19-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Tawhiyd Ni Bora kuliko Mali Na Starehe Za Dunia, Neno La Tawhiyd Ni Zito Siku ya Qiyaamah

 

Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd

 

19-Tawhiyd Ni Bora kuliko Mali Na Starehe Za Dunia,

Neno La Tawhiyd Ni Zito Siku ya Qiyaamah

 

 

 

Makafiri Quraysh wa Makkah walitaka kumpa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mali na starehe za dunia, walitaka kumpa cheo  ili aache kulingania Tawhiyd, lakini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakufadhilisha hayo, bali alijikita katika da’wah yake kwa kuwa aliamini kulingania Tawhiyd ndio haki na ndio itakayomfaa bin Aadam Siku ya Qiyaamah, Siku ambayo mtu atatamani kufidia kwa mali yake yote aliyokuwa nayo duniani ili aepukane na adhabu ya Moto kwa kukanusha Tawhiyd kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَمَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَن يُقْبَلَ مِنْ أَحَدِهِم مِّلْءُ الْأَرْضِ ذَهَبًا وَلَوِ افْتَدَىٰ بِهِ ۗ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٩١﴾

Hakika wale waliokufuru na wakafa nao wakiwa makafiri, basi haitakubaliwa kutoka kwa mmoja wao dhahabu ya ujazo wa dunia nzima lau wakitaka kujifidia nayo. Hao watapata adhabu iumizayo na hawatopata mwenye kuwanusuru. [Aal-‘Imraan: 91]

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

((يَقُولُ اللهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى لِأَهْوَنِ أَهْلِ النَّارِ عَذَابًا: لَوْ كَانَتْ لَكَ الدُّنْيَا وَمَا فِيهَا، أَكُنْتَ مُفْتَدِيًا بِهَا؟ فَيَقُولُ: نَعَمْ ، فَيَقُولُ: قَدْ أَرَدْتُ مِنْكَ أَهْوَنَ مِنْ هَذَا وَأَنْتَ فِي صُلْبِ آدَمَ: أَنْ لَا تُشْرِكَ - أَحْسِبُهُ قَالَ: وَلَا أُدْخِلَكَ النَّارَ - فَأَبَيْتَ إِلَّا الشِّرْك))

((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Atamwambia mtu atakayekuwa na adhabu nyepesi kabisa Motoni: “Je, ungekuwa una dunia nzima na yaliyomo ndani yake [mali n.k.] ungeitolea fidia?” Atajibu: “Ndio.” Atasema Allaah: “Nilikutaka kwa jambo jepesi zaidi kuliko hayo, ulipokuwa katika uti wa mgongo wa Aadam kwamba usinishirikishe.” Nadhani Akasema: “Na sitokuingiza motoni lakini umekataa isipokuwa kunishirikisha”)). [Muslim]

 

Ni dhahiri kwamba neno la Tawhiyd ambalo ni jambo jepesi kabisa kulitamka litakuwa na thamani zaidi kuliko dunia na yaliyomo duniani, bali neno la Tawhiyd; laa ilaa illa Allaah litakuwa zito kabisa katika Miyzaan ya ‘amali Siku ya Qiyaamah:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرَيِّ (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) عَنْ رَسُولِ الله (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ ((قَالَ مُوسَى عَلَيْهِ السَّلامُ يَا رَبِّ! عَلِّمْنِي شَيْئًا أَذْكُرُكَ وَأَدْعُوكَ بِهِ. قَالَ: قُلْ يَا مُوسَى: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللهُ.  قَالَ يَا رَبِّ! كُلُّ عِبَادِكَ يَقُولُونَ هَذَا. قَالَ: يَا مُوسَى،  لَوْ أَنَّ السَّمَوَاتِ السَّبْعَ وَعَامِرَهُنَّ غَيْرِي وَالأَرَضِينَ السَّبْعَ فِي كِفَّةٍ،  وَ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللهُ فِي كِفَّةٍ، مَالَتْ بِهِنَّ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللهُ))  رَوَاهُ ابْنُ حِبَّانَ وَالْحَاكِمُ وَصَحَّحَهُ.

Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه):  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muwsaa alisema: Ee Rabb wangu! Nifundishe kitu mahsusi kwangu ambacho kwacho nitakudhukuru na kukuomba duaa. (Allaah) Akasema: Ee Muwsaa!    Sema:

لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللهُ 

Laa ilaaha illa-Allaah.  

 

Muwsaa akasema: Ee Rabb wangu! Waja Wako wote wanasema hivi. (Allaah) Akasema: Ee Muwsaa, lau kama mbingu saba na kila kilichokuwemo isipokuwa Mimi, na ardhi saba zikiwekwa katika kiganja cha mizani, na laa ilaaha illa-Allaah ikawekwa katika kiganja kingine cha mizani, basi laa ilaaha illa-Allaah itazishinda hizo.” [Ibn Hibaan, na Al-Haakim ameikiri kuwa ni Swahiyh]

 

 

 

 

 

 

Share