كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
النُّشُوْزُ وَعِلَاجُهُ
Uasi Wa Mke Kwa Mume Na Njia Za Kuutibu
04: Hatua Za Kutibu Uasi Wa Mke: (c) Hatua Ya Tatu: Atampiga:
Hili ni halali kwa mume kwa mkewe mwasi ikiwa njia mbili za awali hazikufaa kitu. Lakini katika kupiga, ni lazima achunge haya yafuatayo:
1- Pigo lisiwe la kujeruhi au kuumiza; lisiwe la kuvunja mfupa au kuharibu nyama mithili ya mtu anayelipiza kisasi. Kwani makusudio ya Neno Lake Ta'alaa:
"واضْرِبُوْهُنَّ"
"Na muwapige", ni pigo hafifu lisiloumiza.
Imepokelewa toka kwa 'Amri bin Al-Ahwasw kwamba Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"اسْتَوْصُوا بالنِّسَاءِ خَيْرًا، فَإِنَّمَا هُنَّ عَوَانٌ عِنْدَكُمْ، لَيْسَ تَمْلِكُونَ مِنْهُنَّ شَيْئًا غَيْرَ ذلِكَ، إِلاّ أَنْ يَأْتِيْنَ بِفَاحِشَةً مُبَيِّنَةٍ، فَإِنْ فَعَلْنَ فَاهْجُرُوْهُنَّ في المَضَاجِعِ، واَضْرِبُوهُنّ ضَرْبًا غَيْرَ مُبَرِّحٍ"
"Wafanyieni wema wanawake, kwani wao kwa hakika ni (kama) mateka walio chini ya mamlaka yenu, nanyi hamna jingine lolote zaidi ya hayo (ya kuwatendea wema). Ila tu kama watafanya tendo baya la wazi, na kama watafanya, basi wahameni kitanda, na muwapige pigo hafifu". [Hadiyth Hasan Lighayrihi. Imechakatwa na At-Tirmidhiy (1163), na Ibn Maajah (1851). Kuna udhaifu katika Sanadi yake, lakini ina Hadiyth mwenza kwa Ahmad (5/72)]
Hivyo basi, kusudio la pigo ni kumwadabisha na si kumuumiza au kumharibu. Ni pigo la kumvunja kisaikolojia na kumfanya ajirudi, si la kumvunja kiungo au kumharibu mwili.
2- Asimpige zaidi ya mapigo kumi, kwani Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لا يُجْلَدُ فَوْقَ عَشْرَةِ أَسْوَاطٍ إِلاّ في حَدٍّ منْ حُدُودِ الله"
"Haadhibiwi mtu kwa zaidi ya mijeledi kumi isipokuwa katika adhabu za kisharia za Allaah". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy]
3- Asipige uso wala sehemu hatari. Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyopokelewa na Mu'aawiyah bin Haydata:
"ولا تَضْرِبِ الوَجْهَ، ولا تُقَبِّحْ، ولا تَهْجُرْ إِلا في البَيْتِ"
"Wala usimpige uso, wala usitoe neno la kuutweza uso wake, na wala usimsuse isipokuwa ndani ya nyumba". [Hadiyth Hasan]
Kufanya hivi kunamdhalilisha mwanamke, kunamuumiza hisia na mwili, na pia kunamharibu. Mume akifanya hivyo, basi anapata madhambi, na mke atakuwa na haki ya kuomba talaka na kisasi.
4- Dhana yake ielemee zaidi kwamba kitendo cha kumpiga kitaondosha tatizo la mkewe huyo.
Kwa kuwa kupiga ni sehemu ya kutengeneza na kunyoosha. Na njia hii imehalalishwa ikiwa tu dhana itaelemea zaidi kuwa kuna mafanikio, na kama dhana haina nguvu, basi asimpige.
5- Kama atatii, basi asiendelee kumpiga. Ni kwa Neno Lake Ta'alaa:
"فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا"
"Wakikutiini, basi msitafute njia dhidi yao (ya kuwaudhi). Hakika Allaah daima Ni Mwenye Uluwa, Mkubwa wa Dhati, Vitendo na Sifa". [An-Nisaa: 34]
Angalizo:
Haitakikani kwa mume kuifanya njia hii ya kupiga kama ndio ada na desturi kwake. Akawa sasa anampiga mkewe kwa jambo lolote lile. Hii ni kinyume na maelekezo ya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Ameruhusu kupiga mke katika baadhi ya nyakati (wakati wa uasi), na hii ni baada ya kufeli njia mbili za awali ambazo ni kumnasihi na kumnyima jimai.
1- Imepokelewa toka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaah 'anhaa) akisema:
"مَا رَأَيْتُ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ضَرَبَ خَادِمًا لهُ قَط، ولا المَرْأَةَ، وَلاَ ضَرَبَ بِيَدِهِ شَيْئًا قَط إِلاّ أَنْ يُجَاهِدَ فِيْ سَبِيْل اللهِ"
"Sikumwona kamwe Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) akimpiga mtumishi wake au mwanamke (mke), na hakupiga kwa mkono wake katu kitu chochote isipokuwa kwenye mapambano ya Njia ya Allaah (Jihaad)". [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim, At-Tirmidhiy kwenye "Ash-Shamaail" (331), An-Nasaaiy katika "Al-'Ishrah" (281), na Ibn Maajah (1984)]
2- Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwelezea Abu Jahm kwa sifa mbaya ya kupiga piga sana wanawake na akamnasihi Faatwimah bint Qays kuhusiana na kuolewa na Abu Jahm (akimwambia):
"أَما أَبُو الجَهْمِ فَضَرَّابٌ لِلنِّسَاءِ"
"Ama Abu Jahm, huyo ni mpigaji sana wanawake".
Na katika tamko jingine:
"فَلَا يَضَعُ عَصَاهُ عَنْ عَاثِقِه"
"Haishushi fimbo yake mabegani". [Hadiyth Swahiyh. Muslim (1480), An-Nasaaiy (3245) na Abu Daawuwd (2284)]
3- Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَا يَجْلِدْ أَحَدُكُمُ امْرَأَتَهُ جَلْدَ الْعَبْدِ ثُمَّ يُجَامِعْهَا فِي آخِرِ الْيَوْمِ"
“Asimpige mmoja wenu mkewe kama anavyompiga mtumwa wake, kisha tena aje amuingilie usiku (linawezekana kweli hilo!!)”. [Al-Bukhaariy (4942) na Muslim (2855)]
Ama Hadiyth Marfuw-'u inayohadithiwa na watu isemayo:
"Usimuulize mtu kwa nini amempiga mkewe", hii ni Hadiyth Dhwa'iyf ambayo imechakatwa na Abu Daawuwd (2147), Ibn Maajah (1986) na Ahmad (1/20).