Muenzi Mke Wako

 

 

Muenzi Mke Wako

 

Shaykh 'Abdullaah 'Adhamiy

 

Imefasiriwa na Iliyaasa

 

Alhidaaya.com

 

 

Kwa kuoa huchukui tu mke, Bali unachukua ulimwengu wako mzima. Kuanzia hapo mpaka maisha yako yote mke wako atakuwa mwenzio, mwandani wako, na rafiki yako mpenzi.

 

Atashiriki katika nyakati zako nzuri, siku zako, na miaka yako. Atakuwa pamoja nawe katika furaha na shida, katika mafanikio na tabu, katika ndoto zako na katika wakati wa hofu. Ukiumwa, atakupa huduma bora kabisa. Wakati unapohitaji msaada atafanya vyovyote awezavyo kwa ajili yako. Wakati una siri, ataitunza siri yako, wakati unahitaji ushauri, atakupa ushauri mzuri kabisa.

 

Atakuwa na wewe utakapoamka asubuhi kitu cha kwanza ambacho macho yako yataona ni macho yake. Wakati wa mchana, atakuwa na wewe, kama kuna wakati mchache hatokuwa na wewe kwa kimwili, atakuwa anakufikiria wewe, anakuombea dua kwa moyo wake wote, akili yake yote, na roho yake nyote. Ukienda kulala usiku, kitu cha mwisho macho yako kuona itakuwa ni yeye, na ukilala bado utakuwa unamuona katika ndoto zako. Kwa kifupi atakuwa ni ulimwengu wako mzima na wewe utakuwa ulimwengu wake mzima.  

 

Kielezo bora kabisa ambacho mimi binafsi nishawahi kusoma kinafafanua ukaribu wa wanandoa juu ya wao kwa wao na kielezo hicho kipo katika aya ya Qur-aan ambayo inasema:

 

هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ

Wao ni vazi kwenu na nyinyi ni vazi kwao. .[Al-Baqarah: 187].

 

Na Kweli, wanandoa ni kama vazi juu ya wao kwa wao kwa sababu wanapeana ulinzi, liwazo, kinga (stara), msaada (tegemeo), na mapambo ambayo vazi linampa mtu. Hebu jaribu kufikiri msafara wakati wa siku za baridi kwenda sehemu kama vile Alaska bila ya kuwa na nguo! Wanandoa wetu wanatupa kiwango kile kile cha faraja (liwazo), ulinzi, na msaada  katika msafara wa maisha yetu katika dunia hii kama vile nguo itakavyofanya katika msafara wa Alaska.

 

Mahusiano baina ya wanandoa ni ya kustaajabisha kabisa katika mahusiano yote ya kibinaadamu: Idadi ya mapenzi na mahaba, undani na ukaribu, huruma na imani, amani na utulivu ambao unajaza nyoyo za wanandoa ni jambo lisiloelezeka kwa wepesi. Ufafanuzi pekee wa mantiki ambao unaweza kuelezeka juu ya haya mastaajabu makubwa katika hisia zote za kibinaadamu ni kwamba: Ni kitendo cha Allah Subhanahu wa Ta'aalaa:

وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا

Na Allaah Amekufanyieni wake katika jinsi yenu; [An-Nahl: 72] 

 

Rabb wetu tu Allaah Subhanahu wa Ta'aalaa katika katika Utawala Wake usio na upeo wa huruma Yake  isiyo na mipaka  na Hekima Yake adhimu Anaweza kujenga na kuzididimiza katika akili hizi hisia za kustaajabisha na za kubarikiwa katika nyoyo za wanandoa. Kwa kweli Allah Subhanahu wa Ta'aalaa Anawakumbusha wale ambao wanatafuta ishara Zake katika ulimwengu huu kwamba hisia hizi katika moyo wa wanandoa ni katika ishara Zake ambazo zinatakiwa zimuongoze mwanaadamu katika kuwepo Kwake kama Alivyosema katika Qur-aan,

 

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٢١﴾

Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni kwamba Amekuumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao; na Amekujaalieni baina yenu mapenzi na rahmah. Hakika pana katika hayo, bila shaka Aayah (ishara, zingatio nk) kwa watu wanaotafakari. [Ar-Ruwm: 21]

 

Lakini Allaah Subhanahu Wa Ta’aalaa Anajua kwamba moyo wa binaadamu sio kitu ambacho kiko tuli, wakati mwengine huwa dhaifu na wakati mwengine huwa na nguvu. Hisia zinaweza kubadilika na hubadilika pindi wakati unavyosogea. Mapenzi yanaweza kufifia na kupayuka mbalini. Mshikamano wa ndoa unaweza kuwa dhaifu kama haujahudumiwa vizuri. Furaha katika ndoa haiwezi kudharauliwa; furaha ya kuendelea inahitaji utowaji wa daima kutoka pande zote. Ili mti wa mapenzi ya ndoa ubaki hai na kuendelea kuishi, udongo lazima udumishwe, uhifadhiwe, umwagiwe maji na ulelewe.

 

Kumbuka kwamba Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipata nafasi ya kwenda kwenye majangwa na kushindana mbio na mke wake Bibi 'Aaishah. Bibi 'Aaishah alimshinda Nabiy lakini baadae aliponenepa, Nabiy alimshinda Bibi 'Aaishah. Kumbuka kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimchukua mkewe kwenda kuwatazama vijana wa Ki-Ethiopia wakicheza michezo ya utamaduni wao. Maonyesho ya hisia yanahitajika kuweza kuufanya mshikamano wa ndoa usifanye kutu na kuoza. Kumbuka kwamba utapata thawabu kutoka kwa Allaah (Subhanahu wa Ta'aalaa) kwa hisia zozote unazomuonyesha mkeo kama Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyosema:

 

"Mmoja wenu atapata thawabu kwa chochote ambacho atafanya ili kutafuta radhi za Allaah hata kwa tonge analomlisha mkewe"

 

Kamwe usidharau umuhimu wa vitu vidogo vidogo kama vile kuweka chakula kwenye mdomo wa mkeo, kumfungulia mlango wa gari, na hali kadhalika. Kumbuka kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasogeza goti lake kwa mkewe amkanyage kuweza kumpanda ngamia.

 

Jaribu kutafuta wakati ili nyote wawili muweze kuswali pamoja. Kuuimarisha uhusiano kati yenu na Allaah (Subhanahu wa Ta'aalaa) ni hakikisho kubwa kuwa uhusiano wenu wa kindoa utabaki madhubuti. Kuwa na amani kati yenu na Allah (Subhanahu wa Ta'aalaa)  daima kutapelekea ndani mwenu kuwa na amani zaidi.

 

Kumbuka kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapa habari nzuri (aliwabashiria) wanandoa wanaoamka usiku kuswali pamoja. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anamsisitiza mwanandoa anayeamka mwanzo amuamshe mwenzake, japo kummwagia maji katika uso wake. 

 

Daima jaribu uwezavyo kuwa mtu mzuri kwa mkeo kwa njia ya maneno na vitendo. Ongea nae, mchekee, tafuta ushauri wake, muulize juu ya mawazo yake, tumia wakati maalum na yeye na daima kumbuka kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"Wabora katika nyinyi ni wale ambao ni wabora kwa wake zao".

 

Mwishowe, ni kawaida kwa wanandoa kuahidi kuwapenda na kuwaheshimu wanandoa wenziwe mpaka mauti yawatenganishe. Naamini kwamba ahadi hii ni nzuri au ni bora kabisa, lakini haitoshi! Haitoshi kumpenda mkeo tu. Lazima upende anachokipenda pia. amilia yake, anaowapenda yeye uwapende pia. Usiwe kama mwenzangu mmoja ambaye hakufurahiwa kuja kwa wazazi wa mke wake kukaa kwa wiki chache. Alimwambia wazi mkewe "Mimi siwapendi wazazi wako". Bila ya kusita mkewe alimtazama machoni kwa hasira na kusema, “Na wako pia siwapendi”.

 

Mapenzi yasiishe na pia tunaamini kuna maisha baada ya mauti ambapo wale ambao walifanya wema katika dunia hii wataungana na wanandoa wenzio wataungana na watoto wao. Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa anasema katika Qur-aan Tukufu:

ادْخُلُوا الْجَنَّةَ أَنتُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ تُحْبَرُونَ﴿٧٠﴾

Ingieni Jannah nyinyi na wake zenu mfurahishwe. [Az-Zukhruf: 70]

 

Pia  Na mfano bora katika mintarafu hii itakuwa ni Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye mapenzi yake kwa Bibi Khadiyjah, mkewe aliyeishi naye kwa miaka 25 yalisogea mpaka kwa wale aliowapenda Khadiyjah; mapenzi yake haya yaliendelea hata baada ya kufa Bibi Khadiyjah. Ilikuwa miaka mingi baada ya kifo cha Bibi Khadiyjah na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumsahau na kila panapochinjwa mbuzi katika nyumba yake basi hutuma kifurushi kwa familia ya Bibi Khadiyjah na marafiki zake na kila akihisi kuwa mgeni  anayegonga mlango ni Dada ya Khadiyjah aitwaye Hala, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akiomba huku akisema, "Ee Allaah Jaalia awe ni  Hala."

 

 

 

Share