Kujiua Kwa Sababu Ya Mateso Na Dhiki Za Dunia Nini Hukmu Yake?

 

Kujiua Kwa Sababu Ya Mateso Na Dhiki Za Dunia Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Swali:

 

Salam Alekum,

 

Napenda kuuliza nini hukumu ya wanojiua nafsi zao kutokana na mateso wanyoyapata na taabu. Ahsante!

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tufahamu kuwa mitihani katika hii dunia na haswa kwa Muumini ni lazima. Na kila mmoja anapimwa na Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa kiasi cha Iymaan yake. Allaah ('Azza wa Jalla) Anasema:

 

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ ﴿٢﴾

Je, wanadhani watu kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao ndio wasijaribiwe? 

وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ ﴿٣﴾

Kwa yakini Tuliwajaribu wale wa kabla yao, ili Allaah Awatambulishe wale walio wakweli na ili Awatambulishe walio waongo.   [Al-‘Ankabuwt 29: 2 – 3].

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُم ۖ مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاءُ وَالضَّرَّاءُ وَزُلْزِلُوا حَتَّىٰ يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ مَتَىٰ نَصْرُ اللَّـهِ ۗ أَلَا إِنَّ نَصْرَ اللَّـهِ قَرِيبٌ ﴿٢١٤﴾

Je, mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali bado haijakufikieni (mitihani) kama ya wale waliopita kabla yenu? Iliwagusa dhiki za umasikini na maafa ya magonjwa na njaa na wakatetemeshwa mpaka Rasuli na wale walioamini pamoja naye wanasema: Lini itafika nusura ya Allaah? Tanabahi! Hakika nusura ya Allaah iko karibu. [Al-Baqarah: 2:214]

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ, وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ, وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ)) مسلم

 

((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lakeni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake)) [Muslim]

 

 

 

Kujiua kwa sababu ya mateso ni miongoni mwa madhambi makubwa inayompeleka mwenye kufanya kitendo hicho motoni. Kwa hivyo, mwenye kujiua makaazi yake Siku ya Qiyaamah ni Motoni.  Dalili kutoka Hadiyth zifuatazo:

 

Kutoka kwa Jundab (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtu alifikwa na maafa ya majeraha akajiua, hivyo Allaah Amesema: Mja wangu amejisababisha kufa mwenyewe kwa kuharakiza, hivyo Nimemharamisha Jannah.” [Al-Bukhaary]

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((مَنْ تَرَدَّى مِنْ جَبَلٍ فَقَتَلَ نَفْسَهُ، فَهْوَ فِي نَارِ جَهَنَّمَ، يَتَرَدَّى فِيهِ خَالِدًا مُخَلَّدًا فِيهَا أَبَدًا، وَمَنْ تَحَسَّى سَمًّا فَقَتَلَ نَفْسَهُ، فَسَمُّهُ فِي يَدِهِ، يَتَحَسَّاهُ فِي نَارِ جَهَنَّمَ خَالِدًا مُخَلَّدًا فِيهَا أَبَدًا، وَمَنْ قَتَلَ نَفْسَهُ بِحَدِيدَةٍ، فَحَدِيدَتُهُ فِي يَدِهِ، يَجَأُ بِهَا فِي بَطْنِهِ فِي نَارِ جَهَنَّمَ خَالِدًا مُخَلَّدًا فِيهَا أَبَدًا)) البخاري ومسلم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Yeyote atakayejitupa kutoka mlimani na kujiua, atatupwa ndani ya moto milele. Atakayekunywa sumu na kujiua, basi atatupwa motoni na huko atakuwa akiinywa hiyo sumu milele. Atakayejiua kwa kipande cha chuma, atatiwa motoni akiwa na kipande hicho cha chuma akijitwanga nacho tumboni kwake humo motoni milele))].  [Al-Bukhaariy na Muslim]

  

 

Anas bin Maalik ameripoti kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asiombe mmoja wenu kufa kwa sababu ya shida iliyomfika, bali ikiwa hakupata msaada aombe (du’aa) “Ee Allaah, nijaalie niishi ikiwa uhai kwangu ni kheri na nipe mauti ikiwa mauti kwangu ni kheri kwangu” [Muslim]

 

Kadhaalika, mtu anayejiua, au jambazi, au aliyefariki kwa kutumia madawa ya kulevya au kuuza, mlevi n.k. wote hao watatengwa kuswaliwa na Viongozi wa Dini ili iwe funzo kwa wale wenye tabia hizo waweze kujiepusha na maovu hayo. Lakini, hata hivyo, wanaweza kuswaliwa na watu wa kawaida.

 

Rejea pia kiungo kifuatacho:

Hukmu Ya Muislamu Anayejiua

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share