Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الفَرْق بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
11-Kitabu Cha Kutengana Mke Na Mume
الطَّلَاقُ
Talaka
01: Taarifu Yake Na Dalili Za Uhalali Wake Kisharia:
Neno talaka "الطَّلَاقُ" katika lugha ya kawaida lina maana ya kuvunja agano na kufuta mkataba. Limenyambulika kutokana na neno "الإِطْلَاقُ" lenye maana ya kuachilia.
Ama katika istilahi ya kisharia, ni kuvunja fungamano la ndoa kwa tamko mahsusi la kutaliki au mfano wake, au kulivunja fungamano hilo papo kwa hapo (kwa talaka mtengano, utengano mdogo au mkubwa "طَلَاقٌ بَائِنٌ بَيْنُونَةٌ صُغْرَى أَوْ كُبْرَى"), au baada ya muda kwa kuachilia hadi muda wa eda umalizike (katika talaka rejea "طَلَاقٌ رَجْعِيْ").
Ndoa inayokusudiwa hapa ni ndoa sahihi yenye vigezo vyote vya kisharia. Ikiwa ni ndoa batili, basi talaka yake haiswihi wala haizingatiwi.
Uhalali Wa Talaka Kisharia:
Talaka imeruhusiwa kwa mujibu wa Qur-aan, Sunnah, 'Ijmaa na Kiakili.
(a) Katika Qur-aan:
1- Ni Kauli Yake Ta'aalaa:
"الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ"
"Talaka ni mara mbili. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa shariy’ah au kuachia kwa ihsaan". [Al-Baqarah: 229]
2- Na Neno Lake Ta'aalaa:
"لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً ۚ وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ • وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"
"Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia mahari yao. Wapeni kiliwazo kwa mwenye wasaa kadiri ya uwezo wake na mwenye dhiki kadiri ya uwezo wake. Maliwaza kwa mujibu wa ada, ni haki kwa wafanya ihsaan • Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha". [Al-Baqarah: 36-37]
3- Na Neno Lake Ta'aalaa:
"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ"
"Ee Nabiy! Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda (twaharah) zao, na hesabuni barabara eda". [At-Twalaaq: 01]
4- Na Neno Lake Ta'aalaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا"
"Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu". [Al-Ahzaab: 49]
5- Na Neno Lake Ta'aalaa:
"وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ سَرِّحُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ"
"Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao, basi wazuieni kwa wema au waachilieni kwa wema". [Al-Baqarah: 231]
(b) Katika Sunnah:
1- Toka kwa 'Umar (Radhwiya Allaah 'anhu):
"أّنَّ رَسُولَ الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ طَلَّقَ حَفْصَةَ ثُمَّ رَاجَعَهَا"
"Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaliki Hafswah, kisha akamrejea". [Hadiyth Swahiyh. Abu Daawuwd (2283), An-Nasaaiy (6/213), Ibn Maajah (2016) na wengineo]
2- Toka kwa Ibn 'Umar, amesema:
"كَانَتْ تَحْتِي امْرَأَةٌ وَكُنْتُ أُحِبُّهَا، وَكَانَتْ عُمَرُ يَكْرَهُهَا، فَقَالَ لِيْ: طَلِّقْهَا، فَأَبَيْتُ، فَأَتَى عُمَرُ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فذَكَرَ ذلِكَ لَهُ، فَقَالَ النَّبِيُّ :طَلِّقْهَا"
"Nilikuwa na mke niliyempenda sana, lakini (baba yangu) 'Umar alikuwa hampendi. Kisha akaja kuniambia: Mtaliki, nami nikakataa. 'Umar akamwendea Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamweleza hilo (kwamba nimekataa), na Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniamuru nimtaliki ". [Hadiyth Swahiyh. Abu Daawuwd (5138), At-Tirmidhiy (1189) na Ibn Maajah (2088)]
3- Toka kwa 'Aaswim bin Laqiytw bin Swabirah toka kwa baba yake au babu yake (alikuwa katika ujumbe wa Baniy Al-Muntafiq kwa Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam), alimwambia Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِنَّ لِي امْرَأَةٌ –فَذَكَرَ مِنْ طُوْلِ لِسَانِهَا وَإِيْذَائهَا- فَقَالَ: طَلِّقْهَا، قَالَ: يا رَسُولَ الله: إِنَّهَ ذاتُ صُحْبَةٍ وَوَلَدٍ، قَالَ: فَأَمْسِكْهَا وامُرْهَا، فإِنْ يَكُ فِيْهَا خَيْرٌ فَسَتَفْعَلُ، ولا تَضْرِبْ ظَعِيْنَتَكَ ضَرْبَكَ أَمَتِكَ"
"Mimi nina mke, (akamwelezea tatizo la ulimi wake mchafu na maudhi yake), na Rasuli akamwambia: Mtaliki. Akasema: Lakini yeye ndiye anayesuhubiana nami akinisaidia mimi na watoto ewe Rasuli wa Allaah! Rasuli akamwambia: Basi baki naye na umnasihi (akutii na aache tabia zake), na kama kheri yoyote iko kwake, basi atatii, na wala usimpige mwenza wako kipigo cha mtumwa". [Hadiyth Swahiyh. Abu Daawuwd (142) na Ahmad (4/33)]
(c) 'Ijmaa Na Kiakili:
Ibn Qudaamah (Allaah Amrehemu) amesema: "Watu wamekubaliana juu ya uhalali wa talaka, na mazingatio yanaonyesha kwamba ni jambo linaloruhusika".
Ama kiakili, ni kwamba mahusiano yanaweza kuharibika kati ya mke na mume, na ndoa kuendelea kati yao kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi, kwani mume atawajibikiwa matumizi pamoja na makazi kwa mke, na mke naye ataendelea kuzuilika ndani ya mazingira yaliyochafuka na magomvi yasiyo kwisha. Na kwa ajili hiyo, sharia imeweka talaka ili kuepusha madhara kwa pande zote mbili.