Kuhudhuria Mwaliko Wa Krismasi Na Kupokea Zawadi Za Krismasi Inajuzu?

 

 

Kuhudhuria Mwaliko Wa Krismasi Na Kupokea Zawadi Za Krismasi Inajuzu?

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Swali: 

 

Asalam alikum, suala langu ni hili jee ni vibaya kualikwa na mkristo kula nyumbani kwake siku ya krismas? Na kukupa zawadi siku hio jee ni dhambi? In Shaa Allaah mtanijibu kwa nguvu zake Allaah   

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kula chakula cha Mkristo haikatazwi na Dini ya Kiislamu bali zimekuja nasw za moja kwa moja kuhusu jambo hili.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Anasema:

 

الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ ۖ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ ۖ 

“Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu na chakula chenu ni halali kwao” [Al-Maaidah: 5].

 

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapa ruhusa ya kufanya hivyo.

 

 

Kwa hivyo ki-msingi kula chakula chao kinaruhusiwa kwa Muislamu ila kiwe tu ni cha halali. Ikiwa ni chakula ambacho ni haramu kwetu basi itakuwa haifai kula chakula hicho au kikiwa kimechanganywa chakula ambacho ni haramu na kile kilicho halali, hivyo kukifanya chote kuwa haramu.

 

 

Lakini unapozungumzia kuhusu sherehe zao ambapo kutakuwa na chakula kwa kuadhimisha siku kuu hiyo yao inakuwa haifai kwa Muislamu kushirikiana nao katika jambo hilo. Hivyo, ukialikwa na Mkristo kula nao chakula cha Krismasi inafaa ukatae kwani si halali kabisa, lakini ikiwa ni siku ambayo si sherehe kwao unaweza kula bila ya matatizo yoyote.

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah, watu wa Madiynah walikuwa na siku kuu zao ambazo walikuwa wanasherehekea, naye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewabadilishia kwa siku ambazo ni bora zaidi, nazo ni: 'Iyd  baada ya Ramadhwaan na 'Iyd ya baada ya Hijjah.

 

 

Hivyo, haifai kwa Muislamu kusherehekea siku kuu nyengine zozote mbali na hizo hata zile ambazo Waislamu wenyewe wamezizua kama za Mawlid na mwaka mpya wa Kiislamu na zingine kama za Mi'iraaj na Niswf Sha'baan.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share