Tofauti Ya Miezi Ya Kiislamu Na ya Kikafiri Na Zipi Sifa Zake?

 

SWALI:

 

NI KWA NINI MIEZI YA KIISLAMU INAKUWA SANJARI NA MIEZI YA KIMAGHARIBI LAKINI INAKUWA TOFAUTI KATIKA MUDA:

 

NAOMBA NAKALA YA KALENDA ILIYO NA MCHANGANYIKO WA MIEZI YA PANDE ZOTE. ZIPI SABABU ZA KUITWA MWEZI FULANI NA KISA CHA KILA MWEZI AU SIKU KATIKA MWEZI FULANI, mfano: Siku ya 9 na 10 mfungo nne nilipata kusimuliwa kuwa ndiyo Ban Israil waliangamizwa kwa kumuasi ALLAH (Subhanahu wa ta'ala)

 

KWA NINI KILA MWEZI UNA SIFA ZAKE NA HAKUNA MFANANO WA SIFA NA KAMA ZIPO NIZIPI?

 

ALLAH(Subhanahu wataala) awalipe kwa yote myatendayo na wajaze kheri.Inshaallah.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu miezi ya Kiislamu na ile ya Kimagharibi.

Tutajaribu kufafanua kwa kadiri tulivyolifahamu swali lako.

 

Mwanzo inatafaa tuelewe kuwa kuna tofauti ya msingi baina ya miezi ya Kiislamu na mingine. Miezi ya Kiislamu inafuatana na mwandamo wa mwezi ambao kila mwezi unakuwa na siku 29 au 30 ilhali miezi ya Kimagharibi inafuata jua, hivyo kufanya siku zake kuwa 28, 29 kwa Februari na kawaida ni 30 au 31. Kwa ajili hiyo, mwaka wa Kiislamu unakuwa na takriban siku 11 kidogo kuliko mwaka wa Kimagharibi.

 

Ama kuhusu miezi ya Kiislamu, Allaah Aliyetukuka ndiye Aliyeifanya kuwa kumi na mbili, minne ikiwa ni mitukufu. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Hakika idadi ya miezi kwa Allaah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allaah tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa” (at-Tawbah 9: 36).

 

Ama kuhusu nakala za kalenda kukutumia kwa njia ya mtandao inakuwa si wepesi kwani hizo zinachapishwa na kuuzwa katika miji na nchi tofauti. Kinachotakiwa ni wewe kwenda katika maduka yanayouza vitabu vya Kiislamu na kununua moja ili uweze kuwa nayo na kutazama unayoyahitaji.

 

Ama kuhusu sababu ya kuitwa majina ya miezi ni Allaah Aliyetukuka Mwenye kujua zaidi kwani Yeye haulizwi Anayofanya, sisi ndio wenye kuulizwa.

 

Ama kuhusu siku zina tarehe na majina yake zilizopatiwa na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mfano ni:

 

1.     Tarehe 10 wala sio tisa ya Mfungo Nne (yaani Muharram). Siku hiyo inaitwa ‘Aashuraa’ nayo ni kwa ajili ya Bani Israa’il wakati wa Muusa (‘Alayhis Salaam) waliokolewa na Allaah Aliyetukuka sio kuangamizwa kama ulivyo sema. Kwa ajili ya kuokolewa huko, wakawa wanafunga siku hiyo kama kutoa shukran kwa Allaah Aliyetukuka. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akatuongezea tarehe tisa ambayo inayojulikana kama Taasuaa’ ili tufunge siku hizo mbili tutofautiane na Mayahudi.

 

 

2.     Tarehe 9 ya Dhul Hijjah inajulikana kama siku ya ‘Arafah, kwani katika siku hiyo Mahujaji wanasimama katika wangwa wa ‘Arafah ili kujikurubisha kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Miezi ya Kiislamu ina sifa tofauti kwa kupatiwa sifa hizo na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake, ima kwa sababu ya kufanywa ‘Ibaadah miongoni mwa ‘Ibaadah kwa sababu nyingine yoyote ile.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share