Hukmu Ya Muislamu Anayejiua

 

SWALI:

 NINI HUKUMU YA MUISLAMU KUJIUA AU KUJINYONGA?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hukmu ya Muislamu anayejiua.

Uislamu umetukataza kujiua na yeyote mwenye kujiua atakuwa ametenda madhambi makubwa na yatakayomsababishia kuingia motoni na kuharamishiwa pepo. Isitoshe, ataadhibiwa kwa chombo kilekile alichotumia kujiulia. Allaah Aliyetukuka Atuepushe kabisa na balaa hilo la kujinyonga au kujiua kwa njia yoyote ile.

 

Anasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah,

"Yeyote atakayejitupa kutoka mlimani na kujiua, atatupwa ndani ya moto milele. Atakayekunywa sumu na kujiua, basi atatupwa motoni na huko atakuwa akiinywa hiyo sumu milele. Atakayejiua kwa kipande cha chuma, atatiwamotoni akiwa na kipande hicho cha chuma akijitwanga nacho tumboni kwake humo motoni milele." Al-Bukhaariy na Muslim

 

Kadhaalika, mtu anayejiua, au jambazi, au aliyefariki kwa kutumia madawa ya kulevya au kuuza, mlevi n.k. wote hao watatengwa kuswaliwa na Viongozi wa Dini ili iwe funzo kwa wale wenye tabia hizo waweze kujiepusha na maovu hayo. Lakini, hata hivyo, wanaweza kuswaliwa na watu wa kawaida.

 

Ingia katika kiungo kifuatacho upate majibu zaidi:

 

Nini Hukmu Ya Kujiua Kwa Sababu Ya Mateso Na Tabu Za Dunia

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share