Wazazi Wangu Wako Kwenye Maasi,Ushirikina Wa Waganga Na Albadiri (Ahlul-Badr)

SWALI:

Bismillah rahman rahiim

Asalaam aleykum,

mimi ni muislam mwezenu naishi na wazazi na wadogo zangu.

Ila nyumbani kwetu kuna mtihani mkubwa yani dada yetu mkubwa anaumwa kipindi kirefu kwa kipindi kirefu tulimpeleka hospital ikashindikana sasa wazazi wamempeleka kwa waganga ambao wanaagiza kuku,mbuzi,kusoma albadir,na kutaka kugeuza kitabu cha Allaah kwa kufru wakati haya yakiindelea mimi nipo chuo nasoma na wakati mwingine narudi nyumbani lakini roho ilikuwa inaniuma mno nikiambiwa maneno hayo.

sasa ikafika wakati mgonwa haponi na wazazi wanasema lazima tuwepo wote kwenye tiba hiyo, mimi nikasema sitashiriki mpaka apatikane mtu wa anayetumia ruqya pekee, kutokana na hivyo basi nashangaa wazazi wanaaza kuwa maaadui na mashaka na mimi mpaka wanafikia kusema niache kuswali nitachanganyikiwa nikiendelea.Wazazi wangu hawasalibaba yeye hadi pombe na mungu kamjaliia kifedha lakini anatumia madaraka yake vibaya.

mimi nimeomba dua sana nisigombane nao,warejee kwa Allaah,tutubu zambi lakini sheikh bado ndio chuki inazidi ikipungua kidogo sana mpaka mimi imani yangu najihisi inaudhoohofu kwa Allaah(s.w) yaani sielewi.

Sheik kwa elimu aliowapa Allaah (s.w) na maarifa mazuri naombeni mnishauri cha kufanya nisije nikakosa radhi za Allaah (s.w).

 

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo. Haya nayo ni baadhi ya matatizo ya kijamii ambayo hujitokeza pindi nyumba ikikosa mwelekeo wa kidini. Ikiwa maadili ya wazazi si ya Kiislamu basi matatizo kama haya hutoa kichwa chao nje na huleta mvurugano hasa kukiwa na mtoto ambaye anataka kushika na kutekeleza mas-ala ya Kidini ndani ya nyumba hiyo. Mitihani yake inakuwa mingi kwani anavutwa na jamii yake kuingia katika maasiya na kuacha uchaji Allaah.

Hii inakwenda sambamba na Sunnah (mipango/kanuni) za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika huu ulimwengu, nazo huwa hazibadiliki. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Hii ni ada ya Allaah iliyokuwa kwa wale waliopita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Allaah” (33: 62).

Pia, “Hebu hawatizami kwa yaliyowasibu watu wa kale? Basi hutapata mabadiliko katika Sunnah ya Allaah. Wala hutapata mageuko katika mwenendo wa Allaah” (35: 43).

Tufahamu kuwa katika Sunnah za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni kuwapatia waja wake mitihani. Mitihani hiyo inakuwa kulingana na Imani ya mja mwenyewe.

Wenye mitihani mikubwa na mizito ni Mitume na Manabii (‘Alayhimus Salaam) na wale walio chini yao. Kati ya mitihani ni mtu kuwa mgonjwa au jamaa yake wa karibu sana kuwa katika hali hiyo ya ugonjwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatueleza wale waliotetemeshwa kwa mitihani mikubwa pale Aliposema: “Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyo wajia wale walio pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya Allaah itakuja? Jueni kuwa nusura ya Allaah ipo karibu” (2: 214).

Pia tusidhani kuwa kwa kusema kwetu tumeamini tutaachiliwa tu hivi bila kutiwa katika mitihani. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Je, wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wamesema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe? Hakika Tuliwajaribu waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Allaah Anawatambulisha walio wa kweli na Atawatambulisha walio waongo” (29: 2 – 3).

Mitihani ipo mingi kama alivyotaja Aliyetukuka: “Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri” (2: 155).

Mtu anapotahiniwa ni wajibu wake kuwa mwenye subira, imara na kutoyumbayumba na kutoka katika maadili na muruwa wa Kiislamu. Ni makosa makubwa kwa Muislamu kuingia katika shirki pindi anapotiwa katika misukosuko. Shirki kubwa inamtia mwenye kuifanya daima Motoni nayo ni kwenda kwa wachawi wanaomuagizia kuchinja kuku, mbuzi na kadhalika. Na yote hayo ni udangayifu wa hali ya juu.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema kuhusu jambo hilo kuwa ni dhulma: “Na Luqmaan alipomwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Allaah, kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa” (31: 13). Ovu hilo linamfanya mtu asisamehewe madhambi yake: “Hakika Allaah Hasamehe dhambi la kushirikishwa na chochote na Husamehe dhambi isiyokuwa hiyo kwa Anayemtaka” (4: 48, 116).

Waislamu wengi wasioelewa Dini yao wanatishwa na kutishika kwa kusikia neno hilo lakini hata hawashtuki wala kujali pindi wanaposikia jina la Allaah, Jalla Jalaaluh. Hilo ni kosa na shirki kwani albadir ni neno la Kiarabu lililopotoshwa maana yake na makusudio, kwani usawa ni Ahlul Badr (watu wa Badr). Katika kisomo hicho kunasomwa majina 313 – 319 ya wale Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walioshiriki katika vita baina yao (Waislamu) na makafiri wa kutoka Makkah. Kuyatumia majina hayo kuomba kwayo au kumlaania mtu ni shirki na haifai Muislamu kufanya hilo.

Hakika ni kuwa Muislamu anapopatwa na tatizo au shida anatakiwa amuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), Naye Atamuondolea tatizo lake au matatizo yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Ambaye ndiye Aliyeniumba, na Yeye ndiye Ananiongoa. Na ambaye ndiye Ananilisha na kuninywesha. Na ninapougua ni Yeye ndiye Anayeniponesha” (26: 78 – 80).

Muislamu mwenye Imani thabiti ni lazima ahisi vibaya kwa kuambiwa maneno kama hayo uliyoambiwa miongoni mwa kauli za shirki. Hiyo ni dalili kuwa Alhamdullillah Imani yako ni hali ya juu lakini inatusikitisha kusikia kutoka kwako kuwa Imani hiyo imeanza kupungua na kudhoofu kwa sababu ya kutaka kuwaridhisha wazazi wako.

Ni muhimu kuelewa kuwa ni muhimu sana kwa mtoto kuwatii wazee wake kama alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): “Usimfanye mungu mwengine pamoja na Mwenyeezi Mungu, usije ukawa wa kulaumiwa uliyetupika” (17: 23).

Hata hivyo, inatakiwa tufahamu kuwa twaa hiyo inakuja baada ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haifai kuwafuata katika kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Anasema Aliyetukuka: “Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema duniani” (31: 15).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna twaa kwa viumbe katika kumuasi Muumba”. Kwa hiyo, haifai kabisa kuwatii kwa wanayoyataka kwani yanakwenda kinyume na kanuni za Kiislamu, katika kutekeleza hilo ni lazima usimame wima na uwe imara kabisa. Kwa kuwa jamaa zako wanakushurutisha kufanya maasiya ni mtihani mkubwa. Ndugu yetu katika Imani! Tambua kuwa haupo peke yako kwani Waislamu waliopita walipata mitihani mikubwa zaidi. Pia tunapata wengine katika wakati wetu huu waliofikiwa na zaidi ya hayo lakini walivumulia katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) mpaka faraja ikaja kwao. Kwa hiyo, watu hao walifanikiwa kupita mtihani wao huo.

Tazama jinsi gani Nabii Musa (‘Alayhis Salaam) alivyosumbuliwa na Mayahudi: “Enyi mlioamini! Msiwe kama waliomtaabisha Muusa, lakini Allaah Akamtakasa na waliyoyasema, naye alikuwa mwenye heshima mbele ya Allaah” (33: 69).

Jukumu lako wewe ni kuendelea kuzungumza na jamaa zako pamoja na wazazi wako kwa hekima huenda wakaongoka na usikate tamaa kwa hilo. Jaribu kutumia Mashaykh na wazee wenye busara wazungumze na babako kuhusu madhara kwake kwa kunywa pombe na pia kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), huenda akabadilika. Hiyo ni kuwa mwenye kuongoza ni Allaah aliyetukuka nasi hatuwezi kumuongoa tumtakaye. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Kwa hakika wewe humwongoi umpendaye; lakini Allaah humwongoa amtakaye. Na Yeye ndiye Anawajua zaidi waongokao” (28: 56).

Kuomba du’aa ni miongoni mwa Ibaadah kubwa kwa Muislamu kuitekeleza. Lakini hufai wewe kumwekea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) muda wa Yeye kukujibu maombi yako. Kusema kwako kuwa umeomba sana du’aa unamaanisha nini? Je, unaona kuwa ukiomba kwa muda fulani ni lazima uone tija yake au vipi? Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametoa ahadi kuwa Atatujibu maombi yetu lakini kwa njia ambayo Anaiona kuwa ni maslahi kwako hapa duniani na Kesho Akhera. Mwanachuoni mmoja amesema kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anamjibu mja Wake kwa maombi yake kwa njia zifuatazo:

1.    Kumjibu alivyotaka hapa hapa duniani kwa haraka sana.

2.    Kumbadilishia alichotaka kwa kizuri zaidi.

3.    Kumpatia alichotaka Kesho Akhera.

Kwa hiyo, wewe usiweke sharti katika kujibiwa kwako na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani ndiye Mjuzi wa yote hayo uyatakayo na ni juu yako kuendelea kuomba kwani Yeye Amesema: “Na waja wangu watakapo kuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka” (2: 186).

Na ile kauli yako kuwa watu wanazidi kukuchukia kwa sababu ya kufanya kwako Ibaadah si lolote wala chochote kwani hiyo ni dalili ya ima kuzidi mtihani au kupungua. Mara nyingi mtihani unapokuwa mkubwa nawe ukaweza kuvumilia na kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), Yeye Hukutolea njia kwa tatizo hilo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Na Anayemcha Allaah Humtengenezea njia ya kutokea” (65: 2).

Na pia, “Na anayemtegemea Allaah Yeye humtosha” (65: 3). Tufahamu kuwa mitihani ni aina nyingi kama tulivyotaja hapo awali na mojawapo ni kupigwa vita na jamaa zako wa karibu kwa misimamo yako ya Kidini na Imani yako.

Ni mapema sana kwako kufa moyo. Tutambue kuwa hiyo si sifa ya Muislamu kwa kuwa anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): “…Hakika hawakati tamaa na faraji ya Allaah isipokuwa watu makafiri” (12: 87).

Inafaa ushikilie kabisa kanuni za Dini na ukitofanya hivyo hasara itakuwa kwako hapa duniani na Kesho Akhera. Zama na nyakati hubadilika sana, hupata wakati mmoja ukiwa katika ufanisi na mwingine ukiwa katika janga na matatizo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Allaah awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyeezi Mungu hawapendi madhaalimu” (3: 140).

 

Ni dhahiri kuwa hakuna dhiki wakati wote kwani baada ya dhiki ni faraja. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Hakika pamoja na uzito upo wepesi” (94: 6).

 

Huu si wakati wa kwako kudhoofu Ki-Imani mbali na matatizo bali ni wakati wa kuzidisha ili uweze kupambana vilivyo na mitihani inayokukabili.

 

Njia nzuri kabisa ya kukabiliana ni kutaka msaada wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa subira na kwa kusimamisha Swalah: “Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kuswali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu” (2: 45).

Pia inatakiwa tuwe watiifu zaidi katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni hakika kuwa Imani hupanda (huzidi) kwa twaa na hupomoka kwa maasiya. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Mwenyeezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.

Hao ambao wanashika Swalah na wanatoa katika yale tunayowaruzuku” (8: 2-3).

 

Kwa kutekeleza hayo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakusaidia na InshaAllaah utaweza kuipita mitihani hiyo. Kuwa imara na usife moyo kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) yu pamoja nawe. Nasi ndugu zako tunakuombea at-taawfiyq katika mambo yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share