Zingatio: Chunga Kiapo Chako

 

Zingatio: Chunga Kiapo Chako

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

Uchungaji wa viungo vya Muislamu katika maisha haya umekuwa ni wa chini usio na maana yoyote. Mkono unaiba, mguu unampeleka baa au kuzini, na ulimi unadiriki kutoa kiapo cha uongo.

 

Ulimi ni kiungo kimoja ambacho chatumiwa vibaya mno takriban na wanaadamu wote, na ndani yake kuna kundi kubwa la Waislamu ambao hawajali yale yanayotoka ndani ya vinywa vyao.

 

Tutambue kwamba, kiapo juu ya viumbe ni haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuviapia. Ni kwa mfano pale Anaposema: Ninaapa kwa Siku ya Qiyaamah, Ninaapa kwa Jua na kadhalika. Mwanaadamu yeyote hana ruhusa ya kutoa kiapo kama hicho.

 

Kwa mujibu wa mafundisho ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kiapo cha Muislamu kinaelekezwa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na nini maana ya kiapo? Kiapo ni kuweka dhamana ya lile unalosema kwa Yule Unayemwapia. Kwamba hayo unayoyaapia ni ya kweli unahitaji kusadikiwa na wanaadamu wenzio. Basi ole wake yule ambaye anaweka kwa Muumba wake kiapo cha uongo.

 

Hivyo, kiapo ni chenye kuchungwa mno na wala sio kukifanya kuwa ni dhikri ya ulimi ukataka kila kitu kukifanyia kiapo hadi kuwa ni sababu ya kutumbukia kwenye dimbwi la moto. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuambia tusimtii yule mwenye kuapa kila wakati:

 

وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ﴿١٠﴾

Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, dhalili [Al-Qalam: 10]

 

Kitu ambacho kimejaa ndani ya maisha yetu Waislamu ni viapo visivyokuwa na kichwa wala mguu. Na kila wanapokumbushwa wao wanaufanyia kazi ule msemo: "Kelele za mlango hazimughasi mwenye nyumba". Wanakuwa hawajali wala hawakubali maneno ya Qur-aan au Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Nabiy wetu amekataza mno Muislamu kula kiapo ovyo ovyo. Kinyume chake Muislamu anakula kiapo cha uongo katika biashara ingawa Nabiy wetu amesema kwamba Allaah Hatamuangalia (kwa jicho la huruma) mtu namna hiyo Siku ya Qiyaamah. [Imesimuliwa na Abu Dharr na kupokelewa na Muslim].

 

Lililo kubwa ndani ya jamii zetu ni kufikishana mbele ya vyombo vya sheria kwa namna za udanganyifu, utapeli na uongo mtupu. Muislamu anadiriki kuweka kiapo cha uongo kwa Rabb wake ili apate mali ya mwengine bila ya halali. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesimuliwa akisema kama ilivyopokewa na Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa):

 

 
“Mimi ni binaadamu tu na nyinyi mnaleta migogoro yenu kwangu mimi, mukiwa wenye fasaha katika viapo vyenu kuliko wengine, ili ya kwamba nitoe hukumu kwa niaba yenu kwa mujibu wa ninayoyasikia kutoka kwenu. Hivyo, vyovyote nitakavyoamua kwa yeyote, ambapo kwa haki ni ya ndugu yake, asichukue kwani simpatii chochote ila kipande cha moto.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy].

 

Tunawanasihi wale waliochukua viapo vya uongo wakamilikishwa mali kwa njia za haramu wazirejeshe amana hizo haraka iwezekanavyo. Ya Ar-Rahmaan! Na wapo miongoni mwa viumbe Vyako waliokula kiapo kwa kudhulumu mayatima na wakala kiapo kwa lengo la kuzini na wake za watu. Umetakasika! Shingo zao zipo mikononi Mwako!

 

Ya Allaah! Tunategemea kwako, na tunageuka kuja Kwako, na Kwako tu ndiko marejeo yetu. Basi tunakuomba  wetu! Tutimizie nuru yetu, na Utughufirie, hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

 

Share