08-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume: (ii) Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: Nyumba Ya Kuishi
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الحُقُوْقُ بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume
07: Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: 4-Nyumba Ya Kuishi:
Ni lazima mume ampatie mkewe nyumba ya kuishi au sehemu ya kukaa kwa ‘itifaki ya ‘Ulamaa kutokana na dalili zifuatazo:
1- Kwa sababu Allaah Ta’alaa Amemwajibisha mume aliyemtaliki mkewe talaka rejea ampatie sehemu ya kukaa. Hivyo basi, wakati wa uhai wa ndoa, nyumba ya kuishi mke ni wajibu zaidi kwa mume kumpatia mkewe. Allaah Anasema:
"أَسْكِنُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ سَكَنتُم مِّن وُجْدِكُمْ"
“Wawekeni wanawake (mliowataliki) kwenye majumba mnayokaa nyinyi kwa kadiri ya kipato chenu”. [At-Twalaaq: 06]
2- Allaah Ta’alaa Amewajibisha mtangamano mwema kati ya mke na mume kwa kusema:
"وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ"
“Na kaeni nao kwa wema”. [An-Nisaa: 19]
Sehemu ya wema huo ulioamuriwa ni kumweka mahala ambapo patakuwa salama kwa yeye mwenyewe pamoja na mali yake.
3- Mke ni lazima awe katika sehemu itakayomhifadhi asionekane na watu, aweze kustarehe na mumewe kwa faragha na kuhifadhi mali zake. Hivyo ni lazima kwa mume ampatie sehemu kama hiyo.
Hadhi Ya Nyumba Kisharia:
Hadhi ya nyumba ya mke kisharia inategemea uwezo wa mume na hali ya mke kwa kipimo kimoja na matumizi, kwa kuwa vyote viwili ni haki iliyofungamana na ‘aqdi ya ndoa. Pia ni kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:
"أَسْكِنُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ سَكَنتُم مِّن وُجْدِكُمْ"
“Wawekeni wanawake (mliowataliki) kwenye majumba mnayokaa nyinyi kwa kadiri ya kipato chenu”. [At-Twalaaq: 06]
Na Neno Lake vile vile:
"لِيُنفِقْ ذُو سَعَةٍ مِّن سَعَتِهِ ۖ وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ فَلْيُنفِقْ مِمَّا آتَاهُ اللَّـهُ ۚ لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا مَا آتَاهَا ۚ"
“Ili mwenye wasaa agharimu kwa wasaa wake, na aliyebaniwa riziki yake, basi agharimie katika kile Alichompa Allaah. Allaah Haikalifishi nafsi yeyote ile isipokuwa kwa kile Alichoipa”. [At-Twalaaq: 07]
Wajibu wa matumizi kwa mke ni kwa mujibu wa hali ya mume ya uwezo wa kifedha; wa juu, au wa wastani, au wa chini. Na ndivyo hivyo hivyo kwa upande wa nyumba au makazi. Hii ni kauli ya Jumhuwr.
Faida:
1- Mke Kuishi Nyumba Moja Pamoja Na Jamaa Za Mume Wake.
Wanaokusudiwa hapa ni wazazi wawili wa mume na mtoto wa mume aliyezaa na mke mwingine. Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanaona kwamba haijuzu kuwachanganya wazazi wa mume au jamaa zake pamoja na mke ndani ya nyumba moja. Ni haki ya mke kukataa kukaa na watu hao isipokuwa kama mwenyewe ataridhika na hilo, kwa kuwa nyumba ni haki yake, na mume ni lazima asimshirikishe na mwingine yeyote ndani yake, kwani ni mara nyingi huzuka matatizo kwa uwepo wa watu wengine mbali na kukosekana umahususi kati ya mke na mume.
Ama Wanachuoni wa Kimaalik, wao wametofautisha kati ya mke mwenye hadhi na mke wa hali duni. Wamesema haifai kumweka mke mwenye hadhi pamoja na wazazi wa mume, lakini kwa mke duni wameruhusu isipokuwa tu kama kutakuwa na madhara kwake.
Ama kuishi nyumba moja na mtoto wa kiume wa mume aliyezaa na mke mwingine, ikiwa ni mkubwa anafahamu jimai, basi haitofaa kwa itifaki ya ‘Ulamaa, kwa kuwa uwepo wake utasababisha madhara. Lakini kama ni mdogo haelewi chochote kuhusu jimai, basi kukaa naye kunajuzu, na mke hana haki ya kukataa kukaa naye.
2- Jamaa Wa Mke Kuishi Pamoja Na Mume:
Mwanamke hana haki ya kumweka yeyote katika maharimu zake kwenye nyumba ya mumewe, na mume ana haki ya kukataa, isipokuwa kama ataridhia, hapo hakuna ubaya.
Ama mtoto wake aliyezaa na mume mwingine, haijuzu kwake kukaa naye bila ya ridhaa ya mume wake kwa mujibu wa kauli ya Jumhuwr.
3- Je, Wake Wenza Wanaweza Kuwekwa Nyumba Moja?
Fuqahaa wamekubaliana kwamba haijuzu kuwaweka nyumba moja wake wenza wawili na zaidi kwa kuwa kufanya hivyo si katika mtangamano mwema. Hilo mara nyingi husababisha magomvi ambayo Allaah Amekataza. Kadhalika, kila mmoja kati yao anaweza kusikia kishindo cha mume wakati anapomuingilia mwenzake au akashuhudia tendo lenyewe, na hilo bila shaka huchemsha uadui na wivu kati yao. Ni haki yenye nguvu kwao kukataa kuwekwa nyumba moja isipokuwa kama wenyewe wataridhia hilo, au ikawa hapana budi kutokana na sababu zisizokwepeka.
Ninasema: “Asili ya kila mke kuwekwa kwenye nyumba yake inayojitegemea, ni kitendo cha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Anavyosema Allaah Ta’aalaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ"
“Enyi walioamini! Msiingie nyumba za Nabiy isipokuwa mkipewa idhini ya kwenda kula si kungojea kiive”. [Al-Ahzaab: 53]
Katika aayah hii, Allaah Ta’aalaa Ameziita nyumba na si nyumba moja. Lakini kama wenyewe wataridhia kutokana na mazingira, basi hakuna ubaya, hiyo ni haki yao pia. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
