمْ بَعْدَهُ أَبَدًا)) رواه البخاري  ومسلم 

 

((Allaah Atasema [Peponi]: “Malaika wameshaombea shafaa’ah, Manabii wameshaombea shafaa’ah, Waumini wameshaombea shafaa’ah, hakuna aliyebakia isipokuwa Mwenye Kurehemu kuliko wote wanaorehemu.” Kisha Atateka kutoka motoni na Atatoa watu wasiopata kufanya jema lolote [duniani] na ambao wamebadilika kuwa makaa. Atawatumbukiza katika Mto ulio kingoni mwa Jannah unaoitwa ‘Mto wa Uhai’ watatoka humo kama zinavyotoka mbegu katika ufa wa mafuriko. Kisha watatoka wakiwa kama lulu wakiwa na mapambo shingoni mwao na watu wa Jannah watawatambua. Hawa ni waliofidiwa [waliokombelewa] na Allaah Akawaingiza Jannah bila hata ya kuwa wametenda ‘amali njema au kheri yoyote waliyoitanguliza. Kisha Atasema: “Ingieni Jannah,  mtakayoyaona humo ni yenu.” Watasema: “Ee Rabb wetu, Umetupa ambayo Hujapatapo kumpa yeyote kati wa walimwengu.” Atasema: “Mtapata kutoka Kwangu yaliyo bora kuliko haya” Watasema: “Ee Rabb wetu! Kitu gani tena kitakachokuwa bora kuliko haya?” Atasema: “Radhi Zangu kwani Sitoghadhibika tena nanyi kamwe.”)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Hii ni Hadiyth muhimu ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametaja daraja ya juu kabisa itakavyokuwa ya watu watakaotolewa motoni ambao Rabb wao Atawaruzuku, karama, heshima, na fadhila zikiwemo:

 

  • Kutumbukizwa katika Mto wa Uhai ili wakuwe (waumbike) kama wapya.

 

 

  • Kutoka katika Mto kama kwamba lulu wakiwa wamevaa mapambo shingoni mwao.

 

  • Kupewa kila watakachokiona huko Jannah.

 

 

  • Kudhania kwao kutokana na kheri na baraka na furaha ya hali ya juu watakayoipa kwamba Allaah Amewakirimu kwa jambo Hajapatapo kumkirimu yeyote mwengine.

 

 

  • Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atawaruzuku Radhi Zake na Hatowaghadhibikia tena kamwe.

 

 

Daraja ambazo Allaah Atawakirimu watu watakoingia Jannah zimethibitika katika Hadiyth  ifuatayo:

 

 

Imesimuliwa kutoka kwa ‘Abdulllaah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

  إِنِّي لَأَعْلَمُ آخِرَ أَهْلِ النَّارِ خُرُوجًا مِنْهَا وَآخِرَ أَهْلِ الْجَنَّةِ دُخُولًا، رَجُلٌ يَخْرُجُ مِنْ النَّارِ كَبْوًا فَيَقُولُ اللَّهُ: اذْهَبْ فَادْخُلْ الْجَنَّةَ، فَيَأْتِيهَا فَيُخَيَّلُ إِلَيْهِ أَنَّهَا مَلْأَى، فَيَرْجِعُ فَيَقُولُ: يَا رَبِّ وَجَدْتُهَا مَلْأَى، فَيَقُولُ: اذْهَبْ فَادْخُلْ الْجَنَّةَ، فَيَأْتِيهَا فَيُخَيَّلُ إِلَيْهِ أَنَّهَا مَلْأَى، فَيَرْجِعُ فَيَقُولُ: يَا رَبِّ وَجَدْتُهَا مَلْأَى، فَيَقُولُ: اذْهَبْ فَادْخُلْ الْجَنَّةَ، فَإِنَّ لَكَ مِثْلَ الدُّنْيَا وَعَشَرَةَ أَمْثَالِهَا - أَوْ: إِنَّ لَكَ مِثْلَ عَشَرَةِ أَمْثَالِ الدُّنْيَا - فَيَقُولُ: تَسْخَرُ مِنِّي - أَوْ: تَضْحَكُ مِنِّي - وَأَنْتَ الْمَلِكُ؟ فَلَقَدْ رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ضَحِكَ حَتَّى بَدَتْ نَوَاجِذُهُ، وَكَانَ يَقُولُ: ((ذَاكَ أَدْنَى أَهْلِ الْجَنَّةِ مَنْزِلَةً)) رواه البخاري  ومسلم  

 

Nawajua watu wa mwisho kabisa watakaotoka motoni, na watu wa mwisho kabisa watakaoingia Jannah. Atakuwa ni mtu atakayetoka akitambaa kutoka motoni kisha Allaah Atamwambia: “Nenda na ungie Jannah.” Ataifikia lakini atadhania kwamba imejaa. Atarudi na kusema: “Rabb wangu! Nimeikuta imejaa!” Allaah Atasema: “Nenda ingia Jannah.” Atafikia lakini atadhania kwamba imejaa. Atarudi na kusema: “Rabb wangu! Nimeikuta imejaa!” Allaah Atasema: “Nenda ingia Jannah, kwani utapata mfano wa dunia na mara kumi yake.” Au: “Utapata mfano wa mara kumi ya dunia.” Atasema [mja]: “Je unanifanyia masikhara?” Au: “Je unanidhihaki na hali Wewe ni Al-Malik?” Nikamuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akicheka mpaka magego yake yakadhihirika na huku akisema: ((Huyo ndiyo mtu wa daraja ya chini kabisa Jannah)). [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

 

4. Watajulikana kama ni Al-Jahannamiyuwn (watu wa motoni) au ‘Utaqaa al-Jabbaar’ (waliokombolewa na Mwenye Ujabari) Kisha wataondoshewa jina hilo.

 

 

Maana ya Al-Jahannamiyuwn ni wingi wa Jahannam yaani moto. Ina maana kwamba Allaah Amewakomboa motoni.

 

 

Imesimuliwa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((يَخْرُجُ قَوْمٌ مِنْ النَّارِ بَعْدَ مَا مَسَّهُمْ مِنْهَا سَفْعٌ فَيَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ فَيُسَمِّيهِمْ أَهْلُ الْجَنَّةِ الْجَهَنَّمِيِّينَ)) رواه البخاري 

 

((Miongoni mwa watu watatolewa motoni baada ya miale yake imewagusa [na kuwabadilisha rangi] kisha wataingizwa Jannah. Na watu wa Jannah watawaita al-Jahannamiyuwn)). [Al-Bukhaariy].

 

 

Na pia kauli nyingine kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu): kwa Hadiyth iliyokusanywa na Imaam Ahmad:

 

((... فَيَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ فَيَقُولُ لَهُمْ أَهْلُ الْجَنَّةِ: هَؤُلَاءِ الْجَهَنَّمِيُّونَ! فَيَقُولُ الْجَبَّارُ: بَلْ هَؤُلَاءِ عُتَقَاءُ الْجَبَّارِ عَزَّ وَجَلَّ)) 

 

((…wataingia Jannah na watu wa Jannah watasema: “Hawa ni Al-Jahannamiyuwn lakini Al-Jabbaar [Mwenye Ujabari] Atasema: “Hapana! Bali wao ni waliokombolewa na Al-Jabbaar ‘Azza wa Jalla)). [Imepewa daraja ya Swahiyh na Ibn Mandah katika ‘al-Iymaan’ (2/847), Ibn Khuzaymah (2/710) na Al-Albaaniy katika ‘Hukm Taarik As-Swalaah’ (uk. 33).

 

 

 

Ibn Hibbaan amesimulia kutoka kwa Abuu Sa’iyd al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

((فَيُسَمَّوْنَ فِي الْجَنَّةِ الْجَهَنَّمِيِّينَ مِنْ أَجْلِ سَوَادٍ فِي وُجُوهِهِمْ، فَيَقُولُونَ : بَّنَا أَذْهِبْ عَنَّا هَذَا الاسْمَ ، قَالَ : فَيَأْمُرُهُمْ فَيَغْتَسِلُونَ فِي نَهْرِ الْجَنَّةِ , فَيَذْهَبُ ذَلِكَ مِنْهُمْ)).

 

((Wataitwa humo Jannah: “al-Jahannamiyyuwn” kutokana na weusi katika nyuso zao. Watasema: “Rabb wetu! Tuondoshee jina hili!”)) Akasema: ((Kisha Atawaamrisha waoge katika Mto wa Jannah  wataondoshewa hilo [Jina])). [Imepewa daraja ya Swahiyh na Ibn Hibbaan (16/457) na pia Ash-Shu’ayb al-‘Arnauwtw].

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba mchovyo mmoja tu wa Jannah utamfanya Muislamu asahau tabu zote alizozokabiliana nazo duniani, itakuwaje basi ikiwa Jannah ndio makazi yake ya milele?

 

 

Imesimuliwa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((يُؤْتَى بِأَنْعَمِ أَهْلِ الدُّنْيَا مِنْ أَهْلِ النَّارِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَيُصْبَغُ فِي النَّارِ صَبْغَةً ثُمَّ يُقَالُ : يَا ابْنَ آدَمَ هَلْ رَأَيْتَ خَيْرًا قَطُّ ؟ هَلْ مَرَّ بِكَ نَعِيمٌ قَطُّ ؟ فَيَقُولُ : لَا وَاللَّهِ يَا رَبِّ ، وَيُؤْتَى بِأَشَدِّ النَّاسِ بُؤْسًا فِي الدُّنْيَا مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ فَيُصْبَغُ صَبْغَةً فِي الْجَنَّةِ فَيُقَالُ لَهُ : يَا ابْنَ آدَمَ هَلْ رَأَيْتَ بُؤْسًا قَطُّ ؟ هَلْ مَرَّ بِكَ شِدَّةٌ قَطُّ ؟ فَيَقُولُ : لَا وَاللَّهِ يَا رَبِّ مَا مَرَّ بِي بُؤْسٌ قَطُّ، وَلَا رَأَيْتُ شِدَّةً قَطُّ)) رواه مسلم

 

((Mtu aliyeneemeka kabisa duniani ambaye ni miongoni mwa watu wa motoni ataletwa Siku ya Qiyaamah na atachovywa mara moja motoni kisha ataulizwa: “Ee mwanadamu! Umepatapo kuona zuri lolote?  Umewahi kupata raha yoyote?” Atasema: “Hapana Mola wangu!” Kisha ataletwa mtu aliyepata shida kabisa duniani akiwa miongoni mwa wa watu wa Peponi atachovywa Peponi ataambiwa: “Ee mwan Aadam! Je umepatapo kuona ubaya wowote? Je imekupitia shida yoyote?” Atasema: “Hapana Rabb wangu! Sijapatapo kuona ubaya wowote wala haijanipitia shida yoyote.”)) [Muslim].

 

 

Dalili nyingine kwamba mchovyo mmoja wa neema za Jannah utamuondoshea tabu zote za awali, mpaka tabu za kuadhibiwa motoni. Hivi ni kuhusiana na yaliyotajwa kuhusu kubadilishwa kwake mtu baada ya kutumbukizwa katika ‘Mto wa Uhai’ ni katika mapokezi yaliyosimuliwa na Imaam Muslim (2836) kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anh) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema:

 

((مَنْ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ يَنْعَمُ لَا يَبْأَسُ لَا تَبْلَى ثِيَابُهُ وَلَا يَفْنَى شَبَابُهُ))

 

((Atakayeingia Jannah atastarehe na hatokuwa na kuhuzunika, nguzo zake hazitochakaa wala ujana wake hautatoweka [hatozeeka])).

 

 

Neema hiyo inathibitisha kwamba atakayeingizwa Jannah ataondoshewa tabu zote na inamaanisha kwa ujumla kila atakayeingia Jannah, ikiwa ni mwenye kuingizwa motoni kwanza au hakuingizwa.

 

 

Al-Qaadhwiy amesema: “Kinachomaanishwa hapa ni kwamba Jannah ni makazi ya kuthibiti na neema ambazo hazitobadilika au kuathirika kwa tabu zozote au ufisadi.”  [Tuhfat al-Ahwadhi (7/194)]. 

 

Kwa sababu hizo, Allaah (Subhaanahu wa Taa'alaa) Anatuambia hali za watu wa Jannah watakapoingia humo:

 

 

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَذْهَبَ عَنَّا الْحَزَنَ ۖ إِنَّ رَبَّنَا لَغَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٤﴾

Na watasema: “AlhamduliLLaah, Himidi Anastahiki Allaah Ambaye Ametuondoshea huzuni. Hakika Rabb wetu bila shaka ni Mwingi wa kughufuria,  Mwingi wa kupokea shukurani.

 

 

الَّذِي أَحَلَّنَا دَارَ الْمُقَامَةِ مِن فَضْلِهِ لَا يَمَسُّنَا فِيهَا نَصَبٌ وَلَا يَمَسُّنَا فِيهَا لُغُوبٌ ﴿٣٥﴾

Ambaye Ametuweka nyumba yenye kudumu kwa fadhila Zake, hayatugusi humo taabu na mashaka na wala haitugusi humo machovu. [Faatwir: 34-35].

 

 

 

‘Allaamah As-Sa’diy (Rahimahu Allaah) amesema: “Inamaanisha maskani ya makazi ya milele, maskani ambayo mtu atataka kuishi milele kwa sababu ya mazuri mengi yaliyomo humo na kwa sababu ya starehe zinazodumu na kwa sababu ya kutokuweko cha kuondosha starehe hizo.

 

 

Na hayo ni kutokana ((kwa fadhila Zake)) kwetu na neema Zake, si kwa sababu ya ‘amali zetu, kwani ingelikuwa si fadhila Zake, tusingelifikia tulivyofikia.

 

hayatugusi humo taabu na mashaka na wala haitugusi humo machovu

 

  yaani, hakutakuweko na machofu katika miili yetu, nyoyo au nguvu, wala katika raha nyingi. Hii inaonyesha kwamba Allaah Atafanya miili yao iumbike vizuri upya na Atawafanyia kila sababu za kuwafanyia makazi yao yawe ni yenye raha za kudumu, ili wasiguswe na tabu au wahka wala huzuni.” [Tafsiyr As-’Sa’dy 689].

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share