Nani Aliyesulubiwa Badala ya Nabiy 'Iysaa (عَلَيْهِ السَّلام)?

 

Nani Aliyesulubiwa Badala ya Nabiy 'Iysaa ('Alayhis-Salaam)?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam alaykum,

 

Bismillahi Rahman Rahim.

 

Namshukuru ALLAH kwa yote na kumtakia rahma na salam Mtume (SAW). Naomba kuuliza kuhusu hii dhana ya kifo cha Nabii Issa (AS) Walionayo wenzetu.

 

Nimekuwa naulizwa swali hili mara nyingi na kwa kweli sina jawabu la kuridhisha. Je ni kweli Issa (AS) alikamatwa, kuteswa na kuuwawa? Na kama sio, nani aliye sulubiwa msalabani? Naomba msaada wenu ktk hili.

 

Wabillahi tawfiq. Assalaam alykum

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabisa tunakunasihi kutokufupisha Thanaa au kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au katika maamkizi ya Kiislaam. Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate mwongozo?

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Maandishi

Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu

 

Kuhusu swali lako, hakika ni kuwa Qur-aan iko wazi kabisa kuwa Nabiy 'Iysa ('Alayhis Salaam) hakushikwa, hakusulubiwa wala hakuuawa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuelezea: 

 

وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّـهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ ۚ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ ۚ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ ۚ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا ﴿١٥٧﴾ بَل رَّفَعَهُ اللَّـهُ إِلَيْهِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴿١٥٨﴾ وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا ﴿١٥٩﴾

Na kauli yao: Hakika sisi tumemuua Al-Masiyh ‘Iysaa mwana wa Maryam, Rasuli wa Allaah. Na wala hawakumuua wala hawakumsulubu lakini walishabihishiwa tu. Na hakika wale waliokhitilafiana katika hayo, kwa hakika wamo katika shaka nalo. Hawana ujuzi nalo kabisa isipokuwa kufuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua. Bali Allaah Alimnyanyua Kwake. Na Allaah daima ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote  Na hakuna yeyote katika Ahlil-Kitaabi ila atamwamini kabla ya kufa kwake. Na Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao [An-Nisaa: 157 – 159]  

 

Aayah hizo zinatubainishia wazi kuwa Nabiy 'Iysaa ('Alayhis Salaam) hakuuliwa bali walifananishiwa mtu mwingine kwa sura zake. Katika Injili ya Barnaba (Gospel of Barnabas) inatueleza kuwa huyu aliyefananishwa na Nabiy 'Iysaa ('Alayhis Salaam) ambaye alisulubiwa ni Juda Iskariot ambaye alikuwa ni mfuasi wake lakini akamsaliti kwa maaskari wa Kirumi. Hata hivyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Hamuacha Nabiy Wake ashikwe, Akamgeuza huyu Juda alipoingia katika pango alilokuwemo Nabiy 'Iysaa ('Alayhis Salaam). Huyu ndiye aliyesulubiwa.

 

 

Ama Biblia ambayo ipo mikononi mwetu sasa ina utata mkubwa sana kuhusu suala hilo lakini pia inaonyesha kuwa aliyesulubiwa si 'Iysaa bali ni mtu mwengine kabisa. Sababu ambazo zinatufanya tuseme hivyo ni zifuatazo:

 

 

1) Paulo anasema kuwa yeye anakufa kila siku (1 Wakorintho 15: 31). Hii ina maana anateseka kila siku. Tufahamu kuwa kabla ya kukamatwa kwa Yesu, Biblia inatuarifu kuwa aliswali na kumuomba Mungu amuondoshee kikombe hicho (yaani umauti) kulingana na matakwa yake (Mungu) {Mathayo 26: 39, Marko 14: 35-36) na Luka 22: 42-43}. Na katika Luka tunaelezwa kuwa Malaika alitumwa kumtia nguvu. Je, maombi ya 'Iysa (au Yesu katika Biblia) yalijibiwa? Tunafahamishwa kuwa Yesu alisikilizwa maombi yake kwa ajili ya kumcha Mungu (Waebrania 5: 7). Maombi ya mtu mwema yanasikilizwa (Yakobo 5: 16). Na ni maneno yake (Yesu) aliyosema kuwa omba, nawe utapewa (Mathayo 7: 7-10). Kama tulivyoona hapo juu kuwa Yesu aliomba, naye bila shaka alikubaliwa.

 

 

2)  Yesu alikuwa hai kama alivyotabiri. Yesu alimwambia Maria Magdalene: "Usinishike; sijakwenda bado juu kwa baba …" (Yohane 20: 17). Yesu anaulizwa kuhusu ufufuo, naye anajibu kuwa miili iliyofufuliwa huwa kama Malaika (Luka 20: 34-36). Yesu anawatokea wanafunzi wake na kuwaambia wampapase mikono yake kuwa ndiye yeye naye akachukua kipande cha samaki na kula (Luka 24: 36-42).

 

 

3)  Na ikiwa kweli Yesu alikufa msalabani basi yeye ni Nabii wa uwongo na aliyelaaniwa. Yeyote anayetundikwa mtini amelaaniwa na Mungu (Kumbukumbu la Sheria 21: 22-23). Amelaaniwa anayetundikwa kwenye mti (Wagalatia 3: 13).

 

 

4)  Wakristo wanaamini kufa na kufufuliwa kwa ajili ya kufuata mafundisho ya Paulo (Matendo 17: 18). Ufufuo wa Yesu ni kulingana na Injili ya Paulo (II Timetheo 2: 8).

 

 

5)  Yesu alitabiri aliokolewa kuuliwa (Mathayo 23: 39, Yohane 7: 32-36, 8: 21-29 na 16: 32-33). Yesu hakika hakusulubiwa kabisa (Wagalatia 3: 1).

 

 

6)   Na hakika Yesu anatuhakikishia kuwa Mungu anamsikiliza yeye daima (Yohane 11: 41-42).

 

 

7)  Yohane anatueleza kuwa Yesu hakuvunjwa miguu yake bali alichomwa mkuki na hapo damu ikatoka (Yohane 19: 32-34). Kutokwa kwa damu inaonyesha kuwa alikuwa bado yu hai.

 

 

8)   Na dalili nyingine zipo lakini tutosheke na hayo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share