Rabb Wako Anakuamrisha Uwafanyie Wema Wazazi Wako Ili Akulipe Jannah (Pepo)

 

 Rabb Wako Anakuamrisha Uwafanyie Wema Wazazi Wako Ili Akulipe Jannah (Pepo)

 

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾

Na Rabb wako Amehukumu kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima. Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni. [Al-Israa: 23-24]

 

Kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kumeungamana na kuwaheshimu wazazi kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameamrisha kuwafanyia wema baada ya kuamrisha kumuabudu Yeye kama Alivyounganisha vile vile katika aya nyingine ya kumshukuru kwanza Yeye kisha wazazi:

 

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿١٤﴾

Na Tumemuusia insani kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa katika miaka mwili; ya kwamba, unishukuru Mimi, na wazazi wako; Kwangu ndio mahali pa kuishia. [Luqmaan: 14]

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametupa mafundisho katika Hadiyth zake nyingi kuhusu kuwaheshimu na kuwafanyia wema wazazi wetu:

 

عن أنس وغيره: أن رسول الله صلى الله عليه وسلم لما صعد المنبر قال: ((آمين آمين آمين)): فقالوا: يا رسول الله، علام أمنت؟ قال: ((أتاني جبريل فقال: يا محمد رغم أنف امرئ ذكرت عنده فلم يصل عليك، فقل: آمين. فقلت: آمين. ثم قال: رغم أنف امرئ دخل عليه شهر رمضان ثم خرج ولم يغفر له، قل: آمين. فقلت آمين. ثم قال: رغم أنف امرئ أدرك أبويه أو أحدهما فلم يدخلاه الجنة، قل: آمين. فقلت: آمين))

Kutoka kwa Anas na wengineo kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda katika minbar na akasema:((Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn)). Akaulizwa: Ee Rasuli wa Allaah, mbona umesema Aamiyn? Akasema: ((Amenijia Jibriyl na kuniambia: "Ee Muhammad, amekhasirika yule anayekusikia (unatajwa) na hakuswalii". Akasema: "Sema Aamiyn", ndio nikasema Aamiyn. Kisha akasema: "Amekhasirika unayemfikia mwezi wa Ramadhwaan na ukaondoka naye hakughufuriwa" (dhambi zake). Akasema: "Sema Aamiyn", ndio nikasema Aamiyn. Kisha akasema: "Amekhasirika yule anayekuwa mkubwa kisha wazazi wake wawili au mmoja wao bado yu hai, na wasiwe sababu yake kuingia Jannah (Peponi)". Akasema: "Sema Aamiyn", ndio nikasema Aamiyn)) [Tuhfat Al-Ahwadhiy 5:550]

 

Hadiyth nyingine:

 

 عن أبي هريرة، رضي الله عنه، عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: (( رغم أنف، ثم رغم أنف، ثم رغم أنف رجل أدرك والديه أحدهما أو كلاهما عند الكبر ولم يدخل الجنة))

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Amekhasirika, amekhasirika, amekhasirika, mtu ambaye wazazi wake wawili au mmoja wao wamefikia umri mkubwa (wa uzee) naye yu hai bado na haingii Jannah (Peponi) [kwa sababu ya kutowafanyia wema])) [Ahmad: 2:346] 

 

Kuwafanyia wema wazazi kunaendelea hata kama mzazi mmoja au wote wawili wamefariki, wema huo unaweza kuuendeleza kwa kuwaombea Du'aa, kuwatolea sadaka, kuwafanyia Hajj na kadhalika, na yote yamethibiti katika Sunnah. Kwa hiyo kama tunavyoona umuhimu wa kuwaheshimu  wazazi wetu na kuwafanyia wema, basi tujitahidi kutekeleza amri za Rabb wetu ili kupata Ridhaa Yake na Atulipe Pepo. 

 

 

************

 

Share