Kusoma Halal Badiri au Albadiri (Ahlul-Badr) Kwa Ajili Ya Kinga Na Kuapiza Ni Shirki Na Dhambi Kuu!

 

SWALI:

 

Assalama alikum warahmatullah taala wabarakatu.

Napenda kuanza kwa kumshukuru Mola mlezi wa ulimwengu kwa kuwapa nguvu, afya na uwezo ndugu zetu wa alhidaaya kwa kutuelimisha sisi ndugu zenu Waislam katika musuala mengi yanayohusu dini yetu ya haki. Mola awape kheir, baraka na pepo inshaalah. Ameen.

Na suali langu ni kutaka kujua kama kusoma halal badr ni sawa au si sawa katika uislam? Kuwa kama kinga na kuomba Mungu akuhukumie kwa anetaka kukudhuru au kukufania ubaya.

Asanteni....assalam aleykum.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Halali Badiri. Awali twataka kurekebisha ibara hiyo kwani sivyo inavyokusudiwa au inavyotamkwa au kuandikwa. Ibara hiyo imetoka katika lugha ya Kiarabu lakini kupotolewa au kuandikwa na kusomwa makosa katika Kiswahili. Wapo wanaosema Alibadiri lakini makusudio ni Ahlul-Badr, yenye maana watu wa Badr (wale waliopigana vita vya Badr). Badr ni sehemu iliyo karibu na Madiynah na ndio iliyokuwa sehemu ambayo Waislamu wakiongozwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walipambana na mushirikina wa Makkah katika vita vya kwanza baina ya pande hizo mbili. Waislamu waliohudhuria walikuwa baina ya 313 – 317, lakini pamoja na idadi yao ndogo hiyo waliweza kuwashinda washirikina waliokuwa na idadi kubwa ipatayo mara sita yao.

 

Kisomo cha Ahlul Badri inakuwa ni kutaja majina ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) mmoja baada ya mwingine. Katika kutaja huko ni Imani ya mwenye kusoma hao Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wanamsaidia kwa njia moja au nyingine. Ima kupata kitu alichopoteza au kilichoibiwa au kulaaniwa aliyefanya. Na hii katika Uislamu ni njia moja ya shirki ambayo Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wameikema na kuipiga vita sana. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Hakika Allaah Hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa Amtakaye. Na anayemshirikisha Allaah basi hakika amezua dhambi kubwa” (4: 48). Shirki ni dhuluma kubwa sana.

 

Ingia Katika Kiungo Kifuatacho pia upate maelezo yam as-ala haya:

 

Wazazi Wangu Wako Kwenye Maasi,Ushirikina Wa Waganga Na Albadiri (Ahlul-Badr)

 

Ikiwa unataka kinga basi kinga ni nyingi sana tulizopatiwa na Uislamu ni nyingi. Qur-aan yenyewe ni ponyo na kinga ya mambo mengi na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye hakutuacha hivi hivi ila ametupatia kinga nyingi katika Surah na Aayah za Qur-aan na du’aa alizotuachia. Miongoni mwa kinga ni Muislamu kusoma Surah 112, 113 na 114 mara tatu tatu asubuhi, jioni na wakati wa kulala. Hiswnul Muslim ni kijitabu kizuri cha du’aa na adhkaar katika mas-ala haya.

Utakipata kitabu hicho ndani ya Alhidaaya kwenye kiungo hiki:

 

Hiswnul Muslim

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share